Wakati Shirikisho la Soka (TFF) likianzisha utaratibu mpya wa muundo wa uongozi uliotaka kila klabu ya Ligi Kuu iwe na sekretarieti inayoundwa na waajiri, ilikuwa inalenga kuhakikisha shughhuli za kila siku haziathiriwi na mabadiliko ya viongozi wa kuchaguliwa.
Viongozi hao wa kuchaguliwa huondoka wakati muda wao unapoisha na wanaposhindwa kutetea nafasi zao kwenye uchaguzi, au wakati huo kulikuwa na utamaduni wa mapinduzi ya kuwaondoa kwa makosa yanayotengenezwa.
Waliokuwa wanachaguliwa ni pamoja na mwenyekiti, makamu wake, katibu mkuu, mweka hazina na msaidizi wake pamoja na katibu muenezi, au siku hizi ofisa habari.
Kama ni uchaguzi, ilikuwa ni vigumu kwa safu yote ya uongozi kurejea madarakani, hali iliyokuwa ikisababisha mipango yote kuvurugika labda ipatikane safu ya wenye akili wanaotaka kumalizia yaliyoanzishwa na watangulizi ndipo waanzishe yao.
Na yalipotokea mapinduzi, safu inayoingia huwa ni mpya kabisa, yaani inakuwa ni ile iliyoongoza mapinduzi hayo, ikimtanguliza mmoja kama mwenyekiti na wengine wanagawana vyeo baada ya kufanikisha mapinduzi.
Ulikuwa ni uhuni uliolindwa na kulelewa na vikundi vya watu kwenye klabu vilivyokuwa vinaishi kwa kutegemea mpira, yaani wasimama milangoni, wapambe wa waongoza mapinduzi, au wapambe wa wafadhili wa amapinduzi na shuhghuli nyingine za mpira wa miguu.
SOMA ZAIDI: Serikali Ianze Kutoa Ruzuku kwa Vyama Teule vya Michezo
Kwa hiyo, ilikuwa ni vigumu kwa safu moja ya uongozi kumaliza muda wake bila ya mapinduzi, au jaribio la mapinduzi, hali iliyoyumbisha uendeshaji wa klabu ambao huhitaji pia mambo mengi yawekwe kwenye maandishi, ikiwa ni pamoja na ripoti za fedha, za utendaji na shughuli za kila siku.
Azimio la Bagamoyo
Kwa hiyo, Azimio la Bagamoyo lililowekwa mwishoni mwa muongo wa kwanza wa karne hii, liliweka agizo la kutaka klabu ziajiri watendaji wake badala ya wale wa kuchaguliwa, huku likiweka sharti hilo katika benchi la ufundi na baadaye zikatoka sifa za watu wanaostahili kuwa sehemu hiyo muhimu katika mpira wa miguu.
Huo ukawa mwanzo wa ajira kwenye klabu zetu na mwisho wa kuendesha mambo kwa mazoea, au kwa ule utaratibu wa ’bora liende,’ huku wanufaika wakiwa ni viongozi ambao wasingeweza kuwa na mipango ya muda mrefu kwa kuwa hawakuwa na uhakika wa kukaa madarakani muda mrefu.
Na ukizungumzia ajira ni ile ama ya muda mrefu ama ya mkataba, ikiwa ni masharti ambayo yatamzuia muajiri kujifanyia mambo atakavyo badala ya kuheshimu makubaliano ya ajira au mkataba.
Inaonekana mambo yameanza kurejea kule tulikotoka. Badala ya kuelekea katika kujenga mifumo bora ya kutafuta na kuajiri watendaji, tunarejea kule kwenye uholela wa kupata watu wa kufanya shughuli za kila siku.
Badala ya kuelekea kule ambako watendaji watapata mafunzo ya ndani au nje ya taasisi kwa ajili ya kuboresha utendaji wao, klabu zinatafuta watu wenye mazoea nao, au waliosikia taarifa zao kwamba wanafaa.
SOMA ZAIDI: Tufuatilie Sakata la Man City kwa Makini Tukijitathmini
Kibaya zaidi, kuna klabu ambazo zinadhani mvuto wa mtu unaendana na utendaji bora. Kwa hiyo, mtu mwenye wafuatiliaji wengi kwenye mitandao ya kijamii huwa kwenye nafasi nzuri ya kupata ajira, tena isiyodumu, kuliko yule ambaye ana uwezo.
Watendaji kuyumbishwa
Hivi sasa watendaji ndio wanayumbishwa badala ya viongozi kuyumbishwa na wanachama au wamiliki wa klabu. Ukisikia fulani kawa ofisa mtendaji mkuu wa klabu, fuatilia habari zake baada ya muda mfupi. Bila shaka utakutana na habari kuwa walishaachana naye muda mrefu.
Hali iko hivyo kwa maofisa watendaji wakuu, iko hivyo kwa maofisa habari, iko hivyo kwa watendaji wengine.
Bado sijasikia lolote kuhusu maofisa masoko ambao pengine ni muhimu sana katika soka la kulipwa kwa ajili ya kuunda bidhaa za timu wanazoweza kuziuza kwa kampuni ili kupata udhamini. Naona hili linategemeana na umaarufu kwa kiongozi anayeteua watendaji na si umahiri wa mtu katika tasnia ya masoko.
Ingawaje fedha zimeendelea kumiminika katika mpira wa miguu bila ya juhudi kubwa ya kuzitafuta, lakini hakuna ubishi kwamba klabu zinarudi kwenye uendeshaji wa kizamani na kibaya zaidi unakuwa wa kiimla kuliko weledi.
Ukiangalia mechi za ligi kwenye televisheni au hata ukiwa uwanjani, huoni mabango ya wadhamini wa klabu kwa siku ya mechi, zaidi ya wale wadhamini wakuu. Maana yake fursa hiyo haitumiki ipasavyo, pengine ni kutokana na klabu kutoajiri waofisa masoko mahiri wanaojua kuuza fursa zilizopo kwenye mechi zao.
SOMA ZAIDI: Sakata la Lawi, Kagoma ni Utapeli Katika Soka
Hata unapofuatilia taarifa kuhusu mechi inayotazamiwa kuchezwa, huioni idara ya masoko. Unachoweza kuona ni idara ya habari, tena katika mikutano ya kabla ya mechi ambayo inaandaliwa kikanuni.
Tunahitaji sekretarieti imara za kuweza kuziendesha klabu hizi kiweledi na bila kuyumbishwa na zinazoweza kutumia fursa nyingi zilizopo kwenye klabu na mpira wa miguu kwa ujumla kukuza uchumi wa klabu na hivyoi kuweza kuendesha program nyingine za maendeleo.
Sekretarieti ni nguzo na muhimili wa klabu za kisasa duniani na hivyo hazitakiwi ziyumbishwe kwa utashi wa mtu mmoja au genge. Ni muhimu watu wenye elimu na weledi katika tasnia tofauti watafutwe na kuajiriwa ili waboreshe utendaji wa klabu badala ya kutegemea akili ya mtu mmoja au kigenge cha wachache.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.