Wakati fulani, Shirikisho la Soka (TFF) lililiomba Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) litume maofisa wake ili kuja kuangalia mifumo yetu, katiba, kanuni na uendeshaji wa soka na kutushauri cha kufanya ili mpira wetu wa miguu uende mbele.
Baada ya kupitia nyaraka zote hizo na kuongea na wadau, maofisa waliona hatuna matatizo katika sheria wala kanuni na kama yapo ni madogo, lakini wakasema tatizo kubwa ni ukosefu wa maadili.
Kwao, hili ndilo tatizo kubwa linalokwamisha mpira wetu kusonga mbele, na ili kuanza kuleta utamaduni wa kuheshimu maadili ndipo TFF ilipounda Kamati ya Maadili kwa ajili ya kushughhulikia matatizo yote ya kimaadili.
Ni kweli kabisa. Mambo mengi yanavyoonekana kwa nje ni tofauti na yalivyo ndani. Usije ukaamini hata siku moja utakapoambiwa timu ya vijana ina wachezaji wote wenye umri chini ya miaka 20. Ni lazima asilimia kubwa watakuwa wameshavuka umri huo.
Mtu wa mpira ni rahisi sana kugeuza msimamo pale atakapopewa fursa, au fedha, na mtu aliyekuwa akimpinga kwa nguvu zote. Mtu wa mpira mwenye nafasi ya juu kiuongozi ni rahisi kwenda kuomba nafasi ya chini ya chombo hichohicho alichokuwa kwenye nafasi ya juu ili mradi tu abakie humohumo au ili mradi kina fedha.
SOMA ZAIDI: Tumeanza Vibaya AFCON 2025 Lakini Hatujuti
Mtu wa mpira ni rahisi kutafuta matokeo nje ya uwanja hata kama alitumia mabilioni kukusanya wachezaji bora kutoka kila kona ya Afrika. Masuala ya wachezaji kusajili timu mbili yalishaanza kupotea, lakini yanaonekana kurudi kwa kasi kwa sababu hakuna uungwana wala maadili kwa wahusika.
Katika dunia ya leo, usingetegemea mchezaji ambaye klabu imeshaingia makubaliano ya kuuzwa kwake, halafu kesho ibadili uamuzi eti kwa sababu wanunuzi wamechelewesha fedha! Katika dunia ya leo, huwezi kutegemea mchezaji abadilishe uamuzi baada ya kusaini makubaliano na klabu inayomtaka.
Ukosefu wa maadili
Suala la Lameck Lawi na Yusuf Kagoma linaonyesha dhahiri jinsi ukosefu wa maadili ulivyokomaa miongoni mwa wachezaji na viongozi.
Lawi, beki wa kati wa Coastal Union, aliuzwa na klabu yake kwa Simba. Lakini viongozi hao wakabadili msimamo, wakidai kuwa klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi ilivunja makubaliano kwa kuchelewesha malipo.
Inaonekana hakukuwepo na sababu za kimpira za kubadili uamuzi, kwamba kulikuwa na mpango wa kumleta beki mwingine wa kati katika muda fulani na kama ingeshindikana, basi wangeamua kubaki naye. Kinachoonekana ni kuibuka kwa nafasi nyingine kwa mchezaji kwenda kucheza soka Ubelgiji.
SOMA ZAIDI: Ubashiri Hatma ya Samatta Stars Haukutakiwa Kuwepo
Bado hiyo nafasi angeweza kuipata akiwa Simba, lakini viongozi wa Coastal ni kama waliona wangepoteza fursa kubwa ya kutengeneza fedha zaidi ya zile ambazo wangepata Simba.
Wakaamua kubadilisha uamuzi na kumpa nafasi aende Ubelgiji kufanya majaribio. Alifeli majaribio hayo. Nafasi nzuri kwake ilikuwa ni kupata uzoefu zaidi Simba, lakini hatapata nafasi hiyo, angalau kwa sasa.
Sakata jingine ni la Kagoma ambaye Yanga wanasema walifanya malipo pamoja na kumsafirisha mchezaji huyo kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam kusaini mkataba na akafanya hivyo.
Siyo mnada
Lakini Simba walipoenda na donge nono zaidi, uungwana ukawatoka na kuamua kufuata donge hilo pamoja na kwamba walishachukua fedha za Yanga. Mchezaji hauzwi kama bidhaa mnadani, kwamba anayekuja na donge nono, ndiye anayeondoka nayo. Ama mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama!
Mchezaji ni bidhaa ambayo ina ubinadamu ndani yake. Ndiyo maana bidhaa ya ubinadamu ina tabia tofauti na bidhaa nyingine za vitu. Kwamba ukiingiza chupa 24 kwa ajili ya kutengeneza soda fulani, zote zitatoka zina kiwango sawa cha maji, sukari na gesi, lakini ukiwaingiza binadamu darasani wakafundishwa na walimu sawa, baadhi watatoka na daraja la kwanza na wengine sifuri.
SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Iondoe Hisia Hasi za Udhamini
Kwa hiyo, biashara ya mchezaji ina tabia tofauti na biashara ya bidhaa nyingine. Ni lazima mchezaji akae chini na wanunuzi, wajadiliane mazingira ya ajira mpya, malipo, posho, nafasi ya kucheza, haki nyingine n ahata utamaduni wa klabu inayomtaka.
Si kila mchezaji bora duniani ni lazima atakiwe na Real Madrid, au Barcelona, au Bayern Munich. Hata Andy Cole alipokuja nchini aliweka bayana kuwa Manchester United hainunui mchezaji kwa sababu ni bora, bali kuna mambo inayoangalia kwa karibu zaidi.
Hawa jamaa wa Singida Fountain Gate na Coastal Union wamechukulia biashara ya wachezaji kama biashara ya bidhaa. Hawajali maadili wala kesho ya wachezaji wao. Wameangalia zaidi pesa nzuri.
Makubaliano ya kiungwana
Unapofanya mazungumzo na klabu nyingine kuhusu kumnunua mchezaji hadi kuiruhusu iende kuzungumza na mchezaji, maana yake mmeshafikia makubaliano ya kiungwana ya kibiashara.
Unapogeuka ghafla, maana yake umepuuza uaminifu uliojenga kwanza kwa sababu fursa kubwa zaidi imetokea. Kiungwana, ni lazima urejee kwenye mazungumzo kuueleza upande wa pili kwamba biashara huenda isifanyike kwa sababu ya vikwazo vilivyoibuka.
SOMA ZAIDI: Olimpiki Itupe Mtazamo Mpya Kwenye Michezo
Kama wanamtaka mchezaji kwa dhati, basi wataongeza dau kwa sababu ndiyo uliowapa kipambele.
Na kama bei ilishapangwa na upande wa pili ukafikia makubaliano, huwezi kuvunja kirahisi kwa barua pepe eti kwa sababu fedha zilichelewa bila ya kuuliza kulikoni.
Huu ni ukosefu wa maadili na unaondoa utu katika biashara ya wachezaji.
Ni afadhali Lawi, lakini unapomsikia Kagoma anathibitisha kuwa alisaini mkataba na Yanga, lakini eti “haukuwa na issue,” unaona kabisa jinsi ukosefu wa maadili ulivyo. Ulisaini vipi nyaraka isiyo na “issue?”
Hukuwekewa bunduki ili usaini. Na hata kama ni makubaliano ya awali, bado yamewekwa kwenye maandishi. Mtu yeyote anayeheshimu maadili, ni lazima aheshimu makubaliano yaliyo kwenye maandishi.
Haya si mambo ya kuendekeza. Ni lazima TFF iyachukulie kwa uzito wake kwa sababu yanaleta utapeli kwenye biashara ya wachezaji, kitu ambacho kinaweza kuharibu kabisa fursa za wachezaji wetu hapo baadaye.
Ni lazima TFF ichukulie jambo hili kwa uzito kama ilivyokuwa hapo awali wakati wachezaji walipokuwa wanapewa adhabu ya kutocheza mwaka mzima. Ni lazima uaminifu urejeshwe kwenye biashara ya wachezaji ili usajili uwe sehemu ya mipango ya timu na si mnada wa wachezaji.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.