Wasifu huu wa Mwenyekiti mstaafu wa ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji, ulisomwa kwenye hafla ya kusherehekea maisha ya mwanamageuzi huyo iliyoandaliwa na chama hicho hapo Septemba 4, 2024, Zanzibar. The Chanzo inauchapisha tena wasifu huo hapa kutokana na mchango wa Juma Duni Haji kwenye siasa za Tanzania. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji:
Si rahisi kwa usiku mmoja kwa mtu yeyote yule kuweza kuandika na kuwasilisha kwa ufasaha wasifu wa mtu, na mtu mwenye ni mwanasiasa, mwalimu, mtu wa watu, mtu mwenye ushawishi, mwenye haiba na ambaye amejaa ndani ya nyoyo za watu aliokuwa sehemu ya kuwaongoza kwa miongo mingi—kupitia siasa, ualimu na uongozi kwa jumla.
Juma Duni, Wazungu husema, amekuwa ni household name hapa kwetu Zanzibar na Tanzania nzima na jina la Babu linamiliki ya brand yake hivi sasa. Ukitaja jina ‘Babu’ katika shughuli inayohusu siasa kwa chinjo au nukta moja basi kinachokuja akilini ni Juma Duni, na jina la ukoo, Duni, humaanisha ni yeye.
Babu Duni ataacha alama kubwa katika historia ya nchi hii, na njia aliopitia hadi leo, kwa hakika, haitaota majani maana itaendelea kupitiwa kwa miaka mingi mno. Na kitendo hiki cha kumuenzi na kumshukuru kwa michango yake kwenye siasa, kitaacha alama kubwa, na wazo hili la kumuenzi, kwa hakika, litakuwa ni halali yake kwa jinsi alivyojitoa na Wazungu husema ni a very self less person na mtu wa watu, yaani man of the people.
Mwaminifu, mpenda haki, mkweli, asiye na kinyongo – siku zote japo amekuwa na kauli thabit na sauti kali na ya kishindo lakini hakuwa na makeke katika utendaji wake wa siasa. Na ndio maana unaweza kumkusanyia Duni sifa za wanasiasa wakubwa duniani, katu hakuwa mjivuni kwa karma kuwa na uwezo wa kujenga hoja, kushawishi na hata kuburura watu kama yule Mpiga Filimbi wa Hamalin.
Uwezo wake wa kushawishi na kujenga hoja. Uwezo wa kuzungumza na kila rika. Uwezo wa jambo gumu kulieleza kwa urahisi. Na akiona mnapotea hukurudisheni katikati ya kilenge kwa msemo wake maarufu wa Ohaaa!
Juma Duni Haji akiwapungia mkono wafuasi wa ACT-Wazalendo baada ya chama hicho cha upinzani kumzawadia gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado TX wakati wa hafla ya kusherehekea na kuenzi mchango wake kwa chama na taifa. PICHA | ACT-WAZALENDO.
Visa na mikasa
Babu Duni ni mtu wa visa na mikasa. Humfaidi mpaka uwe karibu nae. Muda wote, hata katika wakati ambapo hakueleweka, alibaki katika msimamo wake na hakuhitaji kujitetea, bali alijaribu kujenga hoja ili aeleweke. Imekuwa ni vigumu kutomuelewa Babu Duni, na itakuwa wewe ndio hueleweki. Na matukio ya kutoeleweka hayakuwa haba.
SOMA ZAIDI: Juma Duni Haji: Tafsiri ya Mwanasiasa Mnyenyekevu
Kwa mfano, kuna wakati alipata msukosuko akiwa Serikalini kwa kuamuru mchele upelekwe Pemba kwa kuwa kulikuwa na uhababa uliokuwa ukipelekea kuwepo kwa njaa. Na bahati mbaya jahazi moja kupotea.
Alichowaambia wakubwa wake ni kuwa alilazimika kufanya hivyo ili kufanikisha mambo mawili. Kwanza, kuwaokoa wakaazi wa Pemba na njaa kwa vile usafiri wa meli za Serikali ulikuwa na ugumu, lakini pili kuiepusha Serikali na lawama hasa ya kisiasa. Alieleweka!
Maamuzi mengine makubwa aliyoyafanya alipokuwa sekta ya biashara miaka hiyo, na kwa maneno ya mjini na wala hajisifu, ni pale alipomkabili Waziri Kiongozi, hayati Maalim Seif Sharif Hamad, na kumpa fikra kuwa wakati umefika kwa Serikali kuruhusu wafanya biashara na watu wenye fedha waruhusiwe kuleta bidhaa na vyakula.
Na yumkini hii ndiyo ilojenga Sera ya Uwazi wa biashara, yaani liberalisation kwa kimombo, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Pia, alihusika kuikoa Serikali kukwama katika uuzaji wa karafuu alipokuja na fikra ya kubadilishana bidhaa na Serikali kununua magari kwa kubadilishana na karafuu. Magari hayo yalihitajika kuimarisha huduma za kilimo.
Kuna mara kadhaa nyingine Babu Duni alitumia kipawa chake, akichanganya pamoja na nyota ya kuaminiwa kwenda extra mile kutimiza wajibu wake, kama palipokuwa na shida ya maji hospitali ya Mnazi Mmoja na akapiga hodi kwa Bwana Said Salim Bakhressa kwenda kuomba fedha ili atengeze mfumo kuikoa Hospitali hio isiwe kaburi la vifo kwa uchafu.
Na bila ya kuwa anamjua Bakhressa alimuamini na akapewa Shilingi milioni 100, na huwezi kuamini fedha zilizotumika zilikuwa ni Shilingi milioni tano tu! Kiasi kilichobaki kikatumika kununulia dawa.
Au pale aliposimamia kujengwa kitengo cha dharura, ICU, hapo Hospitali ya Mnazi Mmoja na Waziri wa Fedha wakati huo, Omar Yussuf Mzee, alipompiga danadana hata baada ya kauli ndani ya Baraza la Wawakilishi kutoa fedha. Babu Duni alipeleka barua ya kujiuzulu, lakini Maalim Seif akaizuia isimfike Rais. Fedha zikatolewa!
SOMA ZAIDI: Safari Yangu ya Gerezani Bila Kupitia Polisi Wala Mahakamani
Au tukio la Chama cha Wananchi, CUF, kukaribia kushindwa kupata fedha za kufanya Mkutano Mkuu. Ilifika siku Babu alimuelekea Mola wake kwa sala za usiku, na siku ya pili akapata rai iliyopelekea chama hicho kupata Shilingi milioni 300 za mkopo. Na bahati iiyoje, kwa njia zake, Maalim Seif akatia kapuni Shilingi milioni 200 kutunisha na kufanikisha mkutano huo.
Ni rahisi kusema kuwa Duni kwa siasa za Zanzibar, na Tanzania, alikuwa, samhani, amekuwa, ni giant. Kama angekuwa ni mwanamuziki, basi angekuwa maestro, na kama ni kabumbu angekuwa GOAT. Yeye si kamusi ya siasa ile, yaani Thesaurus.
Mambo ambayo ameyafanya wakati mwingine unaweza kusema aliishi maisha zaidi ya mamoja. Ukitizama nafasi ambazo amehudumia na uzoefu aliokusanya unaweza kusema Babu Duni ni chuo cha uongozi.
Misukosuko na misokotano
Historia yake imejaa misukosuko na misokotano, na ukinzani wa mambo kadhaa. Bila shaka, mtoto huyo aliyepata fursa ya kusoma kwa bahati tu kuwa alitakiwa amsindikize jamaa yake, Almarhum Jecha Salim Jecha, kwa kuwa alikuwa ni mdogo zaidi na skuli ilikuwa mbali, na aliyetapia maisha yake kutokana na kuanguka kutoka mpapaini na kuzima kwa dakika kadhaa, kisha akaangukiwa na ndizi iliyoongoka na kuumiza vibaya mwili wake wa kitoto. Alikuwa mtundu mtundu kwa kiasi chake, japo sote utoto wetu ulikuwa na visa na mikasa.
Duni, ambaye alizaliwa kutoka familia masikini, alijua mapambano ya maisha mapema sana kwani alikuwa akibeba sinia ya maandazi ya mama yake ili kutafutwa kijio cha kila siku na kwenda na maandazi hayo mpaka skuli, mengine akapangiwa kuwa ni lunch yake.
Lakini alikuwa hodari na ikawa rahisi kuingia Sekondari huko Gamal Abdul Nasser – Beit El Ras, na kisha Skuli ya Lumumba Darasa la 13 na 14. Na akarudi tena baadaye kusomesha Lumumba na katika watu maarufu aliowasomesha ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamo Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo (Zanzibar), Ismail Jussa na Dk Naufal Kassim, ambaye mchango wake wa utabibu ni mkubwa sana hapa Tanzania, kati ya wengine wengi.
Kwa faida ya vijana wetu, Babu Duni alikuwa mpiga ngozi mzuri na alichezea timu ya Daraja la Kwanza, sawa na ligi kuu ya sasa ya Mwembeladu maarufu kama kubwa lijalo, na alikuwa mkata mawasiliano mzuri sana, pengine kwa sasa Yanga na Simba zingemuwania, lakini naamini angechagua Yanga!
SOMA ZAIDI: Wanasiasa, Wanaharakati Wataka Masheha Wapigiwe Kura Zanzibar
Kama Uingereza angewakataa wajivuni wa Manchester na pia wanaojiita miamba ya London, Arsenal na Liverpool, angechagua New Castle United.
Ni katika kipindi cha masomo yake ya Sekondari ndipo aliposhawishika kuingia katika siasa na kugombea na kushinda uongozi wa Afro-Shirazi Party Youth League na kukulia katika harakati za Mapinduzi na akawa ni muumini mkubwa wa itikadi ya ASP na Mapinduzi ya 1964 kwa sababu yalidhamiria kutetea haki, umoja na mashirikiano na kuundwa kwa Serikali ya Wakwezi na Wakulima. Lakini Duni amekuwa mkosoaji mkubwa wa Mapinduzi kuendewa kinyume.
Babu Duni alibahatika kuwa katika kundi kubwa la Wazanzibari waliopelekwa kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Aboud Jumbe ambapo alikuja na utaratibu wa wazi zaidi wa kuongoza nchi, na alipenda wasomi washike nafasi, kinyume kabisa na Father K, au Rais Abeid Karume.
Kundi lao liikuwa na akina Marehemu Abubakar Khamis, Marehemu Maalim Seif Shariff Hamad, Waziri na Mwanasheria Mkuu Marehemu Idd Pandu Hassan, Balozi Muhammed Mwinyi Mzale, na wengine.
Misimamo
Babu Duni siku zote katika maisha yake amekuwa mtu aliyesimama imara katika misimamo yake katika kundi ambalo yuko pamoja nalo, kama kwenye vyama vya siasa, ambavyo hadi leo ni CUF na ACT na husimamia maamuzi ya pamoja. Aliwahi kukataa ofa ya kupewa ubalozi aliyopewa na mjomba yake Salmin Amour ili awachane na upinzani. Akakataa!
Babu Duni amekaa jela mara mblli. Katika kesi ya uhaini na ya kudaiwa kumuua askari Pemba. Na hilo limemsumbua sana maana hata baba yake alikaa jela kwa madai ya kutaka kumdhuru Rais Karume wa mwanzo kwa njia za kilozi kama wasemavyo Wakongo, yaani kichawi.
Alhamdulillah, Babu Duni amekuwa Mgombea Mwenza mara kadhaa kwa kufuata matakwa ya chama chake hata ilipobidi kuumiza maslahi yake kwa sababu siku zote amekuwa mtii wa chama chake na muumini wa maamuzi ya pamoja.
SOMA ZAIDI: Ni Zipi Fursa, Changamoto za Ukuaji wa ACT-Wazalendo Kama Chama cha Upinzani?
Amekwepa na anakwepa tashwishi kadhaa za kusaliti wenziwe kama vile alivyofuatwa ili ajitangaze kuwa mgombea dhidi ya Maalim Seif wakati wa Rais Benjami William Mkapa na akakataa kwa sababu ya uaminifu unaotembea ndani ya damu yake, na sasa, naamini, hatakubali ushawisi wowote wa kuipa mgongo ACT-Wazalendo maana nafsi yake haitakubali hata kidogo.
Historia ya siasa ya Tanzania itamkumbuka na kumuenzi Babu Duni kwa uamuzi huo, ambao naamini ulikuwa mgumu, lakini aliufanya kwa sababu ACT-Wazalendo siyo imo ndani ya moyo wake, bali ACT ni moyo wake, yaani ACT is his beating heart, kama ambavyo Wazungu wangesema. Leo tunaandika historia kubwa katika nchi hii kwa tukio hili. Tunajenga utamaduni mpya na kigezo kipya.
Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama mstaafu wa ACT-Wazalendo, katika makala yake kwenye The Chanzo kushereheke maisha ya Babu Duni anamtaja kuwa na moyo mkubwa kwa uamuzi wake wa kuridhia Bwana Othman Masoud apitishwe kuwa mrithi wa Hayati Maalim Seif.
Muumini wa taasisi
Nilivyotiririka itaonekana kama namjua Babu Duni sana. Hapana. Nilianza kumjua kwa undani nilipojiunga kwenye kampeni ya Uchaguzi wa Chama kujaza nafasi ya Maalim Seif, tena nikawa Mshauri wake.
Kisha tukaja kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Machi 2024, ambapo nataka nitoe ushuhuda wa “moyo mkubwa” tena wa Babu Duni baada ya tishio la kuonekana kutakuwa na mpasuko kwa sababu ya joto la uchaguzi.
Othman Masoud Othman (kushoto) na Juma Duni Haji (kulia) wakipeana mikono wakati wa hafla ya kusherehekea mchango wa Duni kwa chama cha ACT-Wazalendo na taifa. PICHA | ACT-WAZALENDO.
Aliamua kujitoa na kumpisha Bwana Othman siku tano kabla ya Uchaguzi na kututaka timu yake ya kampeni tutayarishe barua na hotuba. Tulipomuuliza kwa nini asitoe jina lake mapema alisema, kwanza, alitaka autumikie uenyekiti wake mpaka mwisho, lakini pili alisema: “Wacha chama kijenge uzoefu wa mitikisiko ili tujenge uimara wake.”
Hivyo ndivyo alivyo Duni: muumini na mjenzi wa taasisi imara. Akatuvusha. Tuko salama na tunajipanga kwa ushindi.
SOMA ZAIDI: Rais Samia, Tunaomba Utuachie Kitabu Chenye Hadithi Nzuri
Ndiyo maana leo tukimuenzi tunamchukulia Juma Duni Haji, maarufu Babu Duni, kuwa mmoja wa wanasiasa wetu ambao wataishi milele na vizazi kwa vizazi vitamtaja kumuenzi na kumuimba. Lakini Babu haondoki. Yupo kwenye Kamati ya Uongozi na bado yupoyupo kwenye mapambano nasi.
Natamani kusoma kitabu chake mwaka huu au mwakani, Inshallah. Tuone utajiri wa maisha yake, si wa fedha bali wa moyo mwema, imani, utu na uzalendo uliotukuka. Tuseme Amin!
Namaliza kwa kipande cha shairi ya nyimbo iloimbwa hapa ambayo ni utunzi wangu mpya kuenzi maisha ya Babu Duni:
Baki nasi safarini,
Umma wakuhitajia.
Fikra zako makini,
Umma njia kutuongezea.
Usituache njiani,
Mamlaka kulengea.
Oktoba ya mwakani,
Pamoja kushangilia.
Ally Saleh ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ACT-Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia allysaleh126@gmail.com au X kama @allysalehznz. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.