The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Sababu za Kukupa Wasiwasi Juu ya Msichana wa Kazi Nyumbani

Si rahisi kujua kama mlezi wa mtoto wako, yaani msaidizi wa kazi za nyumbani, anafanya kazi yake ipasavyo. Lakini inawezekana.

subscribe to our newsletter!

Mara nyingi, si rahisi kujua kama mlezi wa mtoto wako, yaani msaidizi wa kazi za nyumbani, anafanya kazi yake ipasavyo. Ili kubaini hili, baadhi ya wazazi huenda mbali hadi kuweka vifaa vya kurekodi matukio nyumbani wawapo kazini, au nje ya nyumbani. 

Lakini inawezekana kugundua tabia zisizofaa za msaidizi wako wa nyumbani pasi na kuwekeza katika virekodi matukio. Namna moja inayoweza kutusaidia kufanikisha hilo ni kuangalia namna mtoto anavyohusiana na dada wa kazi, ambapo kama anaonekana kumuogopa na hana raha kama unavyomfahamu, basi fahamu kuna tatizo. 

Ingawa ni kweli kwamba watoto huhitaji muda kumzoea mlezi mpya, mathalani mtoto analia pale unapomuaga akitaka muandamane, na kadhalika, iwapo mtoto ataendelea na uoga huu na kupoteza furaha kwa muda mrefu, wazazi na walezi tunahitajika kulitazama hili badiliko kwa jicho la pili.

Msaidizi wa kazi za nyumbani kamwe hawezi kuchukua nafasi ya mama au baba, lakini mtoto anahitaji kujisikia vizuri awapo naye. Labda mtoto na mlezi hawapendani, au msaidizi hajafanya jitihada yoyote kumwonyesha mapenzi mtoto. Mhimili mkuu katika kila uhusiano wa binadamu, ni kupendana.

Dalili nyingine ni pale binti wa kazi za nyumbani anaonekana msiri kuhusu kazi zake za kila siku. Hapana haja ya kuficha namna mtoto na mlezi wake wanavyoishi tukiwa hatupo. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Tunasisitiza Umuhimu wa Malezi Mazuri Kwa Watoto Wetu?

Wazazi na walezi tunahitaji kujua walifanya nini siku hiyo? Muda wao umetumikaje? Siku yao ilikuwaje? Tunapofika nyumbani tunahamu ya kujua juu ya haya na kama hutuambiwi basi labda wasaidizi wetu hawana kawaida ya kuwasiliana na sisi au lipo jambo si zuri hataki tujue. Tuwaeleze wajue kwa nini ni muhimu sisi kuzijua changamoto za kumlea mtoto.

Kingine cha kuangalia ni kama mtoto anapata ajali nyingi mno zinazoepukika kirahisi kila uchao. Binti msaidizi wa kazi lazima aweke jicho lake juu ya mtoto, na kujua anachokifanya wakati wote ili kumsaidia kuepuka kupata majeraha yanayoweza kuzuilika. Yawezekana humuacha mtoto kutwa acheze bila uangalizi.

Au tumegundua hafuati msaidizi wa kazi hafuati maelekezo yetu. Sote tunashirikiana kumlea mtoto na si vyema wasaidizi wetu kujidai wanajua kumlea mtoto zaidi yetu.

Muhimu, kunatakiwa kuwepo na timu. Hivyo, wazazi tunapaswa kukubali ushauri mzuri toka kwa wasaidizi kwani wao hukaa na mtoto kutwa nzima. Lakini iwapo tunapata hisia kwamba mzazi hakubaliani na dada wa kazi, hasa yanapokuja masuala ya msingi kama lishe, muda wa kulala, usalama wa mtoto, uhusiano hautadumu kwa muda mrefu. 

Tutafuta mtu ambaye anajua ana ari na nia ya kujifunza kadiri tunavyomwelekeza, afuate mahitaji yetu. Visingizio vya utoro kazini na uchelewaji uso-maelezo ya kuridhisha ni dalili za kutoipenda kazi yake.

SOMA ZAIDI: Njia Saba Wazazi Tunaweza Kupita Kufanikisha Uadabishaji Chanya kwa Watoto

Kitu kingine cha kuangalia ni kama mtoto anaonekana ‘rafu’ na mchafumchafu isivyo kawaida. Kawaida watoto watachafuka kutoka michezo mbalimbali kutwa nzima, lakini kama mtoto mara zote tunamkuta na mabaki ya chakula cha mchana vidoleni, au daima anahitaji kubadilishwa nguo mara anapotulaki toka kazini, lipo tatizo. 

Kama binti msaidizi hawezi kushughulikia mahitaji madogo-madogo ya msingi kwa mtoto, hafai kuendelea kuwepo kazini.

Au visa vyake si vya kweli. Kamwe tusimvumilie mtu anayeiba, muongo, na asiyeisha vitimbi vya uongo-uongo. Lazima tuwe na uwezo wa kumwamini binti msaidizi, vinginevyo tutamwachia vipi jukumu la kumlea mtoto?

Kingine cha kuangalia ni kama mara zote mtoto ana njaa na uchovu. Tunaporudi kazini, tujaribu kumpa mtoto chakula na iwapo anakula kama vile hajala kutwa nzima ama kachoka kupita kiasi, hii ni hatari. Yawezekana mlezi hampi chakula na hampi muda wa kupumzika mchana.

Kingine ni endapo kama wazazi tuna mashaka na msaidizi anavyolea. Mara zote tuwapo na hisia au mashaka ya namna mtoto anavyolelewa, tuziheshimu na kuzitii hisia hizo kwa kutafuta msaidizi mwingine.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *