Tunaendelea na makala zetu zenye maudhui ya malezi wakati wa likizo. Tarehe zile za kusafiri zimefika kwenda kusalimia babu na bibi na ndugu wengine katika maeneo mbalimbali ya nchi, hasa katika maeneo ambayo si makazi yetu ya kila siku.
Hivyo, leo tutazungumzia mbinu kadhaa zitakazotusaidia wazazi na walezi kusafiri na watoto kwa amani na furaha kulingana na makundi ya umri wa watoto. Kwa kuanzia na watoto wachanga, yaani wenye umri kati ya miaka sifuri na miwili, maandalizi ni muhimu sana ili kuhakikisha wanakuwa na utulivu safarini.
Kubeba nepi za kutosha, kanga, nguo za kubadilisha, na blanketi laini ni muhimu. Pia, tukumbuke kubeba vitu vya kuchezea, au vitabu vya picha ili kumliwaza mtoto hapa na pale, hasa anapokuwa katika mazingira mapya.
Watoto wa umri huu mara nyingi hulala muda mrefu safarini, hivyo tuandae mazingira yatakayowafanya wajihisi salama, hasa ikiwa tunasafiri kwa gari au ndege.
Lishe ni jambo la kipaumbele kwa watoto wachanga. Kama mtoto anakunywa maziwa ya chupa, tuhakikishe tunabeba chupa safi, maziwa ya unga, na maji ya moto. Safari za ndege zinapokuwa na mabadiliko ya shinikizo la hewa na hata magari kukumbana na changamoto za dharura za barabarani, kuwa na akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya mtoto ni muhimu sana na itapunguza usumbufu.
SOMA ZAIDI: Jinsi ya Kuwasaidia Watoto Kupunguza Matumizi ya Vifaa vya Kidijitali Wakati wa Likizo
Pia, kama mtoto bado ananyonya ziwa la mama, ni vyema mama uzingatie lishe yako kwa kubeba chakula na maji ya kutosha, au kuwa na akiba ya pesa ya kuhakikisha utapata chakula wakati wa dharura ili kumuwezesha mtoto kunyonya vya kutosha.
Usalama ni muhimu pia; tujitahidi kutumia kiti maalum cha gari kwa watoto wachanga, au kibebeo cha watoto kama kanga au kitenge ili kuhakikisha wanafarijika na wanalindwa wakati wote bila kusahau kufunga mikanda ya viti vyetu ili tuwe tayari kuhakikisha usalama wetu pamoja na watoto wetu.
Watoto wa umri kati ya miaka mitatu na mitano wanahitaji maandalizi ya kisaikolojia kabla ya safari. Tuwaeleze kwa maneno rahisi kuhusu safari, kwamba wanaenda wapi na kwa nini. Ushawishi wa mawazo yao katika kupanga ratiba ya safari huwasaidia kujihisi kuwa sehemu ya safari, hii inaweza kuhusisha kuwaomba watoe maoni kuhusu vitu wanavyotaka kufanya au kuona.
Ili wasisumbuke sana wakati wa safari, tuchukue vitabu vya kuchora, rangi, au midoli wanayoipenda. Hii itawashughulisha na kuwazuia kuchoka mapema. Watoto wa umri huu hula mara kwa mara, hivyo ni muhimu kuwa tayari kwa mahitaji yao ya chakula.
Hivyo, vitafunwa rahisi kama biskuti, matunda yaliyokatwa, na maji ya kunywa vinashauriwa kubebwa. Wakati wa safari, tuhakikishe wanakaa salama kwa kufunga mikanda ya usalama kwenye viti wanavyokalia na kuzingatia harakati zao kwa karibu kuepusha usumbufu kwa abiria wenzetu, na kama tupo kwenye usafiri binafsi ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwajengea Watoto Ufahamu Juu ya Ukatili wa Kijinsia?
Watoto wa umri wa shule, yaani kati ya miaka sita na 12, wanaelewa zaidi mambo yanayowazunguka, hivyo kushirikishwa katika maandalizi ya safari ni njia bora ya kuwajumuisha. Tunaweza kuwauliza maswali mbalimbali kuhusu shughuli watakazopenda kufanya, au sehemu zipi wangependa kutembelea.
Hawa wanaweza kupewa vitabu vya kusoma, vifaa vya michezo wanayoipendelea, lakini muhimu pia kuwahimiza kuangalia mazingira wakati wa safari ili kujifunza zaidi. Watoto wa umri huu pia wanaweza kusaidia katika kubeba mizigo midogo au kuandaa vitu vidogo kwa ajili ya safari hasa vinayowahusu kama nguo zao, na kadhalika.
Usafi na afya ni muhimu sana, hivyo tuhakikishe wanatumia vitakasa mikono na kufuata kanuni za usafi, hasa mkiwa maeneo yasiyo na maji safi. Pia, tuepuke kula vyakula vya njiani.
Kwa vijana, wenye umri wa miaka 13 na 17, safari ni fursa nzuri ya kuwapatia uhuru wa kuchagua na kuwashirikisha katika maamuzi. Tuwaruhusu vijana wetu wadogo kutusaidia kupanga ratiba ya safari. Hii inaweza kuwa kuchagua maeneo ya kutembelea, au shughuli zinazowavutia, kama kutembelea maeneo ya kihistoria au sehemu za burudani.
Kwa kuwa vijana wanapenda kutumia vifaa vya kidijitali, hakikisha betri za simu au tablets zimejaa kwa ajili ya kujiliwaza na kuchukua matukio ya kumbukumbu ya safari, huku ukihakikisha hawatumii muda mwingi kwenye vifaa hivyo bali tuwapatie muda wa kuzungumza nao kuweza kuwafahamu zaidi mawazo yao juu ya mambo mbalimbali ya maisha na dunia kwa ujumla, malengo, na changamoto wanazokutana nazo.
SOMA ZAIDI: Una Mtoto Mwenye Umri Kati ya Miaka Miwili na Sita? Haya Yatakusaidia Kumjengea Nidhamu
Hii itatusaidia kuongeza ukaribu nao na kufurahia safari zaidi, kitu ambacho kitaweka kumbukumbu nzuri ya mahusiano yao na wazazi na walezi wao.
Safari nyingi nzuri hupangwa mapema, hivyo tujipange kwa wakati, kwa kukata tiketi na kuthibitisha sehemu za malazi mapema. Pia, tujitahidi kufahamu sheria za usafiri zinazohusiana na watoto, kama vile kanuni za LATRA zinazoruhusu watoto wenye umri chini ya shule ya msingi kusafiri bila malipo katika mabasi.
Pia, tufahamu hospitali, au vituo vya afya, vilivyo karibu na maeneo tutakayofikia kwa ajili ya usalama wetu na wa watoto wetu.
Tunawatakia safari njema zenye furaha tele!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.