The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jinsi ya Kuwasaidia Watoto Kupunguza Matumizi ya Vifaa vya Kidijitali Wakati wa Likizo

Pamoja na kwamba vifaa vya kidijitali/kielektroniki vina faida na huwapa furaha watoto, lakini pia vina madhara yake.

subscribe to our newsletter!

Msimu wa likizo umewadia, na watoto wetu wapo nyumbani. Ni wakati wa furaha na ni fursa nzuri kwa wazazi na walezi kukaa na kutumia muda wenye manufaa na watoto wao kwa mazungumzo na ushirikiano wenye tija. 

Hata hivyo, changamoto kubwa hujitokeza pale ambapo watoto wanatumia muda mwingi wakiwa mbele ya simu au TV, wakiangalia video za aina mbalimbali, zikiwemo katuni na kucheza gemu. 

Vifaa hivi vimekuwa sehemu muhimu ya burudani kwa watoto wa rika zote, na mara nyingine sisi wazazi huwahimiza kutumia vifaa hivyo, hasa kwa watoto wadogo, ili kuepusha usumbufu, na kwa wale wakubwa tukijaribu kuwathibitishia upendo na kuwajali.

Lakini, likizo hii inaweza kuwa tofauti. Tunaweza kutumia muda huu kushirikiana na kuzungumza na watoto wetu ili kuwafahamu vizuri zaidi na kuwapa nafasi ya kutufahamu vizuri kujifunza kutokana na mazingira yao, huku wakiweka vifaa vya kidijitali pembeni na kutoa kipaumbele kwenye kukuza ushirikiano wa familia na kujifunza majukumu ambayo yatakuwa muhimu na msaada kwa maisha yao ya baadae.

Pamoja na kwamba vifaa vya kidijitali/kielektroniki vina faida na huwapa furaha watoto, lakini pia vina madhara yake. Wazazi na walezi wengi wamekuwa wakipendelea kuwapa watoto vifaa vya kidijitali kama mbadala wa kukaa nao pamoja bila kufahamu madhara yake. 

Madhara

Madhara haya hutokea endapo mtoto atatumia muda mwingi kwenye skrini – kioo cha TV, simu, nakadhalika – na mara nyingi huathiri ufanisi wa ubongo wa mtoto. Utafiti wa Shirika la Madaktari wa Watoto la Marekani unaonyesha kuwa matumizi ya kupita kiasi ya skrini yanaweza kudhoofisha kumbukumbu, umakini, na uwezo wa kutatua na kukabiliana na changamoto. 

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwajengea Watoto Ufahamu Juu ya Ukatili wa Kijinsia?

Kwa watoto wadogo, haswa walio chini ya miaka tisa, athari hizi ni kubwa zaidi kwa sababu ubongo wao bado ni mteke na upo katika mchakato wa ukuaji. Aidha, tafiti zinaonesha kuwa matumizi ya kupindukia ya skrini yanaweza kusababisha viwango vya juu vya wasiwasi, mfadhaiko, na matatizo ya usingizi, yaani kukosa usingizi kabisa, au kusinzia sana.

Zaidi ya hayo, muda mwingi wa kutumia skrini mara nyingi humaanisha kukaa ndani kwa muda mrefu na kuugandisha ubongo pasipo kushughulisha katika kufikiri, kubuni, kudadisi na kutafakari, hali inayochangia mtindo wa maisha usio na mazoezi na uchangamshi wa mwili na akili. 

Hali hii inaweza kusababisha ongezeko la uzito na matatizo mengine ya kiafya na hasa afya ya akili na kuzalisha vijana wengi wenye uwezo mdogo wa kutatua changamoto.

Kwa hiyo, swali linakuja: Tunawezaje kuwasaidia watoto wetu kupunguza muda wa kutumia vifaa vya kidijitali?

Mbinu mbadala

Kwanza kabisa, wazazi na walezi tunapaswa kufikiria shughuli mbadala wa vifaa vya kielektroniki/kidijitali. Tunapaswa kuwahamasisha watoto kushiriki katika michezo na shughuli za nje katika maeneo ya wazi, kwani zinaleta manufaa makubwa kwa afya yao ya kimwili na kiakili. 

Kwa mfano, michezo kama mpira wa miguu, kombolela, au hata kushiriki shughuli za kifamilia kama kupika chakula rahisi huchangamsha mwili na akili. Tafiti zinaonesha kuwa watoto wanaoshiriki katika shughuli za nje kwa angalau saa moja kila siku huongezeka uwezo wa umakini, udhibiti wa kihisia, na uwezo wa kushirikiana na wenzao. 

SOMA ZAIDI: Una Mtoto Mwenye Umri Kati ya Miaka Miwili na Sita? Haya Yatakusaidia Kumjengea Nidhamu

Kwa watoto wadogo, badala ya kuwapa vifaa vya kidijitali, tuwapatie zana za kuchezea kama kalamu za rangi, gundi, karatasi za rangi ngumu na nyepesi, na kadhalika, ili wacheze michezo ya ubunifu itakayowasaidia kushughulisha vichwa vyao kufikiri na kudadisi.

Aidha, michezo ya nje husaidia kupunguza viwango vya msongo wa mawazo kwa kuongeza uzalishaji wa kemikali za ubongo zinazohusiana na hisia za furaha na utulivu. 

Kwa kuongeza, matembezi ya kifamilia wakati wa jioni si tu huimarisha mahusiano ya kifamilia, bali pia huchangia kuimarisha mazoezi ya mwili, ambayo ni muhimu kwa kudhibiti uzito na kukuza afya bora kwa ujumla.

Ukiachana na michezo, tunaweza kushirikiana na watoto kufanya shughuli za kibunifu kama kuchora, kupaka rangi, au kutengeneza vitu kwa kutumia vifaa vya kawaida vya nyumbani, kama vifuu vya nazi au chupa za plastiki. Ubunifu huu si tu unawaondoa watoto kwenye skrini, bali pia huwafundisha stadi muhimu za maisha.

Pia, tunaweza kuchagua siku moja kwa wiki kwa ajili ya muda wa familia ambapo tunaweza kufanya shughuli kama vile michezo ya mafumbo, karata, kucheza mziki, kuimba au kusali, kusoma vitabu na kuulizana maswali na majibu.

Hii huwa ni njia nzuri ya kujenga uhusiano mzuri na watoto wetu bila kutumia vifaa vya teknolojia. Muda huu wa kucheka na kufurahi pamoja utakuwa wa thamani kubwa kwao na watatunza kumbukumbu hiyo kuliko kumbukumbu ya kuangalia TV au kutumia simu.

SOMA ZAIDI: Watoto wa Miaka Mitano Wana Harakati Nyingi. Mbinu Hizi Zitakusaidia Kukabiliana Vizuri

Tunapaswa pia kuwafundisha watoto umuhimu wa kusaidia wengine. Watoto wanaweza kushiriki kufanya kazi ndogondogo za nyumbani, au hata kutembelea vituo vya watoto yatima na watu wenye mahitaji maalum. Matendo haya hujenga maadili ya wema na uwajibikaji wa kijamii.

Tukumbuke kwamba kupunguza muda wa kutumia vifaa vya teknolojia hakupaswi kuonekana kama adhabu kwa watoto. Kabla ya likizo kuanza, au wakati wowote ambao tutaona matumizi yamezidi, tunaweza kuwaeleza watoto mapema kwamba matumizi ya vifaa hivyo yatapunguzwa. Hii husaidia kuweka matarajio wazi na kuepusha mabishano baadaye.

Sisi wazazi pia tunapaswa kuwa mifano bora kwa kupunguza matumizi yetu ya simu na vifaa vingine vya teknolojia. Kwa kupanga ratiba iliyojaa shughuli za kuvutia zisizo na matumizi ya vifaa vya teknolojia, watoto watafurahia likizo yenye shughuli nyingi zenye manufaa kwa ukuaji wao wa mwili, akili, na kiroho.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts