Rais Samia Suluhu Hassan ametoa majina ya Stesheni mpya za Reli ya Kisasa SGR leo jijini Dodoma, ambapo ameelezea kuwa stesheni hizo zitaitwa majina ya Marais wa Tanzania.
Rais Samia ametoa majina haya wakati akizindua Miundombinu ya Reli na Huduma za Usafiri wa treni ya SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma. Amechukua uamuzi huu baada ya Bodi ya Shirika la Reli kupendekeza stesheni ya Dodoma ipewe jina la Samia.
Stesheni Kuu ya Dar es Salaam ameipa jina la Magufuli, stesheni hiyo ni moja ya vituo vinavyovutia hasa kwa kujengwa kwa umbo la madini ya Tanzanite.
Stesheni Kuu ya Morogoro ameipa jina la Kikwete, stesheni hiyo nayo imejengwa kwa umbo la safu ya milima ya Uluguru. Kwa upande wa Stesheni Kuu ya Dodoma ameipa jina la Samia, stesheni hii imejengwa kwa umbo la kufanana na mawe yanayopatikana Dodoma.
Kwa upande wa Stesheni Kuu ya Tabora ameipa jina la Ali Hassan Mwinyi, na stesheni ya Shinyanga ameipa jina la Amani Abeid Karume. Stesheni ya Mwanza ameipa jina la Mwalimu Nyerere na Kigoma ameipa jina la Mkapa.