The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Michezo Haiwapotezei Muda Watoto, Inawajenga. Tuipe Kipaumbele

Katika dunia ya sasa, mafanikio ya kitaaluma mara nyingi yanapewa kipaumbele katika mafunzo na ukuaji wa watoto, na ni rahisi kusahau kwamba michezo pia ni sehemu muhimu katika maendeleo ya watoto.

subscribe to our newsletter!

Hatua za hivi karibuni, kama Siku ya Kimataifa ya Michezo iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa, zinaonesha kuwa kila mtoto ana haki ya kucheza, ikisisitiza nafasi muhimu ya michezo katika ustawi na ukuaji binafsi wa mtoto. 

Iwe ya kupangiliwa au ile ambayo mtoto anaibuni mwenyewe na haina mpangilio maalumu, michezo huchochea ujuzi muhimu kwa watoto ambao mara nyingi haupewi kipaumbele kinachostahili, ndani na nje ya shule na nyumbani.

Watoto hucheza sio tu kuburidika bali kujifunza katika ukuaji wao. Tafiti zinaonesha kuwa michezo ni msingi wa kukuza ujuzi unaohitajika katika karne ya 21 kama vile utatuzi wa matatizo, ubunifu, ushirikiano, na udhibiti wa hisia.

Tunaweza kujiuliza michezo iliyopangiliwa na isiyopangiliwa ni ipi. Michezo iliyopangiliwa ni ile yenye kanuni na maelekezo mengi na maalumu, kama vile mpira wa miguu, mpira wa mkono, mpira wa pete, riadha, na kadhalika, pamoja na michezo ya bodi kama vile sudoku au chess

SOMA ZAIDI: Dondoo Chache za Kutuwezesha Wazazi Kujenga Mahusiano na Walimu kwa Malezi, Elimu ya Watoto

Michezo hii huwafundisha watoto wetu nidhamu, ushirikiano, kuweka malengo, kufuata sheria na kanuni, na kuwa na uvumilivu—ujuzi ambao ni muhimu sana katika Maisha ya shuleni na nyumbani.

Kwa upande mwingine, michezo isiyopangiliwa ni michezo huru inayowawezesha watoto kuwa wadadisi, wathubutu na huwajengea uvumilivu na ushirikiano, kama vile kukimbia kimbia uwanjani, sebuleni au kubuni mchezo mipya na marafiki.

Michezo isiyopangiliwa huchochea maamuzi binafsi, ubunifu, na wepesi wa kujaribu na kufanya vitu tofauti tofauti. Michezo isiyo na kanuni nyingi, au uangalizi mkubwa ambayo huangukia katika kundi la michezo isiyopangiliwa huwapa watoto nafasi ya kujiachia na kutoa hisia zao kisha kupunguza msongo wa mawazo kwasababu michezo hio haiwabani. 

Tafiti zinaonesha kuwa michezo yenye uhuru wa namna hii huwaruhusu watoto kuwa na uthubutu, hali inayowajengea kujiamini na kuwa na ujuzi wa stadi za kijamii.

Michezo pia hujenga afya ya mwili kwa kudumisha mtindo wa maisha wenye afya, ambao unaweza kutuepusha na magonjwa yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo. 

SOMA ZAIDI: Fikra za Watoto Juu ya Ukuaji Wao

Licha ya hiyo, wazazi wengi bado tunadhani kwamba michezo ni kitu kisicho na maana kivile kwa watoto wetu tukilinganisha muda tunaowahamisha watoto kusoma na muda tunaowahimiza waende nje wakacheze.

Faida nyingine ya michezo ni pamoja na kuimarisha afya ya akili na mwili wa watoto wetu na faida nyingine hazionekani kwa macho bali ni za kihisia zaidi. 

Ripoti ya shirika la Afya Duniani (WHO) inaonesha ongezeko la msongo wa mawazo, sonona na wasiwasi, hasa baada ya janga la UVIKO-19 na namna michezo inavyoweza kusaidia kukabiliana na matatizo haya. 

WHO inashauri wazazi na walezi kuwahamasisha watoto kushiriki katika michezo itakayowapatia zana muhimu za kujitawala na kudhibiti hisia zao pamoja na kukabiliana na hatari ya msongo wa mawazo, sonona na wasiwasi.

Utafiti wa kimataifa ulionesha kuwa asilimia 78 ya watoto wanahisi kuwa watu wazima, pamoja na wazazi wao, hawathamini michezo. Mtazamo huu unaweza kuwanyima watoto nafasi hizi muhimu za kukuza ujuzi wao, hasa ikizingatiwa ongezeko la upotevu wa uwezo wa kujifunza kote duniani baada ya UVIKO-19.

SOMA ZAIDI: Fahamu Namna ya Upangaji wa Ratiba kwa Makuzi Bora ya Mtoto

Tukielewa kwamba michezo haimpotezei mtoto muda wa kusoma na kwamba mtoto anaweza kujifunza huku akicheza, tutaanza kuwatendea haki watoto wetu na kuwatengenezea mazingira yaliyo na usawa na yanayosisitiza maendeleo ya kijamii na kitaaluma kwa kusistiza ushiriki wao katika michezo. 

Pia, Serikali na jamii kwa ujumla tunapaswa kukuza sera rafiki za michezo na kuanzisha maeneo ya kucheza kwa watoto ili kuongeza fursa za michezo kwa watoto.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts