The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Bunge Laazimia Ushirikiano Kati ya Halmashauri na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji

Huduma za zimamoto na uokoaji nchini zilitolewa katika halmashauri nchini mwaka 2007 kufuatia kupitishwa kwa Sheria Namba 14 ya mwaka 2007 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambalo kwa sasa lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Juni 6, 2024 limeitaka Serikali kuja na muswada wa sheria bungeni utakaoweka utaratibu wa kuwezesha halmashauri za jiji, manispaa, miji na wilaya kutenga bajeti kwa ajili ya kununua vifaa kwa ajili kukabiliana na majanga ya moto na uokoaji.

Azimio hilo la Bunge limetokana na hoja binafsi iliyotolewa na mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Jacob Tarimo ambaye ameshauri kuwepo na utaratibu utakaoziwezesha halmashauri nchini kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kutatua tatizo la upungufu wa magari ya zimamoto pamoja na vifaa vitakavyotumika kuzima moto na uokoaji.

Mbunge huyo amesema ukosefu wa magari ya zimamoto na vifaa vingine vya uokoaji katika halmashauri mbalimbali nchini umechangia ongezeko la madhara yatokanayo na ajali za moto na ajali nyingine kwa sababu ya kukosekana ufanisi katika huduma ya kuzima moto na uokoaji.

“Majanga ya moto na ajali yameendelea kuleta madhara makubwa kwa wananchi kwa kuharibiwa kwa mali , kupata vilema vya muda na vya kudumu,” amesema Tarimo, “na madhara ya kiafya na wakati mwingine kusababisha vifo vya wananchi.”

Huduma za zimamoto na uokoaji nchini zilitolewa katika halmashauri nchini mwaka 2007 kufuatia kupitishwa kwa Sheria Namba 14 ya mwaka 2007 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambalo kwa sasa lipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kutokana na ufinyu wa bajeti ya Jeshi hilo, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 imebainisha kuwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina upungufu vifaa kwa asilimia 91 kati ya mahitaji ya vifaa 7,012.

Ripoti hiyo pia ilionesha kuwa vituo vya kuhifadhia maji ya kuzimia moto vinavyohitajika nchini ni takribani 283,370 ambapo kati ya mahitaji hayo vilivyokuwepo ni 2,343, huku 1,630 tu ndio vinafanya kazi.

Wakichangia hoja hiyo baadhi ya wabunge akiwemo mbunge wa viti maalum Felista Njau amesema changamoto zinazoikumba Jeshi hilo linatokana na kutopatiwa bajeti ya kutosha kughulikia matatizo hayo yanayowakabii.

“Mheshimiwa Spika mpaka mwezi wa pili hawakuwa wamepata hata mia. Sasa unawapigaje mawe hawa watu?” Amesema Njau. “Mheshimiwa Spika Serikali ichukue jukumu lake ipeleke fedha kwa wakati halafu tuwabane wakiwa wana fedha”

Kwa mujibu wa mtoa hoja bwana Tarimo amesema kuwa halmashauri zenye uhitaji mkubwa wa huduma zimamoto na uokoaji zinaweza zikanunua vifaa na kujenga miundombinu ambayo itatumiwa na Jeshi kwenye halmashauri yao.

“Ni kama Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ilivyoingia makubaliano na Jeshi la Zimamoto, Mamlaka inanunua magari, ila anayesimamia magari hayo ni Jeshi la Zimamoto” amesema Tarimo.

Naye Mbunge wa Nkasi Aida Kenan amesema kuwa ushirikiano kati ya halmashauri na Jeshi la Zimamoto ni muhimu sana kwani masuala ya kukabiliana na moto au uokoaji yanaendana na mipango miji.

“Leo tunapozungumzia halmashauri, halmashauri inahusika na upangaji wa miji ni wajibu wao. Kwa sababu hata kama zimamoto watapewa fedha kiasi gani kama mipango yetu ya kupanga miji itakuwa hovyo hawatafanya chochote.” Amesema Aida.

Kumekuwepo pia na baadhi ya wabunge waliokuwa na wasiwasi na azimio hilo kutokana na kile wakisema kwamba kitendo cha kuzitaka halmashauri kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kisheria kutabebesha mzigo halmashauri zenye uwezo mdogo wa ukusanyaji mapato.

Mmojawao ni mbunge wa Geita Mjini Costantine Kanyasu ambaye amesema kuwa zipo halmashauri zina makusanyo madogo huku vifaa kama gari la zimamoto lina gharama kubwa ambazo sio rahisi kwa halmashauri hizo kununua.

“Kuna halmashauri makusanyo yake ni milioni mia mbili lakini gari moja la zimamoto ni bilioni moja. Serikali iendelee na wajibu wake.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi anayeandikia The Chanzo kutokea Dodoma. Anapatikana kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *