The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Kuna Uchaguzi, Uteuzi na Uchafuzi. Hapa Tanzania Tuna Nini?

Kwa mfano, endapo washindani wote wameenguliwa kwenye kinyang’anyiro, kitakachofanyika hapa kinastahili kweli kuitwa “uchaguzi?”

subscribe to our newsletter!

Najaribu kuwa mwandishi, na kama mwandishi, inabidi nithamini, na kujaribu kuthaminisha, sana maana na umuhimu wa silaha yangu ya kila siku, yaani maneno.  Maneno yakitumika ipasavyo, yana nguvu, yana uhai; lakini yakitumika vibaya yanapoteza maana.  Labda ndiyo sababu wengine wanapenda kutumia visivyo.

Ndiyo maana nakereka sana watu wanapopenda kubadilisha, au kuvuruga, maana ya maneno kwa ajili ya maslahi yao.  Nguvu ya neno ni katika maana yake, si katika sura yake. Kwa mfano, watu wanapenda kudai kwamba kwenda shule na kupata elimu ni visawe.  

Thubutu! Mtu anaweza kwenda shule isiyo na elimu, au anaweza kuwekewa masomo bila kuelimika, labda kutokana na kuelewa lugha inayotumika. Elimu ni tofauti na shule, ni zaidi ya shule; hivyo kusema asilimia kadhaa wanapata elimu kwa sababu wako shule tu si sahihi. 

Haya, tuachane na hayo. Siku hizi, tumeingia kwenye mjadala wa neno uchaguzi, hivyo ningependa kujadili kuhusu neno hili. Kuna watu wanaopenda kudai kwamba, ili mradi mchakato fulani umefanyika, basi uchaguzi umefanyika. Lakini wameangalia maana halisi ya neno uchaguzi?

Uchaguzi

Kulingana na Kamusi Kuu ya Kiswahili (BAKITA, 2017) kuchagua maana yake ni: “Kuteua kitu, au vitu, miongoni mwa vitu vilivyomo,” na uchaguzi ni: “uteuzi wa kitu, au mtu, unaofanywa kwa mujibu wa sifa zilizobainishwa,” na pia “pigia kura mtu kuonyesha upendeleo wako.” Hapo tutafakari kidogo ni wakati gani katika historia ya nchi yetu, tumekuwa na uchaguzi kwa maana hiyo?

SOMA ZAIDI: Tume ya Uchaguzi Yasema Chama Kisichosaini Maadili ya Uchaguzi Hakitashiriki Uchaguzi. CHADEMA Yasisitiza Haitashiriki Kusaini

Kwa mfano, iwapo washindani wote wameenguliwa isipokuwa mmoja, hakuna uchaguzi maana, kwanza, inabidi kuteua miongoni mwa vitu vilivyomo. Lazima wingi uwepo – vitu, watu.  Vinginevyo ni “uteuzi,” si uchaguzi.   Kweli kuna sababu za kuengua, yaani sifa ya uhalifu, au ufisadi, zilizothibitishwa, lakini si kwa sababu aliteleza katika kujaza fomu, na wakienguliwa wote wengine, basi si uchaguzi. Watu hawajachagua.

Aidha, lazima iwepo “kwa mujibu wa sifa zilizobainishwa.”  Iwapo ni kwa mujibu ya kuiba kura, kuwa na njama ya kuzidisha kura, kubadilisha idadi ya kura kisiri, kuwazuia mawakala wa vyama vingine wasisimamie upigaji kura, n.k., suala la “kwa mujibu wa sifa zilizobainishwa” halipo tena, hivyo hapa tunaongelea uchaguzi au uchafuzi?  Bila uwazi, ni uchaguzi au uchafuzi?

Tena iwapo wanaotakiwa kuchagua wanahongwa, au kutishiwa ili wamchague mtu fulani, ni uchafuzi si uchaguzi pia.  Sisi wazee tunakumbuka malumbano kuhusu neno takrima.  

Ilitetewa sana na wenye mamlaka, lakini baadaye tukakubaliana kwamba takrima haitakiwi kwa sababu takrima, ambayo kimsingi ni hongo, ni kinyume na “sifa zilizobainishwa.”  Mtu kuchaguliwa, au kuteuliwa, au kupachikwa kwa sifa tofauti kabisa si sifa ya mtu.  Ni uchafuzi badala ya uchaguzi.

Na tatizo hili limejikita na kutuama hadi linanuka miongoni mwetu. Wakati wa warsha nimeona washiriki wakigawiwa katika makundi mawili. Kundi la kwanza linapanga safu ya sifa muhimu kwa kiongozi, kwa vipaumbele wakati wa kuchagua. Daima zinatajwa sifa kama uadilifu, itikadi, maono, kuchapa kazi, n.k.  

SOMA ZAIDI: Wadau Wamshukia Makalla Kwa Madai Yake Kuwa CHADEMA inapanga Kusambaza Virusi vya Ebola Kuzuia Uchaguzi: ‘Maneno ya Hovyo’

Kundi la pili linapanga safu ya sifa tunazotumia kiuhalisia katika kuchagua viongozi.  Daima zinatajwa sifa kama kabila, dini, vitenge, ukwasi, n.k.

Yaani, tunajua sifa muhimu ya kiongozi lakini hatutumii sifa hizi katika kuamua tunamchagua nani.  Yaani, tumezoea hali hii hadi tunachagua mtu tukijua kuwa ni fisadi halafu tunabaki kulalamika akiendelea kutufisadia baada ya kuchaguliwa na sisi!

Sasa bila kufuata maana halisi ya uchaguzi, uchaguzi upo kweli au ni zoezi tu lenye sura ya nje ya uchaguzi bila maana halisi ya uchaguzi?  Naamini uchechemuzi wote wa kisasa ni kuhakikisha kwamba tunao uchaguzi wa kweli, sio uteuzi, wala uchafuzi.

Sera za vyama

Haya sasa, na tukiangalia kichama, badala ya kisura – maana shida yetu nyingine tunaangalia sifa ya sura badala ya sera –, inabidi kila upande unadi sera zake.  Ninavyojua, kwa ujumla, mtu hashindi kwa kukashifu upande wa pili tu.  

Ilitokea kwa majirani zetu mara moja walipoimba yote yanawezekana bila Moi, lakini pia waliompinga walikuwa na sera mbadala zilizoeeleweka.  Hata kiongozi wa sasa wa taifa linalojidai lina nguvu kuliko zote alitumia kashfa nyingi, lakini pia alinadi sera zake alizoona ni chanya, kuhusu tariffs, uhamiaji, na vingine vya ku Make America Great Again, au MAGA.  

SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Katiba Yatajwa Kuwa Suluhu ya Uchaguzi Huru na wa Haki

Watu walivutiwa na sera hizi – si mimi, lakini mamilioni walivutiwa.  Natamani sana kuona kwamba, pamoja na kukosoa na kuonesha kasoro katika mfumo wa sasa, na chama kilichopo, kila chama pinzani kinadi sera.  Nikichagua chama hiki, au kile kingine, nategemea mabadiliko gani, au ubora zaidi gani katika sera ya elimu, au vijana, au uchumi na kadhalika.  

Chama tawala kinapenda sana kuimba Maendeleo hayana chama. Ni kweli.  Lakini vipaumbele katika kutafuta maendeleo vina chama. Ndiyo maana tunachagua chama hiki au kile, kwa sababu tunaona vipaumbele vyao na jinsi ambavyo watatekeleza vipaumbele vyao ni bora zaidi.  Ndiyo maana Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa hili, alisema, “kupanga ni kuchagua.”  Uchaguzi mwingine huo.

Kwa mifano michache: Kodi zako zinawalenga akina nani?  Walio nacho au wasio nacho? Vitu vya lazima au vya anasa? Kodi zinatumikaje, kuzidisha fahari ya walio nacho au kuwekeza zaidi kwa huduma za jamii? Mfumo uwe wa kupendelea wazalishaji wa ndani au wa nje? Tupendelee zaidi miundombinu au huduma za jamii.  Uwiano kati ya kuendeleza miundombinu na huduma za jamii uweje? Kwa ujumla, maendeleo yanayopiganiwa ni ya tabaka gani?

Vipaumbele

Na katika kila sera pia tujue. Tunakubaliana na vipaumbele vya elimu, au afya, au maendeleo ya wanawake vya chama tawala au kama wanavyopenda kujiita chama dola, au kuna mibadala? Na mibadala ikoje? 

Kwa mfano, katika elimu, tunaweka vipaumbele kuwatengenezea shule wale wenye uwezo wastani wanaong’ang’ania shule za ung’eng’e, au tunaweka vipaumbele kuajiri walimu wengi wa kutosha na kuboresha shule za wasio nacho? 

SOMA ZAIDI: CCM Hawako Tayari kwa Mageuzi Lakini Suluhu Siyo Kususia Uchaguzi

Napenda kujua kila chama kina mpango gani kupambana na mabadiliko makubwa sana yanayoletwa na akili mnembe.  Bado tunajikita katika ukariri wa mambo muhimu wakati ChatGPT inatupa mambo yote kwa nukta kadhaa.  Na bado hata ChatGPT yenyewe inakiri kwamba inafanya makosa, hivyo tunafundishaje fikra tunduizi, uwezo wa kutambua na kuchambua?  

Tunajiandaa vipi kukubaliana na kuchambua mawazo anuwai, maana watoto wetu wataenda zaidi ya vitabu vya kiada? Jibu moja sahihi kwa kila kitu haliwezi kuwepo tena.  Inabidi kuchekecha isichachakuliwe.

Hii ni mifano michache tu, lakini mimi naamini suala la sera bado halijapewa kipaumbele cha kutosha na vyama vingi vya siasa hapa nchini.  

Kwa hiyo, wakati tunapigania kupata uchaguzi wa kweli, si uteuzi wala uchafuzi, tuthamini maana ya neno lenyewe. Tuoneshwe pia kwamba uchaguzi wa chama hiki au kile unategemea sifa zipi, yaani, sera za maendeleo katika kila nyanja, na uchaguzi wa watu ujengwe juu ya kuchagua kwanza na pili kuchagua kutokana na sifa zilizobainishwa.


Richard Mabala ni mdau wa masuala ya elimu, mshairi na mwandishi wa vitabu. Anapatikana kupitia rmabala@yahoo.com au X kama @MabalaMakengeza. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Je, ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×