The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Njia Saba Wazazi Tunaweza Kupita Kufanikisha Uadabishaji Chanya kwa Watoto

Malezi hayatakiwi kuwa mapambano bali maelekezo yenye maelewano na maskilizano kati ya mtoto na mzazi.

subscribe to our newsletter!

Kila mzazi anapokuwa na mtoto, anakuwa na matarajio chanya juu yake. Kutokana na matarajio hayo, wazazi wengi katika kutekeleza jukumu la malezi hupenda kuwaambia watoto “fanya nitakavyo na si fanya nifanyavyo.”

Tambua kwamba umeingia katika ulingo wa uadabishaji ambapo huwa hakuna mshindi bali maumivu kama ayapatayo mwanamasumbwi yeyote, kuambulia kiu, kupandwa na presha, na kadhalika.

Kumbuka malezi hayatakiwi kuwa mapambano bali maelekezo yenye maelewano na maskilizano kati ya mtoto na mzazi. Uadabishaji chanya humfundisha mtoto kutambua kuwa anaweza na ataweza kuwa na adabu bila vitisho, hongo –vijizawadi–, kukaripiwa na kutiwa masingi ya kichwa, mateke, ngumi na viboko.

Tafiti za malezi zinasema, watoto hupenda kuwa na tabia njema na mwenendo mwema endapo hakuna sababu ya msingi ya kumpelekea kufanya mambo yasiyofaa, kama vile kukosa adabu. 

Kutokana na hili, ni vyema wazazi tutambue kuwa kitu muhimu ni kufahamu kuwa chochote afanyacho mtoto kikawa si cha kupendeza machoni mwetu, tusikimbilie kuwahukumu; ukweli ni kwamba mtoto anajitahidi kadri ya uwezo wake. 

SOMA ZAIDI: Fanya Hivi Kujenga Mahusiano Bora na Mfanyakazi wa Nyumbani

Badala yake, tujaribu kudadisi kwa nini mtoto anafanya hayo afanyayo. Punde tukigundua sababu ya msingi, ni rahisi kumsaidia kuepukana na makosa, kupambanua madhara na kuachana na makosa ama tabia zisizofaa moja kwa moja.

Tuzingatie hisia zetu. Ni vigumu kuwa mpole pale mtoto anapokosea au mtu anapokuudhi, lakini wataalamu wa malezi wanashauri kuwa wazazi wanapaswa kuziishi tabia na matendo amabayo wangependa watoto wao wawe nazo au watende. 

Kumbuka, tukiwa wapigaji na wfokaji, mtoto huiga mambo hayohayo. Kama hasira zimetujaa sana, tuondoke eneo la tukio hadi pale tutakapoona hasira zimeshuka. 

Hatusemi usimuadhibu mtoto pale anapokosea. La hasha! Ila, tujitahidi kutoa adhabu baada ya hisia za hasira kali kutulia, tusijemuumiza mtoto, ama kumpa adhabu kubwa mno isiyoendana na kosa. Ikumbukwe kuwa lengo la adhabu ni kumfundisha kutambua makosa ili asirudie, siyo kumuumiza kutokana na hasira.

Tusiyumbe katika matarajio yetu kwa watoto wetu. Wataalamu wa malezi wanaeleza kuwa mara nyingi wazazi huwa hawazitilii maanani baadhi ya tabia hasi, wakiamini zitaisha zenyewe kadri muda unavyokwenda, lakini ukweli ni kwamba haziishi. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Baba Anapaswa Kumsindikiza Mama Kliniki Kipindi cha Ujauzito?

Ni vyema kukemea kila tabia isiyopendeza. Kwa mfano, kama mtoto anapenda kupiga au kung’ata wenzie, usidharau tabia hii, mshike mkono taratibu na mueleze kuwa tabia hiyo haifai. Akirudia basi ni muda muafaka wa kumsaidia kuondokana na hali hiyo. 

Wakati mwingine mtoto anaweza kufanya kusudi kujaribu mipaka ya kanuni zako, inashauriwa tusilegeze kamba, turudie kanuni yetu ilele mara nyingi tuwezavyo ili watoto watuelewe – tunaweza kurahisisha mjadala kwa kusema ‘nakupenda sana mwanangu nisingependa kurudia sana katazo hili.’

Tusifie tabia tunayoipenda—na kuikandia tusiyoipenda. Mara nyingi watoto hufanya jambo kuvuta uwepo wetu wazazi, itatusaidia tukimpotezea kwa tabia zisizofaa, kwa tabia kama gadhabu na makelele ya makusudi, tufanye kama hatumuoni au tuondoke sehemu ya tukio, mtoto atajifunza kuwa kuna namna nyingine bora ya kuwasiliana na si makelele.

Tusichoke kumuelekeza mtoto. Watoto ambao husikia neno “usifanye hivi/vile”, “acha” hupenda kurudia kosa kutujaribu kama unamaanisha unachokisema. 

Kwa mfano, mtoto anependa kulia makusudi unapomtengea mgeni chakula, kuomba hela kwa wageni, au kuwarukia rukia wageni na kufanya fujo, usichoke; tumuelekeze mara nyingi tuwezavyo kwa kujaribu kumtafutia kitu mbadala cha kufanya ili aachane na tabia isiyofaa.

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwafanya Watoto Wetu Wapende Kunywa Maji?

Tusimlaghai mtoto kwa zawadi. Inaweza kuwa ni vigumu kuepuka kumpa au kumnunulia mtoto chochote kile pale anaposhindwa kutulia wakati tuna maongezi muhimu ama tunapoona kitu mfano mkiwa kwenye gari binafsi ama daladala akaaanza kulilia vitu ili anunuliwe. 

Inashuriwa kuwa ni vyema zaidi kumtuliza kwa maelezo ya kwa nini hawezi pata kitu fulani kwa wakati huo. Kumpatia kila atakacho pale afanyapo fujo kidogo kutamjengea dhana ya kwamba hawezi kuwa na tabia nzuri mpaka alaghaiwe. Inabidi ajifunze tabia kwa kuelekezwa kwa maneno ili ayatilie maanani maneno ya mzazi na ajifunze.

Muda wa mzazi ndiyo zawadi kubwa na ya muhimu kuliko zote kwa mtoto. Tuwe na muda wa kukaa na watoto wetu tuzungumze. 

Inashauriwa kuwa na angalau dakika 15 na watoto wetu kila siku ili kuimarisha uhusiano na upendo na kujenga misingi ya kusikilizana, na mzazai kupata mwanya wa kumjengea mtoto tabia njema. 

Hizi dakika tuzitumie kumtizama mtoto machoni moja kwa moja tunapozungumza, tumnong’oneze kuwa unampenda, tucheze nae; turuke, tukimbie, tuchore, na kadhalika, hii ni moja ya uwekezaji bora tunaoweza kujivunia maishani.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *