The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Fahamu Mbinu Zinazoweza Kuimarisha Mawasiliano Kati ya Mtoto na Mzazi

Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba familia zinazoimarisha maadili na kuwasiliana vizuri hujenga kizazi cha watoto wenye ujasiri na maadili mema

subscribe to our newsletter!

Mwaka mpya unatoa nafasi nzuri ya kutafakari mambo yaliyopita na kupanga kwa ajili ya yajayo. Hii siyo tu kwa watu wazima bali pia kwa watoto. Kama wazazi, huu ni wakati muafaka wa kuimarisha uhusiano na watoto wetu kwa kuzungumza nao, kuonesha mshikamano wa kifamilia, na kutanabaisha maadili yanayoongoza familia zetu.

Tafiti zinaonesha kwamba watoto wanaoishi katika familia zinazoweka mawasiliano wazi, na kufuata maadili thabiti, huwa na ustawi wa kihisia na kijamii wa hali ya juu. Hivyo, tuanze mwaka huu kwa kuzungumza na watoto wetu, kuelewa mahitaji yao, na kujenga misingi imara ya kukuza na kuendeleza maadili ya familia.

Kama wazazi, au walezi, tunaweza kufanikisha hili kwa kuwauliza watoto maswali rahisi na yenye maana yatakayowasaidia kutafakari kuhusu maisha yao na kuimarisha uhusiano baina yetu. Yafuatayo ni baadhi ya maswali na kile yanayowezesha kuzalisha kwenye kuboresha mahusiano ya mzazi, au mlezi, na mtoto.

Ni kitu gani kilikufurahisha sana mwaka uliopita?

Swali hili linawasaidia watoto kutafakari mambo mazuri yaliyowatokea na kuwajenga kuwa na mtazamo wa shukrani. Ikiwa mtoto amesema alipenda kushinda mashindano shuleni, tunaweza kutumia fursa hiyo kumpongeza na kumtia moyo kufanya vizuri zaidi.

Ni jambo gani ulitamani lingekuwa tofauti mwaka jana?

Hii ni fursa ya kuzungumzia changamoto zao na kufikiria njia za kuzitatua mwaka huu. Mtoto akisema alihisi upweke wakati fulani, tunaweza kujadili njia za kumsaidia asijiskie hivyo.

Ungependa kujifunza au kujaribu kitu gani kipya mwaka huu?

SOMA ZAIDI: Tukumbushane Mambo Muhimu Tunayohitaji Katika Kuwaandaa Watoto kwa Mwaka Mpya wa Shule

Swali hili linahamasisha udadisi na kuwasaidia kuweka malengo mapya kwa mwaka 2025. Ikiwa mtoto angependa kujifunza kucheza mpira wa miguu, masuala ya teknolojia au kuchora, tunaweza kujitahidi kupanga ratiba ya mafunzo pamoja naye ili kumuwezesha kufikia ndoto zake.

Nawezaje kuwa mzazi bora kwako mwaka huu?

Swali hili linaonesha kuwa tunathamini maoni ya watoto wetu, jambo linalojenga uaminifu na heshima. Mtoto akisema angependa tuongeze muda wa kucheza naye, kusoma naye, kufanya matembezi nk. tunaweza kupanga siku maalum za kufanya hayo

Ungependa tufanye nini kama familia mwaka huu?

Shughuli za kifamilia huimarisha mshikamano na kuunda kumbukumbu nzuri za pamoja. Hivyo maoni ya mtoto kwenye hili yakizingatiwa yataimarisha uhusiano na ushirikiano wa familia.

Pamoja na kwamba maswali haya yanawasaidia watoto kuutafakari mwaka uliopita na kujiandaa na mwaka huu, maswali haya pia hujenga nafasi ya kutafakari maadili gani tunataka watoto wetu wajifunze mwaka huu wanavyozidi kukua pamoja na kujitathmini mwenendo wetu wa malezi kama wazazi.

Kama tunavyofahamu, maadili ya familia ni dira inayoelekeza mwenendo wa kila mmoja katika familia. Ni muhimu kuyahuisha ili kuhakikisha kila mtu anayaelewa na kuyatekeleza.

SOMA ZAIDI: Sikukuu Zisitufanye Tuzembee Ulinzi wa Watoto Wetu. Waovu Hawalali Tukisherehekea

Tuzungumze na watoto wetu na kuwauliza kama wanafahamu familia yao inasimamia misingi gani ya maadili. Majibu yao yanaweza kutuonesha mtazamo wao na kuanzisha mjadala. 

Tukiwa tunazungumza nao tujitahidi kutafsiri maadili tunayotaka kuwafundisha kwa maneno rahisi sana sana kwa watoto wadogo. Mfano, kuwa mkweli au kusaidiana yanaweza kufafanuliwa kwa mifano rahisi kama Ukimuahidi rafiki yako kitu, ni muhimu kukitimiza au Leo tutashirikiana kufua nguo na kupika chakula cha usiku. Na kuhakikisha mambo hayo yanatekelezeka.

Ili watoto waweze kuyaishi maadili haya inatupasa kuyafanya sehemu ya mwenendo wa maisha ya familia zetu. Tunaweza kufanya hivyo kwa kutengeneza ratiba, au shughuli mfano, kila Ijumaa inaweza kuwa ni siku ya shukrani, ambapo tunakaa na watoto wetu kuzungumza nao kuhusu umuhimu wa shukrani na hata kuwauliza katika wiki ni jambo gani ambalo wanashukuru lilitokea.

Mazungumzo ya wazi kama hayo yanawawezesha watoto kujihisi salama kihisia hivyo kuyashika maadili hayo kwa urahisi. Tafiti zinaonesha kuwa watoto wanaopata msaada wa kihisia kutoka kwa wazazi huwa na ustahimilivu mkubwa wanapokutana na changamoto.

Tunaweza kuimarisha mawasiliano na watoto wetu ili kuwa na mazungumzo ya wazi kwa kuwapa watoto nafasi ya kusema wanachohisi bila kuwakatisha au kuwahukumu. 

SOMA ZAIDI: Dondoo Chache za Kutusaidia Kusafiri na Watoto Msimu Huu wa Sikukuu

Tunaweza kuewaelezea changamoto zetu binafsi au malengo yetu ya mwaka mpya, uwazi wetu kwao utawafanya wawe wazi kwetu. Mfano: “Mwaka jana nilipitia changamoto kazini, kazi zilikua nyingi, lakini nilijifunza kupanga muda wangu vizuri zaidi.” Na kama tulivyoeleza hapo juu tuweke ratiba maalumu kila wiki ya kuwa na mazungumzo ya kifamilia ili kila mtu awe na nafasi ya kueleza mawazo yake.

Haya yote tuliozungumza leo ni muhimu kwa sababu yanaimarisha uwezo wa watoto wa kuelewa hisia zao na za wengine, jambo linalochangia ustawi wa kijamii. Familia zinazoimarisha maadili na kuwasiliana vizuri hujenga kizazi cha watoto wenye ujasiri na maadili mema.

Tujiulize leo, familia zetu zina misingi ya maadili ipi na ni mambo gani tungependa kuwafundisha watoto wetu.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. Mambo mazuri mmeyataja ktk malezi ya watoto wetu. Wanangu wawili wamemaliza vyuo na wameanza kazi. Wawili wa kike bado wako vyuoni mwaka wa tatu na wapili. Tunajitahidi lakini huyo wa kike mdogo ni msiri sana.
    Hafunguki hata kwa mamae mzazi. Tutumie mbinu gani?

    1. Ahsante sana kwa swali lako ndugu Msale. Hongera pia kwa kazi nzuri ya malezi hadi kupata vijana wakubwa waliofikia elimu ya juu. Je?, huyu mdogo ni mmoja kati ya mabinti waliopo chuoni?, kama ni wa chuoni huna budi kuheshimu faragha yake kwakuwa ameshakuwa mtu mzima japo kwako mzazi anakuwa bado ni mtoto. Kikubwa unachoweza kufanya ni kuzidi kuzungumza nae mara kwa mara kwa kumtia moyo kwa mazuri na mafanikio anayoyaonesha, kuonesha ushirikiano nae na kumfanya atambue kuwa unaheshimu maamuzi yake ya usiri huku ukimhasa kutoweka siri zenye madhara kwake au kwa familia. Jitahidi sana kama mzazi usitoe kauli za lawama mara kwa mara na Kama akionesha kitendo au dalili zinazoashiria kuhatarisha maisha yake au kusababisha madhara kwake na kwa familia, usizungumzie hilo jambo kwa muda huo, jipe muda wa kurağa Kari, kushusha jazba na hofu kwanza ndipo mlizungumzie kwa namna ya majadiliano na si lawama, tuhuma, viapo na vitisho. Jitahidi kumwambia kila mara kwamba upo kwa ajili ya kumsikiliza atakapokuwa tayari kukushirikisha.

      Kama mtoto anayeongelewa ni mdogo zaidi kati ya miaka tisa hadi umri wa sekondari, kaa nae chini na kumuuliza maswali yafuatayo:, 1. Ni tabia au vitendo gani nafanya au kuonesha vinavyokufanya ujihisi nakupenda na kukujali? 2. Ni jambo gani ambalo wakati mwingine nalifanya linakutia hofu, woga au huzuni na unafikiri nawezaje kurekebisha ili kufanya vizuri? 3. Je, unadhani mimi ni msikilizaji mzuri na nakupa nafasi ya kuzungumza pale unapotaka kinielezea jambo fulani?. Uliza maswali haya kwa njia ya majadiliano na katika wasaa wa kawaida kama vile mnapata kifungua kinywa, mnangalia runinga , mmepumzika tu nyumbani ,mpo mgahawani au matembezeni. Hii itasaidia kujenga misingi ya uwazi na majadiliano baina yenu hata akiwa mkubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts