The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Hongera TFF kwa Tuzo, Lakini Bado Maboresho Yanahitajika

Ukiangalia tuzo zote, hakuna inayomtofautisha Mwanasoka Bora wa Msimu, na mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kombe la CRDB.

subscribe to our newsletter!

Ijumaa, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya tamasha la kutuza wanamichezo waliofanya vizuri msimu uliopita na wale walio na mchango mkubwa kwenye mchezo huo maarufu nchini.

Tuzo hizo zimefanyika mwanzoni mwa msimu mpya baada ya kuahirishwa kwa maelezo kuwa waandaaji walitaka kuziboresha ziendane na hadhi yake.

Na kweli kumeonekana maboresho makubwa si tu katika uandaaji, bali pia katika kutuza wachezaji na makocha ambao wengi wamekubali kuwa walistahili kushinda tuzo hizo.

Ile dhana iliyokuwa inalalamikiwa na wengi ya kuweka uwiano wa washindi kutoka klabu za Simba, Yanga na Azam haikuonekana katika tuzo za Ligi Kuu, ambako Stephane Aziz Ki aliondoka ukumbini na tuzo kubwa kuliko zote ya Mchezaji Bora wa Msimu na nyingine mbili.

Katika hali ya kawaida na utamaduni wetu, isingekuwa rahisi kwa mchezaji mmoja wa klabu kama Yanga, Simba au Azam kupewa tuzo tatu peke yake. Ni lazima tuzo hizo zingegawanywa kwa timu hizo tatu ili kweka uwiano na kutoudhi mashabiki wa moja ya timu hizo.

SOMA ZAIDI: Kutumia Takwimu Pekee Tuzo za TFF ni Usumbufu

Hata kikosi bora cha msimu hakikuonyesha uwiano huo kwa kuwa ni mchezaji mmoja tu wa Simba aliingia, huku Yanga wakijazana.

Ile dhana nyingine ya uzalendo pia ilizikwa kwenye tuzo hizo. Haikujalisha anayeshinda ni mchezaji wa nje au wa ndani, bali ziliangalia zaidi anayestahili.

Kwa hili, TFF imejitahidi kuboresha tuzo hizo ambazo zamani zilikuwa zikikwepwa na wachezaji kutokana na kutojijengea Imani au kukubalika na mashabiki na wachezaji. 

Imani imejengwa

Lakini mwaka huu, angalau imani imejengwa kuwa yeyote anayestahili anaweza kushinda; iwe anatoka Prisons, Yanga, Simba au KMC au ni mzawa au mgeni.

Lakini kasoro hizo mbili ambazo hulalamikiwa kila mwaka zilichomekwa kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambalo kwa kawaida ya mashindano ya mtoano, yasiyo na hatua ya ligi au makundi, huwa hakuna tuzo.

SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Kuu Iongoze Uboreshaji Kanuni za Ligi

Hii ni kwa sababu timu nyingine hucheza mechi moja, nyingine mbili na nyingine tatu. Timu inayofika fainali hucheza takriban mechi sita. Kwa hiyo, ukiweka tuzo kama ya mchezaji bora, uwezekano wa mchezaji aliyeishia raundi ya 64 bora au 34 bora kuingia kwenye kinyang’anyiro ni mdogo.

Hata yule ambaye timu yake imeishia robo fainali ni nadra sana kuingia kwenye kinyang’anyiro. Kwa hiyo, unashindanisha wachezaji na makocha wasio na uwanja sawa wa mashindano. Wengine wana mechi moja na wengine wana mechi nne, unapataje mchezaji bora katika uwanja huo usio sawa?

Hata uwezekano wa mchezaji wa timu iliyocheza mechi tatu kuibuka na tuzo ya mfungaji bora ni shida, labda timu yake iwe imefanya mauaji katika mechi hiyo moja. Lakini hataweza kushindana na mchezaji ambaye timu yake imefika fainali.

Kwa hiyo, tuzo zilizohusu Kombe la CRDB ndiko kulikofishwa uzalendo na uwiano wa Simba, Yanga na Azam. Ule Utanzania wetu, ambao baadhi huita Uswahili, bado upo. Bado tunataka kuridhisha kila mtu hata pale pasipostahili.

Si lazima kushinda

Si lazima kila mtu ashinde tuzo. Ili tamasha liwe na ushindani na mshawasha wa kutaka kujua mshindi, ni lazima wengine wapate na wengine wakose. Christian Ronaldo na Lionel Messi wameshindana hivyo kwa miaka mingi na wala watoaji tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia hawakuangalia wamridhishe vipi mmoja wao pale anapokosa tuzo.

SOMA ZAIDI: Yusuf Manji Alimuachia Somo Zuri Mohammed Dewji

Hakuna cha kusema kwa sababu Messi ameshinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, basi Ronaldo atafutiwe tuzo nyingine kwenye mashindano mengine. Huku ni kutaka kumridhisha kila mtu na kuogopa lawama za kutompa fulani tuzo.

Ni lazima tufikie kwenye utamaduni huo wa kutoa tuzo kwa anayestahili huku anayekosa akiona kuna haki ya yeye kukosa na si kuonewa. Ukiweka tuzo ya kumpoza aliyeshindwa, ataona kuwa alistahili tuzo aliyokosa na ndio maana waandaaji wameliona hilo na wakaamua kumpoza kwa tuzo nyingine ili mradi aondoke ukumbini na kitu fulani.

Pia, ukiangalia tuzo zote, hakuna inayomtofautisha Mwanasoka Bora wa Msimu, na mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kombe la CRDB. Labda ukisogelea karibu ndio utaona maandishi yanayotofautisha tuzo moja na nyingine.

Hapa kidogo waandaaji na wale waboreshaji tuzo walipitiwa. Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Msimu ni kubwa kuliko zote na hivyo haistahili kutofautishwa kwa maandishi pekee, bali hata muundo wake. Hapa waboreshaji walitakiwa kukuna vichwa, kuingia kwenye historia, mazingira yetu na kuuangalia utamaduni wetu kujua tuzo hiyo na nyingine ziundweje.

Hizi si tuzo za muziki kama za Grammy au sinema kama Oscar hadi tuamue kuwa tuzo zote zifanane. Mpira wa miguu una utamaduni wake na hivyo ni lazima tuendane nao na si kulipua ili mradi tamasha lifanyike na washindi waondoke na kitu mkononi.

Haya ni mambo yanayohitaji muda wa kutosha kufikiri, kubuni na kuangalia wengine wanafanyaje ili upate chako kinachoakisi mazingira yako na kinachojitofautisha kwa kiasi fulani na wengine ili Mmarekani akiona ajiulize hii tuzo yenye uzuri huu ni ya nchi gani na baadaye iwe rahisi kuzitambua tuzo zetu, si kwa zile rangi za bendera pekee.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts