The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Pengine ni Kweli Polisi Hawahusiki na Utekaji. Lakini Mbona Hatuoni Watekaji Wakikamatwa?

Katika mazingira ambapo hakuna mtu hata mmoja aliyetiwa nguvuni mpaka sasa kutokana na vitendo hivyo, tunaanzaje kuacha kuwawajibisha polisi, tunaoaminishwa kwamba wapo kwa ajili ya usalama wetu?

subscribe to our newsletter!

Polisi, na vyombo vingine vilivyokabidhiwa jukumu la kuhakikisha usalama wa watu na mali zao, hawawezi kukwepa kuhojiwa kuhusiana na wimbi la visa vya utekaji linaloendelea kushamiri nchini hivi sasa, na kuwajaza Watanzania kwa mamilioni hofu juu ya usalama wao na ule wa wanaowapenda.

Kama nchi ambayo wananchi wake wamejiwekea taratibu za kuendesha maisha yao, kama vile kwa kuwa na Katiba inayofanya kazi kama mkataba kati ya wanaoongoza na wanaoongozwa, na kuwa na sera, sheria, kanuni na miongozo zinazofafanua namna mkataba huo unavyopaswa kufanya kazi, ni lazima tuwe na mtu wa kumlaumu pale tunapohisi mambo hayaendi kama wananchi tunavyotarajia.

Wajibu wa kuhakikisha Watanzania wako salama na wanaishi kwa uhuru na amani nchini kwao, bila ya kuwa na hofu ya kupotezwa au kudhuriwa, umekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi, na ni wananchi wanaofadhili shughuli zote za taasisi hiyo ili iweze kutimiza wajibu wake huo ipasavyo, ikiwemo kugharamia mishahara ya maafisa wake na stahiki zao zingine.

Namna pekee kama mwananchi naweza kuhalalisha utayari wangu wa kulipa kodi ni kuonesha uhusiano uliopo kati ya kodi hiyo ninayolipa na wananchi wenzangu na kuimarika kwa ustawi wangu kama mwananchi, ikihusisha, pamoja na mambo mengine, ni namna gani najisikia huru kuishi na kutembea kwenye nchi yangu. Kama siwezi kujihakikishia hilo, kwa nini basi nilipe kodi?

Sielewi

Ndiyo maana, nimeamua kutokuulewa utetezi wa Jeshi la Polisi kwamba haihusiki na visa vya utekaji vinavyoendelea kuripotiwa kutoka sehemu mbalimbali za nchi kwani hata kama ingekuwa ni kweli maafisa wa polisi hawahusiki kwenye visa hivyo wao wenyewe moja kwa moja, bado tunaitegemea taasisi hiyo kukomesha vitendo hivyo kwa kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wahusika wa vitendo hivyo.

SOMA ZAIDI: Wananchi Waibane Serikali Kukithiri Matukio ya Utekaji Tanzania

Juhudi za Jeshi la Polisi, na kwa ujumla Serikali, za kujaribu kuosha mikono yao kwenye suala hili, na kujaribu kujenga picha kwamba matukio haya ni masuala binafsi ya wanaoripotiwa kutoweka, zitaendelea kuwa dhaifu, angalau kwangu mimi binafsi, mpaka pale nitakapoona na kushawishika kwamba polisi wanatoa kipaumbele kwa vilio vya Watanzania na kuanza kuwasaka na kuwashikilia wale wote ambao wanaweza kuwa wanahusika kutekeleza vitendo hivi.

Siamini hata kidogo kwamba sababu kwa nini watu hawa bado hawako mbele ya vyombo vya sheria ni kwa sababu wana akili na maarifa mengi sana kuliko watu wetu kwenye idara za ulinzi na usalama, au ufinyu wa bajeti na rasilimali zingine zinazoweza kukwamisha operesheni hizo. Naamini kabisa kwamba sababu kubwa ni Jeshi la Polisi kushindwa kulipa suala hili kipaumbele.

Au sababu nyingine kwa nini wahusika wa vitendo vya utekaji wanaendelea kuwa mbali na mkono mrefu wa sheria ni kwamba watekelezaji wa vitendo hivyo ni watu haohao wanaotegemewa kusimamia utekelezaji wa sheria? Hii inaweza kuwa ni dhana tu, lakini matukio kadhaa yanayoendelea kuripotiwa nchini yanaashiria kunaweza kuwa na ukweli fulani ndani yake.

Uhusika wa polisi

Tuangalie hiki kisa cha kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kombo Twaha Mbwana, ambaye kwa siku 29 aliripotiwa kutoweka, familia yake ikiwa haijuwi chochote kuhusu hatma yake, kabla ya polisi kujitokeza hadharani na kusema inamshikilia kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 eti kwa makosa ya matumizi mabaya ya mtandao!

Siku 29! Polisi haijaeleza kwa nini imemshikilia kwa siku zote hizo, kinyume kabisa na taratibu zinazolitaka Jeshi la Polisi kumfikisha mtuhumiwa mahakamani ndani ya masaa 24. Polisi haikusema pia kwa nini imeamua kujitokeza sasa kukiri kumshikilia kijana huyo ingawaje hatua hiyo imeambatana na kampeni kubwa inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii inayodai kuachiliwa kwa kijana huyo. 

SOMA ZAIDI: Tanzania Imerudi Kwenye Nyakati za Giza?

Au tuangalie hiki kisa cha Edgar Edson Mwakabela, kijana wa miaka 27 aliyetekwa na kupigwa na kuumizwa vibaya kabla ya kutupwa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambaye amedai kabla ya kusafirishwa kwenda huko alilazwa kwenye karakana ya Kituo cha Polisi cha Oysterbay. 

Mwandishi wa habari Salim Kikeke alimbana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kuhusu hili, ambaye alishindwa kutoa majibu yanayoeleweka. Kikeke, anayefanya kazi na kituo cha habari cha Crown Media, alimtaka Muliro watembelee pamoja karakana hiyo ambapo kiongozi huyo wa polisi alidai kufanya hivyo itakuwa ni “kuingilia uchunguzi.”

Haya wala si mapya ukiangalia namna polisi wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Mnamo mwaka 2019, kwa mfano, rafiki yangu na mwanaharakati wa haki za binadamu, Tito Magoti, alitekwa jijini Dar es Salaam na “watu wasiyojulikana” kabla ya polisi kujitokeza siku kadhaa mbeleni, wakikiri kumshikilia kwa tuhuma ambazo baadaye zilikuja kujulikana kama utakatishaji wa fedha haramu!

Sasa, niambie, kama mwananchi wa kawaida, nahitimisha vipi kuhusiana na vitendo vya utekaji vinavyoendelea kuripotiwa nchini katika muktadha wa ripoti kama hizi zinazohusisha ushiriki wa polisi kwenye vitendo hivyo, huku polisi wakishindwa kumkamata mtu hata mmoja ambaye anaweza kuwa anahusika na vitendo hivyo? Siwezi kulaumiwa kwa aina yoyote ya hitimisho nitakayofanikiwa kuifikia.

Uwajibikaji

Polisi, na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wanapaswa kuwajibishwa katika hili na ni muhimu kwa viongozi wetu wa kisiasa, tuliowakabidhi dhamana ya kutuongoza, watusaidie kuhakikisha kwamba kunakuwepo na aina hiyo ya uwajibikaji miongoni mwa wale waliokabidhiwa wajibu wa kulinda usalama wa Watanzania na mali zao.

SOMA ZAIDI: Serikali: Matukio 21 Ya Watu Kutekwa na Kupotea Yamepatiwa Ufumbuzi

Ndiyo maana sidhani kama ilikuwa sahihi sana kwa Rais Samia Suluhu Hassan kulipongeza Jeshi la Polisi kwa “utulivu” uliopo nchini hivi sasa kwani, kwa hakika, familia ya Twaha, Sativa na wenzao kadhaa waathirika wa vitendo vya utekaji wanauhisi utulivu huo ambao Rais Samia anauona na kuuhusisha na utendaji kazi mzuri wa Jeshi la Polisi.

Au, kama mwalimu wangu Richard Mabala, mwandishi wa vitabu na mshairi mahiri, alivyoandika kwenye safu yake Julai 12, 2024, katika chapisho hili, pengine Rais Samia anazungumzia “utulivu” wa walalahai na wawakilishi wenzao kwenye tabaka tawala, wanaotembezwa kwa ving’ora na wanaoishi kwenye nyumba zinazolindwa na mbwa na walinzi wakali?

Pengine, maana ukweli ni kwamba kwa walalahoi na wenzao wengi kwenye tabaka tawaliwa wanaendelea kupambana na hali zao, ikiwemo kutokujua endapo kama kesho wataendelea kubaki na wapendwa wao, au watakuwa takwimu nyingine kwenye mlolongo wa visa vya utekaji vinavyoendelea kuripotiwa nchini Tanzania kwa sasa!


Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts