The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Ni Wakati Sasa Tuanze Kuwatazama Waokota Taka Rejeshi Kwa Jicho la Tatu

Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na wadau wengine, kama vile wa mazingira, inapaswa kuchukua hatua za haraka kutambua mchango wao na kuboresha mazingira ya kazi yao.

subscribe to our newsletter!

Utunzaji wa mazingira ni moja ya masuala muhimu duniani kote, na waokota taka rejeshi wanachangia kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kwamba taka zinazoweza kuchakatwa zinarejeshwa katika mzunguko badala ya kutupwa. 

Hata hivyo, kutokana na kutoonekana kwa mchango wao katika sera za usimamizi wa taka nchini Tanzania, waokota taka rejeshi wanakosa fursa za kiuchumi na kijamii.

Katika muktadha wa uchumi rejelevu, ambapo rasilimali zinachakatwa na kutumika tena, waokota taka rejeshi ni sehemu muhimu ya mfumo wa utunzaji wa mazingira. 

Ripoti ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa ya 2019, na ile ya mwaka 2013 kutoka Shirika la Kazi Duniani zinaonyesha kwamba mchango wa waokota taka ni mkubwa katika kupunguza taka na kuongeza upatikanaji wa bidhaa zinazochakatwa, hivyo kuchangia katika uhifadhi wa rasilimali asili. 

Wanapochakata taka, wanapunguza hitaji la kutumia malighafi mpya, na kwa hiyo kulinda mazingira na kukuza uchumi rejelevu.

Waokota taka rejeshi wanachukua jukumu muhimu katika uchumi wa mzunguko, ambapo bidhaa huchakatwa na kurejeshwa katika mzunguko. Hivyo, mchango wao ni mkubwa katika kupunguza taka na kuongeza upatikanaji wa bidhaa zinazochakatwa. 

SOMA ZAIDI: NEMC Kufanyia Kazi Madai ya Uharibifu wa Mazingira Unaofanywa na Kiwanda cha Wachina

Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya mwaka 2013 inaangazia mchango mkubwa wa waokota taka katika ukuaji wa uchumi rejelevu, hasa katika muktadha wa uchumi wa mzunguko na endelevu. 

Waokota taka wanachangia katika kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira, kupunguza matumizi ya malighafi, na kuongeza kasi ya kurejesha bidhaa zilizozalishwa.

Changamoto

Waokota taka rejeshi nchini Tanzania wanakutana na changamoto mbalimbali, ikiwemo malipo duni, ambapo bei ya chupa za plastiki inayolipwa ni kidogo sana, kutoka Shilingi 100 hadi 500 kwa kilo moja, ambayo ni kidogo ukilinganisha na juhudi wanazoweka.

Changamoto nyingine ni udanganyifu wa vipimo na mizani. Waokota taka wanakutana na udanganyifu kuhusu vipimo na mizani, ambapo mara nyingi wanalipwa kidogo kuliko kile wanachostahili.

Pia, mtazamo hasi wa jamii, ni changamoto nyingine. Waokota taka mara nyingi wanakutana na unyanyapaa wa kijamii, ambapo jamii inawaona kama watu wasio na hadhi au wahalifu.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa vifaa na ulinzi. Waokota taka wanahitaji vifaa vya kujilinda kutokana na hatari za afya zinazotokana na mazingira ya kazi yao, lakini hawapati vifaa hivyo kwa urahisi. 

SOMA ZAIDI: Wadau Waitaka Tanzania Kuwa na Tahadhari Katika Kuhamia Kwenye Nishati Safi

Utafiti uliofanywa na Mtandao wa Waokota Taka Rejeshi Dar es Salaam (MTAWADA) mwaka 2024 unaonyesha kwamba waokota taka katika jiji la Dar es Salaam hufanya kazi kwa saa 10 hadi 15 na kutembea kati ya kilometa 15 hadi 45, huku wakikusanya wastani wa kilo 10 kwa wanawake na wazee na kilo 25 kwa vijana. 

Kilo moja hununuliwa kwa Shilingi 100 hadi 500, kulingana na msimu na utashi wa Mawakala.

Ni wakati Tanzania iungane na nchi zingine duniani, kama vile Brazil, India, Agentina na Colombia, zilizoweka mifumo rasmi ya kutambua waokota taka rejeshi. Nchini Brazil, kwa mfano, waokota taka rejeshi katika miji kama Sao Paulo na Belo Horizonte wanatambuliwa kupitia Sheria ya Kitaifa ya Usimamizi wa Taka Ngumu (PNRS), ambapo wanapata haki za kisheria na msaada.

Nchini India, Sheria ya Usimamizi wa Taka Ngumu ya mwaka 2016 inatambua waokota taka hasa katika miji ya Pune na Bangalore kama sehemu muhimu ya mfumo wa usimamizi wa taka.

Majiji ya Bogotá na Medellin nchini Colombia yameanzisha mfumo wa kuwapa waokota taka vitambulisho rasmi, leseni, na haki za kufanya kazi kisheria, huku Buenos Aires, Argentina, ikianzisha mpango wa kuwajumuisha waokota taka katika mfumo wa usimamizi wa taka.

Hatua zinazohitajika

Serikali ya Tanzania inaweza kuungana na nchi hizi kwa kuchukua hatua mahususi kama vile kutambua rasmi waokota taka rejeshi kwa kuweka sera zinazowatambua waokota taka kama sehemu muhimu ya mfumo wa usimamizi wa taka.

SOMA ZAIDI: Mbunifu Huyu Awaasa Watanzania Kuziangalia Takataka Kwa Jicho la Kijasiriamali

Serikali pia inaweza kuweka bei elekezi ya chupa za plastiki ili kuboresha mapato ya waokota taka.

Hatua nyingine inaweza kuwa ni kusimamia vipimo na mizani kwa kuhakikisha utekelezaji wa sheria za vipimo na mizani ili kuwalinda waokota taka dhidi ya unyonyaji.

Serikali pia inaweza kutoa vifaa vya kujilinda, wajibu unaoweza kutekelezwa pia na wazalishaji wa plastiki. Waokota taka pia wanaweza kupatiwa bima ya afya bure kutokana na mazingira hatarishi wanayofanyia kazi.

Pia, Serikali inaweza kudhibiti chupa za plastiki za rangi kwa kuweka kanuni za kudhibiti chupa za plastiki za rangi, kama ilivyofanyika kwa mifuko ya plastiki.

Kwa kuhitimisha, waokota taka rejeshi wanachangia kwa kiwango kikubwa katika uhifadhi wa mazingira na uchumi rejelevu, lakini bado wanakutana na changamoto nyingi. 

Serikali ya Tanzania inapaswa kuchukua hatua za haraka kutambua mchango wao na kuboresha mazingira ya kazi yao. Kama ilivyofanyika katika nchi nyingine, hatua za kutambua na kusaidia waokota taka Rejeshi zitachangia katika mafanikio ya maendeleo endelevu na uhifadhi bora wa mazingira. 

Serikali ya Tanzania inapaswa kuitambua na kuirasimisha kazi ya uokotaji taka rejeshi.

Abdul-Aziz Carter ni mdau wa mazingira kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia abdulazizcarter500@gmail.com au X kama @aziz_carter. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts