The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tukumbushane Mambo Muhimu Tunayohitaji Katika Kuwaandaa Watoto kwa Mwaka Mpya wa Shule

Kwa msaada wa tafiti za kisayansi na mbinu bora za malezi, tunaweza kuhakikisha kuwa watoto wetu wanakuwa na mazingira bora ya kufanikiwa.

subscribe to our newsletter!

Kama wazazi na walezi tunafurahi mno kuona watoto wetu wakifanikiwa na kufanya vizuri shuleni. Mafanikio yao si matokeo ya bahati, bali ni jitihada za watoto, walimu na maandalizi thabiti na msaada endelevu tunaoonyesha katika safari yao ya elimu. 

Hivyo, ni muhimu kuhakikisha kuwa tunawaandaa vyema mwanzoni mwa mwaka wa shule, na pia tunawaunga mkono kadri mwaka unavyoendelea.

Kwa msaada wa tafiti za kisayansi na mbinu bora za malezi, tunaweza kuhakikisha kuwa watoto wetu wanakuwa na mazingira bora ya kufanikiwa. Leo tujikumbushe mambo muhimu tunayohitaji kufanya kuwaandaa watoto kwa ajili ya mwaka mpya wa shule.

Kwanza kabisa, tuendelee kudumisha uhusiano wa karibu na watoto wetu. Watoto wenye uhusiano mzuri na wazazi wao hufanya vizuri zaidi shuleni. 

Tafiti zinaonyesha kuwa mazungumzo ya mara kwa mara kati ya wazazi na watoto huongeza ujasiri wa mtoto na kuboresha utendaji wake wa kitaaluma. Hii inajumuisha kutenga muda wa kuzungumza na watoto mara kwa mara na kufuatilia maisha yao ya shule.

Kwa watoto wa shule za bweni, tunaweza kuwatembelea katika siku zilizoainishwa na shule na kuzungumza nao ana kwa ana na pia kupitia barua, au njia nyingine ya mawasiliano Inayoruhusiwa na shule.

SOMA ZAIDI: Sikukuu Zisitufanye Tuzembee Ulinzi wa Watoto Wetu. Waovu Hawalali Tukisherehekea

Tutengeneze mazingira rafiki ya kujifunzia nyumbani. Tafiti zinasema kwamba watoto wanaofanya kazi za nyumbani katika mazingira tulivu na yanayofaa hupata alama bora zaidi shuleni. 

Hivyo, tujitahidi kuwapatia watoto sehemu nzuri ya kusomea aidha chumbani kwao au sehemu yoyote itakayofaa nyumbani yenye meza na kiti vya kusomea pamoja na vifaa vyote muhimu kama vitabu na vifaa vya kuandikia. Hata wale wasioweza kupata viti na meza wahakikishiwe mazingira rafiki na tulivu hapo nyumbani.

Pia, tuwe tunafuatilia kazi zao za nyumbani na kuondoa vikwazo kama runinga au michezo ya video wakati wa masomo inayoweza kuwapotezea umakini katika kazi zao.

Tushirikiane vizuri na walimu wa watoto wetu. Ukweli ni kwamba tukishirikiana na walimu, maendeleo ya kitaaluma ya watoto huboreshwa. Tafiti zinaonesha kwamba wazazi wanaoshirikiana na walimu huimarisha maendeleo ya kitaaluma ya watoto kwa asilimia 20 zaidi.

Tufanye juhudi za kuwasiliana mara kwa mara na walimu, kuhudhuria mikutano ya wazazi, na kufuatilia maendeleo ya watoto wetu shuleni. Ushirikiano wetu utasaidia kutambua changamoto wanazopitia watoto wetu pamoja na waalimu wao kuweka mikakati ya kuzitatua mapema.

Tuwapatie watoto mahitaji yao muhimu ya shule. Tafiti zinaonyesha kuwa watoto wanaokosa vifaa muhimu kama vitabu na sare za shule wanakumbana na changamoto kubwa katika masomo. Kwa mfano, ripoti ya UNESCO, Global Education Monitoring, inaonyesha kuwa upatikanaji wa vifaa vya shule unaongeza uwezekano wa kufaulu kwa mtoto kwa asilimia 40.

SOMA ZAIDI: Dondoo Chache za Kutusaidia Kusafiri na Watoto Msimu Huu wa Sikukuu

Basi tujitahidi kuwapatia watoto wetu vitabu,, sare, na vifaa vya michezo, nauli au chakula cha mchana kwa wale wa shule za kutwa na pia ada za masomo ya ziada pale inapohitajika.

Tujenge malengo ya mwaka pamoja na watoto wetu. Tafiti zinasema kuwa watoto walio na malengo mahususi hujitahidi zaidi kufanikisha ndoto zao haswa pale wanapowezeshwa na mzazi au mlezi. 

Malengo kama kuboresha alama za somo flani, au kujifunza stadi mpya ya maisha, ni mifano mizuri. Tunaweza kuwahimiza watoto kuweka jitihada kufikia malengo hayo kwa kuwapa motisha ya ziada, kama kuwapa zawadi ndogo, au kuwapongeza kwa kuwasifia wanapofanikisha malengo yao.

Kwa mfano: “Ukipata alama nzuri, tutakwenda sehemu unayoipenda.” Hii itawatia moyo kuweka juhudi zaidi.

Pia, tunaweza kuandaa ratiba ambayo inajumuisha muda wa kuamka, kula, na kulala, muda wa masomo, mapumziko, na michezo na muda wa kushirikiana na familia. Tafiti zinaonesha kwamba ratiba thabiti husaidia watoto kusimamia muda wao vizuri, kuboresha umakini wao shuleni, na kufanikisha malengo yao ya kielimu na kijamii.

Tuhimize mwenendo wa maisha wenye afya njema. Tafiti zinaonyesha watoto wanaoshiriki mazoezi mara kwa mara na kula lishe bora hupata ufanisi mkubwa wa kitaaluma.

SOMA ZAIDI: Jinsi ya Kuwasaidia Watoto Kupunguza Matumizi ya Vifaa vya Kidijitali Wakati wa Likizo

Tuhakikishe watoto wetu wanashiriki mazoezi mara kwa mara, wanakula mlo wenye virutubisho muhimu kama matunda, mboga, na protini na wanapata nuda wa kupumzika walau masaa 7-9 kulingana na umri wao. Afya bora inachangia ukuaji mzuri wa kimwili na kiakili kwa binadamu wote haswa watoto.

Pia, tufahamu kwamba afya njema ya kihisia huwapa watoto msingi thabiti wa mafanikio. Tujitahidi kuwafundisha mbinu za kukabiliana na msongo wa mawazo, tuwatie moyo na kuwasifia kwa juhudi zao hata wanapokosea na tuwape nafasi ya kueleza matarajio na changamoto zao.

Kwa kuchukua hatua hizi, tutakuwa tumewapa watoto wetu msingi thabiti wa kufanikiwa shuleni na maishani katika mwaka 2025. Tukumbuke kuwa tunawekeza katika maisha ya mbeleni ya watoto wetu kwa kuwaandaa sasa hivi.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts