The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Familia ya Kibao kwa Rais Samia: Bado Tunaamini Hatua Zinaweza Kuchukuliwa Dhidi ya Waliohusika na Mauaji ya Mzee Wetu

Kauli ya mtoto wa mwanasiasa huyo kwa Kiongozi Mkuu wa nchi inakuja takriban miezi miwili tangu kuripotiwa kwa taarifa za kutekwa na kuuwawa kwa mzazi wake.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Familia ya Ali Mohamed Kibao, mwanasiasa mwandamizi wa chama cha upinzani CHADEMA, aliyetekwa na kuuwawa mwezi Septemba, mwaka huu wa 2024, imejitokeza hadharani na kumtaka Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati kuhakikisha haki inatendeka dhidi ya watu waliohusika na uhalifu huo.

Mwili wa Kibao, ambaye anatajwa kuwa mwanamikakati wa CHADEMA, ulipatikana mnamo Septemba 8, 2024, maeneo ya Ununio, Dar es Salaam, siku mbili baada ya watu waliojitambulisha kama polisi kumchukua kutoka kwenye basi alilokuwa akisafiri nalo kuelekea Tanga, na kuibua mjadala mkubwa wa kitaifa.

Rais Samia, kupitia ukurasa wake rasmi wa X, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kulaani vikali tukio hilo hapo Septemba 8, 2024, akiviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo, na kumpatia majibu ya haraka. “Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi,” Samia alisema. “Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii.”

Lakini akizungumza kwa niaba ya familia yao kwenye video fupi aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii leo, Octoba 25, 2024, mtoto wa Kibao, Mohamed Ali Kibao, alisema uchunguzi kwenye tukio hilo unaenda kwa kusuasua, akimtaka Rais Samia kuingilia kati kuhakikisha unakamilika kwa haraka, na wahusika wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

“Jambo la kwanza, tunaomba uwazi kidogo katika harakati za uchunguzi huu kwa sababu mpaka sasa ilichukua karibu wiki mbili baada ya mauaji polisi kuja kuongea na familia,” anasema Mohamed. “Hatuna tunalolijua, tunashindwa kuomboleza, tunashindwa kuhitimisha. Tunaomba uwazi kidogo katika uchunguzi huu.”

David Misime, Msemaji wa Jeshi la Polisi, taasisi yenye jukumu la kukamilisha uchunguzi huo, aligoma kutoa taarifa zozote kuhusiana na hatua taasisi yake imefikia kwenye kuchunguza tukio hilo, akiiambia The Chanzo kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo kabla ya kuona taarifa ya wanafamilia hao kwanza.

Ifuatayo ni taarifa kamili ambayo Mohamed Ali Kibao, mtoto wa Kibao, ameitoa kupitia video fupi aliyoiweka kwenye mitandao ya kijamii. Uhariri umefanyika kuboresha usomaji:

As-salamu alaykum!

Kwa jina naitwa Mohamed Ali Kibao, mtoto wa marehemu Ali Mohamed Kibao, ambaye alitekwa, kuteswa, na kuuwawa kikatili mwezi Septemba 2024. 

Leo, nina ujumbe mfupi kuja kwako, Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba ya watoto wa Mzee Kibao, familia na mama yetu. 

Katika mauaji ya Mzee Kibao kuna mengi ambayo hatuyafahamu, lakini vilevile kuna mambo kadhaa ambayo tunayafahamu, na mengine yanaendelea kujitokeza kadri siku zinavyozidi kwenda.

Katika hayo, ningependa nigusie mambo makubwa manne. Jambo la kwanza, tunafahamu kwamba Mzee Kibao alitekwa mchana kweupe, akateswa, akauawa kikatili. Hili halipingiki, tunalifahamu wote. Nitalirejea hilo. 

Jambo la pili ambalo tunalifahamu ni kwamba Serikali yako ina uwezo na uhodari mkubwa wa kuzuia mambo usiyoyataka yasifanikiwe. Mfano mkubwa, na wa karibuni, ni jinsi ambavyo Serikali ilizuia maandamano ya CHADEMA, tuliona mabavu makubwa na uoneshaji wa uhodari kabisa katika hilo.

Sasa, tukitofautisha jinsi ambavyo hilo lilichukuliwa, na jinsi ya utekaji na mauaji ya Mzee Kibao yalichukuliwa, siyo kwamba tunataka upendeleo katika kesi hii, hapana. Isipokuwa, tukiona tofauti hizi, inatupa mashaka, na kutufanya tupoteze imani katika vyombo vya dola ambavyo vimepewa dhamana ya kulinda uhai wa Watanzania na mali zao. 

Jambo la tatu, na jambo ambalo lilitupa majonzi sana kama wanafamilia ni jinsi ambavyo uliliongelea suala la mauaji haya. Ilikuwa ni matumaini yetu kwamba ungekemea siyo tu tukio hilo, bali wale ambao wanafanya matukio haya kuwatia mashaka na hofu katika nafsi zao, kama ambavyo wametutia mashaka na hofu katika nafsi zetu sisi wanafamilia, na ninadhani pia Watanzania kwa ujumla. 

Lakini, badala yake, tulikusikia ukisema kwamba kifo ni kifo tu, na ulishangazwa sana kwamba kwa nini watu wametaharuki kuhusu kifo na mauaji ya Mzee Kibao. Hili linatupa mashaka na linatupa majonzi, linatukosesha faraja kama wanafamilia.

Jambo la mwisho ambalo ningependa niligusie hapa na linafahamika ni kwamba Watanzania tuna hofu na tunapoteza imani na vyombo vya dola. Sasa basi, kwa nini nasema tunapoteza imani? 

Tunapoteza imani kwa sababu sisi kama wanafamilia, hata sisi wenyewe, siku ambayo alitekwa Mzee Kibao, siku ya Ijumaa ile, hatukukimbilia kwanza polisi bali tulikimbilia mitandaoni kuwaomba kina Maria [Sarungi Tsehai] watupigie kelele sisi. 

Na huu ni mfano mmoja katika mingi ambapo Watanzania wakiona ukiukwaji wa haki wanakimbilia mitandaoni badala ya kwenda polisi. Kwa nini pia nasema Watanzania pia tunahofu? 

Nasema Watanzania tuna hofu kwa sababu sisi kama familia yalipotokea mauaji ya Mzee Kibao tulitafuta ushauri wa wanasheria Tanzania, katika wanasheria wote tulioongea nao hakuna hata mmoja aliyeitaka hii kesi, na siwezi kuwalaumu kwa sababu na wao pia wanaweza kuwa wanahofia maisha yao. 

Sasa kama tunajisifia kwamba sisi ni kisiwa cha amani, ni amani ya aina gani ambayo tunayo ambayo hata wanasheria wanashindwa kufanya kazi zao, kufanya shughuli zao za kutetea na kulinda haki za Watanzania kwa uhuru?

Sasa basi, tukiyachanganya haya yote manne – Mzee Kibao kutekwa mchana kweupe na kuuwawa; kuona kwamba Serikali ina uhodari mkubwa wa kuzuia wasiyoyataka yatokee yasitokee; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongelea suala hili kwa wepesi, kusema kwamba kifo ni kifo tu; na Watanzania kuingia hofu na kupoteza imani– tunapoyaona haya manne tunajiuliza, kama wanafamilia, na pengine Watanzania kwa ujumla, je, hawa wanafanya haya matukio wanafanya bila kuogopa kwa sababu gani? 

Na hisia zetu [ni kwamba] wanafanya hivi kwa sababu wanahisi wanakinga ya Serikali, au wanajijua kwamba wao ni mahodari zaidi kuliko Serikali, kwa sababu hawaogopi, wanafanya kiuwazi, mchana kweupe. 

Sasa basi, ombi letu kwako Dk Samia ni mambo makubwa mawili. Jambo la kwanza, tunaomba uwazi kidogo katika harakati za uchunguzi huu kwa sababu mpaka sasa ilichukua karibu wiki mbili baada ya mauaji polisi kuja kuongea na familia. 

Na pamoja na kwamba Waziri [wa Mambo ya Ndani, Hamad] Masauni, alikuwepo katika msiba, akaongea na dada yetu, Mariam, na akatupa namba za simu za kupiga ili kupata taarifa za uchunguzi huo, [lakini] mpaka sasa kimya. Hatuna tunalolijua, tunashindwa kuomboleza, tunashindwa kuhitimisha. Tunaomba uwazi kidogo katika uchunguzi huu.

Suala la pili ambalo tunakuomba kama Amiri Jeshi Mkuu ni kutoa kauli kali dhidi ya wale wanaohusika na matukio haya. Dhidi ya wahusika, siyo tukio tu, hapana, dhidi ya wahusika, ili na wao waishi kwa wasiwasi kama ambavyo tunaishi kwa wasiwasi sisi wanafamilia na Watanzania kwa ujumla. 

Haya mawili nadhani yanaweza yakawa ni hatua za mwanzo za kurejesha imani katika Serikali kutoka kwa wananchi na vilevile sisi kama wanafamilia kutupa faraja kiasi. Ni hayo tu kwa leo, ahsante kwa kusikiliza, ni matumaini yangu kwamba tutakusikia hivi karibuni.

As-salamu alaykum!

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts