Kuna sababu nyingi za Serikali kumpa uraia mgeni yeyote anayeutaka baada ya kuuomba na kufikia sifa zilizowekwa kisheria, yaani akili timamu, umri na mambo mengine.
Kwa kawaida, sifa hizo ni pamoja na kuishi nchini kwa takriban miaka 10, huku katika mwaka ambao anaomba uraia, awe ameishi nchini kwa miezi 12 mfululizo. Yaani, kama alikuwa ameishi kwa miaka saba, basi miezi 12 ya mwaka wa saba awe ameishi miezi 12 mfululizo ndani ya mipaka ya Tanzania.
Lakini sheria pia inampa Waziri wa Mambo ya Ndani mamlaka ya kumpa mgeni uraia na uamuzi wake usikatiwe rufaa wala kuhojiwa mahakamani, yaani kuiomba mahakama ipitie upya uamuzi huo.
Ingawa sheria zinaeleza moja kwa moja, ni lazima kuwe na taratibu za kumuwezesha waziri kufanya uamuzi ambao hauwezi kukatiwa rufaa wala kuombewa mapitio mahakamani, kuondoa hisia zozote, au tuhuma, za kufanya uamuzi kwa maslahi binafsi.
Wiki iliyoisha Jumamosi ilikuwa na mjadala mkubwa baada ya klabu ya Singida Big Stars kutoa taarifa kuwa wachezaji wake watatu – Josephat Arthur Bada kutoka Ivory Coast, Mohamed Camara (Guinea) na Emmanuel Keyekehi (Ghana) – wameombewa na kupewa uraia wa Tanzania ili kuiwezesha klabu hiyo kujaza nafasi hizo kwa kununua wachezaji wengine wa kigeni.
Sifa za uraia
Baadaye Wizara ya Mambo ya Ndani ikathibitisha hilo, ikisema kuwa walipewa uraia kwa kutumia vifungu Nambari 9 na 23 vya Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 357.
SOMA ZAIDI: Yanga Haikufanya Uamuzi Sahihi kwa Wakati Sahihi Ilipoamua Kuachana na Miguel Gamondi
Kifungu Nambari 9 cha sheria hiyo kinazungumzia sifa za mgeni anayetakiwa kuomba uraia, kwamba awe ana uwezo huo wa kuomba uraia, anayekidhi vigezo vilivyowekwa katika jedwali la pili la sheria hiyo. Kifungu hicho pia kinasema awe ni yule aliyezaliwa ndani ya mipaka ya Tanzania au nje na ambaye amejaza fomu za kuukana uraia wake wa awali.
Kifungu namba 23 kinakinga uamuzi wa kumpa uraia mgeni huyo, awe ni yule mwenye sifa ya uhalifu, ujasusi au mwenye sifa ya ukwepa kodi. Sheria haitaji kasoro hizo bali inasema kuwa uamuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani utakuwa ni wa mwisho na haitaruhusiwa kuukatia rufani, au kuiomba mahakama iupitie upya.
Kama uligundua baadaye kuwa aliyepewa uraia ni jasusi ambaye amekuwa akisakwa miaka kadhaa, kaa kimya. Acha sifa zake zingine mbaya ambazo anaweza kuwa nazo!
Awali, mjadala ulilenga katika kuhusisha uamuzi huo na mikakati ya Serikali na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) ya kujenga timu imara kwa ajili ya fainali za mashindano ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) yatakayofanyika mwezi Agosti na zile za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2027.
Kanuni za FIFA
Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), ni vigumu kwa raia wa nchi moja kuchezea nyingine kama hana asili hata chembe ya nchi anayotaka aichezee baada ya kubadili uraia.
SOMA ZAIDI: ‘Ilala ni Soka’ Ina Lengo Zuri Kukuza Soka Ngazi ya Vitongoji. Lakini Kuna Kasoro za Msingi
Kwa mujibu wa kanuni ya kuanzia 15 hadi 18, mchezaji ambaye anaweza kupewa kibali cha kuchezea taifa jingine lililompa uraia kama alizaliwa ndani ya mipaka ya taifa hilo, au mzazi wake mmoja alizaliwa ndani ya taifa hilo, au babu au bibi yake alizaliwa ndani ya mipaka ya taifa hilo, au awe ni yule aliyeishi ndani ya taifa hilo kwa angalau miaka mitano mfululizo baada ya kufikisha umri wa miaka 18.
Yako masharti mengi, lakini kwa kifu unaona kuwa ni vigumu kwa wachezaji hao watatu kuchezea timu yetu ya taifa, au wengine ambao klabu nyingine zinakusudia kuwasilisha maombi ya kutaka wapewe uraia wa Tanzania.
Kwa hiyo, uamuzi huo hauna jambo lolote lile kwa maslahi ya moja kwa moja ya taifa, labda yale ambayo yamekuwa yakisemwa siku zote kuwa wageni watasaidia kuchangamsha wachezaji wazawa ili nao wakuze viwango vyao, jambo ambalo hatujaona likisaidia tangu takriban miongo miwili tangu tuanza kuruhusu wageni waje kucheza ligi yetu ya juu.
Walichoweza kufanya hawa wageni ni kusaidia kutangaza ligi yetu kwa sababu kwa ubora wao wamewezesha klabu zetu kupambana katika kiwango kinachokaribiana na timu kutoka mataifa ya kaskazini na magharibi mwa Afrika, ambazo zimekuwa zikitawala soka barani.
Hali mbaya
Tulianzia wachezaji watatu wa kigeni na leo tuna wachezaji 12 wanaoruhusiwa kusajili ndani ya msimu mmoja, huku 11 wakiruhusiwa kuanza kikosini. Lakini hali inazidi kuwa mbaya kwa kuwa mahitaji ya wachezaji wageni yanaongezeka, kiasi kwamba hata zile klabu zilizokuwa zikitegemea wazawa, nazo zimeingia katika mkumbo huo wa kusaka wageni.
SOMA ZAIDI: Tanzania Inahitaji Wachezaji Wenye Moyo wa Messi
Na kwa uamuzi huo wa Idara ya Uhamiaji kuwapa wachezaji watatu wa Singida BS uraia wa Tanzania, hali inaweza kuwa mbaya zaidi katika nchi ambayo ligi yake ya juu inamiminika fedha kutoka kampuni zinazowekeza, huku asilimia kubwa ya vijana wazawa wakiwa wanakua bila ya kupata mafunzo yoyote rasmi ya mpira wa miguu.
Kwa mchezaji ambaye hajapata mafunzo rasmi na sahihi ya mpira wa miguu hadi kufikisha miaka 17, atakuwa katika nafasi finyu sana kushindana na mchezaji kama Gibril Silla wa Azam au wakati ule Kipre Junior. Haikuwa rahisi kwa mchezaji mzawa kumpokonya namba Kipre Junior na si rahisi kwa sasa kwa mzawa kumpokonya namba Silla.
Kwa hiyo, ni kujidanganya kama tunataka kuanza kuwapa uraia wageni eti waje waongeze ushindani kwa wachezaji wazawa na hivyo kukuza vipaji na kukuza mpira wetu.
Kama tunataka kukuza vipaji vya wazawa, au mpira wetu kwa ujumla, hatutakiwi kutumia njia za mkato bali njia zilizojaribiwa kote duniani na zimedhihirisha ufanisi. Kwa hiyo, si vizuri kutafuta njia za mkato kwa ajili ya kutafuta mafanikio na sifa za bandia.
Ni lazima tukubali kufuata mchakato ambao kwa kawaida ni mrefu ili kuliweka soka letu sehemu ya juu na salama isiyotetereshwa na kuporomoka kiwango kwa wachezaji wachache.
Hivyo, kama Idara ya Uhamiaji, au wizara kwa ujumla, ilipata ushauri kutoka mamlaka za soka kuruhusu watatu hao kupewa uraia, ni muhimu kujiuliza, na ikiwezekana kubatilisha, uamuzi huo kwa manufaa ya soka la Tanzania, ajira za wazawa na uchumi wa nchi kwa ujumla.
SOMA ZAIDI: FIFA Yatoa Kanuni Mpya za Uhamisho wa Wachezaji. Klabu Zetu Zinafuatilia?
Katika picha kubwa, naamini athari za uamuzi huu si kwa mpira wa miguu pekee, bali sekta nyingine zote ambazo, kwa namna moja au nyingine, zinategemea ujuzi na ustadi wa wageni wachache kufanikisha shughuli zake.
Sipati picha halisi ya hali itakuwaje iwapo klabu 15 zilizobaki za Ligi Kuu zitaomba angalau wachezaji wake watatu wapewe uraia. Sipati picha kama sekta nyingine zote zitafuata mkondo huo wa kuombea uraia watumishi wake ambao hawakidhi vigezo vya kawaida vilivyowekwa kisheria.
Idara ya Uhamiaji, au wizara, hazina budi kusimamisha suala hilo na kukaribishja maoni tofauti ya wadau kabla ya kuweka misingi ya maamuzi ya kuwapa uraia wanamichezo tofauti na sheria ya sasa inavyoeleza.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.