Hakuna namna Rais Samia Suluhu Hassan angeweza kuendeleza pande mbili kwenye namna anavyoendesha Serikali yake, akisema hivi lakini akitenda vile, akiwafanyia hivi Watanzania na kuonesha vile washirika wa kimataifa wa maendeleo ya Tanzania, kama vile wahisani na mashirika mengine ya kidunia.
Msimamo huo ambao Samia aliuchukua punde tu baada ya kurithi uongozi wa nchi kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, uliohusisha ufanyaji mambo wenye sura mbili, moja kwa ajili ya Watanzania na nyingine kwa ajili ya wahisani, ulionekana usiyowezekana kuendelezwa na ilikuwa ni suala la muda tu kabla ya watu kukishtukia kiini macho hicho.
Rais Samia anajali sana kuhusu haiba yake ya kimataifa, akionekana kuwa na mkakati maalum wa namna ya kuifanya dunia imuangalie kwenye taswira iliyo chanya. Sehemu ya mkakati huu inajumuisha Samia kuzungumza lugha ambayo wakubwa wa dunia wanapenda kuisikia, ikiwemo ile ya kukuza demokrasia na haki za binadamu; mapambano dhidi ya rushwa; usawa wa kijinsia; na masuala ya tabia nchi, ikiwemo matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akiwa na bahati ya kutanguliwa na kiongozi ambaye kwenye macho ya wengi alionekana kutokujali sana kuhusiana na mambo haya na namna dunia inavyomuangalia kuhusu misimamo yake hiyo, Samia alionekana kudhamiria kutorudia ‘makosa’ hayo ya Magufuli kwa kuhakikisha anashiriki kikamilifu kwenye majukwaa makubwa ya kidunia, akitoa mchango wake wa mawazo kwenye mada anuwai zinazojadiliwa kwenye majukwaa hayo.
Ushiriki
Miongoni mwa majukwaa machache ambayo Samia ameshiriki, na ambayo yanahusiana na lengo la safu hii, ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambao kiongozi huyo mkuu wa nchi wa kwanza mwanamke nchini aliihutubia hapo Septemba 23, 2021, miezi sita tu baada ya kuchukua hatamu za uongozi.
SOMA ZAIDI: CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi
Pamoja na mambo mengine, Samia alieleza kwamba anaelewa uhusiano uliopo kati ya ukuaji wa uchumi na utawala bora, akijivunia demokrasia aliyodai inashamiri Tanzania, pamoja na utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu, na kudhamiria kuviendeleza.
Mnamo Julai 1, 2022, kama sehemu ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, Rais Samia alichapisha maoni kwenye gazeti la Serikali la Daily News, ambapo, pamoja na mambo mengine, alielezea dhamira yake ya ujenzi wa Tanzania kwenye misingi ya maridhiano na maelewano, akisema analenga kuchukua hatua zitakazoimarisha ushindani kwenye chaguzi kwani demokrasia ni nyenzo muhimu za kujenga taifa analoliota.
Machi 23, 2023, pia, Rais Samia aliuhutubia Mkutano wa Demokrasia unaoandaliwa na Serikali ya Marekani ambapo alizungumza kwa kirefu kuhusu umuhimu wa demokrasia na mipango aliyonayo kwa ajili ya Tanzania. Mipango hiyo, Samia alisema, ni pamoja na kuirejesha Tanzania ndani ya mpango wa Open Government Partneship ambako mtangulizi wake alijitoa. Mpaka sasa hajafanya hivyo!
Lakini kuidhihirishia hadhira yake lengwa kwamba anamaanisha anachokisema, Rais Samia alichukua hatua kadhaa zilizowaaminisha hata baadhi ya mahasimu wake ndani ya nchi kwamba kweli ana nia ya kuitoa Tanzania gizani na kuiweka kwenye mwanga.
Mageuzi
Kwa mfano, Samia aliunda kikosi kazi kupata maoni ya wadau juu ya namna ya kuboresha demokrasia ya vyama vingi nchini na kuunda tume maalumu ya kuchunguza changamoto za utoaji na upatikanaji wa haki jinai nchini.
SOMA ZAIDI: Labda Suluhu ya Serikali Kudharau Maoni ya Wananchi ni Kuacha Kushirikiana Nayo?
Samia aliondoa zuio lililowekwa na mtangulizi wake dhidi ya mikutano ya hadhara na kufungulia vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa, na hata kuifanyia ‘maboresho’ sheria iliyokuwa inalalamikiwa ya huduma za habari ya mwaka 2016. Hatua hizi na nyingine zikazidi kumpatia sifa Samia kimataifa mpaka kumvutia Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris kutembelea Tanzania Machi 30, 2023.
Lakini Samia siyo Rais wa Tanzania tu bali pia mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), chama tawala kilichodhamiria kubaki madarakani kwa muda mrefu zaidi kadiri inavyowezekana, na Samia mwenyewe akitegemewa kukiwakilisha kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Ukweli huu umekuwa ukimpa changamoto Samia juu ya namna ya kuweka katika mizania dhamira yake ya kutaka dunia imchukulie kama mwanamageuzi na ile ya kukihakikishia chama chake, na yeye mwenyewe kusema kweli, ushindi kwenye chaguzi.
Dhamira mbili hizi za kiongozi huyu zinakinzana sana kwani hakuna mageuzi ya maana ambayo dunia inamtegemea Samia kuyatekeleza ili kuboresha demokrasia ya vyama vingi nchini ambayo yataiacha CCM kuwa na uhakika usiohojiwa wa kuendelea kubaki madarakani. Chaguo ni moja tu, tufanye mageuzi kupanua demokrasia au tuzidishe uimla CCM iendelee kubaki madarakani.
Maneno dhidi ya vitendo
Mwanzoni, Rais Samia alionekana kukusudia kukabiliana na changamoto hii kwa kuukita mpango wake wa mageuzi zaidi kwenye maneno kuliko vitendo, yaani alikuwa anazungumza mageuzi bila kufanya mageuzi yoyote. Imedhihirika hivyo kwenye kwenye kile Serikali imekifanya kama utekelezaji wa maoni ya kikosi kazi ambacho wadau wamekipanga, wakisema sicho walichokubaliana kutekelezwa.
SOMA ZAIDI: Bila Uhuru, Vyombo vya Habari Vitaendelea Kubaki Kuwa Midomo ya Serikali
Imetokea hivyo pia kwenye yale yanayoitwa maboresho kwenye Sheria ya Huduma za Habari, 2016, ambayo wadau pia wameyapinga, wakisema hayawakilishi kile walichokubaliana na wizara yenye dhamana. Kwenye haki jinai, Serikali mpaka hivi sasa haijaeleza utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na tume utaanza lini ili kurekebisha kasoro zilizoibuliwa.
Lakini joto la uchaguzi likiendelea kupanda, Samia ameona kwamba mkakati wake huo hauwezi kumvusha yeye na chama chake kwenye uchaguzi unaokuja, na kwamba hawezi tena kujifanya amedhamiria mageuzi wakati upepo unaonekana kwenda dhidi yake. Hali ngumu ya maisha, kukithiri kwa vitendo vya rusha na ufisadi Serikalini, na hali tete ya usalama wa raia ni vitu vichache vinavyoweza kumugharimu Samia kwenye uchaguzi.
Mbinu za kale
Kwa hiyo, Rais Samia na Serikali yake wameamua kurudia mbinu zilizokuwa zikitumiwa na mtangulizi wake kushughulika na wakosoaji wake na vyama vya upinzani, hali inayomaliza ukinzani uliokuwepo kati ya lugha yake na vitendo vyake kuhusu mchakato wa ‘mageuzi.’
Moja ya mbinu hizi ambayo utekelezwaji wake unaonekana kushamiri hivi sasa ni kupotezwa kwa wakosoaji wa Serikali ya Rais Samia ambapo watu wanafuatwa nyumbani kwao na watu wanaojitambulisha kama polisi na kutoweka na kutokuonekana kabisa au kuonekana baada ya siku kadhaa kupita wakiwa katika hali zisizoridhisha.
Taarifa hizi zimekuwa zikisambaa sana kwa siku za hivi karibuni, huku polisi wakidaiwa kuhusika na vitendo hivyo. Polisi wanadai hawahusiki, lakini kwenye baadhi ya kesi wameonekana kujitokeza hadharani kudai kumshikilia mtu ambaye kwa siku kadhaa wamekuwa wakidai kutokomshikilia pale ndugu zake wakimtafuta kwenye vituo mbalimbali vya polisi.
SOMA ZAIDI: Pengine ni Kweli Polisi Hawahusiki na Utekaji. Lakini Mbona Hatuoni Watekaji Wakikamatwa?
Lakini kama kuna tukio lolote linalodhihirisha mwisho wa kiini macho cha mageuzi Samia amekuwa akikifanya ni hili la kukamatwa kwa viongozi na wanachama 520 wa CHADEMA, wakiteshwa na kusulubiwa kwa maagizo ya maafisa waandamizi wa polisi, huku uhalifu wao pekee ukiwa ni kutaka kuungana na watu wengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Vijana!
Polisi wanadai eti kulikuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani kwenye kongamano hilo lililokuwa lifanyike mjini Mbeya hapo Agosti 12, 2024, lakini wameshindwa kuelezea ulazima wa maafisa wake kutumia nguvu zilizopitiliza kukabiliana na viongozi na wanachama wa CHADEMA ambao hawakuwa wakitoa ukinzani wowote dhidi ya katazo la mkutano huo.
Hakuna mashaka
Ingawaje tangu mwanzo Serikali imeonekana ikichukua hatua zinazokinzana na lugha ya mageuzi na haki za binadamu inayosemwa na Rais Samia, kama vile ukiukwaji mkubwa haki za binadamu dhidi ya watu wa jamii ya Kimasai na jamii zingine zinazopakana na hifadhi za taifa, ni maoni yangu kwamba ukatili dhidi ya watu wa CHADEMA unaondoa mashaka yoyote yaliyokuwepo kama kweli Samia anamaanisha anachokisema au anahadaa tu watu.
Baadhi yetu tulikuwa tunajua toka zamani kwamba mageuzi yanayoahidiwa na Samia ni kiini macho tu na kwamba Serikali ya CCM haiwezi kutekeleza mageuzi yoyote yatakayotishia uwepo wake madarakani. Labda sasa ni zamu ya wengine kufumbua macho yao na kuanza kuukabili ukweli huu mchungu.
Mbali na baadhi ya wananchi wenzetu, watakaopaswa kufikia hitimisho hilo pia ni pamoja na wakubwa wengine wa dunia, hadhira lengwa ya lugha ya mageuzi ya Rais Samia, wanaotoa mikopo, misaada na ruzuku nyingine mbalimbali baada ya kushawishika na lugha tamu ya mageuzi inayoongelewa na Serikali ya awamu ya sita.
Swali linalobaki kuulizwa ni je, watafanya hivyo, na hata wakifanya, hatua hiyo itamaanisha nini kwenye vuguvugu zima la ujenzi wa taifa jipya la Tanzania, lenye taasisi imara za kidemokrasia zinazoweza kuhakikisha maendeleo ya wote na endelevu, ulinzi wa haki muhimu za kila raia, na ambalo viongozi wanawajibika kwa wananchi?
Hii inaweza kuwa mada ya safu nyingine zinazokuja!
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
2 responses
Duh
Kwa kweli hali ni ngumu sana. Bima ya Afya iliyoboreshwa ICHF ikitusaidia sana wananchi wenye kipato cha chini. Ukitoa 2000/ kwa wakala inabidi uee na 2400!
400 ni makato! Kila kitu kwa mfanya biashara ndogondogo imekuwa X!
AlHaamduliLLAHI 🤲🏼 AHimidiwe MwenyeEnziMunguMlezi Milele na Milele. TunShukuru kwa yote. MwenyeEnziMunguMlezi AtuSimamie 💔🇹🇿😱