The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mfumo wa Utoaji Haki Tanzania Hauwasaidii Masikini. Serikali Ianzishe Ofisi ya Uwakili Raia

Mchakato wa kudai na kupambania haki unauhitaji wa fedha katika viwango na hatua mbalimbali ambazo wananchi wengi wa kawaida hawamudu.

subscribe to our newsletter!

Ama kweli, vya kale ni dhahabu. Ilikuwepo kale iliyokuwa ya heri na njema, tena wala si kale sana ya kuitafuta kwa manati, la hasha! Ni kale ya jana kama si juzi. Kale hiyo ilikuwa kale kuu, yaani kale iliyobora, kwani ilikuwa ni kale tuliyozungumza na kuuthamini utu.

Suala la utu lilikuwa ni suala la kitaifa, na hata kiulimwengu. Tulizingatia na kuhamasisha utu kwa kusisitiza misingi ya usawa na kuheshimiana. Nayo misingi hiyo miwili ilitamkwa na kutiliwa mkazo awali kabisa katika kale ya Azimio la Arusha.

Sehemu ya kwanza ya Azimio ilitamka na kueleza imani ya TANU, kilichokuwa chama tawala kabla ya kuundwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM): “Kwa kuwa TANU inaamini: (a) Kwamba binadamu wote ni sawa; (b) Kwamba kila mtu anastahili heshima…”

Kutokana na kuthamini dhana ya utu, kuamini katika usawa na kushadadia heshima kwa watu wote, Azimio likaenda mbali zaidi na kutamka, kwa msisitizo, kuwa, pamoja na mambo mengine, makusudi na madhumuni ya TANU yatakuwa ni, “Kuona kwamba Serikali inatumia mali yote ya nchi yetu kwa kuondoshea umaskini, ujinga, na maradhi.”

Adui umaskini

Haihitaji mtu kulijua Azimio la Arusha au au Katiba au awe Mjamaa, Mmaksi, Mlenin; na haihitaji mtu kumsoma Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Angela Davis au Frantz Fanon ili kutambua kuwa umasikini ni mbaya.

Haikuwa kwa bahati mbaya wazee wetu kutangaza vita dhidi ya umasikini. Inahitaji utashi na maarifa ya kawaida tu kubaini kuwa umasikini ni kikwazo kikubwa cha maisha ya binadamu.

Jamii yoyote inayohimiza usawa, heshima na utu, haina budi kupambana na umasikini kwani hamna heshima kwenye umasikini, hakuna utu katika umasikini, na haupo usawa palipo na umasikini. Kimsingi, haiwezekani, na haipaswi kuwepo, hali ya jamii nzima kuwa masikini.

SOMA ZAIDI: Askari wa Uhifadhi Kilwa Wadaiwa Kukiuka Haki za Binadamu Wakihamisha Wananchi Kwenye Ardhi Yenye Mgogoro

Hivyo basi, ni sahihi kabisa kusema ya kwamba, umasikini ni adui wa maendeleo, ustawi, utu, usawa, heshima na vinginevyo. Umasikini ni adui kwa walimwengu na ulimwengu!

Miaka 56 iliyopita, Azimio la Arusha lilitamka kuwa linataka “Kuona kwamba Serikali inaondoa kila namna ya dhulma, vitisho, ubaguzi, rushwa na upotofu.” Wananchi nao, pamoja na mambo mengine, wakasisitiza, na kukiri, kuwa, rushwa ni adui wa haki!

Licha ya kwamba kuta za Mahakama zimepambwa na nakshi na vibao vya kusisitiza watu kutotoa rushwa, rushwa imesalia kuwa ni adui wa haki, na ni dhahiri kuwa hata hivyo, hivi sasa adui mkuu wa haki ni umasikini.

Isivyo bahati, kama jamii, ama kwa kujua au kutokujua, hatujaweza kuliwekea msisitizo jambo hili. Si Mahakama, Bunge wala Serikali, wala si hata Ripoti ya Tume ya Haki Jinai, iliyoweza kuonesha kuwa adui mkuu wa haki ni umasikini.

Aghalabu, tunapozungumzia umasikini huwa tuna uhusianisha na umasikini katika mali. Licha ya kwamba umasikini wa mali ni mkubwa, binafsi ninaamini changamoto kubwa katika haki ni umasikini katika hali.

SOMA ZAIDI: Takribani Mwaka Tangu Wapendwa Wao Wauwawe Kikatili, Familia Hizi Zataka Haki Kutendeka

Uzoefu wangu katika viunga vya Mahakama na vyombo vya kisheria, idadi kubwa ya watu niliokutana nao wakiwa na maswahibu yao humo wamekuwa ni watu wa hali ya chini zaidi, yani walalahoi, kuliko idadi ya walalahai na walalakheri.

Pamoja na kwamba yapo mashauri kati ya walalahoi, wao kwa wao, lakini mengi ni kati ya walalahai dhidi ya walalahoi na walalakheri dhidi ya walalahoi. Kimsingi, hata hivyo, nitaangazia na kuweka msisitizo kuhusiana na mahusiano ya haki na walalahoi.

Ni jambo lisilopingika kwamba jamii ya walalahoi ni jamii yenye maendeleo duni. Tabaka hili huhusisha ama watu ambao hawajapata kabisa elimu, au waliopata elimu isiyokidhi viwango, yaani duni au mbovu. Hivyo basi, kundi hili huhusisha na kujumuisha watu wasiokuwa na uelewa madhubuti wa mambo.

Ukosefu wa uelewa hulifanya kundi hili kuukosa ujasiri wa kujisimamia na kujipambania kwenye masuala ya kisheria na katika kutetea haki zao, hali inayolifanya kundi hili kujiona kuwa duni na hivyo kushindwa kusema na kushughulika na masuala ambayo pengine yanahitaji utashi wa kawaida kabisa kuyashughulikia.

Hali hii huliweka tabaka hili kwenye hatari ya kurubuniwa na walalahai na walalakheri, wakisukumwa, kuyumbishwa na kushurutishwa na Serikali na viongozi na watumishi wake kwa ujumla, katika kutii na kufanya mambo ambayo hayana tija kwao. 

SOMA ZAIDI: Ucheleweshaji Kesi Mahakamani Unavyokwamisha Upatikanaji wa Haki

Adui mkubwa wa tabaka la walalahoi, kwa hiyo, ni udhaifu na unyonge wao, utokanao na umasikini. Udhaifu na unyonge wao ni adui hatari zaidi kutokana na jamii yetu kuendelea kukumbatia mfumo dhalimu wa ubepari wa kiliberali, ambao unasisitiza na kuamini katika survival of the fittest, au uhimili wa walio madhubuti, au wenye nguvu.

Katika dunia ya leo, dunia iliyoweka rehani na kunadi utu na thamani ya watu, ni namna gani masikini ataweza kuhimili vishindo na misuli ya wenye mtaji? Haiwezekani! 

Kutokana na mfumo huu na kutokana na masikini kukosa nguvu na kutokuwa madhubuti huishia kukandamizwa, kunyonywa, kuteketezwa, kutelekezwa na hata kupoteza haki zao za msingi kabisa.

Umasikini katika mali

Katika miaka yangu kadhaa ya kufanya kazi kama wakili na kujishughulisha na masuala ya kisheria, nikiri na niweke wazi kuwa mapambano na madai ya haki yanauhitaji mkubwa sana wa pesa. Hili si la siri wala la kuficha hata kidogo.

Nazungumzia fedha ile halali na si ya makando – ambayo nayo pia ipo, tena sana. Endapo mtu, au mamlaka, yeyote inataka kulipinga hili, basi watembelee vituo vya haki mbalimbali, wajionee utitiri wa mabango ya kupinga rushwa. Kwa nini mabango mengi hivyo kama hilo jambo halipo?

SOMA ZAIDI: Rasimu ya Warioba Ina Majibu Yote Samia Anayahitaji Kuhusu Mfumo wa Haki Jinai

Mchakato wa kudai na kupambania haki unauhitaji wa fedha katika viwango na hatua mbalimbali. Hatua ya awali kabisa ni katika kusaka ushauri na uelewa wa jambo linalokukabili. Kisha baada ya hapo ni huduma ya kuendea hilo jambo – iwapo ni kufungua au kujibu shauri.

Wakati sehemu ya kwanza mtu hushughulika na gharama za mwanasheria, sehemu ya pili mtu atapambana na gharama za wanasheria na gharama za Mahakama – kwani mashauri hufunguliwa na hujibiwa kwa pesa. Mahakama zinapaswa kujiendesha, si ndiyo?

Baada ya hapo kuna hatua ya ufuatiliaji na usikilizaji wa shauri. Humu ndiyo kuna utitiri wa gharama. Zipo gharama za uwakili wa jumla, gharama za ufuatiliaji wa shauri, gharama za usafiri na uwakilishi siku ya shauri, gharama za mashahidi – la sivyo utapambana na hali yako–, gharama binafsi, gharama za muda, nakadhalika.

Ni vipi hapa masikini atatoboa na hizi gharama? Si ajabu hata kidogo masikini kuiachia kudra, si kupenda kwao, ni dhiki!

Umasikini katika jinai

Walau kidogo kuna unafuu katika mashauri ya madai, japo kidogo, katika jinai hali ndiyo tete haswa na ndiyo sababu hii nimestaajabu kuona Ripoti ya Tume ya Haki Jinai haijazungumza na kuainisha tatizo la umasikini kama tatizo sugu.

SOMA ZAIDI: Apigania Haki Yake ya Ardhi Kwa Miaka 36 Bila Mafanikio

Huko gharama ni lukuki, gharama za kulishwa na kuwa tegemezi angali mtu yuko rumande na mahabusu, bado kuna gharama za masuala ya dhamana na kubwa kuliko ni ufuatiliaji na uendeshaji wa kesi.

Tukiachana na kesi kuhairishwa hairishwa kutokana na sababu mbalimbali za Jamhuri, bado kuna gharama za uendeshaji wa kesi. Tofauti na mashauri ya kesi za madai ambazo huweza kuhairishwa na muda mrefu, kesi za jinai hupangiwa tarehe za karibu zaidi.

Maana yake ni nini hili kifedha? Maana yake ni kwamba utapaswa ndani ya wiki mbili au pungufu, au zikizidi pengine wiki tatu, mshtakiwa atahitaji kuwa na fedha ya uwezeshaji wa wakili kufika na kumtetea mahakamani.

Huyu masikini ataitafuta saa ngapi hiyo pesa? Ataitafutia wapi? Huu nao ni mtihani. Kutokana na hali hiyo, zipo nyakati mawakili huishia njiani na nyakati nyingi tu, wale wasiojiweza kiuchumi huishia kukomaa, au kupambana, wenyewe mahakamani.

Janga la hatia

Kutokana na uzoefu wangu kwenye hii tasnia ya sheria, akheri kidogo ukose uwakilishi kwenye mashauri ya madai na si ya jinai. Wakati madai yanaweza kupelekea kupoteza mali yako mara nyingi, jinai inaweza kukupeleka jela na kupoteza sehemu kubwa ya maisha yako kama si kuyaharibu kabisa.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?

Isitoshe, kwenye madai mnaweza kuishia kupambana raia kwa raia, yaani pande zote mbili panaweza pasiwe na mawakili. Lakini kwenye jinai, masikini huyu, kwa mara zote, atakuwa akipambana na Jamhuri, ambapo lazima patakuwepo na wakili, kama si mawakili, wa Serikali.

Hali hii inamuweka zaidi mshtakiwa kwenye hati hati ya kuikosa haki yake, kwani, pamoja na mambo mengine, kuna utaratibu na utaalamu fulani katika uendeshaji wa kesi; utaalamu ambao upande mmoja –Jamhuri– utakuwa na uelewa nao na upande wa pili – raia wa kawaida, au masikini – hana ujuzi nao. 

Je, ni nini cha kutegemea katika mtanange kama huu? Je, si kwamba hapa hatia iko nje nje?

Msanii nguli, hayati Joni Woka, aliwahi kuimba na kuhoji, “Umasikini huu, umasikini huu, umasikini huu, utaisha lini?” Zaidi ya miaka kumi baadaye na mimi bado ninajiuliza swali hilohilo.

SOMA ZAIDI: Hivi Ndivyo Serikali Inavyoweza Kuuboresha Mfumo wa Haki Jinai Tanzania

Ni kweli jitihada za kutoa msaada wa kisheria zinasaidia kupunguza makali, lakini je, ni kwa kiwango gani? Msaada huu ni finyu mno na unazo changamoto zake lukuki, ambazo ninafahamu zinaendelea kushughulikiwa. 

Hata hivyo, wakati yote haya yakiendelea, nao watu wengi tu wanaendelea kuishi katika hatari ya kupoteza haki zao, kutokana na umasikini wao.

Ni wakati sasa kwa Serikali, yenye kujali utu na kuthamini maisha, ustawi na maendeleo ya watu wake, kufikiria na kuanza mchakato wa kuanzisha Ofisi ya Uwakili Raia katika kila wilaya kusaidia wananchi wote wanaoshindwa kupata huduma za mawakili binafsi, ili kuweza kuwasimamia kila nyakati, walau kwenye mashauri ya jinai.

Pia, kama jamii, tunapaswa kupambana kuutokomeza umasikini, iwapo kama kweli tutanataka kuwa na jamii inayosimamia na kufurahia misingi ya haki. 

Tunapaswa kupambana kuondokana na mifumo yote inayowezesha kuneemeka au kutajirika kwa watu wachache, huku wengi wetu tukibaki kuwa masikini na mafukara wa kutupwa.

Tuukatae umasikini! Tuukatae mfumo dhalimu wa sasa unaopalilia umasikini! Tuhimizane na tukumbuke kuwa, umasikini ni adui wa haki!

Jasper “Kido” Sabuni ni mchambuzi wa masuala ya kijamii. Anuwani yake ya barua pepe ni kidojasper@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *