The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mbunifu Huyu Awaasa Watanzania Kuziangalia Takataka Kwa Jicho la Kijasiriamali

Laurian Adolph Mchau anageuza taka-ngumu na taka-maji kuwezesha ufanyikaji wa kilimo rununu pamoja na utunzaji wa mazingira.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wito umetolewa kwa Watanzania kubadilisha namna wanavyoziangalia takataka, badala ya kuziona kama uchafu unaopaswa kutupwa na kuanza kuziangalia kama nyenzo zinazoweza kuwawezesha kufanya ujasiriamali, kama vile kujikita na kilimo rununu, au mobile farming kwa kimombo.

Laurian Adolph Mchau, Mtanzania anayetambulika kwa kubuni teknolojia hiyo, aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum kwamba gharama za aina hiyo ya kilimo ni hafifu sana ukilinganisha na faida inayopatikana, ikiwemo siyo tu kuipatia familia mazao mbalimbali ya kilimo, bali pia fedha kwa kuuza mazao hayo.

Mchau, 54, ni mtafiti na mbunifu wa teknolojia mbalimbali mwenye maskani yake katika eneo la Ubungo External, jijini Dar es Salaam, aliyebuni teknolojia hiyo ya kutumia taka-ngumu na taka-maji ambayo mbali na kuwezesha ufanyikaji wa kilimo rununu, bali pia husaidia kwenye utunzaji wa mazingira.

“Kilichonichochea zaidi ni baada ya kuona taka nyingi zinachukuliwa na kwenda kutupwa,” Mchau aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika katika karakana yake iliyopo Ubungo External, jijini Dar es Salaam. “Sasa nilijifunza kwa nchi za wenzetu ambao ni jirani zetu [Kenya].” 

“Wao [Kenya] wamekua, kwa miaka mingi, wanatumia hizi taka kavu na ngumu na taka maji kwa ajili ya uzalishaji kwenye mashamba,” aliongeza mbunifu huyo ambaye pia ni mkulima. “Mazao mengi pia ambayo hayana kemikali huweza kuzalishwa kupitia teknolojia hii. Hicho ndicho ambacho na mimi ninakifanya.”

Mchakato mzima

Mbunifu huyu hukusanya taka za aina mbalimbali na kuzisindika kwenye mapipa ya maji yaliyotumika au mifuko ya nailoni kwenye sehemu zilizojengwa. Huzimwagilia takataka hizo maji kuondoa gesi na harufu, kuzichanganya na udongo, kabla ya kuzisindika tena kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kuondoa gesi na harufu zisizohitajika.

Mchau huchukua udongo uliozalishwa kupitia mchakato huu, uliojumuisha umwagiliwaji wa maji wa mara kwa mara, na kuuchanganya na ule anaouchukua ardhini, hususan ule wa juu, na kusindikza kwenye chumba kidogo kilichosakafiwa vizuri. 

Kukabiliana na wadudu wanaotokana na udongo aliouchukua ardhini, mbunifu huyu hutengeneza kaboni kwa kutumia magome ya miti ya asili yaliyokobolewa, yanayochanganywa kwa kuchomwa na majivu ya kuni na mkaa.

Udongo unaowekwa kwenye chumba hiki unasindikwa kwa ajili ya kuendelea kuuondolea kemikali ambapo bomba maalum huunganishwa kutoka kwenye chumba hicho kwenda nje kwa ajili ya kuuwezesha udongo unaosindikwa “kupumua.” Kujua kama kemikali zimetoka, Mchau huotesha miche kwenye udongo huo ambapo kufa kwake kutadhihirisha mabaki ya kemikali zinazopaswa kutolewa.

Mchau anasema mchakato huu mzima huchukua takriban siku tisini na udongo unaozalishwa unakuwa tayari unaweza kutumika kwa ajili ya kilimo rununu. Mbunifu huyu anasema udongo unaozalishwa huutumia yeye mwenye kwa ajili ya kilimo. 

Pia, huwauzia wengine wanaouhitaji kwa ajili ya kufanyia kilimo rununu, ambapo huuza kilo moja kwa Shilingi 2,500. Mnunuzi anaweza kutembelea karakana ya Mchau External, jijini Dar es Salaam, au kumpigia simu kupitia +255 712 507 214.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts