Ujumbe mkubwa ambao chama cha upinzani CHADEMA kilikusudia kuutuma kwenye maandamano yake ya Jumatatu ya Septemba 23, 2024, ni kwamba Serikali, na vyombo vyake vya dola, haifanyi vya kutosha kulinda maisha na uhai wa wananchi kwa kushindwa kukomesha vitendo vya utekaji, ikiwemo kuwawajibisha wanaohusika na vitendo hivyo.
Haijalishi watu watatoa tathmini gani juu ya maandamano hayo, ni imani yangu kwamba ujumbe huo umewafikia mamilioni ya wananchi, na umeendelea kuchagiza mazungumzo muhimu kwenye jamii kuhusu kushindwa huko kwa Serikali kwenye kulipatia ufumbuzi tatizo hilo la watu kupotea kiholela, linaloendelea kuwajaza Watanzania hofu wakiwa ndani ya nchi yao.
Kwangu mimi binafsi, hatua ya kufanikisha ujumbe huo unawafikia walipa kodi wengi zaidi, katika mazingira ambayo watu wachache zaidi wameumizwa, ni ya kupongezwa sana.
Hata kama wana CHADEMA kwa mamilioni wangeingia barabarani, nusu yao wakauwawa na wengine kuachwa na ulemavu wa kudumu, ni ujumbe huohuo maandamano hayo yangetuma.
Hakuna ujasiri wowote kwenye kuikingia risasi, au kirungu, kifua, ukihatarisha maisha yako, kwa sababu tu unataka kuwafikishia watawala ujumbe fulani ambao unaweza kuwafikishia kwa njia itakayokutunzia uhai wako.
Maandamano ni haki ya kikatiba, ndiyo, lakini kama una watu walioapa kuchukua uhai wako, au kukupa kilema cha milele kwa kutekeleza haki hiyo, ukijua kabisa hawatawajibishwa kamwe, ni muhimu kuchukua hatua za kujinusuru.
SOMA ZAIDI: Maandamano ya Septemba 23 ya CHADEMA na Mustakabali wa Siasa za Tanzania
Binafsi, kama ningekuwa kiongozi wa chama ningewasihi wafuasi wangu kuweka kipaumbele kwenye hilo baada ya kuona dola na vibaraka wake wamedhamiria kuwaumiza.
Ningefanya hivyo kwa kujua kwamba nitalazimika kuwajibika, mbele ya mahakama za kitaifa na kimataifa, kwa kuwahamasisha watu kujitokeza ili kuuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyofunzwa siyo kutii Katiba ya nchi na sheria, bali wanasiasa.
CHADEMA wameepuka hatma hiyo kwa kufanikisha kutuma salamu zao bila kuwepo kwa umwagaji wowote wa damu.
Imefanikiwa kuwaonesha Watanzania kwamba Serikali inayochukua hatua kadhaa kama vile kutoza kodi, kuomba mikopo, na kutunga sheria kwa jina la ‘Watanzania,’ kimsingi haijali kuhusu maslahi ya Watanzania, kiasi ya kutokuwaruhusu hata kutoa maoni yao kwa njia za kikatiba kuhusu mambo yanayoendelea nchini mwao!
Mabadiliko ya kimtazamo
CHADEMA pia wamefanikiwa kuendeleza mchakato mrefu, lakini muhimu, wa mabadiliko ya kimtazamo na kiutamaduni miongoni mwa wananchi ambayo matokeo yake ni ngumu kuyaona kwa sasa.
Hatua yao ya kulitisha dola la kiimla linalowakandamiza Watanzania itasaidia kuwajengea raia kujiamini na kujithamini, vitu ambavyo ni msingi imara wa mapambano ya mageuzi ya siku zinazokuja.
SOMA ZAIDI: Kila Wakati Ambapo Watu Walisimama Pamoja Kutetea Maslahi Yao, Walifanikiwa
Ujenzi wa uelewa wa kiraia ambao ni muhimu kufanikisha uwajibikaji wa umma ni mchakato mrefu, unaolazimika kuvuka milima na mabonde, mpaka kufanikishwa, na inanipa faraja kuona CHADEMA inashiriki kikamilifu kwenye mchakato huo.
Utamaduni inaosaidia kuujenga, ule wa kuhoji mamlaka, ni msingi imara wa taifa la kidemokrasia ambalo Watanzania wanatamani kuliona.
Kwa hiyo, siyo CHADEMA waliopoteza kwenye maandamano ya Septemba 23 yaliyoshindwa kuendelea kama yalivyokuwa yamepangwa awali.
Tuliopoteza ni sisi wananchi wa Tanzania ambao tutaendelea kuishi kwa wasiwasi juu ya hatma ya usalama wetu na wale tuwapendao, tukijua kwamba yoyote kati yetu anaweza “kupotea” muda wowote na tusiwe na uwezo wowote wa kuzilazimisha mamlaka kutupatia majibu.
Tumepoteza kwa kuendelea kuwahakikishia watawala kwamba wanaweza kufanya mambo kadiri wanavyotaka, kinyume cha Katiba na sheria zingine za nchi, bila ya kuwa na hofu ya kuwajibishwa na wananchi wanaoitwa eti ni chanzo cha mamlaka yote wale waliopo madarakani wanaendelea kuyatumia, siyo kwa maslahi mapana ya umma, bali kwa maslahi yao finyu ya kibinafsi.
Tusihukumiwe
Ni wajibu wetu kama wananchi kuhakikisha kwamba hali hii inabadilika. Lakini tofauti na wengine walioamua kuchukua misimamo ya kuwahukumu na kuwalaumu wananchi kwa kushindwa kusimama na kutetea maslahi yao, ikiwemo kuitikia wito wa kuandamana, niseme kwamba mimi binafsi nawaelewa wananchi, kwa umoja wao, na msimamo waliouchukua kwenye suala hili.
Sisi wananchi siyo wajinga wala punguani. Tunajua kutofautisha kati ya baya na jema, na tunajua tofauti kati ya anayeonea na anayeonewa.
SOMA ZAIDI: Pengine ni Kweli Polisi Hawahusiki na Utekaji. Lakini Mbona Hatuoni Watekaji Wakikamatwa?
Tunafahamu kwamba polisi hawapo kuhakikisha usalama wetu, huku wakihusika kutuziba midomo tusitoe maoni yetu. Tunafahamu kwamba vilio vyetu vya maisha magumu na ukosefu wa huduma muhimu za kijamii siyo kipaumbele cha wale waliojipa dhamana ya uongozi.
Lakini kama wananchi pia tuna hofu nyingi. Tuna hofu ya kutekwa na ndugu zetu wasijue tuko wapi. Tuna hofu ya kuuwawa. Tuna hofu ya kukamatwa na kuwekwa rumande bila dhamana wala uwezo wa kuwasiliana na familia zetu au mawakili.
Tuna hofu ya kupoteza vibarua vyetu. Tuna hofu watoto wetu kunyimwa kazi na fursa nyingine Serikalini kwa kuonekana kujihusisha na siasa za upinzani.
Mategemeo yetu kama wananchi ni kwa wanaharakati kuzielewa hofu hizi tulizonazo na kutusaidia, kidogokidogo, kuzishinda, au kuzikabili, na hivyo kuchochea ushiriki wetu wa kina kwenye michakato ya mageuzi nchini kwetu.
Mchakato huo wa kuzikabili hofu zetu unaweza ukawa mrefu, na hivyo tunategemea wanaharakati wawe waelewa na wavumilivu wakiwa wanatimiza jukumu hilo muhimu la kuibua mwamko wa kiraia na kisiasa miongoni mwetu.
Labda kabla ya kutuita tushiriki maandamano dhidi ya Serikali, pengine tunaweza kuunganishwa kuwakabili wenye nyumba wetu wanaoweka sharti la kulipwa kodi ya miezi sita, kinyume na sheria na taratibu za upangishaji nyumba, au kuwakabili madalali wa mazao wanaotunyonya.
SOMA ZAIDI: Ni Wakati Kama Wananchi Tuache Visingizio na Kuanza Kutimiza Wajibu Wetu wa Kiraia
Hatua kama hizi na nyinginezo zinaweza kutusaidia kupata uzoefu wa tunachoweza kuvuna kwa kusimama pamoja na kutujengea uaminifu wa kushiriki kwenye harakati kubwa zaidi zenye faida kitaifa.
Kutukebehi na kutuhukumu kwa kushindwa kufanya kama wanaharakati wanavyotutarajia tufanye ni kuzihujumu juhudi zenyewe za ukombozi kwani kufanya hivyo ni kujiziba macho na hivyo kushindwa kuona picha kubwa na kudhoofisha jitihada za kuja na afua stahiki za kukabiliana na hali ilivyo katika jamii zetu na taifa kwa ujumla.
Pengine kwa kuwaelewa wananchi pamoja na hofu zao kutawasaidia wanaharakati kuja na mbinu bunifu zaidi za kuchochea mwamko wa kisiasa na kiraia miongoni mwetu wananchi, na hivyo kuweza kushiriki kikamilifu kwenye maandamano mengine CHADEMA itayatangaza na kupaisha mafanikio yake, ikiwemo kuwakumbusha watawala kwamba mamlaka, kimsingi, hazipo mikononi mwao, bali kwenye mikono yetu wananchi.
Khalifa Said ni mwandishi na mhariri wa The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia Khalifa@thechanzo.com au X kama @ThatBoyKhalifax. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.