Katika familia, na jamii kwa ujumla, baba ni nguzo thabiti ya ustawi. Baba ana nafasi ya kipekee katika kuunda msingi wa maadili, hisia, na maarifa kwa watoto wake. Ni muhimu kutambua mabadiliko yanayoendelea katika dhana ya u-baba, huku tukisisItiza mchango mkubwa wa akina baba walio makini na kuhimiza mbinu bora za kuimarisha malezi ya watoto katika familia.
Tafiti zinaonesha wazi kwamba ushiriki wa baba anayejitolea kikamilifu una athari chanya kwa maendeleo ya mtoto. Watoto walio na baba wanaojihusisha nao kwa karibu wana tabia ya kujiamini zaidi, hufanya vyema katika masomo, na kuwa na uhusiano mzuri wa kijamii. Kwa Tanzania, mila na desturi pia zimejenga msingi wa familia zenye mshikamano pale wazazi wote wawili wanaposhirikiana.
Jukumu la baba mara nyingi hutafsiriwa kama ni kulinda na kuhudumia familia, haswa kifedha na kuwa “mtafutaji.” Katika malezi, akina baba mara nyingi huchukuliwa kama waadabishaji tu wa watoto, dhana hii huwaonesha baba kama watu “wakali” na wanaopaswa kuogopwa na watoto.
Hali hii ina hatari ya kupunguza ushiriki wa akina baba kihisia katika familia na katika suala zima la malezi. Hivyo, kuhimiza uwajibikaji wa pamoja kati ya mzazi wa kiume na wa kike katika malezi ya watoto ni muhimu, hatuna budi kubadili mitazamo hasi ya kijamii ili tuanze kuwaona wanaume kama walezi wakamilifu.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024 kutoka Huduma ya Simu kwa Mtoto namba 116, asilimia kubwa ya wahusika wa matukio ya Ukatili Dhidi ya Watoto na Ukatili wa Kijinsia walikuwa ni akina baba. Hii ni changamoto kubwa, lakini pia ni fursa ya kuwaelimisha wanaume kuhusu jukumu lao la kulinda na kuimarisha familia zao.
SOMA ZAIDI: Leo Tuzungumze Mchango wa Kauli Chanya za Wazazi Katika Ukuaji wa Hisia, Akili wa Watoto
Akina baba wana nafasi ya kipekee ya kuvunja mnyororo wa ukatili kwa kueneza heshima, huruma, na mbinu za utatuzi wa migogoro zenye amani, upendo na majadiliano.
Akina baba tunaweza kunikisha hili kwa kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuweka kipaumbele katika kuwa na mawasiliano chanya na watoto wetu, kwa kuhakikisha tunazungumza nao mara kwa mara, tunasikiliza ndoto, changamoto, na mawazo yao kwa umakini. Mawasiliano mazuri huimarisha uhusiano na hujenga uaminifu kati yetu na wao.
Uwepo wetu katika maisha ya watoto wetu na wake zetu ni muhimu mno. Uwepo huu sio tu kimwili bali na kihisia pia. Tujenge hali ya urafiki nyumbani kwetu ili tusionekane kama watu wakuogopwa. Tunaweza fanya hivyo kwa kushiriki shughuli za pamoja kama kukaa pamoja na kupiga stori/soga za hapa na pale, kucheza pamoja na kuwasaidia watoto kazi za shule.
Tuwe mifano ya kuigwa. Watoto hujifunza kutokana na kile wanachokiona. Tukiwaonesha uaminifu, huruma, na heshima kupitia matendo yetu, watatuiga, ila tukiwaonesha ukali, dharau na ukatili wataiga tabia hizo pia.
Wazazi wa kiume tujifunze kutofautisha kati ya malezi na matunzo. Matunzo ni pale tunapohakikisha watoto wamepata mahitaji muhimu kama chakula, malazi, makazi, matibabu na elimu na malezi ni pale tunapokuwepo kwenye maisha ya kila siku na watoto wetu kwa kufanya yote yaliyotajwa hapo juu. Hıi itatusaidia wakina baba kushiriki kikamilifu katika malezi na kuvunja mtazamo hasi dhidi yetu kwenye jamii.
SOMA ZAIDI: Fahamu Mbinu Zinazoweza Kuimarisha Mawasiliano Kati ya Mtoto na Mzazi
Elimu ni msingi wa maisha mazuri kwa watoto wetu, hivyo tuhakikishe tunaweka juhudi zetu zote katika kuwapeleka watoto – wa kike na wa kiume – shule. Pia, tushirikiane kikamilifu katika elimu kuhudhuria wito na hafla zao za shule na kuhimiza mafanikio yao pale wanapofanya vizuri na kuwaelekeza kwa upendo pale wanapokosea.
Kwa familia zilizotengana, tunahamasishwa kuwa na malezi ya pamoja, au co-parenting kwa kimombo, ambayo hufafanuliwa kama jukumu la pamoja la kuwalea watoto baada ya talaka au wazazi kutengana.Tafiti zinaonesha kwamba malezi ya pamoja yenye mafanikio yanahitaji mawasiliano, kuheshimiana, na ushiriki wa mara kwa mara kutoka kwa wazazi wote wawili.
Pia, inatupasa kusimama imara dhidi ya aina yoyote ya ukatili katika familia zetu na jamii. Tujifunze kustahimili hisia zetu ili tuwe na mbinu za malezi zisizo za vurugu au mafadhaiko, na tuwahimize wengine katika jamii kufanya hivyo.
Tukumbuke kuwa kuheshimu maadili ya tamaduni zetu haituzuii kuhamasisha usawa wa kijinsia na mahusiano chanya katika jamii zetu, na hasa katika utekelezaji wa jukumu la malezi kwa watoto wetu.
Kuwawezesha wanaume kukumbatia jukumu la kuwa wazazi zaidi na si baba tu ni jambo linalohitaji mabadiliko ya kijamii. Kampeni kama “Fathers Matter” za ICS na mipango ya Parenting Africa hutoa mafunzo na rasilimali kuwasaidia wazazi wa kiume kukabiliana na changamoto za malezi.
Hivyo basi, tuwapongeze na kuwaunga mkono wanaume kama baba bora, tukitambua kuwa tunaweza kuwa wazazi na walezi kamili tukikusudia kuwa hivyo.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.