Wiki iliyoishia Aprili 19, Simba ilimtangaza mdhamini mpya wa vifaa aliyeshinda zabuni ya udhamini wa vifaa atakayembadili mdhamini wa sasa ambaye ni kampuni ya michezo ya kubahatisha ya Sandalandi.
Jayrutty Investment Company Limited imeingia mkataba wa miaka mitano na Simba Sports Club, mkataba ambao una thamani ya Shilingi bilioni 38 ulio na vipengele vingi vya kuiwezesha klabu hiyo kuendeshwa kisasa na kuwa na vifaa na miundombinu ya kisasa.
Jayrutty Investments imejinadi kwenye tovuti yake kama kampuni inayofanya kazi ya kuwezesha wanamichezo kufikia viwango vya juu kwa kuwapatia vifaa bora kama viatu, mipira, vifaa vya gym, miundombinu ya michezo na shule za michezo. Vifaa hivyo, kwa mujibu wa jayruttyinvestment.com ni vile vyenye ubora, imara, vinavyowezesha ufanisi na vya viwango vya juu.
Ingawa kampuni hii bado haijawa na chapa kubwa hapa Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, bado katika dunia ya sasa lolote linawezekana kutokana na dunia kudogoshwa na kuwa kama kijiji kinachowezesha teknolojia hata iliyopo maelfu ya kilomita kutoka hapa kutumika popote pale duniani.
Kati ya mambo takriban kumi yaliyoahidiwa kwenye mkataba huo, kwangu nalichukulia kwa uzito suala la ujenzi wa uwanja utakaokuwa nje ya jiji la Dar es Salaam, na ujenzi wa ofisi za makao makuu ya klabu ambazo kwa sasa ziko Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo, ambako hakufai tena kuwa eneo la kufanyia shughuli za kiofisi za klabu za Ligi Kuu kutokana na hekaheka nyingi za kibiashara na uwingi wa watu.
SOMA ZAIDI: Kama Ligi za Wilaya na Mkoa Hazisikiki, Kuna Haja ya Kuwa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es Salaam?
Ujenzi wa uwanja
Suala la ujenzi wa uwanja limekuwa gumu kwa klabu kongwe za jijini Dar es Salaam baada ya waasisi wake kufanikiwa kujenga ofisi za makao makuu katikati ya jiji lilipokuwa dogo na idadi ndogo ya watu.
Yanga ilimudu kuzungushia ukuta uwanja wake wa Kaunda uliopo makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani, wakati Simba ililazimika kuacha uwanja wake uliokuwa Jangwani kutokana na sababu kadhaa.
Jangwani ndiko kulikokuwa na viwanja vingi vya klabu za zamani kama Cosmopolitan, Pan African na Simba kabla ya maeneo hayo kuanza kuvamiwa kwa ajili ya makazi, kuanza kutumika kwa ajili ya mikutano ya hadhara na baadaye kuzingirwa na mafuriko kila wakati mvua kubwa ziliponyesha.
Viongozi kadhaa wa klabu hizo wamekuwa wakiahidi kujenga viwanja, lakini ahadi zao zimekuwa zikiyeyuka kama ambavyo walivyokuwa wakiyeyuka.
Jaribio la hivi karibuni la Simba lilikuwa ni kushirikisha wanachama kuchangia ujenzi, lakini inaonekana haikuweza kukusanya hata Shilingi milioni 100.
SOMA ZAIDI: TFF Wagombane na Simba, Yanga Katika Maendeleo, Siyo Kutuhumiana Kuhusu Hujuma
Hata hivyo, klabu hiyo imejenga uwanja wa mazoezi uliopo Bunju unaoitwa Mo Arena kutokana na mwekezaji, Mohamed Dewji, kuweka fedha zake katika miundombinu hiyo. Na hapo ndipo Jayrutty imeahidi kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua watu kati ya 10,000 na 12,000, ahadi ambayo inawezekana.
Haijaelezwa hasa uwanja huu utagharimu shilingi ngapi, lakini kama mkataba wa vifaa utakuwa na ufanisi, hakuna litakaloshindikana katika kipindi cha miaka mitano.
Maana yake hapo, Jayrutty atakuwa ameingia makubaliano ya haki za kutumia jina lake katika uwanja mara baada ya kukamilika kwa kuwa hizo Shilingi bilioni 38 ni katika masuala ya vifaa kama ilivyokuwa kwa mdhamini aliyepita, Sandaland, ambaye aliingia mkataba wa Shilingi bilioni 26.
Kufikiria
Huu ni mpango ambao unaonyesha viongozi wa Simba walikaa chini kufikiria wanalimalizaje tatizo la kutokuwa na uwanja wao na ndipo wakaamua kuliegemeza kwenye mkataba wa vifaa, ambavyo kama si wasimamizi wa biashara kuwa walegevu, vinaweza kuwa mtaji mkubwa wa kupunguza tatizo la kiuchumi.
Mauzo ya vifaa vya klabu, kama jezi, lesso, fulana, kofia, kalamu, vikombe na bilauri vyenye nembo ya klabu na mdhamini ni kati ya vyanzo vikuu vya makapo kwa klabu za michezo ndio maana klabu kubwa kama za barani Ulaya huangalia nchi kama za bara la Asia ambako kuna idadi kubwa ya watu.
SOMA ZAIDI: Sakata la Simba, Yanga na TFF: Ni Muhimu Serikali Ilinde Mashabiki Kisheria
Hii ni mojawapo ya njia ambazo zinaweza kutumika kufanikisha ujenzi wa miundombinu kama uwanja kwa kuwa ina uhakika wa mapato.
Hii pia imewezekana kutokana na klabu hiyo kujali na kuheshimu wadhamini, tofauti na klabu kama Yanga, ambayo mdhamini mmoja anaonekana kutawala kila eneo na hivyo kufinya mwonekano wa wadhamini wengine.
Kampuni zinapoona wadhamini wanapata nafasi yao kwa kadri zinavyostahili, zinaona hapo ndipo sehemu sahihi ya kutumbukiza fedha kwa matarajio ya mafanikio baada ya muda mrefu.
Si Sports Pesa, VunjaBei, M-Bet au Mo Foundation ambao wamewahi kusikika wakilaumu klabu kwa kutoheshimu makubaliano. Wote wameingia na kutoka kwa heshima na hata pale udhamini ulipogongana na wadhamini wa mashindano ya Afrika, bado hakukuwa na kelele.
Hiki ni kitu ambacho klabu hazina budi kuiga kutoka kwa viongozi na menejimenti ya Simba. Kwa utamaduni huu, sioni ajabu kwamba kwa vipindi viwili mfululizo, Simba imesaini mikataba minono kuliko mingine ya klabu za Tanzania na Afrika Mashariki kuanzia mwaka 2022.
Kama Singida Black Stars walionyesha kuwa wanaweza kushirikisha wawekezaji wengine katika kutatua tatizo la ujenzi wa uwanja, Simba wameonyesha mbinu nyingine na huu unaweza kuwa mwanzo wa klabu zetu, hasa zinazomilikiwa na wanachama, kuondokana na tatizo la viwanja.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.