The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wananchi Waibane Serikali Kukithiri Matukio ya Utekaji Tanzania

Matukio yote ya utekaji yatendewe kama dharura, hatua madhubuti zichukuliwe kubaini ukweli na kuwawajibisha wote waliohusika.

subscribe to our newsletter!

Kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia msuguano kati ya Jeshi la Polisi na raia kufuatia taarifa za matukio ya utekaji. Polisi wamejihami kwa kuwakamata na kuwashitaki Mstahiki Meya (Mstaafu) wa Ubungo na Kinondoni, Boniface Jacob, na mwanaharakati Godlisten Malisa. Suala hili limenitazamisha upya kuhusu matukio ya utekaji na wajibu wa Serikali.

Utekaji katika muktadha huu ni matumizi ya nguvu ya dola kumnyakua raia bila idhini yake, ama pasi na kufuata utaratibu, kwa nia ovu. Shabaha inaweza kuwa ni kuogofya, kudhuru, kupoteza, kutesa na pengine kuuwa. Utekaji mwingine unafanywa kwa nia ya kupora mali na kufilisi, hususani kwa wafanyabiashara.

Ukiachana na utekaji ambao kimsingi lengo lake ni kuteka na kupoteza, kutofuatwa taratibu za ukamataji kunaweza hesabika kuwa utekaji. Polisi wanafanya utekaji mara kwa mara kwa kutokufuata taratibu za ukamataji. Na ikitokea utekaji ukafanikiwa, uwezekano wao wa kukwepa wajibu ni mkubwa.

Kuna visa chungu nzima vya watu waliotekwa na kupotezwa. Wenye bahati walirejea uraiani wakiwa sivyo walivyokuwa awali. Mwanaharakati maarufu nchini, Mdude Nyagali, ni muathirika maarufu wa utekaji. Ametekwa na kuteswa zaidi ya mara mbili. Wamo pia msanii Roma Mkatoliki, tajiri Mohammed ‘MO’ Dewji, Raphael Ongangi, na wengine wengi.

Kuna waliotekwa wakapotezwa na hawajapatikana hadi leo. Mfano, Ben Rabiu Saanane, Azory Gwanda, Simon Kanguye, kijana wa Mzee William Sije, na wengine. Mwaka 2023 ulianza kwa taarifa ya kutekwa kwa vijana watano waliokuwa wakiishi Dar es Salaam. Kumekuwa na mwendelezo wa matukio mengi ya utekaji.

Wajibu wa Serikali

Hivi karibuni, Boniface Jacob amekuwa akichapisha katika ukurasa wake wa X, zamani Twitter, matukio ya watu kupotea ama kutekwa. Taarifa za Jacob zimefuatiwa na tafiti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inayoonesha hali ya Haki za Binadamu Tanzania kwa mwaka 2023, ilionesha ongezeko la matuko ya utekaji.

SOMA ZAIDI: Teuzi za Watu Wasio Waadilifu Zinawapa Motisha Viongozi Kutumia Vibaya Ofisi za Umma

Pamoja na mambo mengine, tafiti ya LHRC imeonesha ongezeko la matukio ya utekaji kwa asilimia 30 kwa mwaka 2023, ukilinganisha na mwaka 2022. Matukio 200 yaliripotiwa katika tafiti hiyo.

Hata hivyo, ni vema kufahamu kwamba matukio yaliyoripotiwa katika tafiti ya LHRC ni yale yanayokusanywa kupitia nyenzo zao. Upo uwezekano kwamba kuna matukio mengi zaidi ya yaliyokusanywa. Ongezeko la matukio ya utekaji linaogofya. Utekaji unahatarisha haki ya kuishi na usalama wa raia.

Tuangalie matukio 200 kwa taswira ya watu. Kwamba, watu 200 waliripotiwa kutekwa. Namba za matukio ya utekaji zinaogofya kwa kuwa hatufahamu atakayefuatia kutekwa; na vilevile, hatufahamu watu wakitekwa, wasiporudi, wanakuwa wapi, na wanafanyiwa nini!

Vilevile, fikiria utekaji kwa muktadha kwamba waliotekwa waliamini wako salama katika nchi yao. Hawakuwahi kufikiria kama siku moja watatekwa, kuteswa na kupotezwa. Sasa ziangalie familia zao. Zina majonzi kiasi gani? Wanaionaje Serikali? Na wanaitafakarije? Ni zipi athari za utekaji katika saikolojia za watu na uhusiano wao na Serikali?

Kati ya visa 200 vilivyoripotiwa katika tafiti ya LHRC, asilimia 60 vilihusisha utekaji nyara wa watu wa kawaida, wakiwemo wafanyabiashara, wanaharakati wa haki za binadamu, na raia wa kawaida. 

Mchanganuo huo unaonesha kuwa mradi wa utekaji hauwaathiri wakosoaji wa Serikali tu bali pia watu binafsi vilevile. Kwa hiyo, ni sahihi kusema kwamba udhalimu utamkuta kila mtu kwa wakati wake. Ni motisha kwetu sote kuamka na kutafakari usalama wetu.

SOMA ZAIDI: Mahakama Tanzania Isikwepe Wajibu Wake wa Kusimamia Utoaji Haki

Mwaka 2020 nilitembelewa gerezani na mdogo wake Ben Saanane. Alipoondoka, kiubinadamu, niliwaza: “Pengine anatamani angekuwa anakuja kumuona kaka yake gerezani.” 

Kwamba, ni nafuu zaidi kufahamu ndugu yuko kizuizini kuliko kutofahamu uanzie wapi kumtafuta. Haya yote hayapaswi kutokea na dhana yangu inaweza isiwe kweli. Lakini fikra za watu wanaowatafuta ndugu zao zinachakata nini? Ninadhani, wanateseka sana!

Serikali haitaki kuhusishwa na matukio ya utekaji. Lakini katika baadhi ya matukio, taarifa zinadai ni polisi, au watu wenye nguvu sawa na polisi, waliomchukua huyu ama yule. Dhana ni kwamba wanapelekwa vituo vya polisi. Kumbe haikuwa hivyo!

Hata hivyo, kimsingi, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha usalama wa kila raia kwa mujibu wa Katiba. Serikali inapaswa kuhakikisha haki ya kuishi, hifadhi katika jamii, na usalama wa kila raia.

Serikali inatakiwa kufuatilia na kukomesha uhalifu, ikiwemo utekaji. Itafanya hivyo kwa kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wanaohusika. Na labda hapa nitapoteza uhalisia kidogo. lakini namaanisha Serikali zote za watu zinawajibika kwa watu – ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama wao na mali zao.

Je, tuna Serikali ya watu? Huu ni mwiba. Kwa kuwa Serikali yetu haijali hata kidogo kuhusu uwajibikaji, na kwa kuwa kumekuwa na ongezeko la visa vya utekaji bila uwajibikaji, basi Serikali yetu inapoteza sifa za kuwa Serikali ya watu.

SOMA ZAIDI: Mahakama Imdhibiti DPP Kuondokana na Kero ya Futa Kesi, Kamata, Shitaki Upya

Serikali ya watu haiwezi kuwatumia askari kinyume cha wito na maadili wao. Maana utekaji siyo moja kati ya kazi za dola la watu. Ni katika dola za kidikteta na kimabavu pekee utasikia utekaji umehalalishwa ama kukubaliwa.

Wananchi wako wapi?

Nataka nitembee na nadharia kwamba hatuna Serikali ya watu. Kwa hiyo, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya wananchi na Serikali. Matokeo yake hakuna ufuatiliaji na uwajibikaji.

Lakini Serikali ilipaswa kuhusiana na wananchi kupitia Bunge na Baraza, au Mahakama, au vikao vya Serikali za mitaa. Ombwe lililopo katika mfumo wa uendeshaji wa, na matumizi ya mamlaka ya, nchi yetu limewaweka wananchi shimoni na viongozi kileleni, jambo ambalo limetengeza uhusiano wa bwana na mtumwa.

Takwimu za LHRC zinaonesha watu 200 wametekwa. Wananchi wastaarabu wangejadili suala hili usiku na mchana, kwa kujihadhari na kujitazamisha kama wako salama pia. Lakini mijadala ya namna hii si ya kitaifa. Haipo bungeni. Na wala hakuna kesi mahakamani kujaribu kujihami au kuiwajibisha Serikali.

Ninaamini Serikali inafurahi ukimya wananchi – kwa kuwa haina mpango wa kujirejesha kuwa Serikali ya watu. Ndiyo maana wanaotoa taarifa wanashambuliwa na kupewa kesi, kwamba wamezua taharuki. Na hiyo taharuki wameipata polisi – maana hakuna malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba taarifa hizo ni uzushi na zimewapa tahatuki.

Wananchi tumejisalimisha kwa Serikali na kuiacha ijiendeshe bila udhibiti. Ndiyo maana matukio ya utekaji yanajirudia, na yanaongezeka. Ninafamu, ipo miito ya kuitaka Serikali, kama sehemu ya wajibu wake, iwarejeshe watu waliotekwa. 

SOMA ZAIDI: Je, Ni Haki kwa Serikali Kuwaweka Rumande Washtakiwa Halafu Kufuta Kesi Bila Kuwalipa Fidia?

Pia, miito ya kuchukua hatua kuhakikisha watekaji wanafahamika na kuwajibishwa. Hata hivyo, jitihada hizo hazijafua dafu.

Kupata haki

Tafiti ya LHRC inadai asilimia 70 ya familia za waathirika zililalamikia ugumu kupita kiasi wa kupata haki na ukweli kuhusu ndugu zao waliotekwa. Hakuna uwazi, ama utaratibu maalum, wa kuwasilisha malalamiko, kusikilizwa na kupewa taarifa. 

Suala hili limepelekea baadhi ya wadau kuomba kuundwa kwa mamlaka huru ya kusimamia utendaji wa polisi. Ninarudia tena mwito huu kwa kuwa utasaidia kutatua migogoro ambayo polisi wanahusishwa.

Serikali isitishe mara moja usumbufu kwa watu wanaotoa taarifa za matukio ya utekaji. Badala yake, Serikali ijihimu kurejesha imani yake kwa wananchi. Matukio yote ya utekaji yatendewe kama dharura, hatua madhubuti zichukuliwe kubaini ukweli na kuwawajibisha wote waliohusika.

Ni muhimu kwa wananchi kufahamu kwamba hakuna anayepeleka wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama ama makundi ya watekaji ili atekwe. Ni kwamba, kama nilivyosema awali, udhalimu una mzungumko. 

Siku ukifikiwa utatamani isiwe kweli. Kwa hiyo sote tushiriki, na tushirikiane, kutokomeza utekaji.

Tito Magoti ni wakili na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia titomagoti@gmail.com au X kama @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Wakili Magoti hii Makala ni very sensitive, Kwa logic rahisi tu kuhusishwa Jeshi la Polisi katika kuteka, kutesa, kujeruhi, kkutia ulemavu wa Kudumu na hata Kuua ni matokeo ya udhalimu walionao viongozi wetu.

    Sidhani kama polisi wanaojiamulia tu kuwa leo tumteke nani au tumpore nani au tumuue nani isipokuwa walio juu Yao ndiyo watoaji wa maagizo.

    Kinachoumiza na kusikitisha siyo wabunge wala mawaziri wala Rais anayekemea au kuwahi kutoa tamko dhidi ya uonevu na uvunjwaji haki zetu kwa sababu ya kutofautiana kimtazamo.

    Na Kwa kuwa Wabunge, machawa wa Rais, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na mawaziri kama Mwigulu, Ummy, Tulia, Makonda, Katambi, Hapi, Sabaya, Dr Tulia na wengine kibao wanahusika basi tunazo sababu kuamini kuwa matukio haya ya kidhalimu, kikatili, kionevi na kivunjaji haki za binadamu yapo nyuma ya uratibu wao.
    Sababu kuu ni kutofautiana Mitazamo na misimamo yetu kisiasa. Wajue tu kwamba TUMECHOKA,TUNATAKA KUIKOMBOA TANZANIA.
    TUMEJUFUNZA KWA KENYA, haiwezekani kuendelea na unyonge Kwa kuchagua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts