Ndugu Katibu Mkuu, Amani iwe nawe!
Ni imani yangu kuwa barua hii itakufikia ukiwa mwenye afya njema, ukiendelea na majukumu ya kulitumikia taifa letu ambalo leo tunasherekea Uhuru wa Tanganyika, moja ya nchi inayounda Tanzania.
Nianze kwa kukupongeza kwa kazi nzuri ya kukitumikia Chama cha Mapinduzi ambacho ndio chama kilichopigania Uhuru wa nchi yetu licha ya changamoto nyingi. Kwa muda uliodumu katika nafasi hiyo, ni hakika umeonesha uwezo, uzalendo, maono, bidii na uvumilivu mkubwa.
Umeonesha kuwa kuongoza ni kuonyesha njia; kusikiliza na si kufoka; kushirikisha na si kuamrisha; kufikika na si kutisha na, muhimu zaidi, kuwa mtoa matumaini kwa wengine ndani ya chama chetu.
Ndugu Katibu Mkuu, ninazo sababu kuu mbili ya kukuandikia barua hii.
Moja ni kukutaarifu hujuma ninayofanyiwa na viongozi wa Chama cha Mapinduzi, wilaya na mkoa wa Simiyu. Mimi ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya wilaya ya Bariadi kutoka kundi la vijana niliechaguliwa Oktoba 2, 2022, kwa kura 656.
Nimekuwa nikikosa kualikwa kwenye vikao halali bila taarifa yoyote ile, hivyo nimekuwa nikijipeleka hata nisipopata mwaliko ndani ya vikao hivyo, nikihoji kwa nini mimi sialikwi kwa taarifa maalum, sipewi sababu yoyote ile.
SOMA : Abdul Nondo Ahofiwa Kutekwa
Hili ni tatizo maana mjumbe anao uhalali wa kualikwa kwenye vikao ili kukidhi akidi ya vikao na uhalali wake. Kundi la vijana ni kundi muhimu, linahitaji wawakilishi ndani ya vikao vya Halmashauri Kuu na sivinginevyo.
Ndugu Katibu Mkuu, sababu nyingine kuu hasa ya kuandika barua hii ni pamoja na kutoa taarifa juu ya kutekwa kwangu baada ya kupigiwa simu na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) wilaya ya Bariadi aitwaye Tinana Masanja.
Ndugu Katibu Mkuu, kipindi cha nyuma hatujawahi kuwa na matukio haya ndani ya wilaya ya Bariadi pamoja na mkoa wote wa Simiyu.
Ndugu Katibu Mkuu, suala la kutekwa kwangu, nikateswa kwa kupigwa na mikanda, bisibisi, plaizi, ngumi, mateke na kunisababishia ulemavu wa mwili hadi sasa limetokana na kutofautiana kwangu kimawazo na Mkuu wa Mkoa wa sasa, Kenani Laban Kihongosi.
Yeye anaamini kwenye kutumia nguvu kuongoza wananchi wanaokinzana nae kimtazamo na kimawazo, kinyume kabisa na falsafa, pamoja na mingozo ya Chama cha Mapinduzi.
Kabla ya hapo aliwahikunitisha kwa kunitumia ujumbe kwenye WhatsApp, akisema kuwa atanishughulikia. Haikuishia hapo, pia aliwahi kunitishia kwenye msiba wa Mwenyekiti wa CCM, wilaya ya Bariadi, Septemba 21, 2024, kuwa atafanya vita na mimi pamoja na kunipoteza kama nitaendelea na tabia hiyo ya kukosoa na kutoa maoni penye changamoto.
Ndugu Katibu Mkuu, chama chetu kinaamini kwenye uhuru wa kutoa mawazo na maoni, na pia uhuru wa kuishi kama Katiba ya nchi inavyotaka. Nakuomba, hili jambo la kutekwa kwangu lifanyiwe uchunguzi wa kina ili haki yangu ipatikane maana Jeshi la Polisi mkoa wa Simiyu nilienda kuripoti Novemba 28, 2024, na kupewa RB BAT/RB/2102/2024.
Hata hivyo, ndugu Katibu Mkuu, bado kuna ukakasi wa uchunguzi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wote waliohusika na kuniteka. Pamoja na hayo, watuhumiwa wote niliowataja wapo uraiani, na nina wasiwasi na maisha yangu hadi sasa.
Ningeomba pia kupitia wewe uongee na mamlaka za kiuteuzi juu ya jambo hili la Mkuu wa Mkoa kutishia watu wanaotoa maoni kinyume na yeye zimuite na kumkanya, hata kumpa majukumu mengine nje ya mkoa huu maana nashindwa kuishi kwa amani.
Maisha yangu yako matatani sababu ya utoaji maoni ndani ya mkoa wangu; na pia mamlaka ya uteuzi zifanye uchunguzi wa kina kwa wananchi wengine ili ipate maoni juu ya huyu kiongozi anaetishia watu wake anaowaongoza kwa lugha za matusi.
Mwenyezi Mungu yu pamoja nawe.
Wako katika Kazi
Levinus Kidamabi
Mwandishi amejitambulisha kama kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoka wilaya ya Simiyu, mkoa wa Simiyu. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.
One Response
Inatisha sana hii hali kama CCM tunafanyiana haya je hao wengine? Pole sana kijana