The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Watanzania Walioipeperusha Vyema Bendera ya Taifa 2024, Kongole

Tunawapongeza kwa huduma zao hizo kwa jamii, na kutumai kwamba kutambuliwa kwao huko kutawahamasisha wengine kubuni mbinu anuwai zitakazowawezesha kuzitumikia vyema jamii zao.

subscribe to our newsletter!

Tungependa kutumia siku hizi chache zilizobakia za mwaka 2024 kuwapa maua yao, kama inavyopendwa kusemwa siku hizi, baadhi ya Watanzania walioiwakilisha vyema Tanzania mwaka huu, wakipaisha heshima na sifa za nchi yao na wananchi wenzao.

Wapo wengi walioing’arisha Tanzania 2024 katika nyanja tofauti, na tungependa, kwa kuanzia, kumuorodhesha hapa Faustine Ndugulile ambaye mnamo Agosti 27, 2024, alipata imani ya wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN), na kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Afya la Dunia (WHO), Kanda ya Afrika.

Dk Ndugulile, ambaye alinyakua wadhifa huo akihudumu kama Mbunge wa Kigamboni (Chama cha Mapinduzi – CCM), alikuwa anatarajiwa kumrithi Dk Matshidiso Moeti, raia wa Bostwana, ambaye alikuwa anahitimisha uongozi wake baada ya kulihudumia shirika hilo la UN kwa kipindi cha miaka mitano.

Hata hivyo, Dk Ndugulile hakuweza kuishi kuihudumia nafasi hiyo kwani alifariki mnamo Novemba 27, 2024, nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu. Tanzania imetangaza kwamba badala yake itamtuma Profesa Mohamed Janabi, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kujaza nafasi hiyo.

Dk Ndugulile atakumbukwa kama kiongozi na mwanasiasa aliyejali maadili ya uongozi na yale ya kitaaluma, asiyekuwa na hofu ya kusimamia misingi hiyo hata pale misimamo yake inapoonekana kukinzana na misimamo ya mamlaka za kiuteuzi. Alilidhihirisha hili kwenye namna alivyolikabili janga la UVIKO-19 wakati akiwa Naibu Waziri wa Afya mnamo mwaka 2020.

Lydia wa Her Initiative

Mwingine katika orodha hii ni Lydia Charles Moyo, mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Her Initiative, shirika lisilo la kiserikali linalowajengea uwezo wa kifedha mabinti, ambaye alitangazwa kuwa mshindi wa King Baudouin Foundation Africa Prize kwa mwaka 2024.

SOMA ZAIDI: Hongera TFF kwa Tuzo, Lakini Bado Maboresho Yanahitajika

Lydia alipokea tuzo hiyo katika hafla maalumu iliyofanyika jijini Brussels, Ubelgiji, Juni 27, 2024, na kuhudhuriwa na Mfalme Philippe wa Ubelgiji, viongozi wengine wa Serikali ya Ubelgiji, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao hapa Brussels.

Lydia na timu yake wanakisiwa kuwafikia wasichana zaidi ya 31,000, na kuwapatia mafunzo ya kifedha, mbinu za kidijitali na nyingine za kifedha zinazolenga kuwawezesha kubadilisha maisha yao. Sambamba na tuzo hiyo, Lydia na timu yake pia walijishindia €200,000, sawa na Shilingi milioni 504 za Kitanzania, kusaidia kwenye shughuli zao.

Lydia ametajwa pia kama mshindi wa Tuzo ya Global Citizen kwa mwaka 2024. Tuzo hii huandaliwa kwa ajili ya kuwasherehekea na kuwafurahia viongozi na wanaharakati kutoka duniani kote wanaobuni mbinu anuwai za kukabiliana na changamoto za kijamii.

Profesa Manji wa MUHAS

Hapa pia tungependa kumuorodhesha Karim Manji, profesa kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS) ambaye mnamo Septemba 27, 2024, alipokea tuzo ya Harvard T.H Chan School of Public Health Alumni Merit Award 2024, au tuzo ya mhitimu bora wa Chuo Kikuu cha Harvard.

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, tuzo hiyo hutolewa kwa aliyewahi kuwa mhitimu wa chuo hicho mashuhuri kwa wanafunzi ‘vipanga’ duniani na aliyejitoa kwa ajili ya afya ya jamii. Profesa Manji, akiwa Mtanzania wa kwanza kuwahi kupata tuzo hiyo, aliipokea tuzo hiyo mjini Boston, Marekani.

SOMA ZAIDI: Furaha, Hamasa Zatawala Msimu wa Pili wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu

Kwenye orodha pia yumo Dk Never Mwambela, mwanasayansi na mbunifu aliyeibuka mshindi wa tuzo ya Agroecological Food Futures Prize 2024

Ubunifu wake wa mbinu ya kukabiliana na waharibifu mazao, inayotunza mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, ijulikanayo kama Vuruga Biocide, uliibuka kama ubunifu bora miongoni mwa bunifu nyingine 200 zilizoshindanishwa Afrika Mashariki.

Dk Mwambela, ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Plant Biodefenders, alipokea tuzo hiyo Disemba 5, 2024, jijini Kigali, Rwanda, iliyoambatana na Dola za Kimarekani 20,000, sawa na Shilingi milioni 48.4 za Kitanzania. 

Hatusahau watoto

Hatutakuwa tumeitendea haki orodha hii kama hatutamjumuisha mtoto Barka Seif Mpanda ambaye Septemba 27, 2024, alitangazwa mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya kifakhari ya Ballon d’Or of the Champions Dream, huko nchini Hispania.

Barka, aliyepo kwenye akademi ya CF Damm ya Hispania, anaripotiwa kuonesha uwezo wa hali ya juu ndani ya msimu huo, hali iliyopelekea kuwashinda wachezaji wengine wa kimataifa waliokuwa wakiiwania tuzo hiyo.

SOMA ZAIDI: Kutumia Takwimu Pekee Tuzo za TFF ni Usumbufu

Tukibaki hapo hapo kwa watoto, tunamuorodhesha pia mtoto Neev Chohan, ambaye Oktoba 7, 2024, alitangazwa mshindi kwenye mashindano ya dunia ya Shindano la Sanaa la Gari la Ndoto la Toyota.

Shindano hilo hufanyika kila mwaka ambapo watoto, wenye umri wa miaka nane mpaka 11, hushiriki kwa kuchora gari ambalo wanadhani wanaweza kulitengeneza. Neev, mtoto wa Kitanzania, ndiye aliyeweza kuibuka mshindi wa shindano hilo kwa bara zima la Afrika kwa mwaka huu wa 2024.

Kwa niaba yetu sote hapa, The Chanzo ingependa kuwapongeza Watanzania hawa, na wengine wengi walioipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwa mwaka huu wa 2024, na ambao hatujabahatika kuwaweka hapa, kwa huduma zao wanazoendelea kuifanyia Tanzania na dunia kwa ujumla.

Tunatumai kwamba huduma zao hizo muhimu sana, na kutambuliwa kwao huko kunakostahili, kutakuwa chachu ya hamasa kwa wananchi wengine zaidi kubuni mbinu na shughuli zitakazotoa mchango chanya na kulisukuma taifa mbele na kufanikisha malengo yake ya kimaendeleo, ikiwemo lile la kukuza uchumi wa nchi na wananchi na kupunguza umasikini.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts