The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Aliyepewa Kesi na Askari wa Hifadhi na Kufungwa Miaka 20 Aachiliwa Huru. Ushahidi Ulipikwa, Mahakama Yatoa Onyo

Ni wakati sasa vyombo vya usimamizi wa sheria kuboresha namna wanavyofanya ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa kesi zinazohusu wanayamapori na haki jinai kwa ujumla,” Mahakama yaamuru.

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Aprili 24, 2024, ni tarehe ambayo itabaki kwenye historia katika maisha ya Richard Changei Ng’ombe, mkazi wa Serengeti aliyeachiwa huru baada ya kuanza kutumikia kifungo chake cha miaka 20.

Historia hii haiishii tu kwa Ng’ombe, bali hata kwa Watanzania wengine kutokana na maagizo  muhimu yaliyoachiliwa na Mahakama chini ya  Jaji wa Mahakama Kuu, Kamazima Idd Kafanabo, katika hukumu yake ya kesi ya rufaa namba 40809 ya mwaka 2023.

Chimbuko la kesi hii ni jioni ya Agosti 12, 2022, majira ya saa kumi na mbili. Richard Changei Ng’ombe, aliyekuwa akijongea kurudi nyumbani kwake, huku mkononi ameshika kidumu chake cha pombe za kienyeji, anaeleleza alipewa lifti na maaskari wa hifadhi walioukutana naye njiani.

Hata hivyo, lifti hiyo ilibadilika na kuwa shubiri baada ya maafisa hao kumpeleka moja kwa moja kwenye kambi yao, na kumshikilia mpaka asubuhi ya Agosti 13, 2022, huku wakimpa kipigo kikali. 

Ng’ombe anasema maafisa hao wa hifadhi walichotaka ni awaeleze mahali anapoenda kuuza pombe ya kienyeji, ambapo maafisa hao walilisitiza kuna wawindaji majangili, jambo ambalo alikataa na kueleza hafahamu wawindaji wowote haramu. 

Asubuhi ya siku iliyofuata, yaani Agosti 13, Ng’ombe alipelekwa mpaka Kituo cha Polisi cha Mugumu kilichopo wilayani Serengeti, na mnamo Agosti 17, 2022, alifikishwa mahakamani. Jambo lilomshangaza ni makosa aliyokutwa nayo, ikiwemo  kukutwa hifadhini bila kibali, kukutwa hifadhini na silaha na kukutwa na nyara za Serikali.

Huu ndio ulikua mwisho wa Ng’ombe kufahamu uhuru. Aliendelea kusota mahabusu kwa muda wa mwaka mmoja hadi kesi yake ilipoamuliwa mnamo Oktoba 3, 2023, ambapo alipewa hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela.

SOMA ZAIDI: Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki

Haya ni maelezo ya mtuhumiwa yaliyoelezwa mbele ya Jaji Kafanabo aliyeamua hatma yake kama ataendelea kutumikia kifungo chake cha miaka 20 au la.

Upande wa askari wa uhifadhi wanaeleza kuwa mtuhumiwa alikamatwa hifadhini na nyaya nane za  kutega wanyama pori, panga moja pamoja na nyara za Serikali, yaani miguu miwili, mbavu na kichwa cha pundamilia. 

Maafisa hao walidai kwamba mahali alipokamatiwa palinakiliwa kwa kutumia mfumo wa GPS kwa alama namba 36M 0629945 UTM 977087. Wanadai alikamatwa katika Pori la Akiba la Ikorongo.

Ni katika njiapanda hii ambapo Jaji kafanabo anafanya maamuzi, huku kukiwa na mashahidi watano walioitwa na upande wa mashtaka, wakiwemo askari wa uhifadhi wawili, mtathmini wa nyara za Serikali, mpelelezi wa polisi na mchora ramani.

Ushahidi wa uongo

Mahakama Kuu inaingia kazini kupitia kila kielelezo na kila ushahidi ili kuamua hatma ya maisha ya ndugu Richard Ng’ombe. Moja ya vielelezo vya ushahidi vilivyoonekana kuwa ni vya mashaka ni ramani iliyotumiwa kuonesha mtuhumiwa alikutwa hifadhini, jambo ambalo mtuhumiwa alilikataa. 

Mtuhumiwa alieleza kuwa yeye alikuwa akitembea njiani kuelekea nyumbani kwake na hakuwa katika eneo la hifadhi.

Je, Ng’ombe alikutwa hifadhini au la? Ili kujibu swali hili, Mahakama inapitia ushahidi wa ‘GPS Coordinate’ na ramani iliyochorwa kuonesha kuwa mtuhumiwa alikamatwa ndani ya hifadhi.

Mahakama inauliza maswali ni nani aliyechukua alama za GPS na ni kifaa kipi kilitumika kuchukua alama hizi. Kwenye kundi la maafisa hifadhi watano waliomkamata Richard, hakuna yeyote aliyetaja kwamba alirekodi GPS na wala kifaa kilichotumika hakikuelezewa.

SOMA ZAIDI: Mahakama Imdhibiti DPP Kuondokana na Kero ya Futa Kesi, Kamata, Shitaki Upya

Kwa kesi zinazohusisha kuingia hifadhini kinyume na sheria, alama za mtu alipokutwa ni moja ya msingi mkuu wa kesi. 

Mahakama pia inaenda hatua ya mbele na kuonesha mkanganyiko juu ya alama hizo, ambapo shahidi wa kwanza anataja alama za GPS alipokamatiwa Richard ni 36M 0629945 UTM 9770872 na shahidi wa tatu anataja alama za GPS 36M 0229045 UTM 9770872. Alama hizi ni tofauti, ingawa wawili hawa walikua pamoja siku wanamkamata mtuhumiwa. Jambo hili linawasha taa nyekundu juu ya kesi hii.

Mahakama ikaenda mbali kuangalia mchoro wa ramani uliotengenezwa kwa kutumia alama za coordinate zilizotolewa na askari wa uhifadhi. Hata hivyo, Mahakama haikuridhishwa na kielelezo cha ramani hiyo kwani kilionekana kutumia alama, au coordinate, tofauti kabisa na zilizotajwa na askari wa hifadhi. 

Hii inafanya kuwa ramani iliyotumika kama ushahidi kuonesha mtuhumiwa alikuwa na hatia ya kuingia hifadhi kuwa haina mantiki, kwani ni ramani ya kutunga isiyokuwa na uhusiano na vielelezo vya alama zilizotolewa na waliomkamata Richard.  

Mahakama inapigilia msumari kwa kusema kielelezo hicho ni cha uongo.

“Makosa yaliyoonekana katika uandaaji wa ramani hayahitaji mtaalamu kuonesha kuwa eneo linalosemekana mtuhumiwa alikamatwa halina uhusiano wowote na sehemu anayodaiwa kukamatiwa,” Mahakama ilisema. “Ramani sahihi ingetumia alama zilezile zinazodaiwa kuwa ni sehemu mtuhumiwa alipokamatiwa. Kwa ufupi, ramani iliyoletwa Mahakamani kama kielelezo P5 ni ya uongo.”

Kuachiliwa huru

Mahakama ikaendelea kupitia kosa lingine lilomkabili Richard Ng’ombe ambalo ni kukutwa na nyara za Serikali. 

Moja ya mambo yaliyoibua maswali ni maafisa hifadhi wawili waliosimama kama shahidi wa kwanza na wa tatu kutofautiana kuhusu nyara iliyokamatwa. Shahidi wa kwanza alisema ni pundamilia, huku shahidi wa tatu akisema ilikuwa ni nyumbu, wanyama wasiofanana hata kidogo. Muhimu zaidi ni kuwa  wawili hawa walikua pamoja wakati wa kumkamata mtuhumiwa.

SOMA ZAIDI: Maamuzi ya Kumnyima Mtuhumiwa Dhamana Yatolewe na Mahakama, Tume Yashauri

Shahidi mwingine ambaye ni mtathmini wa nyara za Serikali katika ripoti yake aliwasilisha kuwa mtuhumiwa alikamatwa na miguu miwili ya nyumbu, mbavu na kichwa chake vilivyoungana pamoja. Mtathmini huyo alisema thamani ya nyara hizo ilikuwa ni Shilingi 2,779,200.

Kutofautiana huku kwa nyara hiyo iliifanya Mahakama iulize mtuhumiwa alikamatwa na pundamilia au nyumbu? Katika utetezi, wakili wa Serikali aliomba Mahakama ifuate maelezo ya mtathmini wa Serikali kwa kuwa ndiye mtaalamu.

Mahakama ikaendelea kuonyesha vielelezo mbalimbali vinavyoonesha hata mtuhumiwa alivyopelekwa mbele ya hakimu hakuna uthibitisho kuwa hakimu aliweza kuona nyara husika.

Namna ambavyo maafisa hao wanadai kuwa walikabidhiana nyara hiyo ni jambo ambalo linaishangaza Mahakama, ambapo maafisa hifadhi hao wanadai walimkabidhi nyara hizo askari kwenye kituo cha Mugumu kwa jina la Said, ambapo Said anadai alimuita mtathmini kwa ajili ya kufanya tathmini. 

Pia, hakukua na vielelezo vyovyote vya kimaandishi vinavyoonesha silaha alizodaiwa kukutwa nazo namna zilivyoweza kuhifadhiwa mpaka kufikishwa Mahakamani.

Mahakama inashangazwa na namna kanuni za kufuata mnyororo wa kielelezo cha ushahidi zilivyonajisiwa: “Ni kama walikuwa wakipeana vitu vya utani na siyo kielelezo kinachoweza mfunga mtu maiaka 20.”

SOMA ZAIDI: Safari Yangu ya Gerezani Bila Kupitia Polisi Wala Mahakamani

Kufuatia matundu hayo yaliyoonekana kila kona kwenye ushahidi, Mahakama iliamua kumuachia huru Richard  Ng’ombe.

Mahakama yatoa onyo

Hata hivyo, Mahakama haikuridhishwa na mwenendo mzima wa shauri lililofanya Ng’ombe kufungwa miaka 20, na hivyo kutoa onyo kwa maafisa wa hifadhi na wengineo katika mfumo wa haki jinai.

“Mahakama haiwezi kufumbia macho jambo hili linaloonekana kuzoeleka na linalojirudia la kutofuata maadili ya kazi kunakofanywa na maofisa wengi wa uhifadhi na wengineo katika haki jinai, hasa katika ukamataji watuhumiwa na uchukuaji wa vielelezo,” ilieleza Mahakama chini ya Jaji kafanabo. 

“Ni jambo linaloonekana la kuzoeleka na kujirudia katika kutofuata maadili ya kazi kwa sababu maofisa wanaosimamia sheria wanaonekana hawajali kwamba hawafanyi inavyotakiwa, au hawaelewi wanachotakiwa kufanya, huku wakipoteza fedha za umma.

“Tabia hii ya kutofuata maadili ya kazi ni matumizi mabaya ya madaraka, na  inaminya uhuru wa watuhumiwa ambao hawajathibitika kuwa na hatia, huu ni uvunjaji wa haki.

“Ni wakati sasa vyombo vya usimamizi wa sheria kuboresha namna wanavyofanya ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa kesi zinazohusu wanayamapori na haki jinai kwa ujumla,” Mahakama ilihitimisha hukumu yake.

Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Sheria ingetakiwa itoe adhabu au mamlaka husika iwawajibishe waliohusika katika kufanya kitendo hiki cha uongo na kubambikia kesi Richard ili iwe fundisho kwa wengine

  2. Unapata uhuru wa aina gani unampa mtu kesi na vielelezo vya uongo ili afungwe …je! Unaijua kesho ikoje ___naamini malipo hapahapa

  3. Katika kufungua mashauri uwekwe utaratibu ikithibitika kuwa kesi ni malicious basi wahusika wallwajibike ata kulipa fidia automatic bila mchakato wowote mgumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *