The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uvamizi Dhidi ya Tasnia ya Habari? Tuzungumze Matumizi Mabovu ya Kiswahili Yafanywao na Waandishi wa Habari

Uanzishwaji holela wa vyombo vya habari na ukosefu wa wahariri maalumu wa lugha katika vyombo vingi vya habari huchangia pa kubwa kulikuza tatizo hili.

subscribe to our newsletter!

Mcheza ngoma si yake, daima huharibu. 

Huu ni msemo wa wenye hekima, unaodokeza umuhimu wa kufanya jambo kitaalamu. Ni nadra kupata samani zenye ubora wa kimuonekano na umadhubuti wa kiufundi pasi na seremala mweledi. 

Majengo ya maroshani, magari yabebayo tani na meli zijazazo kani, huhitaji wahandisi makini wakati wa ujenzi wake. Ndipo watumiaji na waendeshaji hukiri utulivu na kupoteza hofu ya ajali isokinga.

Kwa namna kama hii, ndivyo itakiwavyo kwa tasnia ya habari na mawasiliano. Tasnia hii hubeba dhima kubwa ya kuelimisha, kuburudisha, kupasha habari, kuamsha ari, kuibua hisia na hatimaye kuchochea mabadiliko na maendeleo ya jamii.

Dhima hii ndiyo inayowajibisha uwepo wa wanahabari weledi waliyobobea katika misingi ya kitaaluma na kiutendaji. Halikadhalika wajuzi na washititi wa matumizi ya lugha kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazoiongoza lugha hiyo, kama mtaji wa uzalishaji na usambazaji habari.

Hofu ya uvamizi

Pamoja na uzito wa tasnia hii na dhima yake, inastaajabisha kama si kufadhaisha inaposhuhudiwa ikikabiliwa na uvamizi mkubwa wa wanahabari wasiyotaalamika; si kwenye taaluma ya habari tu, bali hata kwenye misingi ya lugha sanifu na fasaha.

SOMA ZAIDI: Uchanganyaji R na L na Makosa Mengine ya Kiswahili Yafanywayo na Wanahabari

Uanzishwaji holela wa vyombo vya habari – hasa vya mtandaoni; ukosefu wa wahariri maalumu wa lugha katika vyombo vingi vya habari; bezo na dharau juu ya umuhimu wa matumizi ya lugha sanifu na fasaha na uzembe wa kiutendaji ni miongoni mwa nukta changishi zinazochochea uvamizi wa tasnia ya habari na uchafuzi wa lugha ya Kiswahili katika utangazaji na uandishi.

Yumkini sipaswi kuweka mashaka makubwa mno kwenye mavamizi ya tasnia hii. Ingawa inanipa hofu kuwa, huenda ikaporomoshwa na ikakosa imani ya hadhira yake. Au pengine ikawa inapotosha na kuharibu mustakbali mzima wa kifikra, kimitazamo, kifalsafa, kimwelekeo na dira ya maisha ya mtu mmoja mmoja, familia, jamii na hata taifa.

Huenda baadaye mavamizi yakizidi, tasniya hii ikawa ni fimbo ya kuichapa jamii, kuharibu maadili na kuondosha heshima na haiba ya hadhira inayojielewa; hususan kwa vile vizazi vinavyonyanyukia. Hii yaweza kuwa hofu kubwa kwangu.

Hata hivyo, wahka unaoupa mashaka moyo wangu na kutingisha kichwa cha masikitiko, kuhangaisha fikra na nadhari zangu na kunifanya nikose amani ya nafsi, ni namna mtaji wa tasnia hii unavyotumika. Nao si mwengine, ni lugha adhimu ya Kiswahili.

Natafakari na kujiuliza, ikiwa wavamizi hawaijui hata ngoma yenyewe, vipi wataweza kuicheza kuendana na mapigo yake? Ikiwa wavamizi hawaijui hata tasnia yenyewe, ni kwa kiasi gani wataweza kuitumia nyenzo na rasilimali ya lugha; ambayo ndiyo inayochakata, kufinyanga na kusuka habari, taarifa na makala mbalimbali zinazoijenga tasnia hii?

Vyombo hivi ni rasmi?

Hapa ndipo ninaposhangazwa na gazeti la JAMVI LA HABARI, ikiwa kweli ni gazeti rasmi, linalotambulika kisheria. Au kama fikra zangu si sahihi, basi sidhani kwamba waandishi na wahariri wake ni wataalamu wa tasnia hiyo. Au kama sivyo, basi sidhani kama ni weledi wa lugha kama nyenzo kuu ya usukaji wa tasnia hiyo.

SOMA ZAIDI: ZBC, HabariLeo Waongeze Umakini Matumizi ya Kiswahili Fasaha, Sanifu

Katika gazeti hilo, nimekutana na taarifa ya ajabu na ya kizembe kabisa. Iliyokiuka weledi na umakini wa matumizi sahihi ya lugha. Ukurasa wa mbele wa gazeti hilo kuna taarifa inayosomeka hivi: Pigo Wanahisa Azania Benki. Uzembe wa kilugha unaoonekana hapa ni matumizi ya mfumo wa Kiingereza katika lugha ya Kiswahili kwenye maneno Azania Benki, ambapo kwa Kiingereza ni Azania Bank.

Kwa Kiswahili sanifu ilitakiwa kutumiwa kivumishi cha a-unganifu (V) au kihusishi (H) kwa baadhi ya wataalamu. Kwa msingi huu kifungu hiki kilitakiwa kuwa Pigo Wanahisa Benki ya Azania. Au Pigo Wanahisa Azania.

Taarifa nyingine ni ile iliyochapishwa katika ukurasa wa Facebook wa chombo kinachojiita BONGO MEDIA. Taarifa hii haijuzu hata kusema imeandikwa na mwanafunzi wa darasa la saba, seuze chombo kinachojinasibu kuwa ni cha habari. Hapa ninakuu taarifa hii kama ilivyochapishwa:

CLAM VEVO 

muigizaji tena comedi anaendelea kufanya vizuri kwenye siries Snake boy pia na Mistake ,team clam inazidi kukuza vipaji kwa imara zaidi 

mimi uwa najiuliza je mastar wetu nchini tz kuwa na ma bodyguards ,inakuja kufatana naumaarufu aidha nipesa ,ukosefu wausalama?

Taarifa hii inatuthibitishia uvamizi wa hali ya juu na wa kutisha katika tasnia ya habari. Taarifa kama hizi zichapishwazo mitandaoni, hufika mbali na kwa muda mfupi mno. Pamoja na kuichafua tasnia ya habari, hali hii inatishia uhai, ubora na hadhi ya lugha ya Kiswahili.

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Matumizi ya Kiswahili Sanifu, Fasaha Katika Tasnia ya Habari?

Taarifa hii ina makosa mengi mno. Yakiwemo matumizi makubwa ya lugha isiyofahamika kuwa ni Kiingereza au Kiswahili. Kwa mfano, maneno kama comedi, siries, team clam, mastar na mabodyguard ni maneno ambayo kimsingi kwa yalivyoandikwa, hayapo katika mfumo wa Kiingereza wala Kiswahili, ingawa mwandishi alikusudia Kiingereza ambalo nalo ni kosa. 

Maneno haya pia yapo yaliyotumia viambishi vya Kiswahili vilivyoambikwa katika mizizi ya Kiingereza katika neno moja.

Kadhalika, kuna matumizi ya maneno ya Kiswahili pasipo mahala pake. Maneno hayo ni tena, pia na, kwa imara, inakuja, aidha na ukosefu. Maneno yote haya hayakutumiwa inavyostahiki.

Pia, kuna uchanganyaji wa maneno mawili kuwa neno moja. Maneno hayo ni naumaarufu, nipesa na wausalama. Taarifa hii pia haikuzingatia kabisa alama za uakifishaji. Kwa mfano, mwandishi anaanza na herufi ndogo mwanzoni mwa sentesi, katika vifungu vyote viwili.

Alama ya mkato (,) imejitokeza mara tatu ikiwa imewekwa nyuma ya herufi inayoanzia neno jipya au baada ya nafasi inayotenganisha maneno mawili. Alama ya kituo kikubwa haikutumika kabisa katika taarifa hii, licha ya kuhitajika kwake.

SOMA ZAIDI: Matokeo Kidato Cha Nne 2023: Somo La Kiswahili Laendelea Kuongoza Kwa Ufaulu

Taarifa pia ina maneno ya Kiswahili yaliyoandikwa kimakosa. Maneno hayo ni anaendelea, uwa na kufatana. Pamoja na makosa haya, mwandishi anaandika jina la nchi kwa kifupisho cha tz, jambo ambalo ni kosa kubwa katika matumizi rasmi ya lugha.

Usahihi na usanifu wa vifungu vya taarifa hii ulitakiwa kuwa hivi:

CLAM VEVO, muigizaji wa komedi anayeendelea tena kufanya vizuri kwenye tamthiliya za Snake Boy na Mistake. Timu ya Clam inazidi kukuza vipaji kuwa imara zaidi. Mimi huwa najiuliza, je, nyota wetu nchini Tanzania kuwa na walinzi, kunatokana na umaarufu, fedha au hofu ya usalama wao?

Hatukuziba ufa, sasa tujenge ukuta

Hii ni mifano michache niliyofanikiwa kuieleza hapa. Hata hivyo, kuna wimbi la vyombo babaishi vya habari Tanzania, hususan vya mtandaoni. Vyombo hivi, kwa kukosekana kwa weledi na taaluma ya tasnia ya habari pamoja na lugha kwa waendeshaji wake, vinaashiria uvamizi wa tasnia hii, jambo ambalo kama tulivyotanabahisha awali, linaweza kuwa na madhara makubwa.

Madhara hayo yanaweza kuitahikili tasnia husika, jamii na hata lugha yenyewe. Ipo haja ya kuwa na mfumo madhubuti wa kiserikali utakaoweza kudhibiti uanzishwaji holela wa vyombo vya habari. 

Vyenginevyo, chambilecho watoto wa mjini, itakula kwetu. Hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa katika kujenga ukuta huu uliyokwisha kuanguka kwa kuzembea kwetu kuziba ufa.

Ally Harith ni mtafiti na mchambuzi wa masuala ya elimu na mtaalam wa lugha ya Kiswahili kutoka Zanzibar. Unaweza kumpata kupitia drharith09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Unataka kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahiriri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

  1. Maalim Ally Bin Harith! Nakuunga mkono. Tasnia ya Habari imevamiwa na makanjanja. Watu hawana ueledi wa Lugha ya Kiswahili Wala Habari.
    Mashaka matupu. Cha kustaajabisha hata Wahariri makini hamna katika vyombo. Mimi Mohamed Mzee Ali Huwa napiga kelele siku zote kuhusu lugha. Naandika makala Zanzibar Leo zisaidie, lakini watu hawajifunzi. Insikitisha.

  2. Kwa kweli Kuna Kuna kazi kubwa sana kujenga ukuta amabo ufa wake ulipuuzwa. Na kadri siku zinavyoendelea uanzishaji wa vyombo vya habari umekuwa ni ushindani wa wanamuziki na wengineo katika tasniya hiyo hiyo ya burudani jambo ambalo limeifanya tasniya hiyo hata kukosa maadili, si kwa kivazi wala uongeaji. Kwa kweli vyombo vya habari si sehemu salama tena ya kujifunza na kujichotea maarifa stahiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *