The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mikoko:Uhifadhi wa Bahari Unaoangamizwa na Shughuli za Kibinadamu Zanzibar

Wadau waonya kuwa mikoko iko katika hatari ya kupotea ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Kuna hali ya kustaajabisha, kupendezesha macho na kuliwaza kila wakati macho yanapokutana na utando wa mikoko, iliyojikita pembezoni wa fukwe za Zanzibar.

Ukijani wake unapopigwa na mwanga wa jua, na kugonga katika kingo za maji ya bahari yanayozunguka mikoko hiyo,inatengeneza picha ambayo ni vigumu kuisahau, ni utambulisho wa kipekee, kila eneo ambapo mikoko inaposimama, ni kama muhuri wa asili.

Hii ndiyo hali niliyoiona hapa katika kijiji cha Kishelisheli, kilichopo wilaya ya Mjini Magahribi, nilipofika kufuatilia hali ya utunzaji wa mikoko.

“Tumeshindwa kuilinda mikoko,” ananieleza mwenyeji wangu Maryam Ali Haji (74), mama wa watoto saba, kauli anayoitumia ni kama mama anayesikitika kushindwa kulinda mtoto wake. Kuna hali ya uchungu ambayo ni ngumu kuitathmini kama haujaona tofauti ya mikoko iliyotunzwa na sehemu mikoko ikiwa imekatwa.

Marym ni mmoja ya wadau wanaounda kikundi cha mazingira ni uhai, kikundi chenye miaka minne kinachoangalia namna ya kuitunza mikoko katika eneo hili.

“Tulianza kama wana kikundi tukiwa watu wanne pamoja na kiongozi wa mtaa, [tukafanya jukumu la] kulinda mikoko ya hapa kwetu,” Maryam ananieleza tukiendelea kuzunguka katika eneo hili.

“Ila niseme ukweli kwa miaka zaidi ya 20 ni kwamba tumeshindwa kuilinda mikoko. Mimi sijasoma ila niliweza kusimamia suala hili la kuitunza hii mikoko yetu kwa kuwa na vikao kadhaa na wenzangu na makubaliano ila bado wenzangu watoto wao wakawa wanakata wakaturudisha nyuma,” Maryam anafafanua zaidi.

Kasi ya upotevu wa mikoko

Ukiacha faida ya kupendezesha mazingira, mikoko ina kazi kubwa katika kulinda ustahimilivu wa mazingira ya bahari. Kwanza inazuia mmonyoko wa sehemu za fukwe na kingo za bahari pale hali ya bahari inapochafuka, umbo lake na muundo wa mizizi yake ni kama kuzuizi cha asili katika bahari. Misitu ya mikoko inatajwa kuweza kupunguza majanga mbalimbali ya baharini ikiwemo Tsunami.

Mikoko pia ni moja ya hifadhi ya muhimu ya viumbe mbalimbali wa baharini ikiwemo samaki. Lakini pia mikoko  hufanya kazi kama chujio la asili linalohakikisha maji ya bahari yanaendelea kuwa katika hali nzuri kulinda uhai wote katika bahari.

Hata hivyo kuna hali ya hatari juu ya Mikoko ya Zanzibar. Ripoti ya Sensa ya Misitu ya mwaka 2013 iliyofanywa na Idara za Misitu Zanzibar, ilionesha kuwa visiwani hapa kuna hekta 16,488 za mikoko, ambapo kwa Pemba kulikuwa na hekta 11,214 na Unguja kulikuwa na hekta 5, 274.  

Ripoti hiyo ilionesha kuwa kila mwaka eneo la mikoko linapungua kwa asilimia 4, hii ikiwa na maana kwamba kwa kipindi cha miaka 10 kutoka mwaka 2013 hadi 2023 hekta takribani 647 za mikoko zitakuwa zimepotea. 

Hayfa Nassor ni mwafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), anayemalizia mosomo ya elimu yake ya Shahada ya Umahiri kwenye masuala ya Rasimali Hai na Mabadiliko ya Tabianchi. Hayfa amefanya utafiti juu ya kupotea kwa miti ya mikoko kwenye eneo la Kisakakasa lililopo wilaya ya Magharibi B, mkoa Mjini Magharibi kwa kipindi cha miaka 30 kuanzia mwaka 1990 hadi 2020. Eneo hilo lilikuwa na hekta 360 za mikoko ila hadi kufikia mwaka 2020 hekta zilizopo ni 217.

Hifadhi ya Mikoko ya Uzi ,kabla ya kukatwa kupisha ujenzi wa daraja

“Kwa kipindi cha miaka hiyo 30 inaonesha kwamba mikoko mingi imepotea kwa sababu ya shughuli za kibinadamu na wingi wa ongezeko la watu kwenye shughuli za uchomaji mkaa na uuzaji wa miti hiyo kwa ajili ya ujenzi,” anaeleza Hafya.

Upotevu huu wa misitu wa mikoko umeanza kuathiri hata hali ya kipato ya watu wanaozunguka maeneo ambapo mikoko ilikua ni jambo la kawaida.

Seif Said Mshenga (56) ni mvuvi wa kaa katika kijiji cha Kishelisheli ambaye hapo awali alikuwa akimiliki mashua ya kuvulia. Mshenga ambaye pia ni Mwalimu, anaelezea namna maisha yao yalivyoathirika kutokana na ukataji mikoko. 

“Enzi hizo wazungu wakija hapa kuona mikoko walikuwa wakilipa 40,000 hadi 60,000 na hizo pesa zilisaidia sana kujengwa shule uliyoiona kule barabarani na pamoja na kituo cha afya, hayo ni mapato ya hii koko inayomalizika,” anaeleza Mshenga.

Mshenga ambaye anaishi kijijini hapa na mkewe akiwa ni baba wa watoto watatu ambapo kati yao wawili wameshafariki akanieleza kuwa watu wanaokata mikoko wamekuwa wakiikata kwa msumeno, zana ambayo inapelekea mimea hiyo ikikatwa usichipue tena.

Visiwani hapa miti ya mikoko hutumika sana kutengenezea dari, lakini pia mkaa imara ambao watumiaji wake hudai kuwa hauishi haraka na ni ghali sana, ambapo kwa gunia moja huuzwa hadi Shilingi 90,000. 

Juhudi zaidi zinahitajika

Nikiendelea kutembelea maeneo ya mikoko nilikwenda hadi kijiji cha Michamvi Kae, kilichopo Wilaya ya Kusini, mkoa wa Kusini Unguja, kwa ajili ya kuona ni kwa jinsi gani wanajamii wake hutunza mikoko na kuitumia kama sehemu ya utalii. 

Nilikutana na Vuai Idi Mlenge( 48) mjumbe wa kamati ya mazingira katika kijiji hapa, akanieleza kwamba kijiji hicho kinaithamini sana mikoko na kinailinda kwa kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kuikata au hata kuchukua mti wake uliokakuka. 

Vuai Iddi Mlenge, Katibu wa Kikundi Cha Mazingira cha Utunzanji Mikoko huko Michamvi Kae

“Hapa kila mtu ni mlinzi na huwezi kukata au kutoka na mti wake hadi ukafika barabarani hujakamatwa, maana sisi hii mikoko watalii na wajasiriamali wanatulipa kuja kuitizama,” amesema Mlenge huku akiwa ananionesha sehemu ya mikoko iliyostawi vizuri. 

Yussuf Zubeir ni mmoja wa wanufaika wa utalii wa mikoko ambapo amekuwa akitumia mashua ndogo kuwatembeza watalii mbalimbali ambao wamekuwa wakifika kijijini hapo kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo.  

“Nimewekeza hapa na vijana saba wamepata nafasi ya kuonesha ujuzi wao na sisi tumenunua mashua ndogo za kutembea katikati ya msitu huu wa mikoko na watalii wanatulipa,” anasema Zubeir ambaye pia ni mwanamazingira na mwanzilishi wa kituo cha YUSUP kinachofanya kazi ya kutembeza watalii kwenye mikoko. 

Zubeir anaeleza toka mwaka 2023 tayari wamaeshapanda mikoko zaidi ya 2000 kwa kushirikiana na wadau. Mafanikio ya Kijiji cha Michamvi Kae yanaweza kufanywa chachu ya maeneo mengine hasa kwa kuonesha faida zinazopatikana mikoko ikitunzwa.

Hata hivyo takwimu za serikali zinaonesha muamko wa kupanda mikoko unashuka kadri muda unavyoenda. Takwimu kutoka Idara ya Misitu Zanzibar zinaonesha kuwa kwa mwaka 2018 jumla ya mikoko hekta 55.5 zilipandwa, mwaka 2019 hekta 3.5 zilipandwa, mwaka 2020 zilipandwa hekta nane na mwaka 2021 hekta 13.5 za mikoko zilipandwa. Hata hivyo kwa mwaka 2022 na 2023 ni hekta 5.5 zilizopandwa pekee kwa kila mwaka.

“Serikali tunachofanya ni kulinda misitu hii na kuwakumbusha wananchi kuwa mikoko ni sehemu ya kuleta samaki na sehemu ya kujipatia fedha na kuwainua kiuchumi kupitia utalii, ” anaeleza Mwatima Abdallah Khamis Afisa Misitu ya Jamii kutoka Idara ya Misitu Zanzibar.

Moja ya jambo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi ni juu ya kuweka mizania hasa katika kilimo cha mwani, ambapo kilimo hiki muhimu kwa uchumi wa wengi  ila kimekua kikichangia ukataji wa mikoko.

“Serikali inahimia sana watu wafanye kilimo cha mwani ila huku wananchi wanakata mikoko kwa ajili ya kilimo hicho,” anaeleza Mbarouk Mussa Omar ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Community Forests Pemba (CFP).

Jitihada zaidi zinahitajika kuhakikisha Zanzibar haipotezi urithi wake wa mikoko, kwa faida za muda mfupi, mipango pia ya kuitunza mikoko na kudhibiti maeneo yanayoruhusiwa uvunaji wa mikoko inahitajika.

Najjat Omar ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Zanzibar, anapatikana kupitia najjatomar@gmail.com 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. I’m a freelance journalist resides in Tanga

    I want to contribute my news story both in English and Swahili Languages.

    Send me email address to post feature, photo and newsstory

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts