Hivi karibuni tulikuwa na maongezi na Siegfried Mbuya, mwanasaikolojia na mtaalamu wa makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto, juu ya mustakabali wa malezi na mahusiano ya watoto na wazazi. Makala hii inaangazia matokeo ya mazungumzo hayo.
Mbuya anaeleza kwamba, hivi karibuni, kuna kizazi tunaendelea kukitengeneza, kizazi kinachochoshwa na upendo, kinachokosa uvumilivu wa kupenda na kupendwa kwa dhati. Hiki ni kizazi kilichozaliwa na wazazi wasomi, waliofanikiwa kimaisha, lakini waliobanwa na majukumu, waliokosa muda, hisia, na uwepo wa kweli kwa maisha ya watoto wao.
Wazazi waliopo kimwili lakini wasiopatikana kihisia. Hawazungumzi, hawasikilizi, hawahusiani kwa ukaribu. Katika ombwe hilo la kutokupatikana, tumekuwa tukitumia vitu kama mbadala wa mahusiano ya kweli.
Tunaziba mapengo ya hisia kwa zawadi na vifaa. Mtoto akilia, au kutuita na kutaka kutuongelesha, hatutafakari chanzo, wala kushughulika na hisia zake, tunampa kishikwambi, au kumuwashia runinga atulie. Tunatumia katuni na gemu kufunika hitaji la mtoto la kusikika na kuonekana.
Kukosa uhusiano wa moja kwa moja kunatufanya tuwekeze katika burudani na vitu badala ya mazungumzo na ukaribu. Wazazi wanapokosa muda wa kulea, huchagua kumpeleka mtoto chekechea ya bweni, si kwa sababu ya mahitaji halisi, bali kwa sababu hawana muda wa kihisia wa kuwepo na watoto wao.
SOMA ZAIDI: Wazazi na Walezi, Uelewa Juu ya Mahusiano Yenye Afya ni Muhimu kwa Watoto Wetu
Katika mazingira haya, mtoto analazimika kujifunza namna ya kushughulikia mahitaji yake ya kihisia kwa njia zisizo salama. Anafundwa kimya kimya kuwa upweke, kupuuzwa, ubinafsi, na tamaa ya vitu ni sehemu ya maisha.
Anaanza kuamini kuwa thamani ya mtu inapimwa kwa alichonacho, yaani, anakuwa mtu kitu, na sio mtumwenye utu. Hili linageuka kuwa msingi wa mahusiano yake ya baadaye, mahusiano ya kuepuka maumivu ya upendo usiopatikana.
Wakiwa watu wazima, wanaingia katika mahusiano wakiwa na njaa ya kupendwa, lakini pia na hofu kubwa ya kupenda. Wanahitaji upendo, lakini hawajui namna ya kuupokea wala kuutoa. Wanataka mtu awapende, lakini wanachoka haraka pale wanapodaiwa kupenda.
Wanataka kuaminiwa, lakini hawajalelewa kuwa wa kuaminika. Wanatamani mtu aoneshe kujali, lakini wanakinai pale wanapohitajika kujali kwa kurudisha. Wamezoea kutumia vitu kufunika pengo la ukaribu wa kihisia, zawadi badala ya mazungumzo, miili badala ya miunganiko ya kweli.
Hali hii inazaa kizazi ambacho kinaamini pesa na zawadi ni ishara ya upendo. Ukimpa mtu pesa, hata kama humpi muda wako wala ushirikiano, anaweza kuona umemthamini.
SOMA ZAIDI: Ubongo wa Mwanamke Hupungua Ukubwa Kipindi cha Ujauzito. Hii ni Habari Njema, Siyo Mbaya
Lakini ukimpa muda wako, usikivu, na uwepo pasipo kuwa na fedha anaweza kuona unamchosha. Tumeunda mfumo wa thamani ambao hautambui uhusiano wa kihisia isipokuwa uwe na manufaa ya haraka na ya kimwili.
Ukimpa mtu ngono, lakini ukakosa kumpa dhamira ya kudumu, atakuchagua bado. Lakini ukimpa dhamira bila mihemko ya kimwili, anaona kama unaota ndoto zisizowezekana. Tunataka mapenzi, lakini tusiyo na gharama zake. Tunapenda uhusiano ilimradi hauhitaji uwekezaji wa kweli.
Leo, tunalea kizazi ambacho:
· Hakitaki kuwekeza, kinataka kupita.
· Hakina nia ya kudumu, kinataka kusisimka.
· Hakihitaji kufahamiana, kinataka kutumiana.
· Hakina muda wa kujenga, kinataka kilichokwisha andaliwa.
· Hakihitaji gharama, kinataka matokeo ya haraka.
· Hakina subira ya kutafuta, kinataka vya kupewa.
· Hakisubiri, kinataka matokeo papo kwa papo.
· Hakina nafasi ya uaminifu, kinadai uhuru wa kibinafsi.
· Hakitamani “sisi,” kinatafuta “mimi.”
Hiki ndicho kizazi kinachoishi matokeo halisi ya utoto uliotelekezwa kihisia — kizazi kilichonyimwa fursa ya kujifunza maana ya uwepo wa kweli, upendo wa dhati, na mawasiliano ya kina.
Tunahitaji kufikiria upya malezi yetu, thamani tunazoweka kwenye vitu dhidi ya watu, na namna tunavyofundisha watoto maana ya kuhusiana kwa upendo, kwa heshima, na kwa uwepo wa kweli. Tahadhari ni muhimu katika maisha ya malezi ya sasa.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.