Kama wazazi tunaothamini safari zetu za malezi, ni vyema kujitathmini kama tunawalea watoto wetu kwa njia zilizo sahihi.
Kama wanapata mahitaji yao yote – kimwili, kihisia, na kiakili. Kama watoto wetu wanafuraha. Kama kuna vitu ambavyo tunaweza kufanya ili watoto wetu wakue katika hali ya usalama na ustawi ulio bora na pia kama sisi wenyewe ni wazazi bora.
Ukweli ni kwamba hakuna njia moja iliyo sahihi ya kulea watoto, lakini kuna mwongozo ambao wataalamu wa malezi wanashauri unaweza kutusaidia kuwa wazazi bora zaidi. Kwa mfano, wataalamu wanakubaliana kwamba mzazi bora anafahamu kuwa kuna kuteleza na kukosea katika malezi, hivyo anaendelea kujifunza.
Mzazi bora pia anawasikiliza watoto wake, anajadiliana nao, na kuwawezesha kutumia sauti zao. Tunapowatengenezea watoto wetu mazingira ya kuwasiliana na sisi kwa uhuru, tunawajengea ujasiri na uwezo wa kueleza mawazo yao siyo kwetu tu wazazi bali pia kwa marafiki zao, kwa walimu shuleni na kwa watu wanaowazunguka.
Hii inawasaidia watoto kutokuonewa na kurubuniwa kwa urahisi kwa sababu wanaweza kutafakari matendo wanayotendewa na kujitetea au kufanya maamuzi sahihi. Wataalamu wanasema, “Ikiwa mtoto wako anakuogopa, hawezi kukuamini, ikiwa hakuamini, hawezi kujifunza kutoka kwako.”
SOMA ZAIDI: Tunachoweza Kufanya Wazazi Kuwanusuru Watoto Wetu na Matatizo ya Afya ya Akili
Mzazi bora anafahamu kwamba anaweza kuwa mlezi kamili kwa mtoto. Tafiti zinaonyesha kuwa watoto wanaolelewa na wazazi wanaojihusisha kikamilifu katika malezi wana uwezekano mkubwa wa kufaulu kimasomo na kuwa na afya bora ya kiakili.
Hii ina maana ya kwamba wazazi tunahitaji kujihusisha na maisha ya watoto wetu, siyo kuwafuatilia sana mpaka tuzidi mipaka, lakini tujue watoto wetu wanapitia nini katika maisha yao ya kila siku.
Tuwafahamu marafiki zao, wapi huwa wanaenda kucheza, vitu gani wanapenda na vitu gani hawapendi pamoja na masomo wanayoyapenda na ambayo hawapendi, na kwa nini.
Mzazi bora anashiriki katika shughuli za malezi ya watoto sawa na mwenza wake. Uwiano katika majukumu ya malezi hutusaidia kupunguza mzigo kwa mzazi mmoja, na pia huleta utulivu na ushirikiano ndani ya familia. Familia ambazo wazazi wote wawili wanashiriki kwa usawa katika malezi zina viwango vya chini vya migogoro ya kifamilia.
Ina maana kwamba kama baba, au mama, tunahitaji kugawana majukumu ya malezi kwasababu mtoto sio wa mzazi mmoja.
SOMA ZAIDI: Sababu za Kukupa Wasiwasi Juu ya Msichana wa Kazi Nyumbani
Mzazi bora pia anawajengea watoto wake uwezo wa kutekeleza majukumu ya kazi za nyumbani bila kujali mipaka ya kijinsia. Kuwafundisha watoto wetu kwamba kazi zote ni za wote, bila kujali jinsia, kunawajenga kuwa watu wenye fikra za usawa na haki.
Mazoea ya kwamba kazi za kupika na kufanya usafi ni kazi za jinsia moja tu hayajengi. Watoto wetu wa kike na wa kiume wanahitaji kufahamu namna za kujihudumia na hii huanza kwa kujifunza vile vitu vya msingi kama kupika na kufanya usafi wa nyumbani na mazingira.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kijinsia (TGNP), asilimia 76 ya wazazi nchini Tanzania tumeanza kuelewa umuhimu wa kugawa majukumu ya nyumbani kwa usawa kwa watoto wa kiume na wa kike.
Mzazi bora anajenga heshima na upendo kwa watoto bila kutumia nguvu au umangi-meza. Hii ina maana kwamba, tuwalee watoto wetu kwa upendo na heshima ili wao pia watupende na kutuheshimu, sio kwa mamlaka ambayo tunayo juu yao lakini kwa sababu wanatambua thamani yao kwetu na sisi tunawathamini pia.
Kuna mambo mengi katika suala hili lakini, tuseme kwamba, mzazi bora ni yule anayejituma kutimiza wajibu wake kama mzazi.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Umuhimu wa Malezi Mazuri Kwa Watoto Wetu?
Wote tunaweza kuwa wazazi bora kama tukijitahidi kadri ya uwezo wetu kufanya vitu vilivyozungumzwa hapo juu na kuishi maisha yanayowapa usalama, upendo, na yanayowajengea mazingira ya kufikia uwezo wao kamili.
Mwisho kabisa, mzazi bora ni yule anayeishi kuwa mfano wa kuigwa kwa watoto wake!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.