The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tathmini Inahitajika Kuondoa Mazoea Kwenye Soka la Tanzania

Tathmini ni kitu muhimu sana kwa kila kitu kwa kuwa huonyesha mambo yalivyoendeshwa, udhaifu uko wapi, changamoto ni zipi na kwa nini kulikuwa na mafanikio eneo fulani.

subscribe to our newsletter!

Kwa karibu michezo yote, msimu ndiyo unaelekea mwishoni kwa mabingwa kutangazwa, timu zinazoshuka daraja kujulikana na zile zinazopanda baadhi zimeshajulikana na nyingine zinasubiri mechi za mtoano.

Ni kipindi ambacho wale wachezaji waliojituma, kufuata maelekezo na kuunganisha wenzao ndani na nje ya uwanja hutambuliwa kwa kupewa tuzo, sambamba na walimu na wahusika wengine kwenye michezo.

Kwa wenzetu hiki ndicho kipindi ambacho wahusika wa maeneo mbalimbali huanza kutathmini jinsi msimu ulivyokwenda, matatizo, changamoto na mafanikio na kutafuta suluhisho au kuboresha pale walipofanya vizuri.

Ni kipindi ambacho makocha hukutanishwa na kujadili hali ilivyokwenda na kutoa maoni ya kuboresha uendeshaji ligi katika maeneo kama ya ukaribu wa mechi moja hadi nyingine, muda wa kutosha wa kupumzika baada ya timu kucheza ugenini mbali na kituo chake, mfano Tanzania Prisons anapotoka kucheza mechi mkoani Kagera, na mengine mengi.

Ni wakati pia wa viongozi wa klabu kukutanishwa na Bodi ya Ligi kwa ajili ya kujadili jinsi msimu ulivyokwenda, kanuni, matukio makubwa yaliyojitokeza, udhamini, haki za matangazo na uwezekano wa kufanyia marekebisho maeneo fulani kwa lengo la kuboresha uendeshaji ligi na kuipandisha viwango.

Ratiba

Tumekuwa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi kila mwanzoni mwa mwaka, lakini ni kama vile hayajawekwa kwenye ratiba ya shughuli za Shirikisho la Soka (TFF) wala Bodi ya Ligi. Matokeo yake imekuwa ni kutangaza kuahirisha mechi kana kwamba mashindano hayo yameshuka kama mvua.

SOMA ZAIDI: CAF Ilitafutie Suluhu ya Kudumu Suala la Morocco

Timu ya taifa hujulikana mechi zake kwa kuwa hilo limo kwenye kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA). Hata kama nchi haijajua itacheza na timu gani mechi za kirafiki, kalenda ya FIFA imeweka muda wa mechi hizo, huku kanuni zake za kuruhusu wachezaji wa kimataifa zikieleza bayana muda ambao wachezaji hutakiwa kuruhusiwa.

Mwaka huu timu yetu ilienda kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) zilizofanyika Ivory Coast. Ni fainali ambazo muda wake ulijulikana tangu mwaka juzi wakati Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lilipouamua kuzihamishia Januari kutokana na hali mbaya ya hewa inavyokuwa nchini Ivory Coast katikati yam waka.

Lakini huku ikawa ndio sababu ya kupangua ratiba ambayo ingeshapangwa vizuri kuruhusu ushiriki kikamilifu wa timu yetu bila kuvuruga ratiba.

Ratiba za michuano ya klabu ya Afrika hujulikana mapema; kwa hiyo, hata timu zinapofuzu kutoka hatua moja kwenda nyingine, mechi za hatua inayofuata hujulikana zitachezwa kipindi gani, lakini huku ilikuwa kama kusthukizwa wakati Simba na Yanga zilipokuwa zinafuzu kutoka hatua moja kwenda nyingine. 

Hata pale tarehe za mechi zilipojulikana, katikati ya hatua ya makundi, bado ratiba ilipanguliwa kutoa muda zaidi kwa wawakilishi wetu kujiandaa.

Vurugu

Hii ni sababu ambayo imekuwa ikitumika kuvuruga ligi kwa kile kinachoitwa uzalendo. Uzalendo si kuvuruga utaratibu wako bali kupanga utaratibu bora utakaoruhusu timu kupata muda wa kutosha wa maandalizi badala ya kuvuruga ratiba iliyopangwa tangu mwanzoni mwa msimu.

SOMA ZAIDI: Tutapataje Mabondia Bora Bila Ngumi za Ridhaa?

Hata pale ilipovurugika, bado makossa hayakusahihishwa kwa wakati. Leo hii, Yanga ambayo ilikuwa ya mwisho kutolewa Ligi ya Mabingwa, ndiyo imecheza mechi zake zote kulingana na timu nyingine ambazo hazikushiriki.

Labda tutazungumzia kisingizio cha michuano iliyoshuka kama mvua ya Kombe la Muungano. Lakini pia utaona, Azam FC iliyofungwa na Simba katika fainali, imeshacheza mechi zote kulinganisha na vigogo hao wa Mtaa wa Msimbazi. Ukiuliza kwa nini bado Simba ina viporo, hakuna sababu ya maana. 

Huku ni kutojipanga na kutopata muda wa kutathmini kwa kina matukio yaliyotokea msimu uliopita na kuyatafutia suluhisho.

Tulipoanzisha Bodi ya Ligi tulijua kuwa kwa klabu kuendesha zenyewe mashindano yao, haitakuwa rahisi kwa kiongozi wa TFF kuvuruga mashindano yao kirahisi kwa kuwa kila klabu itakuwa makini kuangalia mwingine anafanyaje, na kama kuna dalili za upendeleo hatua zichukuliwe mara moja kwa kuwa wenye ligi ndio wanaoiendesha. Hali haionekani kulingana na malengo. Ni kama hakuna Bodi ya Ligi, zaidi ya idara mojawapo za TFF.

Ni muhimu sana kwa mambo haya kujadiliwa kwa kina mwishoni mwa msimu badala ya kuyaona ya kawaida na kwamba tumeyazoea. Wengine wanasonga mbele kwa kuwa hawataki matatizo kujirudiarudia kana kwamba hayawezi kuzuilika. Tathmini ya msmu ni muhimu sana.

Tathmini

Leo hii tuna Chama cha Makocha wa Soka (TAFCA). Hiki chama kinaonekana kipo kwa ajili ya kushiriki mkutano mkuu wa TFF na siasa nyingine za uchaguzi wa soka. Ni vigumu kusikia kimeitisha mkutano mwishoni mwa msimu kujadili kiufundi ligi ilivyokwenda au kusomea wanachama wake ripoti ya kiufundi ya msimu mzima na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike.

SOMA ZAIDI: Wimbi la Wachezaji Kuvunja Mikataba Lidhibitiwe

Tungetegemea kusoma kwenye ripoti yao magoli mengi yaliyofungwa msimu huu yalikuwa ama ya kona, au mashambulizi ya kushtukiza, ama mipira ya adhabu, ama mashuti ya mbali, na hivyo kupata picha ya mwelekeo wa ligi yetu au kujua sababu zilizosababisha hayo. Makocha nao huokota kitu kutoka kwenye ripoti kama hizo.

Ungetegemea Bodi ya Ligi iwe na utaratibu wa kuitisha kikao chake mwishoni mwa msimu na kuwasilisha ripoti ya jinsi msimu ulivyokuwa, matatizo na mafanikio pamoja na mipango iliyopo kwa ajili ya msimu unaofuata, kama matumizi zaidi ya teknolojia, udhamini na kukaribisha maoni kuhusu marekebisho ya katiba.

Hili pia linahusu viongozi wa Chama cha Madaktari wa Michezo (TASMA), Chama cha Wanasoka (SPUTANZA) na Chama cha Soka la Wanawake (TWFA).

Tathmini ni kitu muhimu sana kwa kila kitu kwa kuwa huonyesha mambo yalivyoendeshwa, udhaifu uko wapi, changamoto ni zipi na kwa nini kulikuwa na mafanikio eneo fulani. Hapa unapata picha ya huko tunakoelekea kunakuwaje.

Mwishoni mwa yote, ikitoka ripoti moja kubwa inayoeleza kinagaubaga tathmini ya msimu mzima, ni rahisi kwa wadau kufanyia kazi kila eneo linalomgusa na pia kutoa picha wa mwelekeo wa michezo yetu. Huenda tathmini huwa inafanyika, lakini si katika ukubwa huo nilioueleza.

Ni muhimu kwa wahusika kuanza kufikiria nini cha kufanya kuweza kufanya tathmini ya kina kwa michezo yetu ili kuondokana na tabia iliyokomaa ya kuzoea matatizo. Tathmini itatufanbya tuchukie mazoea.


Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts