Watanzania hawawahitaji wakuu wa mikoa na wilaya, na walilisema hili hadharani wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba, maarufu kama Tume ya Warioba, ilipotembea nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mfumo wa kiutawala wanaoutaka, na tume hiyo ikayaheshimu mawazo hayo kwa kupendekeza kuondokana na utaratibu huo kwenye rasimu yake, maarufu kama Rasimu ya Warioba.
Kuna sababu nyingi Watanzania, ambao leo, katika hali inayodhihirisha dharau kubwa ya tabaka tawala kwa wananchi, tunaambiwa eti wanahitaji elimu ya miaka mitatu ya Katiba, walizitoa kwa nini wanataka nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya zifutwe, ikiwemo, moja, watu hawa hawajulikana wanafanya kazi gani haswa na, mbili, wao siyo wawakilishi wa wananchi, bali wanamuwakilisha rais katika maeneo yao husika. Hii sababu ya pili, nadhani, ni ya msingi sana.
Disemba 9 ya kila mwaka Watanzania wanasherehekea Uhuru, lakini, tujiulize, Uhuru una maana gani haswa kwa watu ambao bado hawaruhusiwi kujitawala? Ujamhuri una maana gani kwa Watanzania ambao bado wanalazimishwa kumtegemea rais, anayechaguliwa kwenye chaguzi zinazobishaniwa sana, awapelekee wawakilishi wake kwenye ngazi ya mkoa na wilaya kutawala, kama ambavyo gavana tu alikuwa anafanya wakati wa ukoloni?
Mwaka huu wa 2024, Watanzania watasherehekea miaka 63 ya Uhuru, lakini watafanya hivyo wakiwa chini ya watawala –siyo viongozi–, katika ngazi ya mkoa na wilaya, walio na uwezo mkubwa wa kuamua hatma za maisha yao, kama vile kusimamia ulinzi na usalama wa maeneo husika, lakini wanaowajibika kwa rais, siyo kwa wananchi, na kipaumbele chao namba moja ni kukidhi matakwa ya aliyewateua badala ya wale wanaowatawala.
Mambo yanayokera
Katika mazingira hayo, inashangaza kuona wakuu wa mikoa na wilaya wakifanya mambo yanayokera na kutia kinyaa kwenye macho ya wanaowatawala, lakini wakiendelea kushikilia nafasi zao?
SOMA ZAIDI: Teuzi za Watu Wasio Waadilifu Zinawapa Motisha Viongozi Kutumia Vibaya Ofisi za Umma
Kwa mfano, Albert Chalamila, ambaye ungetegemea awe mstari wa mbele kuhimiza na kuheshimu utawala wa sheria, aliwahi kuwaagiza polisi, ambao nao wamekuwa wakituhumiwa kwa vitendo vya uvujifu wa sheria, waue watu wanaoshukiwa kuwa wezi, akisema hicho ndicho watu hao wanachokihitaji na siyo sawa kwa polisi kuwanyima! Chalamila alitoa kauli hiyo akiwa mkuu wa mkoa wa Mbeya.
Huko Arusha, mkuu wa mkoa, Paul Makonda, mtu aliyejijengea heshima ya kutokujali kabisa sheria, kanuni na maadili ya uongozi wa umma, anadhalilisha mtumishi wa umma mwanamke hadharani, na anakuwa na jeuri na kiburi cha kujitokeza hadharani na kuwakebehi na kuwasimanga wale wanaojitokeza kulaani vitendo hivyo, wengine wakiwa ni kutoka ndani ya chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kuna matukio ya wakuu wa mikoa, au wilaya, wakidaiwa kufanya mambo yasiyoingia kabisa akilini kwamba yanaweza kufanywa na mtu aliyepewa dhima ya uongozi, kama vile kuchapa wafanyakazi, kupiga watu ngumi, na kuchapa wanafunzi viboko, miongoni mwa vitendo vingine vingi vinavyoacha maswali mengi miongoni mwa wanajamii.
Haya ni matukio machache tu ya vituko na vimbwanga ambavyo wakuu wa mikoa na wilaya wanafanya nchi nzima vinavyoenda kinyume kabisa na sheria na maadili ya uongozi wa umma, na ambavyo vinawaudhi wananchi walio wengi ambao hawana namna yoyote ya kufanya kwani hawahusiki na uwepo wa watawala hao na kwa hiyo hawawezi kuwaondoa.
Ukinzani
Mara ya mwisho wananchi walipojaribu kuibua ukinzani dhidi ya utaratibu huu wa kikoloni, na kufanikiwa kuingiza mawazo hayo kwenye Rasimu ya Katiba, watawala, wakiongozwa na CCM, chama chenye maslahi kwenye kuendeleza ukoloni huo, walilikataa pendekezo hilo, pamoja na mengine mengi yaliyokuwemo kwenye Rasimu ya Warioba, na kurudisha utaratibu uliopo hivi sasa kwenye Katiba Inayopendekezwa ambayo mpaka leo imeshindwa kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maamuzi.
SOMA ZAIDI: Rasimu ya Warioba Ina Majibu Yote Samia Anayahitaji Kuhusu Mfumo wa Haki Jinai
Kwa bahati nzuri wananchi wanajua utaratibu huu uliorithiwa kutoka kwa wakoloni, unaokwenda kinyume kabisa na dhana ya watu kujitawala wenyewe, dhana iliyo katika moyo wa Uhuru na Ujamhuri wa Tanzania, haupo kwa ajili ya kukidhi matakwa yao, na tunaweza kuwa na uhakika kwamba wataendelea kuupinga vikali kadiri nafasi ya kufanya hivyo itakavyopatikana.
Na ni lazima wananchi waupinge utaratibu huu kwani hatuwezi kuruhusu mtu aliyezaliwa Chake-Chake, Pemba, aonekane anastahili kuwa ‘kiongozi’ wa watu wa Kasulu, Kigoma, sehemu ambayo hajawahi kufika, hajuwi utamaduni wa watu wake, wala mahitaji ya watu wa huko, na watu wa huko wala hawakuulizwa kama wanaridhia uteuzi wake au la. Huyo ni mtawala na hawakilishi matakwa ya wananchi.
Kama ambavyo hatuwezi kuruhusu mtu kutoka Chicago, Marekani aje kuwaeletea ‘maendeleo’ watu wa Singida, vivyo hivyo, hatuwezi kuruhusu mtu kutoka Singida, kwa sababu tu ameshindwa kwenye uchaguzi wa ndani wa CCM, au anaropoka sana mitandaoni kuhusu sifa za kiongozi, atumwe na rais kuwapelekea ‘maendeleo’ watu wa Lindi.
Tubadili fikra
Ni wakati tuwe tunamaanisha tunachokisema na kukibainisha kwenye Katiba, sheria, na miongozo mingine ya nchi. Kama kweli tunaona kuna umuhimu kwenye kugatua madaraka, basi ifike wakati tuwaache wananchi wachague wawakilishi wao, watakaojituma na kuwajibika kwao. Nchi hii ni kubwa sana kuongozwa kutokea Magogoni au Chamwino, na ni muda tubadilishe fikra zetu kuendana na ukweli huo.
Haijalishi nia ya kiongozi wa nchi ni nzuri kiasi gani, na siamini hata kidogo kama rais anaongozwa na nia ovu anapotuma mwakilishi kwenye mkoa huu au wilaya ile, na anaweza kuwa anaongozwa na nia nzuri kabisa, ukweli utabaki kwamba hakuna mtu anaweza kumletea mtu mwingine maendeleo, na kwamba ni watu wenyewe pekee ndiyo wanaoweza kufanikisha mchakato huo.
SOMA ZAIDI: Labda Suluhu ya Serikali Kudharau Maoni ya Wananchi ni Kuacha Kushirikiana Nayo?
Kuruhusu wananchi wachague viongozi wao, badala ya rais kuwachagulia, na kuwaruhusu watu hao kuwa na mamlaka makubwa zaidi kuliko wateule wa rais, ni hatua muhimu ya kuwasaidia watu hao kufanikisha michakato yao ya kimaendeleo, na, cha muhimu zaidi, kuuendea Ujamhuri wetu pamoja na kuutafsiri Uhuru wetu, tulioupata kwa tabu sana, kwa vitendo.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.