The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ni Muda Makocha Wazawa Tanzania Waanze Kufanya Kazi Kisasa

Ni muhimu kwa makocha wetu kuanza kufikiria zaidi thamani yao na kuitengenezea njia ya kuonekana katika mazungumzo ya ajira zao.

subscribe to our newsletter!

Kuna kilio kinaendelea cha kutaka kocha wa muda wa Simba, Juma Mgunda, apewe mkataba wa kuifundisha timu hiyo kwa sababu ameonyesha mafanikio tangu alipoichukua timu baada ya Mualgeria, Adel Benchikha, kuachia ngazi mapema mwezi huu.

Wito huo unaongezwa nguvu na uraia wa Mgunda. Kwamba ni kocha Mtanzania na kwamba imefika wakati sasa klabu zetu kuheshimu walimu wazawa na kuwapa ajira rasmi kwa kuingia mikataba ya muda mrefu badala ya hali ilivyo sasa.

Mgunda amekuwa akiifundisha Simba kama kocha wa muda kila wakati klabu hiyo inapotengana na kocha mgeni na kila wakati anapoichukua timu huwa na matokeo mazuri bila ya kujali kiwango cha mashindano au aina ya mpinzani.

Lakini wengi wanaamini kuwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union huwa anaingia makubaliano ya kiungwana na viongozi wa Simba na ndiyo maana huwa hakuna matatizo wanapoamua kumuondoa kwenye timu kuu na kumpeleka timu nyingine kama ya wanawake au vijana.

Hali huonekana hivyohivyo kwa Coastal Union wanapohitaji huduma ya Mgunda. Wanaweza wakampa timu halafu baada ya muda mfupi wakatafuta kocha mgeni na kumuondoa Mgunda.

Makocha wengi

Mgunda ni mmoja tu kati ya makocha wengi ambao wamewahi kutumika kwa njia hii. Yupo Fred Felix Minziro ambaye amewahi kutumika kwa njia hiyo mara kadhaa kwenye klabu ya Yanga.

SOMA ZAIDI: Tathmini Inahitajika Kuondoa Mazoea Kwenye Soka la Tanzania

Alikuwepo pia Badi Salehe na Mansour Magram ambaye alikuwa akitumika Coastal Union na Sigara na Azam walikuwa na Idd Nassor Cheche, ambaye walikuwa wakimpa timu na kumpokonya kila watakapo.

Wanapokuwa Yanga, Simba au Azam ni rahisi kuonekana na kuwa gumzo kwamba wapewe mikataba ya kudumu, walipwe vizuri na mambo mengine, lakini vipi wanapokuwa klabu nyingine kama Kagera Sugar, Mtibwa, KMC, Geita Gold au Dodoma Jiji?

Huko huwa kuna mikataba ya kudumu au mishahara mizuri kama wanayolipwa wageni? Bila shaka hakuna kwa sababu huoni kocha mzawa akidai haki zake anapoondolewa Simba, Yanga, Azam au klabu nyingine. 

Lakini kesi za kudai haki za malipo kwa wageni huwa nyingi na baadhi hufika Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) ambayo mara kadhaa huamuru walipwe na kutishia kuifungia klabu kusajili.

Tatizo ni nini kwa makocha wazawa? Kwamba hawajui haki zao? Kwamba hawajui kuweka thamani yao wakati wa mazungumzo ya kuajiriwa? Kwamba hawaoni sababu ya kuwa na mikataba? Au makubaliano ya kiungwana kwao yanatosha na hawapendi kuwasumbua watu wanaowajua na ambao huwapa ‘upendeleo’ wa kufundisha timu kubwa?

Kujenga thamani

Pengine ni wakati sasa wa makocha wazawa kuanza kujenga thamani yao, au kuanza kufanya kazi kama taasisi. Haiwezekani wakawa kimbilio wakati wa shida na shida ikiisha wanatupwa jalalani kusubiri shida nyingine. Ni lazima waanze kufanya kazi kisasa.

SOMA ZAIDI: CAF Ilitafutie Suluhu ya Kudumu Suala la Morocco

Nyuma ya kocha raia wa Afrika Kusini, Pitso Mosimane, kuna mlolongo wa watu. Mosimane ana matatizo kibao na waajiri wake wa zamani, lakini si yeye anayeshughulika na kesi dhidi ya Mamelodi Sundowns au wengine. Ni wanasheria walio katika timu yake wanaoshughulikia kila kitu.

Si Mosimane anayeshughhulikia mikataba yake ya ajira, bali wanasheria walio kwenye timu yake wanaofanya kazi hizo zote na kumuachia jukumu la kutia saini tu baada ya kila kitu kuhusu ajira, mishahara, posho na bonasi kuangaliwa kwa makini na wataalamu.

Katika uwanja wa mazoezi, Mosimane anashughulika na kuunganisha timu, mbinu na usimamizi wa timu kwa ujumla, lakini chini yake wako makocha wa kila idara wanaomfanyia kazi ili timu iwe bora. 

Mchezaji anayeshuka kiwango anashughulikiwa na mtu tofauti kumrejesha kwenye ubora wake hadi pale inaposhindikana. Washambuliaji wananolewa na mtu tofauti, hali kadhalika viungo, mabeki na makipa.

Mosimane amejinyanyua na kuwa taasisi na si ajabu kwamba kwa sasa Mosimane ni mmoja wa makocha wanaolipwa vizuri si Afrika tu, bali duniani na si rahisi kwa klabu kama Simba, Yanga na Azam kumfuata kwa sababu atakuja na mlolongo wa wasaidizi wake na hivyo thamani yake kuwa kubwa.

SOMA ZAIDI: Tutapataje Mabondia Bora Bila Ngumi za Ridhaa?

Hatutaki makocha wazawa kufikia huko katika muda mfupi, lakini angalau sasa waanze kujenga thamani yao kwa kuunda timu ya kufanya nayo kazi. Isiwe ni rahisi kumuita Mgunda ofisini, kuzungumza naye na kesho yake kumtangaza kuwa anaanza kazi. 

Bali ichukue muda wa kutosha kwa viongozi kutafakari thamani yake na watu ambao atakuwa anaambatana nao. Na hivyo, hata kumpa mkataba wa muda, kutazingatia mambo muhimu kama kocha.

Kuunda timu

Kuunda timu si kwa sababu ya kujijenga kuwa taasisi bila manufaa yoyote. La hasha! Kuunda timu kutasaidia makocha wazawa kuwa bora zaidi. Yaani, kama akishughulika na mambo machache na wasaidizi wake kujazia sehemu nyingine, ataweka akili nyingi zaidi kwenye jambo dogo, huku mengine yakifanywa kwa ubora zaidi na wenzake.

Huenda kocha mzawa anapopewa timu kwenye klabu za Ligi Kuu hukuta makocha wa idara nyingine kama walimu wa washambuliaji, makipa na viungo, lakini hawa wanakuwa si wa falsafa yake na pengine anakuwa hana nguvu juu yao kwa sababu kila mmoja amekuja kivyake, hivyo si rahisi kusema hamtaki hata kama si bora au hamtii.

Kuunda timu pia kutaondoa uholela wa viongozi wetu kudhani kuwa kocha mzawa anaweza kupatikana wakati wowote. Yaani kumuita ofisini kwa simu moja, kuzungumza naye kwa dakika chache na baadaye kumtangaza. 

SOMA ZAIDI: Wimbi la Wachezaji Kuvunja Mikataba Lidhibitiwe

Ndiyo ni lazima ahusike sehemu fulani ya mazungumzo, lakini masuala mengine ya haki zake ni lazima yashughulikiwe na watu waliobobea kwenye eneo hilo.

Na inawezekana asiwe ameajiri hao watu, lakini wanaweza kuwa chini ya kampuni za menejimenti ambazo nazo hunufaika kwa kuwa na wataalamu wengi chini yao na kushughulikia maslahi yao.

Ni muhimu kwa makocha wetu kuanza kufikiria zaidi thamani yao na kuitengenezea njia ya kuonekana katika mazungumzo ya ajira zao. Kwa dunia ya sasa, huwezi kufanya vizuri kimaslahi bila ya kujenga thamani ya kitu. Kama huduma yako ni ualimu wa mpira wa miguu, basi ni lazima uutengenezee thamani ionekane na inunuliwe kwa jinsi inavyostahili.

Mambo ya kufanya kazi kwa kujuana ni lazima yafikie mwisho. Mpira wa miguu kwa sasa ni sekta kubwa inayolipa vizuri. Kwa nini makocha wazawa waendelee kuwa wa kubahatisha?


Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *