Moja ya vitabu nilivyovisoma mwanzoni mwa mwaka huu wa 2025 ni kile cha mwandishi na mshairi wa Kiingereza, George Orwell, kiitwacho Animal Farm, ambacho, kwa tafsiri isiyo rasmi, nitakiita Shamba la Wanyama kwenye uhakiki wake huu mfupi.
Kitabu hiki kilichapishwa mnamo mwaka 1945, kipindi cha Vita ya Pili ya Dunia ambapo maeneo mengi yalikuwa katika machafuko. Orwell ni miongoni mwa waandishi nguli na wanaovutia katika uga wa fasihi andishi. Ujumbe mahususi katika kitabu hiki unaakisi waziwazi hulka ya binadamu na hali ya kisiasa na uongozi tunayoishuhudia duniani, na hata hapa kwetu Tanzania.
Shamba la Wanyama ni istiara ya kihistoria ambapo wanyama wanapanga mapinduzi dhidi ya mwanadamu. Wanapinga uonevu, dhuluma na utawala wa kiimla uliokithiri. Bwana Jones, kama mmiliki wa shamba mwanadamu, alitumia ujeuri na ulaghai kushikilia mamlaka na hakujali haki na hali za wanyama.
Baada ya wanyama kuvumilia mateso na manyanyaso mengi, hatimaye siku moja, Nguruwe mmoja mzee sana aitwaye Old Major, aliitisha kikao cha wanyama wote kwa siri katika kasri fulani.
Old Major aliwaeleza wanyama wenzake jinsi, Jones anavyowatumikisha wanyama kufanya kazi zake na kuvuna matunda ya juhudi zao kwa faida yake mwenyewe, huku wao wakiishi kwa mateso. Alifafanua, na kusisitiza, namna ambavyo maisha ya wanyama yamekuwa ya kilio na kusaga meno kutokana na tamaa ya wanadamu. Hivyo, kwa azma, lazima waungane bila kujali tofauti zao, ili kujikomboa na kujenga jamii ya usawa.
Siku chache baada ya Old Major kufa, wanyama wote, kwa pamoja, walifanikiwa kufanya mapinduzi na kuchukua madaraka. Baada ya mapinduzi, Jones na wafanyakazi wake walifukuzwa kisha shamba likabaki chini ya uongozi wa wanyama wenyewe wakiongozwa na nguruwe wawili kwa majina ya Napoleon na Snowball.
SOMA ZAIDI: ‘Elimu Isipomkomboa Maskini, Basi Ndoto Yake ni Kuwa Mnyonyaji’
Awali, kipindi cha harakati za kudai uhuru wanyama wote walikuwa sawa sawia. Walitengeneza katiba yao yenye vipengele vizuri vilivyompa kila mmoja haki na uhuru wa kuishi. Moja ya vipengele hivyo kilisema kwamba wanyama wote ni sawa, hakuna mnyama atakayemuua mnyama mwingine na hakuna mnyama atakayekunywa pombe kama wafanyavyo wanadamu.
Wanyama walivyoona hizo sheria nzuri walifurahi na kujiaminisha kuwa sasa maisha wameyapatia; shamba linakuwa mali yao na salama. Kweli wakawa na umiliki shirikishi na ushirika wa shamba. Wakawa wanakaa pamoja kujadili mambo, kupiga kura, na kupitisha maamuzi mbalimbali.
Kuanza kwa hila
Baada ya muda mfupi, Napoleon, ambaye ndiye pekee alijua kusoma na kuandika, akabadilika visivyo kimkakati, si kwa bahati mbaya, na akaanza kuwafanyia hila wenzake, kuwatia hofu na kuwateka; wengine kwa mabavu na wengine kimahaba kwa kuwageuza mateja na chawa.
Ama kweli, lila na fila havitengamani, alisema mfasihi wa Kiingereza William Shakespeare. Mnyama yeyote aliyempinga Napoleon akageuka adui. Nguruwe kwa jina la Snowball alikuwa wa kwanza kukiona cha mtemakuni na kushugulikiwa ipasavyo, alafu kufukuzwa uhamishoni, nje ya shamba.
Taratibu bila taabu ya dhamira, na bila haki, uonevu ulitamalaki. Ule utamaduni wa mijadala ya pamoja kuhusu mustakabali wa shamba ukaisha. Sasa shamba likawa linaendeshwa kwa naksi na utashi wa Napoleon pekee yake.
Napoleon akaanza kuwaaminisha wanyama kuwa kazi yake ya kusoma na kuwasaidia wanyama kuelewa nini cha kufanya inahitaji utulivu wa hali ya juu. Na kwa kuwa yeye “anawatumikia wengine” usiku na mchana, akaomba aruhusiwe kuishi kwenye nyumba ya binadamu ingawa hatalalia godoro. Wanyama wakakubali.
SOMA ZAIDI: Kwaheri Amir Sudi Andanenga, Tanzania Itakukumbuka Daima
Punde si punde, lile katazo la wanyama wote kutokunywa pombe likabadilishwa, hatimaye Napoleon na nguruwe wengine wachache wakaanza, kama mzaha, kunywa pombe kidogo bila kulewa. Hayo yote ni kwa kisingizio kuwa kazi yao ni nyeti, hivyo wanahitaji kujiburudisha kidogo ili kuwa timamu.
Kwa hiyo, hali na ari ya wanyama wengine shambani iliendelea kuzorota, maana hata amri ya wanyama kutoshirikiana na wanadamu nayo ikaota mbawa; Napoleon akaanza kuwa karibu na mwanadamu kama mshirika na mrika wake kwa kuwauzia maziwa, mayai na baadhi ya wanyama kama farasi aliyeitwa Boxer.
Ingawa wanyama wote walikuwa sawa, kinadharia, baadhi yao, kama nguruwe, walikuwa na usawa zaidi kuliko wenzao. Wanyama kama mbwa wakawa karibu na Napoleon kama walinzi. Wanyama kama punda kwa jina la Benjamini walikaa kimya licha ya kujua mpango mzima wa kushamiri na kustawi kwa udikteta.
Kanuni za usawa zikatupwa chini, wanyama wakakosa haki na usawa waliotarajia. Ndoto ya ukombozi ikapotea na demokrasia ikazikwa shimoni. Wanyama wakaanza kusema, “Heri utumwa wa kwanza kuliko wa sasa!”
Muktadha wa riwaya
Riwaya hii imeandikwa katika dhana ya anthropomofiki, yaani sifa, hisia na hulka za binadamu zimefanywa na kutekelezwa na wanyama, ili kusawiri mapinduzi ya kiutawala yaliyofanyika huko Urusi miaka ya 1917. Baada ya mapinduzi, Joseph Stalin na viongozi wenzake walikengeuka na kugeuka kuwa madikteta waliojifanya miungu watu.
Orwell alitunga riwaya hii katika kipindi ambacho misukosuko na migogoro mingi ilitamalaki ulimwenguni kote. Vita ya Pili vya Dunia, mfululizo wa mapinduzi, vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na vita baridi vilishamiri. Orwell aliamua kutumia fasihi kukemea ubinafsi, uchoyo, na rushwa ambazo ndizo zilikuwa sababu kubwa ya machafuko.
SOMA ZAIDI: ‘Binadamu na Maendeleo’ Kinaonesha Kazi Tanzania Inapaswa Kufanya Kufanikisha Dira Alizohubiri Nyerere
Shamba la Wanyama linaashiria mataifa fukara ya ulimwenguni, ilhali wanyama wanaashiria wananchi ambao hupambana na uongozi mbaya na umaskini unaotengenezwa kwa sera mbaya za ukoloni-mamboleo.
Mafunzo
Riwaya hii inamuachia msomaji mafunzo mengi, ikiwemo lile la kwamba madaraka hulevya. Katika historia ya chochoro za madaraka hilo la madaraka kulevya lipo wazi tena mubashara kila uchao. Ndiyo maana wahenga walisema kuwa “Si pesa pekee inayofukua nafsi ya mtu, hata mapenzi na madaraka pia.”
Utamu wa madaraka huwalevya watu na kuwafanya wasitake kuyaachia kwa wengine. Ni muhimu kupunguza madaraka yasiwe chini ya kundi fulani, au mtu mmoja. Ukomo wa madaraka ni tunu ya kidemokrasia. Sehemu nyingi duniani watawala wanatumia wananchi na matatizo yao kama dodoki kupata wanachokitaka kisha kuwatelekeza.
Na hili lilitabiriwa na wataalamu wa sayansi ya siasa kama Thomas Hobbes. Athari na hatari ya udikteta – uwe wa mtu mmoja dhidi ya wengi au wengi dhidi ya wachache – katika riwaya ipo waziwazi. Wanyama kama nguruwe walitumia mbinu zote za kiimla kama kueneza hofu, siasa za viinimacho, na kueneza propaganda za kupumbaza umma ili kubaki madarakani.
Pia, kuna somo juu ya usaliti wa kisiasa. Toka awali lengo la mapinduzi lilikuwa bora, ambapo ni kuundwa kwa jamii ya haki na maendeleo kwa wote, lakini baada ya nguruwe kufanya figisu wanyama wengine walipoteza imani na kususia harakati zozote za mageuzi ya kweli. Tafsiri yake ni kuwa nguruwe alifanya utapeli wa imani ya wanyama kwa maslahi yake finyu.
Na mwisho, tunaona kuwa elimu ya kiraia na kushiriki kikamilifu masuala ya umma ni funzo katika kitabu hiki. Raia kama vile wanyama katika shamba walishindwa kutambua mapema harufu na ishara za kidikteta za nguruwe, hasa alipoanza kuvunja sheria na kujilimbikizia madaraka na mali.
SOMA ZAIDI: Zainab Burhani Anavyouchora Mchango Chanya wa Baba Katika Malezi ya Watoto Kwenye ‘Mali ya Maskini’
Kumbe, kutoa elimu ya uraia, kusambaza taarifa sahihi bila kulishwa propaganda na kukuza mijadala kuhusu maendeleo, katiba na haki jamii husaidia katika kuimarisha taasisi na uwajibikaji.
Katika jamii yeyote, lazima kuwe na nia na njia ya kudhibiti mianya inayodhoofisha utawala bora, demokrasia na haki. Watu wakishapewa elimu tunduizi, watajua hata pale na namna gani Serikali inavunja Katiba ya nchi, iwe katika kunyanyasa wananchi, kuiba kura, rushwa na kutakasa maovu.
Isaac Mdindile ni mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira. Kwa mrejesho anapatikana kupitia ezyone.one@gmail.com au X kama @IsaacGaitanJr. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.