The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kiini cha Maandamano ya 18-08 ya Wamasai wa Ngorongoro

Maandamano haya yanakuja wakati ambapo serikali ikendelea na mpango wake wa kuwahamisha Wamasai zaidi ya 110,000 kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, Sauni, na Kitwai zaidi ya kilomita 300 kutoka makazi yao ya sasa. 

subscribe to our newsletter!

Jumapili, Agosti 18, 2024, mamia ya wanajamii wa Kimasai—wanaume, wanawake, na vijana waliandamana  kupinga kunyimwa huduma za msingi, ubaguzi, na haki ya kuishi katika ardhi ya Ngorongoro, mahali wanapopafahamu kama makazi yao ya asili.

Wakiwa wamevaa mavazi yao ya kitamaduni ya rangi nyekundu  huku wakibeba  majani kama ishara ya amani, waandamanaji walifunga barabara yenye shughuli nyingi ya Ngorongoro-Serengeti. Waandamanaji hao walitumia muda mwingi kulia, kuomba sala kwa kimasai, kuimba nyimbo za pamoja huku wakionesha mabango mbalimbali yenye kuonesha hisia zao

Sehemu ya Wamasai wakiwa katika maandamano

Maandamano haya yanakuja wakati ambapo serikali ikendelea na mpango wake wa kuwahamisha Wamasai zaidi ya 110,000 kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, Sauni, na Kitwai zaidi ya kilomita 300 kutoka makazi yao ya sasa.  Serikali inaeleza kuwa uhamisho huo ni muhimu kwa ajili ya kuhifadhi Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, ambalo ni sehemu ya Urithi wa Dunia wa UNESCO.

Pamoja na kuwa serikali imeendelea kusisitiza kuwa zaoezi la uhamisho ni hiari, Waziri wa Maliasili na Utalii mnamo Juni 22,2022, pamoja na Msemaji wa Serikali Mnamo Disemba 02,2023, walieleza kuwa serikali inapanga kuja na sheria itakayofuta hali ya sasa inayoruhusu makazi ya watu ndani ya Ngorongoro.

Ili kuvutia wakazi wengi kuhama kwa hiari serikali imeendelea kujenga nyumba wanazopewa bure watu wanaohama, ikiwa ni pamoja na kupewa usafiri wa kutoka Ngorongoro mpaka Msomera. Hadi kufikia Aprili 2024, serikali iliripoti kutumia Tsh. bilioni 286 katika juhudi za uhamisho huo, ambapo takriban wakazi 8,364 wamehamishwa tangu Julai 2022. 

Wamasai wakiwa wamebeba mabango mbalimbalia yenye jumbe

Hata hivyo, Wamasai wengi waliobaki Ngorongoro wameeleza wasiwasi wao kuhusu vitendo vya kibaguzi, ikiwa ni pamoja na takwa la kuwa na  vibali maalum vya kuingia na kutoka Ngorongoro. Wakazi pia wamelalamikia kuondolewa kwa huduma muhimu kama vile elimu na afya, ambapo fedha zinaripotiwa kuelekezwa Msomera. Mbunge wa Ngorongoro na mashirika ya haki za binadamu wamethibitisha kuwa sehemu kubwa ya fedha za maendeleo na huduma za jamii zimeendelea kuondolewa Ngorongoro.

Haki ya Kupiga Kura

Ingawa kunyimwa huduma za msingi limekuwa suala linalolalamikiwa  kwa muda mrefu, kichocheo kikubwa cha maandamano ya leo inaonekana ni madai kwamba wakazi hawa wamepokonywa haki yao ya kupiga kura ndani ya Ngorongoro.

Tarehe 3 Agosti 2024, baadhi ya viongozi na wakazi wa Ngorongoro walifanya mkutano na waandishi wa habari, wakidai kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imehamisha majina ya wapiga kura kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, eneo ambalo ni asilimia 2 tu ya wakazi wa Ngorongoro wamehamia. 

“Tumeshangaa na kusikitishwa kwamba Tarafa nzima ya Ngorongoro ambayo imebaki na wakazi 110,000 hatutapiga kura kwenye vituo vyetu ndio maana tumekuja kupaza sauti,” alieleza James Moringe Mollel, Diwani wa Loitile. “Walisema uhamisho ni hiari, lakini mfano mimi nimepangiwa kitongoji sijui kinaitwaje Msomera kama sehemu ya kuigia kura.Ni jambo la uonevu, ni jambo la kusikitisha.” 

“Katika listi iliyotolewa Tarafa ya Ngorongoro yenye kata 11 na vijiji 25 hawapo, kwenye mfumo tulivyofuatilia mfano mimi nilivyosimama kadi yangu inaonesha Napiga kura katika kituo cha Msomera B, eneo ambalo sijawahi fika,  hata tunapozungumza usalama wetu ni mdogo tunawindwa,tunanyanyaswa,” aligusia pia Sabore Ngarusi Mwenyekiti wa Kijiji cha Bulati.

” Tumenyanyapaliwa,tumepuuzwa,ikifikia kiasi cha kunyima haki ya kuchagua kiongozi ni zaidi ya manyanyaso. Nadhani kuna kisasi, kuna kitu ambacho tumeikosea serikali haijasema. Nimepangiwa kituo cha Afya Msomera, msomera mimi sijawahi kufika imetokea wapi hiyo, huduma za msingi hatupati, kwa sababu gani?”aliongeza Moses Oleseki, mkazi wa Enduleni. 

Tarehe 6 Agosti 2024,  The Chanzo lilimtafuta Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele, ambaye alisema hakuwa amepokea malalamiko yoyote lakini aliahidi kuongea na Mkurugenzi Mtendaji wa INEC kuhusu suala hilo. The Chanzo ilijulishwa kuwa INEC itatoa taarifa rasmi kufafanua suala hilo, taarifa ambayo bado haijatolewa.

Foleni ya magari ya watalii kutokana na maandamano hayo

Agosti 10, 2024, The Chanzo lilimtafuta Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai, ambaye alieleza kuwa bado anaendelea mazungumzo na serikali na kama akiwa na taarifa rasmi ya kuzungumza juu ya jambo hilo ataliongelea.

Katika taarifa yeke leo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imeleza kuwa shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida na serikali itaendelea kuhakikisha usalama wa wageni wanaofika hifadhini.

“Maandamano yaliyoripotiwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii yanaidhihirishia dunia na jumuiya za kimataifa, vyombo vya habari na asasi za kimtaifa kwamba ndani ya hifadhi hiyo hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi,” inaeleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uhusiano kwa Umma, Hamis Dambaya.

NCAA ni moja ya vyanzo vikubwa vya mapato ya utalii nchini Tanzania. Mwaka 2023, watalii 843,473 walitembelea eneo hilo, wakiwemo watalii wa kigeni 515,961, na kuzalisha Sh. Bilioni 195.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *