The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Afya ya Akili:  Tuzungumze Kuhusu Ugonjwa wa Sonona

Kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya akili na afya ya mwili, haki za binadamu, maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya jamii, hali inayotulazimisha, kama taifa, kuboresha huduma kukabiliana na matatizo ya afya ya akili.

subscribe to our newsletter!

Matatizo ya afya ya akili yamekuwa yakiongezeka nchini na duniani kwa ujumla. Oktoba 10 ya kila mwaka huwa ni siku maalumu ya kuadhimisha Siku ya Afya ya Akili Duniani, lengo kubwa ikiwa ni kuongeza ufahamu wa matatizo ya afya ya akili kwenye jamii. 

Kauli mbiu ya mwaka huu ni Afya ya Akili Ipewe Kipaumbele Mahali pa Kazi. Nchini Tanzania tumejenga mazoea ya kujadili masuala ya afya ya akili katika siku maalumu, mfano siku ya Afya ya Akili Duniani. 

Lakini ni muhimu kujadili na kuongea kuhusu matatizo ya afya ya akili wakati wowote, iwe kabla au baada ya siku ya Afya ya Akili Duniani, na kupambana, kama taifa, kuhakikisha mbinu mwafaka zinatumika katika kuzuia tatizo hili na kupunguza madhara yake kwa jamii. 

Sonona, au depression kwa kimombo, ni moja ya magonjwa ya afya ya akili yanayoshika kasi mahala pa kazi na kuathiri watu walio kwenye sekta rasmi na isiyo rasmi hali kadhalika, ni tatizo la afya ya akili linaolowapata watu wengi zaidi nchini hasa vijana.

Sonona huathiri hali, au hisia, za mwathirika, na kuingilia uwezo wake wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi, na kuathiri utaratibu wake wa maisha ya kila siku, ikiwa ni pamoja na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi. 

Sonona husababisha madhara kimwili, kiakili, na mahusiano na watu wengine. Ugonjwa huu unaweza kusababisha kuongezeka kwa shinikizo la juu la damu, unene uliopilitiza au matumizi ya vilevi, tabia ambazo zinaongeza hatari ya kupata magonjwa kama vile ya moyo na kisukari. Aidha, watu wenye sonona wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kujiua.

SOMA ZAIDI: Tunachoweza Kufanya Wazazi Kuwanusuru Watoto Wetu na Matatizo ya Afya ya Akili

Dalili za sonona hutofautiana kutoka sonona ya wastani hadi sonona kali, na huweza kudumu kwa wiki kadhaa, miezi hadi miaka. Kuna dalili kadhaa za sonona lakini dalili kuu ni kujisikia huzuni, utupu, au kukosa matumaini.

Dalili nyingine ni kupoteza hamasa ya kufanya shughuli za kawaida za kila siku kama usafi, kwenda kazini, darasani na kutofurahia mambo ambayo mtu alikuwa anayafurahia hapo awali, kama vile michezo na kukutana na marafiki kwa muda wa zaidi ya wiki mbili. 

Ugonjwa wa sonona ni tofauti na kujisikia huzuni, au kuchoshwa baada ya kupata matukio ya maisha, au kupitia vipindi vigumu vya maisha, hali ambayo ni ya kawaida kwa mtu yoyote kupitia kwa kipind kifupi, kwa kawaida kisichozidi wiki mbili, bila kuathiri kwa kiasi kikubwa utaratibu wake wa maisha ya kila siku. 

Baadhi ya wanawake hupata sonona ndani ya mwaka mmoja baada ya kujifungua, au postpartum depression kama ambavyo hali hiyo inajulikana kwa kimombo. Ugonjwa huu huweza kutambuliwa na wataalamu wa magonjwa ya afya ya akili.

Hatari ya kupata sonona huongezeka kuanzia umri wa miaka 20 hadi 64, hivyo kusababisha hatari ya vijana wengi kuingia katika utu uzima wakiwa na matatizo ya afya ya akili. 

Baadhi ya tafiti kwenye makundi mbalimbali zinaonyesha uwepo wa sonona unatofautiana kwa makundi mbalimbali, mfano asilimia 5.8 kwa vijana na asilimia 44.4 kwa wazee waliofanyiwa utafiti wa makundi walionyesha kuwa na sonona.

SOMA ZAIDI: Huduma za Afya ya Akili Ziingizwe Kwenye Huduma za Mama na Mtoto

Tafiti chache zilizofanyika Tanzania zinaonyesha watu walio kwenye hatari zaidi ya kupata msongo wa mawazo, na hatimaye sonona, ni wale wanaojihisi hawapati msaada wa jamii, watu wasio na kipato cha uhakika, iwe kwa kujiajiri au kuajiriwa. 

Watu wasio na uwezo wa kufanya kazi wapo kwenye hatari zaidi ya kupata sonona, hali kadhalika watu wenye magonjwa ya muda mrefu, kama vile maambukizi ya virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Sababu mbalimbali

Sonona inaweza kusababishwa na matatizo ya kibaolojia, kisaikolojia na kijamii. Mfano wa sababu za kibaolojia ni pamoja na matumizi ya dawa zenye kusababisha sonona, magonjwa yanayosababisha sonona, na upungufu wa virutubisho mwilini unaosababishwa na ukosefu wa chakula bora, tabia -bwete, yaani kutokufanya mazoezi ya mwili. 

Sababu za kisaikolojia zina husisha namna mtu anavyotafsiri, au kile anachoamini, kuhusiana na matukio na madhila yaliyompata, au yanayompata maishani. Changamoto za mahusiano kwenye jamii zinaweza kusababisha msongo wa mawazo hadi muathirika kupata sonona. 

Kuwa na imani na mtazamo hasi kuhusu maisha, watu na jamii, na kuwa na uwezo mdogo wa kustahmili na kukabili changamoto mbalimbali za maisha, kunaweza kusababisha ongezeko la hatari ya kupata sonona.

Mazingira wanayoishi watoto yanaweza kusababisha wapate sonona ya utotoni, au hata watapokuwa watu wazima. Watoto wa mzazi mwenye sonona wana uwezekano mkubwa wa kupata sonona kulinganisha na watoto wa mzazi asiye na sonona. 

SOMA ZAIDI: Afya ya Akili: Ushuhuda wa Mhanga na Mapambano ya Kupata Matibabu

Watu waliopitia unyanyasaji wakiwa watoto wana hatari zaidi ya kupata sonona. Unyanyasaji huo unaweza kuwa ni wa kimwili, kingono au kisaikolojia, kutelekezwa, kuishi kwenye mazingira ya ukatili au hata mazingira yasiyo na mahusiano mazuri ya kifamilia.

Ulevi wa kupindukia na matumizi ya vilevi kama bangi na dawa za kulevya huongeza hatari ya kupata sonona. Taarifa za Health Data za mwaka 2021 zinaonyesha kuwepo kwa watu wengi zaidi Tanzania wenye matatizo ya matumizi mabaya ya vilevi kulinganisha na nchi nyingine kama vile Kenya na Uganda

Matibabu

Kuna njia za aina mbalimbali za kutibu sonona kwa kutumia tiba ya mazungumzo, dawa na njia nyingine kutegemea na ukubwa wa tatizo. 

Mafunzo ya mbinu za kukabiliana na matatizo na changamoto za maisha na kudhibiti msongo wa mawazo yameonyesha mafanikio makubwa kwenye kupunguza hatari ya kupata sonona, hasa yanapotolewa kwa watoto kati ya miaka minne hadi 14. 

Ni muhimu sana ugonjwa wa sonona kutambuliwa mapema na ni haki ya mgonjwa kupatiwa matibabu stahiki kwa wakati mwafaka.

Watu wenye sonona wana haki ya kupata matibabu na huduma nyingine za afya zenye ubora na kwa wakati. Huduma za afya ya akili, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa sonona, hazipatikani kwenye vituo vingi vya huduma ya afya ngazi zote nchini.

SOMA ZAIDI: Kama Mzazi, Unawezaje Kujali, Kulinda Afya Yako ya Akili?

Uhaba mkubwa zaidi upo kwenye ngazi ya msingi nchini, yaani katika zahanati na vituo vya afya na pale huduma zinapopatikana mara nyingi huwa hazina ubora kwani kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wa kutoa huduma za afya, ikiwa ni pamoja na huduma za afya ya akili, hivyo watu wengi wenye sonona wanajikuta njia panda linapokuja suala la kupata msaada wa kitaalamu. 

Aidha, kuna uhaba mkubwa wa ukosefu wa huduma za kisaikolojia katika ngazi ya jamii, uhaba wa vifaatiba na dawa, na utekelezaji hafifu wa kampeni za uhamasishaji wa huduma ya afya ya akili. 

Utambuzi wa watu wenye changamoto ya afya ya akili kwenye ngazi ya jamii husimamiwa na maofisa wa ustawi wa jamii waliopatiwa mafunzo, utambuzi haufanywi kwa ufanisi kutokana na uhaba mkubwa wa maofisa hao, aidha umelenga zaidi kwa wazee, wasiojiweza na watu wengine wenye mahitaji maalumu.

Mgawanyo wa fedha ya Bajeti ya Wizara ya Afya 2024/2025 haujatoa kipaumbele kwenye huduma za afya ya akili. Hakuna Sera ya Afya ya Akili, huku Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008 ikishindwa kutoa suluhisho kwa changamoto na mahitaji ya sasa kwani imepitwa na wakati.

Ukosefu wa mfumo bora wa kugharamia huduma za afya unapelekea watu wengi, hasa walio kwenye sekta isiyo rasmi, kushindwa kumudu gharama za matibabu. Katika kila Watanzania 100, 85 hawana bima ya afya, wanagharamia huduma za afya kutoka mifukoni. 

Gharama za matibabu ya magonjwa ya afya ya akili huweza kusababisha matatizo makubwa ya kiuchumi kwenye familia za wagonjwa.

Wito kwa Serikali, wadau

Sisi ndani ya ACT Wazalendo tumeendelea kuitaka Serikali iweke mfumo imara wa hifadhi ya jamii ili kuwapa wananchi kinga ya kuingia kwenye umaskini na kuwawezesha kupata huduma za afya kadiri ya mahitaji yao na sio kadiri ya kipato chao kama ilivyo sasa.

SOMA ZAIDI: Jitihada Zaidi Zinahitajika Kuwakinga Watanzania Dhidi ya Magonjwa Yasiyoambukiza

Pia, tumeendelea kutoa wito kwa Serikali kuondoa mianya ya ubadhirifu wa mali za umma, ili kukuza uchumi na kupunguza matatizo ya ukosefu wa ajira, ukosefu wa pensheni, na kuondoa umaskini ambao ni chanzo kikubwa cha matatizo ya afya ya akili nchini.

Serikali itunge Sera ya Afya ya Akili ili kuboresha na kutoa huduma bora za afya ya akili, pamoja na kurekebisha Sheria ya Afya ya Akili ya mwaka 2008. Bajeti ya kugharamia tafiti za magonjwa hayo pia iongezwe ili kuweza kupata uelewa mpana wa tatizo la afya ya akili nchini.

Huduma za afya ya msingi, yaani zahanati na vituo vya afya, zinahitaji kuboreshwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa wafanyakazi na wataalamu wa kutoa huduma za afya, vifaa-tiba, vitendanishi na dawa ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya. 

Wataalamu wa afya ngazi zote, hasa kwenye ngazi ya msingi, wajengewe uwezo wa kutoa huduma za afya ya akili, na kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujikinga na kupambana na matatizo ya afya ya akili ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa sonona.

Mitaala ya elimu ya shule za msingi na sekondari ijumuishe elimu ya kuwawezesha watoto na vijana kupata ujuzi na mbinu za kupambanua, kukabili na kutatua changamoto, mbali mbali za maisha. Serikali pia inapaswa kuwezesha elimu ya afya ya akili kidigitali kwa njia ya mtandao, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya afya ya akili na afya ya mwili, haki za binadamu, maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya jamii. Kwa hiyo, kuboresha sera za kuzuia matatizo ya afya ya akili na huduma za afya ya akili ni faida kwa mtu mmoja mmoja, na jamii yote. 

Ni muhimu kujadili na kushirikiana, kama jamii, katika kupunguza matatizo ya afya ya akili. 

Hata hivyo, ni muhimu zaidi kwa kila mwananchi kupambania kupata mfumo bora wa kuendesha nchi utakaowawezesha wananchi kuwawajibisha viongozi waliopewa dhamana ya kuhakikisha uwepo na utekelezaji wa sera bora za kuondoa nchi kwenye umaskini, na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii, kama vile huduma muhimu ya afya, zinapatikana kwa wote.

Dk Elizabeth Sanga ni mtaalamu wa afya ya jamii na Msemaji wa Sekta ya Afya ya chama cha upinzani ACT-Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia elizabethbenedict2013@gmail.com au X kama @DrBSanga. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts