Naafiki madai ya mwanazuoni fulani kwamba labda sina haki ya kuongelea mgogoro wa chama chake ingawa, kwa kweli, sijamwona akikasirika tukivisema vyama vingine. Mimi si mwanaCHADEMA, sina chama maana nimesema tangu zamani nimeamini aheri makengeza kuliko chongo.
Napenda uhuru wangu wa kukubali au kukataa pande zote na mara nyingine, kukaa ndani ya chama inabidi uchongwe ubaki na chongo la chama chako tu.
Lakini haina maana kwamba wenye makengeza kama mimi hatufuatilii kwa ukaribu yanayotokea katika vyama, na hata kujaribu kushawishi kama raia wenye matumaini na uchungu juu ya taifa letu maana tupende, tusipende, vyama vya siasa vinaathiri maisha yetu hata kama si wanachama wa chama hiki au kile.
Katika hilo mimi, kama watu wengi, tumependa kuona CHADEMA, au ACT-Wazalendo, au vyama vile vilivyosambaratika huko nyuma kuwa na nguvu maana katika mfumo wetu usio na vyama vya kiraia vyenye nguvu, vyama vya siasa vimebaki pekee kuwajibisha chama tawala.
Ndiyo maana wengi tumefumbia macho mambo mengine kwa kutotaka kutingisha hawa waliobaki pekee. Lakini upande wangu, nilianza kuwa na mashaka makubwa, hususan dhidi ya CHADEMA, tangu chama hicho kiamue kumsimamisha waliomshutumu miaka nenda rudi kuwa mgombea wao.
Hapo chama hiki kiliitupa sera pekee iliyoeleweka na watu, sera ya kupinga ufisadi, maana, utapingaje ufisadi kwa kuweka uliyemwita fisadi kuwa mgombea wenu wa nafasi ya urais wa nchi?
Sera mbadala
Hivyo, chama tawala kilipiga makofi na kuiiba sera hiyohiyo na “kushinda” nayo. Baada ya hapo tuliona vyama vya upinzani vikinyanyaswa bila sababu na ilibidi tupiganie haki yao ya kuishi na kufanya siasa. Lakini, ukweli ni kwamba nimesubiri miaka nenda rudi, nimeuliza na kuomba mara nyingi, lakini inabidi nikiri, sijui sera mbadala za chama hiki ni zipi.
SOMA ZAIDI: CHADEMA Kuelekea 2025: Mivutano Hii Itaiacha Salama?
Ndiyo. Huwezi kushinda kwa kupinga tu. Lazima uwe na sera mbadala, sera ya elimu, ya vijana, ya wanawake, ya afya, ya maendeleo, na kadhalika. Hata kama ni muhimu kiasi gani, na kweli ni muhimu, kupigania Katiba tu hakutoshi.
Kwanza, kwa hali ilivyo, huenda tutapata Katiba mbovu zaidi wakati Katiba iliyopo wala haifuatwi. Bila mchakato shirikishi unaosimamiwa na watu wasio na chongo, tunaweza kuliwa sana. Angalia Bunge la Katiba lililopita.
Pili, na labda muhimu zaidi kwa wakati huu, ukitaka kuwavutia watu, katika hali yetu ya sasa, watu wanavutiwa na masuala ya ugumu wa maisha, au bread and butter issues kama alivyosema mwanasiasa mmoja wa Kimarekani, Bernie Sanders, akielezea kushindwa kwa Democrats kwenye uchaguzi mkuu wa taifa hilo Novemba 5, 2024.
Chama chake hakikumsikiliza na matokeo yake tunaona sasa. Haitoshi kusema kwamba tukipata Katiba Mpya tutaingia kwenye nchi ya maziwa na asali. Bread and butter issues, mambo yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, lazima yapewe kipaumbele pia.
Mambo ya wafanyakazi. Ya machinga. Ya wakulima wadogo. Ya wanawake ndani ya sekta isiyo rasmi. Ya ukuaji wa matabaka na watoto wengi kuhukumiwa kusoma katika shule mbovu. Ya waathirika wa mlipuko wa ukatili wa kijinsia. Ya watoto –na wazazi wao– wanaosoma bila kuelimika. Na kadhalika.
Ili watu waone chama chako ni kizuri zaidi kuliko ‘zimwi likujualo’ lazima waone kwamba mko upande gani katika mapambano yao ya kila siku. Labda mimi ni kiziwi na kipofu, lakini sioni na sisikii. Badala yake, naona naitwa kwenye maandamano ya kupigwa mwanzo mwisho na kuambiwa kwamba sina akili kwa sababu sikujitokeza.
Sintofahamu vyamani
Baada ya kusema hivyo, mimi sishangai, na sisumbuliwi na migogoro inayoibuka katika vyama vya siasa. Ni jambo la kawaida, tena ni uthibitisho wa uhai. Lina maana kwamba watu si misukule, hawajauza bongo zao kwa ajili ya maslahi tu. Tatizo ni kwamba, bila uwazi na usimamzi mzuri, uhai huo unaweza kusababisha kifo maana watu wanaishia kutukanana tu bila kushughulikia mzizi wa fitina.
SOMA ZAIDI: Maandamano ya CHADEMA Yalifanikiwa, Tena Sana
La kusikitisha ni kwamba, katika dunia ya leo, mara nyingi mgogoro huishia kwa wanaolinda maslahi na tabaka tawala kuwaondoa wanaopendwa na wananchi kwa sababu wanatishia maslahi na nguvu ya tabaka tawala.
Huko Uingereza, mwanasiasa Jeremy Corbyn alipendwa sana na watu na ni mtu ambaye amesimama upande sahihi wa historia tena na tena kuanzia alipopinga ukaburu akiwa kijana. Akapinga vita ya Iraq, akawaunga mkono Wapalestina dhidi ya ukaburu wa Wazayuni, na kadhalika.
Akaonesha kwamba adui wa kweli wa wananchi wa kawaida si wahamiaji, bali ni tabaka tawala linalojitajirisha juu ya migongo yao. Ndiyo maana tabaka lote tawala, wakiwemo watu wa chama chake, kwa ushirikiano wa karibu na waandishi wa habari na waandishi wao, walizua uongo na visingizio visivyoisha vya kumwondoa.
Bernie Sanders naye alikuwa mtu pekee wa kuweza kumzuia Trump, lakini alitisha tabaka tawala la Democrats pia ndiyo maana waliwapachika wagombea wa kutetea mfumo, na matokeo yake tunayajua. Mgogoro huwa unatokea watu wakiamka na kutaka kutetea maslahi ya wasio nacho. Hapa, walio nacho watafanya juu chini kuunyamazisha.
Uchambuzi wa migogoro
Katika hali hii naamini inabidi kuangalia migogoro kama hii kwa namna tatu. Na siongelei chama hiki kimoja kinachomulikwa kwa sasa ingawa inawahusu, naongelea vyama vyote vya siasa kwa ujumla wao.
Mgogoro kati ya mtu na mtu au watu na watu. Tunaangalia sifa binafsi za watu hawa. Naona ndivyo tunavyofanya sasa kwenye hili la CHADEMA, na ina umuhimu wake, lakini tofauti za watu binafsi huwa ni kama dalili za ugonjwa, si ugonjwa wenyewe.
Pili, kama tunavyoona sasa, mgogoro huwa unaibua shutuma za aina mbalimbali, zaweza kuwa za kweli au za uongo, lakini zinaathiri si wanachama tu bali hata sisi kwenye namna tunavyoviangalia vyama hivi. Vitu vilivyofichwa sasa vinaonekana wazi na tunabaki tumeduwaa. Kama hata moja ya kumi ya shutuma hizi ni za kweli, basi kuna tatizo na tunaanza kujiuliza maswali.
SOMA ZAIDI: Maandamano ya Septemba 23 ya CHADEMA na Mustakabali wa Siasa za Tanzania
Kwa nini watu wengi wenye akili waliondoka? Waliitwa wahaini lakini labda … Kwa nini wakati chama tawala kinatumia mbinu ya kutembea nchi nzima kufanya kazi vijijini, kampeni nyingi za wapinzani ziliishia kwenye wilaya moja au mbili tu?
Ni wazi kwamba hawana hela kama watawala wetu, lakini nakumbuka wakati nazungumza na mtu aliyekuwa miongoni mwa watu wa kwanzakwanza kujiunga na TANU. Yeye naye alikuwa amegundua kwamba CCM si mama yake.
Nilimuuliza kwa nini asijiunge na watu na kuanzisha chama kingine. Akacheka na kusema: “Bwana wee! Enzi zile tulitembea kwa mguu kijiji hadi kijiji kuwahamasisha watu, bila hata posho. Sasa nimezeeka, nitaweza kweli? Ni kazi ya kizazi kingine.”
Naam, kama alivyosema mwanazuoni Frantz Fanon, Each generation must, out of relative obscurity, discover its mission, fulfill it, or betray it. Kwa tafsiri isiyo rasmi sana, anasema Inabidi kila kizazi, kutoka pale wasipoonekana kiasi, kutambua dhamira yake, kuitimiza au kuisaliti.
Vizazi vinavyofuata kizazi cha kupigania uhuru, ndani ya chama tawala na kwenye vyama vya upinzani, vipi? Jibu unalo!
Suala la itikadi
Na hapo tunakuja kwenye suala la tatu, ambalo si la chama hiki kimoja, suala la itikadi. Yawezekana maslahi tu yanatosha kuwaunganisha watu, hasa wale wenye nafasi. Kwa nini niache maslahi niliyonayo na kuingia msituni bila kujua kama nitafanikiwa?
Kweli aheri nusu mkate. Na pia, hakuna chama kitakatifu duniani, hivyo, ngoja nivumilie kasoro zilizopo, au siyo kuvumilia bali kujaribu kurekebisha ndani kwa ndani.
SOMA ZAIDI: Kamata Kamata ya Wanachama na Viongozi wa CHADEMA Yaendelea. Lissu, Mnyika na Sugu Wakamatwa
Kumbe, suala lisiloshughulikiwa linakuwa kama saratani. Linazidi kukua hatimaye suala la itikadi litaibuka hata katika vyama ambavyo si zao la mapambano ya kitabaka bali vyama vinavyotegemea ruzuku ya dola. Na hapo naona mgogoro uliopo katika CHADEMA kimsingi ni suala la itikadi, na la tabaka. Ni mkinzano ambao umekuwepo tangu mwanzo.
Upande mmoja chama kilianzishwa na watu wenye itikadi ya kibepari na waliopinga sera ya ujamaa ya chama tawala. Walisema wenyewe na kudai ubepari ndio ukombozi wa wote.
Lakini wananchi wengi waliona kitu tofauti. Walikiona chama kama kimbilio la wote waliochoka mfumo wa chama tawala, hivyo walikiunga mkono, si kwa sababu ya itikadi, bali kwa sababu walitamani mabadiliko, na bila shaka si mabadiliko ya kuwanufaisha mabepari.
Naona mkinzano huu sasa ndio kiini cha mgogoro huu. Matumaini ya watu ni yale ya itikadi ya waanzilishi wa chama hiki? Labda ndiyo maana hatuoni sera kwa sababu chini kwa chini, hakuna makubaliano juu ya hayo.
Hivyo, kweli tunawaona watu wenyewe maana ni muhimu pia. Kweli tunashitushwa na malumbano na “siri zinazofichuka” hadi tunajiuliza watu waliiishije pamoja miaka yote hii.
Lakini, naamini kwamba suala la msingi ni mkinzano utakaokumba vyama vyote vya siasa kwa kadiri pengo kati ya walala hoi na walalahai linazidi kuongezeka na ahadi za maisha bora zinaonekana hazitatimia maana si kwamba hazijatekelezwa bado, bali ni kwa sababu hazitekelezeki.
Mwisho wa siku, kilicho cha muhimu si sura bali sera!
Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.