The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mauaji, Ubakaji na Vipigo: Simulizi za Kutisha za Mamia ya Wananchi Tabora Waliobaki Bila Makazi Baada ya Serikali Kugeuza Ardhi Yao Kuwa Hifadhi

Wananchi wanalalamika Serikali kutumia mabavu kuwahamisha kwenye ardhi yao iliyobadilishwa kuwa hifadhi bila ushirikishwaji wa wanavijiji.

subscribe to our newsletter!

Kaliua, Tabora. Hata bila ya kuongea kitu chochote, mtu yoyote anayeweza kuwa karibu na Shamsha Salum* anaweza kuhitimisha kwamba mama huyu wa watoto saba hawezi kuwa mtu mwenye furaha. Majonzi na simanzi yamejiandika kwenye uso wote wa mama huyu mwenye umri wa miaka 50, kumlazimisha yoyote kutamani kujua simulizi yake ya maisha.

Mkazi huyu wa kitongoji cha Ntintimo, kijiji cha Usinge, wilayani hapa amepitia masaibu ambayo yanaweza kumfanya mtu ahoji utofauti uliopo kati ya binadamu na mnyama, siyo kwa kosa lingine lolote lile isipokuwa kuishi kwenye ardhi ambayo babu na bibi zake waliishi kwa miaka, ambayo sasa Serikali imeamua kuitwaa na kuigeuza kuwa eneo la hifadhi.

Akiwa ameketi juu ya kiti, akizungukwa na shamba la mahindi  yaliyostawi vizuri, Shamsa anakumbuka tukio lililotokea mwaka 2022 – hakumbuki mwezi wala siku, lakini anajua ilikuwa majira ya asubuhi– lililomuachia kumbukumbu mbaya na mateso mengi ambayo hakuwahi kufikiria ingetokea siku katika maisha yake kutokewa na masaibu hayo.

“Nikiwa nje ya nyumba yangu, niliona rundo la watu likija pale nilipo, huku nikiona nyumba zingine zikiteketea kwa moto baada ya watu hao kuzichoma,” anakumbuka Shamsa, akizungumzia kwa uchungu kisa hicho kinachohusisha askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA). “Nikampigia kelele mume wangu, aliyekuwa ndani ya nyumba, atoke, lakini ile kutoka tu, wale watu wakanishika.”

Kilichotokea baada ya hapo Shamsa hataki kukikumbuka. Walimchapa na fimbo kama apigwavyo pweza kabla ya kupikwa. Walimbaka kwa mpigo, mmoja baada ya mwingine, mpaka akapoteza fahamu. Hakumbuki walimbaka watu wangapi, lakini anajua kwamba alipoteza fahamu wakati mtu wa tatu akimuingilia kwa nguvu.

Shamsa alipozinduka, aliona nyumba yake tayari imechomwa moto. Pembeni yake, mtoto wake pia ameuwawa. Wakati analalamika, shemeji yake alikamatwa na kupigwa marungu, na wengine walikuwa na mabunduki, mpaka akafa. Mume wake alipigwa na kufanywa mlemavu hadi leo hii ambapo akiugua anatapika mpaka damu.

Kuingiliwa kimwili kwa nguvu kulimuachia Shamsa maumivu makali na magonjwa mengine ya hatari. Uke wake ulikuwa unatoa uchafu mwingi, na haja ndogo ilimtoka bila kuwa na taarifa. Alipelekwa hospitali na kufanyiwa upasuaji, akitolewa uvimbe wenye uzito wa kilo tatu.

SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro

“Kumbe alikuwemo mtoto humo [tumboni], nikaambiwa kumbe huyu alikuwa ni mtoto,” anasimulia Shamsa, machozi yakiwa yamejaa kwenye macho yake. “Nikatolewa na kizazi. Sasa huu mshono unanisumbua. Sasa hivi naweka vitambaa kuzuia haja ndogo, ni kama nipo kwenye siku zangu.”

Mgogoro

Simulizi ya Shamsa inaakisi maisha ya wenzake wengi kutoka katika kata za Usinge, Nzugimulole, Usenye, Igagala na Ugunga, katika wilaya ya Kaliua, mkoani Tabora, ambao tangu mwaka 2021 wamekuwa katika mgogoro na TAWA na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kufuatia hatua ya Serikali kutwaa sehemu ya ardhi ya vijiji na kuigeuza kuwa hifadhi, na kuziacha kaya takriban 7,000 bila makazi.

Serikali inadaiwa kutwaa ardhi hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,300, au hekari 1,300,000, kinyume na sheria za nchi, kama Sheria ya Ardhi ya Kijiji, 1999, inayoupa Mkutano wa Kijiji jukumu la kuridhia katika kubadilisha matumizi ya ardhi ya kijiji. 

Lakini wanavijiji wanalalamika pia hawakupewa taarifa, au notisi, inayotakiwa wakati wa kubadilisha ardhi kutoka kundi moja kwenda jingine kama sheria tajwa inavyotaka. TAWA na TFS wanadaiwa kutekeleza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika kuhamisha wananchi kwenye vijiji vilivyogeuzwa kuwa hifadhi.

Askari wa TAWA, TFS na mgambo, kwa mfano, wanadaiwa kubaka wanawake, kuchoma nyumba za wananchi, kubomoa shule iliyojengwa kwa nguvu za wananchi, kuuwa wananchi kwa kuwapiga risasi za moto, kuuwa mifugo ya wananchi kwa kuipiga risasi, pamoja na kupora na kufilisi mali za wananchi, ikiwemo mifugo.

Shule iliyokuwepo kwenye ardhi yenye mgogoro ambayo askari wa uhifadhi wanadaiwa kuivunja kushinikiza wanavijiji waondoke kwenye ardhi hiyo. PICHA | WANAKIJIJI WA ISAWIMA.

Ebrantino Mgiye, Kamishina Mwandamamizi wa TFS mkoani Tabora, alikanusha askari wa mamlaka hiyo kuhusika na matukio hayo, akiiambia The Chanzo kwamba wakala huo hauna wajibu wa kufanya kazi kweye maeneo ambayo wananchi hao wanalalamika.

TAWA mkoani Tabora ilikataa kutolea maelezo shutuma hizo, ikimuelekeza mwandishi TAWA makao makuu. Mpaka wakati wa kuchapisha habari hii mamlaka hiyo ilikuwa haijarudi kwa mwandishi kwa ajili ya majibu.

SOMA ZAIDI: Kashfa ya Loliondo Inatuonyesha Kwamba Uhifadhi Tanzania Upo Kwa Malengo ya Kibiashara, Siyo Kulinda Mazingira

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Rashid Chuachua, aliiambia The Chanzo kwamba madai hayo ya wananchi hayana ukweli wowote, akimtaka mwandishi ampatie mawasiliano ya mwathirika yoyote wa matukio hayo ili hatua stahiki zichukuliwe.

“Sheria iko wazi tu, kwamba wananchi hawaruhusiwi kwenda [hifadhini],” Chuachua alisema kwa sauti iliyoashiria jazba. “Lakini hakuna mgogoro wowote uliofika mezani kwangu, kwamba kuna mgogoro wowote, sijapata tatizo lolote mezani.”

Uchunguzi wa The Chanzo umebaini kwamba ardhi iliyotwaliwa na Serikali ilikuwa sehemu ya hifadhi jamii – inayotambulika rasmi kama Igombe and Sagara Wildlife Management Area (ISAWIMA)–iliyoanzishwa mwaka 2007 na vijiji 11 katika tarafa ya Igagala, wilaya ya Kaliua, iliyohusisha kilomita za mraba 1,800, au hekari 1,800,000, za ardhi ya vijiji ili kuzuia matumizi holela ya maeneo ya kila kijiji mshirika.

Baadaye, Serikali ilitwaa kilomita za mraba 1,300, kutoka katika kilomita za mraba 1,800, kuanzisha hifadhi ya Igombe Game Reserve, na kuwaachia wananchi kilomita za mraba 500 kwa ajili ya matumizi yao.

Hata hivyo, wananchi hawajapata hizo kilomita za mraba 500 na badala yake hifadhi jamii ya ISAWIMA inadaiwa kupora ardhi hiyo. Hifadhi jamii ya ISAWIMA inadaiwa kushirikiana na TAWA kudhulumu ardhi hiyo kwa kutumia mabavu, vipigo, uharibifu wa mazao, faini zisizo halali na ubakaji.

Serikali ya mkoa na ile ya wilaya zimeendelea kuitambua ISAWIMA licha ya ukweli kwamba kwa sasa, kwa mujibu wa GN No. 455 ya 2021, Hifadhi Jamii ya ISAWIMA haina ardhi, ikikalia ardhi ya wananchi, na kupelekea mgogoro kati yake na wanavijiji.

Wananchi wanaitaka Serikali iwapatie kilomita za mraba 500 zilizobaki baada ya Serikali kutwaa eneo la Igombe Game Reserve, ardhi ambayo inashikiliwa na ISAWIMA katika namna ambayo wananchi wanaamini siyo kihalali.

Ushahidi

Ingawaje Chuachua anadai kwamba hakuna matukio yoyote ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye utekelezaji wa operesheni ya kuwaondoa wanavijiji kwenye maeneo yanayodaiwa kuwa ni ya hifadhi, The Chanzo imepatiwa ushahidi wa kutosha, wa maandishi na picha, unaoonesha ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi na misingi ya haki za binadamu kwenye utekelezaji wa operesheni hiyo.

SOMA ZAIDI: Aliyepewa Kesi na Askari wa Hifadhi na Kufungwa Miaka 20 Aachiliwa Huru. Ushahidi Ulipikwa, Mahakama Yatoa Onyo

Kwa mfano, askari wa uhifadhi wanadaiwa kumkamata Maganga Mkito, mkazi wa kijiji cha Mtakuja, nyumbani kwake mnamo Mei 12, 2023, na kupelekwa kusikojulikana. Mwili wa Mkito ulipatikana siku mbili baadaye, Mei 14, 2023, ukiwa ndani ya mto. Oktoba 3, 2021, askari walimpiga risasi za moto Pagi Mailoni Sumba, mkazi wa Mtakuja, akiwa na mwenzake katika malisho ya mifugo.

Picha iliyopigwa na wananchi ikionesha mwili wa mwanakijiji katika eneo la ISAWIMA aliyefariki baada ya kudaiwa kupigwa na risasi za moto na askari wa uhifadhi. PICHA | WANANCHI WA ISAWIMA. (picha imehaririwa (blurred) kupunguza makali)

Pia, mnamo Novemba 23, 2021, majira ya saa nne asubuhi, gari za doria zaidi ya tano, zikiwa zimejaa askari, zilifika katika kijiji cha Ufulaga Mtakuja Magharibi kuwaondoa wananchi kwenye eneo linalodaiwa ni la uhifadhi. Askari wanadaiwa kufanya ukatili mkubwa, ikiwemo kuwabaka wanawake, kuchoma nyumba moto, na kuharibu mazao. Watu watatu walifariki kwa kupigwa risasi, ambao ni Saidi Msapa, Masele Mnyeti na Nsoka Ilinga.

Askari pia walidaiwa kufika kwenye familia moja na kusababisha kifo cha Mihangwa Lutamula, ambaye ni baba, na mtoto wake, Amosi Mihangwa, waliokufa kwa kupigwa risasi za moto. Askari wanadaiwa kuchukua miili hii mitano ya watu waliowaua na kuiteketeza kwa moto ili kupoteza ushahidi.

Wananchi wanalalamika Serikali kutumia mabavu kuwahamisha kwenye ardhi yao iliyobadilishwa kuwa hifadhi bila ushirikishwaji wa wanavijiji.
Stakabadhi za malipo zinazoonesha fedha walizotozwa wanakijiji na mamlaka za uhifadhi kwa madai ya mifugo yao kuonekana kwenye eneo la uhifadhi. PICHA | WANAKIJIJI WA ISAWIMA.

Mbali na matukio haya ya mauaji, askari wa uhifadhi pia wanadaiwa kupora na kufilisi mali za wananchi zenye thamani ya mamilioni ya shilingi kama ilivyo kwa Makula Lyankami ambaye mnamo Julai 30, 2022, alivamiwa nyumbani kwake na askari wa uhifadhi na kumuibia Shilingi milioni 14. Pius Shaaban aliibiwa Shilingi 300,000. Mbogo Tungu aliibiwa Shilingi 3,050,000. Manji Juma aliibiwa pikipiki yake.

Askari wa uhifadhi pia wamedaiwa kupiga wanyama risasi, ambapo mnamo Januari 1, 2023, walipiga risasi ng’ombe 39 waliokuwa wanamilikiwa na Juma Adili na kufariki papo hapo. Wanakijiji wengi pia wameshuhudia ng’ombe wao wengi wakipigwa risasi na askari wa uhifadhi au kuchinjwa bila idhini yao.

Ng’ombe ambao wananchi wa ISAWIMA wanadai wameuliwa kwa kupigwa risasi za moto na askari wa uhifadhi baada ya kuonekana kwenye ardhi yenye mgogoro. PICHA | WANAKIJIJI WA ISAWIMA.

Wenyeviti wawili wa vijiji vilivyoathiriwa zaidi na vitendo hivi, ambao The Chanzo imeamua kutoweka hadharani majina yao kwa sababu za kiusalama, walithibitisha kutokea kwa matukio haya, wakielekeza lawama kwa TAWA, wakiitaka Serikali ya wilaya kuingilia kati kuwanusuru na mateso na manyanyaso kutoka kwa askari wa uhifadhi. 

“TAWA ipo chini ya mkuu wa wilaya, inatupiga sana, inayanyasa sana,” alisema mwenyekiti mmoja wa kijiji. “Mkuu wa wilaya ajaribu kukaa nao ili wasizidi kutudhalilisha, sisi ni Watanzania. Hatuna nchi nyingine ya kwenda kuishi. Sisi kuishi kwetu ni hapahapa Tanzania. Tuna haki ya kuishi.”

SOMA ZAIDI: Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania Hauwasaidii Masikini. Serikali Ianzishe Ofisi ya Uwakili Raia

Chuachua, mkuu wa wilaya ya Kaliua, aliiambia The Chanzo kwamba hayafahamu madai yote haya, akisema kwamba kama kuna mwananchi anadhani hajatendewa haki afike ofisini kwake kuyawasilisha.

Picha zinazoonesha matukio ya uchomaji moto unaodaiwa kutekelezwa na askari wa uhifadhi katika vijiji vya ISAWIMA. PICHA | WANAKIJIJI WA ISAWIMA.

“Kama wanaonewa waje ofisini tuweze kuchukua hatua,” alisema Chuachua. “Kwa sababu sisi tuko hapa kwa ajili ya kuhudumia wananchi, na mwananchi yoyote ambaye ana changamoto tunamsikiliza. Kwa hiyo, wanakuambia wewe [mwandishi] wamepigwa wakati kwangu hawajafika. Hilo ni tatizo. Waje tuweze kuchukua hatua, hao waliopigwa.”

Sera za kikoloni

Hii siyo mara ya kwanza kwa askari wa TAWA na TFS kulalamikiwa kujihusisha na vitendo vya uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu, wakishukiwa kujihusisha na vitendo hivyo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, hali iliyopelekea Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kulaani vitendo hivyo hapo Mei 30, 2023, na kuhimiza uwajibikaji.

Sababu mbalimbali zimekuwa zikitolewa juu ya kwa nini askari wa mamlaka hizi hujihusisha na vitendo hivi, huku Tume ya Haki Jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikihusisha tabia hizo na sura za kijeshi ambazo mamlaka kama TAWA na TFS zimepewa na Serikali, ikitaka mabadiliko kufanyika ili msisitizo uwe kwenye utoaji wa huduma badala ya mamlaka hizo kupewa sura za kijeshi.

Mahusiano kati ya mamlaka za uhifadhi na jamii zinazozunguka maeneo hayo yamekuwa yakizidi kuharibika kwa siku za hivi karibuni kutokana na mpango wa Serikali wa kutenga maeneo mengi zaidi kwa ajili ya uhifadhi, hali inayopelekea mivutano kati ya wananchi na mamlaka za uhifadhi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Wataalamu wanaamini kwamba migogoro hii inaweza kutatuliwa kwa Serikali kubadilisha sera na sheria zake za uhifadhi, ambazo nyingi inadaiwa kuzirithi kutoka kwa wakoloni bila kuzifanyia maboresho yoyote, ili ziakisi mahitaji halisi ya Kitanzania, ikiwemo maslahi ya watu wa jamii zinazozunguka maeneo ya uhifadhi.

Moja kati ya wataalamu ambao wamekuwa wakitoa pendekezo hili ni Dk Ronald Ndesanjo, mwanaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambaye ametafiti sana kuhusiana na migogoro ya aina hii. Dk Ndesanjo aliiambia The Chanzo Aprili 24, 2024, kwamba bila mabadiliko hayo ya kisera na kisheria, Tanzania itaendelea kushuhudia migogoro hii ikitokea sehemu mbalimbali za nchi.

SOMA ZAIDI: Tume Yaitaka Serikali Kuacha Kuanzisha Taasisi Zenye Taswira ya Kijeshi

“Rasilimali zinazohifadhiwa kwa ajili ya utalii ndiyo nguzo muhimu pia kwa maisha ya wananchi wengi,” Dk Ndesanjo alisema. “Kuendelea kudhibiti matumizi ya rasilimali hizi dhidi ya jamii na kushindwa kutoa vyanzo mbadala na stahiki kwa jamii husika kuendesha maisha yao kutaendeleza migogoro hii.”

“Swali la msingi kuelekea mabadiliko ni: Je, kiasi gani cha faida itokanayo na uhifadhi wa utalii kinabaki, au hupelekwa, kwa jamii?” alihoji mtaalamu huyo. “Kama mgao ni kidogo kuliko faida jamii wanazopata kwa kutumia moja kwa moja rasilimali husika, migogoro hii itaendelea kuwepo.”

*Siyo jina lake halisi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

5 Responses

  1. Utalii unatugandamiza. Uhifadhi kiholela bila kujali maslahi ya waishio karibu na eneo husika unazaa migogoro. Hatma yake ni mateso na ukatili kwa wananchi kutokana na vyombo vya mabavu ya serikali kutokuthibitiwa na kutokuwajibishwa. Chanzo cha migogoro mingi ya ardhi nchini ni serikali yenyewe. Ukatili na mateso hayatakoma kama jamii utakaa kimya. Uvumilivu una mwisho! Utulivu bila haki ni feki. Unasubiri kulipuka.

  2. Ni maeneo mangapi nchini yanapitia hichi kitu?Ni WaTanzania wangapi wanapitia mateso ndani ya nchi yao?
    Hivi vitu vinamnufaisha nani?(maana kama ni utalii inabidi kunufaisha wananchi, sio kuwanyonya damu na uhai wao).
    Hivi vitu vinabidi vichukuliwe hatua,ni kinyume na sheria za nchi yetu,ni kinyume na ubinadamu, ni kinyume hata na dini zetu.

  3. Kuna mambo yanatia simanzi sana ,huwez amin kama yanafanywa na binadamu mwenzako yaaan ardhi inatifanya wanadamu tugeuke wanyama hii ni aibu sana ,unaondoa utu wa mtu kisa ardhi how jaman sasa mama wawatu had sasa wamepa ulemavu wa milele na baba wawatu ulemavu wa milele maana yake wamewafanya wanafamilia hawa kuwa watumwa maisha Yao yote kisa ardhi ,hii laana Haitokaa imwache mtu salama hakika MUUMBA kayaona yote yaliyotendeka hata kama ni miaka mingap dhambi hiii itawaandama walio husika na vizazi vyao na watailaani bila kujua chanzo chake ,MUNGU hadhiakiwi hata kidogo utu wa mtu unathaman Zaid ya ardhi tunayoipigania ,na viongoz tulio wapa madaraka kama wameshindwa kusimamia sheria ya ardhi kwa wananchi ni bora kukaa kando kuepusha ghashabu ya MUNGU,Watu hawaelew kwann tunapitia majanga kila kukicha hii ni ghadhabu ya MUNGU kwa matendo yanayofanywa na watu kisa mali ardhi inawalilia damu zao zilizo mwagika bila hatia mtazilipa
    Amina

  4. Inasikitisha sana kusikia matukio kama haya yametokea, na tena yamefanywa na askari wetu, kama kweli haya yametokea! Hakuna kitu chochote kinachohalalisha mauaji ya mwanadamu. Kama Kweli kuna askari wamefanya hivyo basi wachukuliwe hatua za kisheria, na uongozi wa jeshi usu utazame namna nzuri ya kudhibiti matukio kama haya.

    Kiukweli, wananchi wamekuwa wakihamia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwa kasi ya ajabu, jambo linalohatarisha uendelevu wa maeneo haya muhimu kwa ustawi wa Taifa lijalo. Wengi ni wafugaji na wakulima wanaohama hama. Kila wakihamia sehemu wanaharibu uoto wa asili, baioanuwai, kimsingi, ikolojia na kiwango cha mvua na maji kwenye eneo husika. Pakiishaharibika wanahamia kwenye hifadhi nyingine. Mpaka lini? Mpaka hifadhi zote ziishe?

    Kila wanapohamia husema ni kwao. Bahati mbaya sana siku hizi kuna jeshi usu na ulinzi mkali wa maeneo haya. Hivyo, inakuwa ngumu kwao kuhamia sehemu na ku-settle na hatimaye kudai kuwa ni kwao.

    Kumekuwa na matukio ya askari kuuwawa na wananchi waliojioganaizi kupinga kuondolewa kwenye hifadhi, siyo eneo moja ama mara moja.

    Siku nyingine itapendeza kama The Chanzo mtatuletea takwimu na matukio ya aina hii pia.

    Kama Taifa ni lazima tulinde urithi wetu wa Maliasili kwa wivu mkubwa. Maeneo haya ni muhimu sana kwa Taifa siyo tu kwa utalii (kama alivyosema Prof. Shivji hapo juu!) bali yanatengeneza vyanzo vya maji tunayotumia kuzalisha umeme, majumbani, mvua, oxygen n.k.

    Utajiri wa vyanzo vya maji baridi utakuja kuwa neema kubwa kwa watu wetu hususan tutakapozidi idadi ya 100m, maana tutatumia kwa kilimo cha umwagiliaji na tutapata uhakika wa chakula kwa watu wetu. Tutafika zaidi ya 100m Katika miaka si zaidi ya 30 ijayo! Sisi wa leo tusiwe wabinafsi kiasi cha kuharibu kila kitu tulichokirithi. Tulirithishwa, tuwarithishe.

    Masuala ya mazingira si ya kuchezea chezea ama kuyaongea kwa mihemko tu. Tutafakari.

    1. Bwana Kigwangala unazungumza mambo kwa jumla jumla. Madai ya wananchi kuingia maeneo ya Hifadhi ni uzushi tu, angalia takwimu za maene ya hifadhi kabla ya uhuru, baada ya uhuru na hata sasa. Kila uchao Serikali inapanua zaidi maeneo ya hifadhi kwa kutwaa maeneo ya wananchi.

      Kwa kuwa Serikali inatumia vyombo vya mabavu na propaganda ndio inakuja na lugha kama hizi unazozitoa.

      Ushahidi wa kihistoria na kisheria kuhusu eneo za tarafa zilizoripotiwa kutoka Wilaya ya Kaliua inaonesha dhahiri Serikali ndio imetwaa eneo hilo sio wananchi.

      Nasaha zako kwa kutunza urithi unatumia busara na hekima za kikoloni ni kama kuwafanya wananchi ndio waharibifu na Serikali ndio mkombozi. Jiulize Hifadhi zipo kwa ajili ya nani? Ikiwa askari pori wanawateketeza?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *