The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Dorothy Semu: Kwa nini ACT-Wazalendo Tumeandaa Ilani ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa?

Utunzi wa ilani ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unakusudia kutoa dira na muelekeo wa pamoja, kama chama, kuhusiana na vijiji na mitaa tunayotaka kuijenga.

subscribe to our newsletter!

Novemba 17, 2024, kwa mara ya kwanza nchini, kwa chama chochote cha siasa, Chama chetu cha ACT Wazalendo tulizindua, ilani ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. 

Licha ya uzinduzi wetu kuibua maoni na maswali mengi sana, miongoni mwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii; muitikio wa viongozi wagombea, wanachama wetu na wananchi mitaani umekuwa mkubwa sana.

Pamoja na mapokezi na muitikio mkubwa na mzuri katika jamii, nikiwa kiongozi wa chama, ninalazimika kujadili baadhi ya maswali na masuala kuhusu ilani yetu ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kutokana na mjadala mkubwa ulioibuka tangu tuzindue.

Kwa nini ilani?

Kwa zaidi ya miaka 30 ya demokrasia ya vyama vingi tumeshuhudia kufanyika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa; hata hivyo, tofauti na uchaguzi mkuu, uchaguzi wa Serikali za Mitaa umekuwa ukiachwa kufanyika “kiholela”. Vyama havitengi muda kufanya uchambuzi wa kisayansi utakaoongoza maamuzi ya chama, viongozi na jamii zetu, kwenye kujenga mitaa, vijiji na vitongoji imara na vilivyoendelea nchini.

Wagombea wameishia kutelekezwa na kuachwa kufanya siasa za mihemko na mazoea; zisizokuwa na maono na mipango mipana na jumuishi. Kwa lugha rahisi, ahadi na sera za uchaguzi wa Serikali za Mitaa zimekuwa zenye maono ya urefu wa pua. Ndio maana si ajabu kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuishia kujadili kuhusu ukusanyaji wa pango za minara ya simu pekee yake.

SOMA ZAIDI: Hatimaye ACT-Wazalendo Wanatoka Mafichoni?

Mtazamo huu duni na finyu unaihujumu azma, msingi na dhana nzima ya serikali za mitaa na vijiji; ambayo inalenga kuchochea maendeleo kutoka chini (mitaani na vijijini), kama inavyoelezwa kwenye ibara ya 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hali na kitendo cha kuwaacha wagombea kutumia uchaguzi huu kuzungumza kuhusu masuala ya vijiji na mitaa yao kwa utengano; yani kila kijiji kuwa na ajenda na mipango yake isiyo husiana na vijiji vingine, hususani vijiji jirani, inaleta mikanganyiko katika mchakato mzima wa maendeleo.

Utunzi wa ilani ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unakusudia kutoa dira na muelekeo wa pamoja, kama chama, kuhusiana na vijiji na mitaa tunayotaka kuijenga. Kupitia ilani hii, tunataka mitaa na vijiji vilivyopo Kibondo, Kaliua, Same, Manyoni, Kilwa, Kilombero, Ubungo, Ilemela na Kilindi viwe na hali na maendeleo yenye kuwiana; na sio mitaa ya Dar es Salaam kuendelea na vijiji Tabora na kwengineko kudumaa.

Hatuwezi kuwa na maendeleo yenye usawa na ya kweli katika vitongoji, vijiji na mitaa yote, kama hatutakuwa na mtazamo na mpango wa pamoja wa kujenga mitaa na vijiji tuvitakavyo. 

Ni kupitia ilani hii inayotupa taswira na mkakati wa kitaifa wa kujenga vijiji na mitaa iliyoendelea. Ni kupitia ilani hii tunakusudia kutoa viongozi watakao kuwa na mtazamo mpana wa ujenzi wa vijiji na mitaa kama kitovu cha maendeleo ya watu na ya kitaifa.

Uwajibikaji na Uadilifu

Uchambuzi tulioufanya katika uandishi na utunzi wa ilani ya serikali za mitaa ulibaini kuwa kilio kikubwa cha wananchi na chanzo kikubwa cha kuwa na vijiji duni ni pamoja na kuwepo kwa uongozi mbovu na jamii iliyodhorota.

Kutokana na udhaifu na ubabaifu wa chama kilichopo madarakani, hususani katika ngazi ya Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji, Chama chetu cha ACT Wazalendo tunaeleza kwa ujumla kauli mbiu na msingi wetu wa uongozi kuwa ni “Uwajibikaji na Uadilifu”.

Tunataka kuwa na viongozi watakao wajibika na waadilifu; na tunalisisitiza hili kwa kueleza kwamba; hatutaonea haya kuwafukuza uanachama viongozi wote watakaokiuka misingi hii miwili; tutawachukulia hatua kali za kisheria viongozi na watumishi wote wasiowajibika na wasiowaadilifu; tutakagua mali na mitindo ya maisha ya viongozi kabla na wakati wa uongozi wao.

Tutakitumia chama katika nyenzo ya kusimamia matendo na mienendo ya viongozi; na vivyo hivyo tutavitumia kwa ukamilifu vyombo vya kisheria kwa ajili ya kusimamia uwajibikaji na uadilifu miongoni mwa watumishi na viongozi wa serikali.

Hata hivyo, nyenzo na msingi mkuu wa kuhakikisha tunasimamia uwajibikaji na uadilifu, itakuwa ni kupitia nguvu ya wananchi. Tunasisitiza kwamba hatuwezi kuwa na viongozi au uongozi imara na madhubuti bila kuwa jamii imara na madhubuti. 

Tunahitaji kuwa na jamii itakayowasimamia viongozi katika serikali za mitaa na vijiji; na itakayo hakikisha kwamba viongozi hao wanawajibika kwa maslahi yao wananchi na sio maslahi ya mabwana wakubwa wachache.

Ni kutokana na msingi na msisitizo huu, ilani yetu inaeleza kwamba tutarejesha nguvu ya Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji mikononi mwa wananchi; na tutafanya hivyo kwa kuvijengea uwezo vyombo vya uwakilishi vya wananchi na majukwaa ya maamuzi ya wananchi. Ni rai yetu kwamba ili kuhakikisha uwajibikaji na uadilifu wa kweli, lazima wananchi ndio wawe wasimamizi wakuu wa uwajibikaji.

Ilani baada ya uchaguzi

Pamoja na kwamba ilani hii ni ilani ya Chama chetu cha ACT Wazalendo, hata hivyo, madai na maudhui ya ilani hii si ya Chama chetu, bali ni ya wananchi. Hivyo, ni kusudio letu kama chama kuhakikisha kwamba tunasimamia madai na ajenda zote zilizoorodheshwa na kuwekwa kwenye ilani hii kwa ajili ya utekelezaji ndani na nje ya chama.

Tumeshuhudia, kwa uwezeshaji wa TAMISEMI, kuna maeneo ambayo chama chetu hakitaweza kutoa uongozi wa moja kwa moja; hata hivyo hatuwezi kuyapuuza maeneo hayo kwa kuwa hayataongozwa na chama chetu. Badala yake, tunakusudia kuhakikisha ajenda, mipango na ahadi zilizoorodheshwa kwenye ilani na zinazolenga kuboresha mazingira na maisha ya Watanzania zinatekelezwa, licha ya kwamba hatutakuwa tunatoa uongozi wa moja kwa moja.

SOMA ZAIDI: Dorothy Semu: Serikali Haipaswi Kucheza na Suala la Chakula

Ni kusudio letu kuwa kupitia ilani hii, miongoni mwa mambo mengine, tutahakikisha tutoa msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa watu walioathiriwa na vitendo vya ukatili; tunaanzisha kampeni za kijamii za kujenga na uboresha makazi binafsi ya wazee, wajane na watu wenye ulemavu wenye uhitaji; tutagawa vitaulo vya kujisitiri kwa wasichana (pedi) katika shule, ili kuweka mazingira mazuri na salama kwa wanafunzi wa kike; na tutahakikisha upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada kwa ajili ya kukuza usomaji na maarifa miongoni mwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla, katika mitaa, vijiji na vitongoji vyote nchini.

Ilani hii ni dira na muongozo wetu tutakayoitumia katika kuihudumia mitaa, vijiji na vitongoji vyetu. Ilani hii ni kipimo chetu tutakachotumia wakati wa kutathmini shughuli zetu kama chama katika jamii. Ilani hii ni azimio letu la kuhakikisha serikali za mitaa, vijiji na vitongoji zinasimamia maslahi ya wote. Ilani hii ni tamko letu la kuleta tumaini, mabadiliko na maendeleo ya kweli kwa wananchi.

Dorothy Semu ni Kiongozi wa chama cha siasa cha Kiongozi wa ACT-Wazalendo na anapatikana kupitia dorothysemu@gmail.com.  Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts