The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kama Ligi za Wilaya na Mkoa Hazisikiki, Kuna Haja ya Kuwa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es Salaam?

Viongozi wa DRFA wako wapi? Hivi kazi yao ni kushiriki mkutano mkuu wa TFF au kuhudhuria mechi za Ligi Kuu na za kimataifa na kuchukua mgao wao?

subscribe to our newsletter!

Wakati tukiwa wadogo ilikuwa ni burudani kwetu kwenda kufuatilia ligi za wilaya za mkoa wa Dar es Salaam na baadaye ligi ya mkoa kwa ajili ya kupata wawakilishi kwenye ligi ya Kanda ya Mashariki.

Ilikuwa ni lazima kila mwaka kufika viwanja vya Tandika Mabatini, Karume, Msasani Magunia na Kifa Mburahati kwa kuwa huko ndiko ligi hizo zilikuwa zinachezwa.

Ilikuwa kila mara unasikilizia ni klabu gani zitavuka kutoka ligi za wilaya na kuja kupambana kutafuta bingwa wa mkoa, na subira hiyo ilitengeneza msisimko wakati ligi hiyo ilipofika kwa kuwa mpambano wa kupata bingwa ulikuwa mkali, kiasi kwamba fikra za Yanga na Simba ziliwekwa kando na mashabiki wa soka wa Dar es Salaam wakati mashindano hayo yanapofika.

Leo hii, hakuna tena huo msisimko wa ligi za wilaya. Na ile ya mkoa wa Dar es Salaam ndio kama haipo kabisa. Mkoa wa Dar es Salaam hautegemei timu kutoka katika ligi zake ipande hadi Ligi Kuu, bali inategemea klabu za jijini kufanya ule mchezo wa kununua klabu zilizo Championship au Ligi ya Kwanza (First League) ili izipandishe hadi Ligi Kuu.

Hapo ndipo unapokutana na Pan African, ambayo kwa miongo takriban minne sasa imekuwa ikifanya jitihada za kununua timu zilizo madaraja ya juu ili ipate urahisi wa kurejea Ligi Kuu. Hapo pia unakutana na Cosmopolitan, moja ya klabu kongwe nchini, ikifanya jitihada hizo bila ya mafanikio.

SOMA ZAIDI: TFF Wagombane na Simba, Yanga Katika Maendeleo, Siyo Kutuhumiana Kuhusu Hujuma

Lakini pia unakutana na timu za taasisi za Serikali nazo zikitumia mtindo huo kujaribu kufikia ligi za juu nchini.

Na huu si mtindo wa klabu za Dar es Salaam tu, bali nchi nzima. Kuna jitihada za kurejesha zile timu zilizokuwa na msisimko enzi za zamani kama Pamba na African Sports, huku taasisi na kampuni binafsi nazo zikitumia mtindo huo kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu.

Kwa maana hiyo, ligi nyingi za ubingwa wa mikoa zimepoteza hadhi, zimepoteza mvuto, na pale zinapotoa timu shindani katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa, hujiweka katika soko zuri la kununuliwa na wataka mafanikio ya haraka na mwisho wake huwa ni kupoteza utambulisho wake, ambao ni muhimu katika kujenga wigo wa mashabiki.

Viongozi wa mikoa wamebakia kupigania timu ambazo zimeshapata nafasi ya kucheza Ligi Kuu na kuzihangaikia katika kila kitu, huku wakisahau majukumu yao makubwa ya kuhakikisha maeneo yao yanakuwa na mashindano yenye msisimko na mvuto ili kuvutia wawekezaji na wadhamini.

Ukiacha mikoa mingine, ambayo miundombinu ya usafiri inaweza kuwa kikwazo kwa uchumi wa klabu, mkoa wa Dar es Salaam hauwezi kuwa na kisingizio cha kushindwa kujenga ligi bora inayoweza kuufanya kuingia kwenye mgogoro wa kugombea wadhamini na Shirikisho la Soka (TFF).

SOMA ZAIDI: Sakata la Simba, Yanga na TFF: Ni Muhimu Serikali Ilinde Mashabiki Kisheria

Dar es Salaam

Kwanza, mkoa una miundombinu bora ya usafiri inayowezesha klabu kusafiri kokote kufuata mechi zitakazopangiwa. Iwe kucheza Tandika Mabatini—siku hizi Tefa—Mburahati, KMC Mwenge, Kigamboni, Jenerali Isamuhyo, Azam Complex, Bandari au Uwanja wa Uhuru.

Pia, kama nilivyotaja hapo juu, Dar es Salaam ina miundombinu mizuri ya kuchezea mpira wa miguu. Viwanja vingi nilivyovitaja hapo juu vina sehemu za kisasa za kuchezea, mfano Azam Complex, KMC, Uhuru, TFF Kigamboni, ambavyo ni vya nyasi bandia, Jenerali Isamuhyo vyenye nyasi nzuri asilia na hivyo wa zamani wa Bandari, Tefa na Kifa.

Pia, Dar es Salaam ndio mkoa wenye ofisi za makao makuu ya vyombo vingi vya habari, vinavyoweza kuyapa nguvu mashindano ya mkoa kwa kuyatangaza, na hivyo wawekezaji na wadhamini kujitokeza kuyadhamini, na hata kuweka fedha kwenye klabu shiriki.

Lakini huoni shughuli yoyote ambayo Chama cha Soka cha Dar es Salaam (DRFA) kinafanya kuyapa thamani mashindano ambayo kikatiba ndiyo yanakipa chama hicho sababu na haki ya kuwepo kwake, au ndiyo sababu kubwa ya kuanzishwa kwake.

Leo hii viongozi wa DRFA wamebanwa na shughuli za maandalizi ya mashindano yasiyo rasmi katika kalenda ya shirikisho ya Ndondo Cup, ambayo hushirikisha timu zinazoundwa kabla ya kuanza mashindano.

Maswali kwa DRFA

Viongozi wa DRFA wako wapi? Hivi kazi yao ni kushiriki mkutano mkuu wa TFF au kuhudhuria mechi za Ligi Kuu na za kimataifa na kuchukua mgao wao? DRFA iko kwa ajili gani hasa kama hakuna mashindano mazuri kwenye mkoa wenye wingi wa fursa za udhamini?

SOMA ZAIDI: Waliovurunda ‘Dabi ya Kariakoo’ Walazimishwe Kuomba Radhi Hadharani

Kama Chama cha Mpira wa Wavu cha Dar es Salaam (DAREVA) kiliweza kujipanga na kutengeneza andiko lililovutia wadhamini hadi kikawa na fedha kuliko chama cha kitaifa, DRFA inashindwa vipi?

Kama Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (DB) kiliweza kuvutia wadhamini wakubwa kuliko chama cha kitaifa, DRFA inashindwa vipi?

Kama Clouds Media inaweza kuandaa mashindano ya Ndondo Cup na kupata wadhamini wakubwa, DRFA inashindwa vipi?

Kuna haja tena ya kuwa na DRFA? Kwa nini vyama vya wilaya za Dar es Salaam visipewe hadhi ya mkoa na DRFA ikaondolewa? TFF inaweza kuwa na mikoa ya kisoka kulingana na mahitaji na jiografia ya nchi.

Vyama vya wilaya

Umuhimu wa DRFA ulishapotea na viongozi wameshindwa kuonyesha thamani ya chombo hicho, hivyo ni muhimu kuangalia upya ili, ikiwezekana, vyama vya wilaya vipewe hadhi, hasa ikizingatiwa kuwa Chama cha Soka cha Wilaya ya Ilala (IDFA) ndio chimbuko la TFF ya sasa. 

SOMA ZAIDI: Kwa Kuifokea Yanga, Karia Ameonesha Upande Kwenye Sakata Kati ya Klabu Hiyo na Simba

Ilala ndipo Chama cha Soka (FAT) kilipoanzia na kwa kustahili hadhi hiyo maaluM, wilaya nyingine zinaweza kuwa mikoa ya kisoka.

DRFA haistahili kuwa ngazi ya viongozi kwenda katika uongozi wa kitaifa, wala kuwa tiketi ya kuingilia mechi za Ligi Kuu na kimataifa, bali kitovu cha maendeleo ya mpira mkoani Dar es Salaam. 

Kama ligi za wilaya hazisikiki, hali kadhalika ya mkoa, kuna shughuli zozote za maendeleo ya soka mkoani Dar es Salaam yanayoendeshwa na DRFA? Na kama hakuna, kuna haja tena ya kuwa na DRFA?

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×