Toka Aprili 12, 2025, mjadala wa kisheria umeendelea katika majukwaa mbalimbali, baada ya Tume ya Uchaguzi kueleza kuwa chama ambacho hakikusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi katika siku hiyo, hakitaruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa mwaka 2025. Hoja hii imeendelea kuzua mjadala katika taifa, huku sehemu kubwa ya wataalamu wa sheria wakionesha kuwa kuna walakini kwenye tafsiri ya Tume juu ya suala hilo.
Chama kikuu cha upinzani nchini, CHADEMA, chenye mamilioni ya wafuasi na wanachama, hakikusaini kanuni hizo kwa kudai mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi, huku mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu, akieleza kuwa chaguzi za Tanzania zimekuwa kama ‘kwenda machinjioni’, hasa kwa wanachama wao, akitolea mfano wa mauaji ya wagombea wao, katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.
Tume kwa upande wake imesisitiza hakutakuwa na nafasi tena, na chama ambacho hakijasaini hakitaruhusiwa kushiriki uchaguzi. Msingi wa hoja ya Tume juu ya kuzuia chama ambacho hakijasaini kanuni, unatokana na kanuni zenyewe, ambazo ndizo zimeweka zuio la chama kutoshiriki uchaguzi, kama alivyoeleza Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima mnamo Aprili 12, 2025, akiongea na Wanahabari.
“Ukisoma kanuni namba moja na kanuni ndogo ya tano ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, [kifungu] kinasema, chama cha siasa ambacho hakitasaini au mgombea ambaye hatasaini fomu namba 10 hatateuliwa kuwa mgombea; na chama cha siasa ambacho hakijasaini kanuni za maadili hakitaweza kusimamisha mgombea na kushiriki kwenye uchaguzi,” alifafanua Kailima.
“Kama kuna chama cha siasa ambacho hakijasaini maana yake hakitashughulika na shughuli zozote zinazohusika na maswala ya uchaguzi. Sasa mtu anaweza kudhania kwamba anaweza akasaini kesho,hapana kusaini ilikuwa ni leo,” alisisitiza zaidi.
“Chama ambacho hakikusaini maadili ya uchaguzi hakitoshiri Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na hakitoshiriki chaguzi zingine ndogo zitakazotokea katika uhai wa miaka hii mitano kuanzia 2025 mpaka 2030 hapo kanuni zitakapotungwa,” alifafanua zaidi.
Msingi wa Sheria
Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024 inayotoa utengenezaji wa Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, haijaeleza moja kwa moja juu ya kuzuia chama kushiriki uchaguzi. Kifungu cha 162 cha sheria hiyo kinaeleza:
“Kwa madhumuni ya kusimamia uchaguzi wa haki, huru na amani, na baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, Tume itaandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake. (2) Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitasainiwa na- (a) kila chama cha siasa; (b) kila mgombea kabla hajawasilisha fomu ya uteuzi; (c) Serikali; na (d) Tume, na zitapaswa kuzingatiwa na wahusika wote waliosaini. (3) Mtu ambaye atakiuka masharti ya Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni hizo.”
Akichangia katika mjadala unaoendelea, kupitia jukwaa lake la Mtandao wa X, Rais wa Chama cha Mawakili, Boniface Mwabukusi, ameeleza kuwa Tume imevuka mipaka yake iliyopewa na Katiba na Sheria.
“Huwezi kuondoa haki iliyotolewa Kikatiba na kisheria kupitia Kanuni. Kusaini Kanuni za Maadili ni kanuni wezeshi kurahisisha ushiriki wa vyama na wagombea na si vinginevyo. Tume ya Uchaguzi siyo Bunge haina uwezo wa kufuta haki iliyothibitishwa na Bunge kupitia Katiba na Sheria. Ni kushindwa kuwajibika,” anasisitiza msomi huyo wa sheria.
Wakili William Maduhu anaeyefanya kazi na Kituoc cha Sheria na Haki za Binadamu akizungumza na The Chanzo kwa njia ya simu naye ameungana na Mwabukusi kwa kusisitiza kuwa kanuni za Tume ya Uchaguzi haziwezi kuwa juu ya Katiba, “Kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi ni suala la kisheria maana uchaguzi ni mchakato wa kisheria. Ila kanuni hizo haijaelezewa kwenye kifungu hicho kwamba ni lini kanuni hizo zinapaswa kusainiwa.”
Maduhu pia ameongeza kuwa bado kanuni hizo hazifanyi kazi kwa sasa: “Kwa hiyo hata hao waliosaini juzi hizo kanuni bado hazifanyi kazi.Mimi nadhani kama CHADEMA wanataka kushiriki uchaguzi bado nafasi wanayo sio kwa sababu eti hawajasaini kanuni”.
Kuhusu muda wa kuanza kutumika, Kanuni zenyewe zinaeleza: ‘Kanuni hizi za Maadili zitatumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, kuanzia siku moja baada ya tarehe ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi mkuu hadi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo. Vilevile, Kanuni hizi zitatumika katika chaguzi ndogo zitakazofuata.”
Kanuni na Haki ya Kikatiba
Aliyekuwa Rais wa Chama cha Mawakili, ambaye kwa sasa ni Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, naye ameeleza kuwa Tume imejielekeza kwa namna inayopishana na misingi ya Katiba.
“Haki ya kuchaguliwa kuwa mgombea inatolewa na Katiba na muongozo wa sheria wa kitu gani kinamnyima mtu kuwa mgombea kimetajwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo tunasema Tume imejielekeza vibaya imefanya hivyo kwa nia ambayo sio sahihi,” alifafanua Nshala akiongea na waandishi.
Kwa upande wa Wakili Paul Kisabo, Mtetezi wa Haki za Binadamu anayefanya kazi na Shirika la THRDC amesema kuwa kifungu namba 162 kifungu kidogo cha pili cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani hakitoi ulazima wa kusaini kifungu hicho cha maadili. “Kifungu hicho hakisema kuwa chama kisiposaini hizo kanuni za maadili hakitakuwa na nafasi ya kushiriki uchagauzi”.
”Vilevile kanuni ambazo zimetungwa na Tume ya Uchaguzi chini ya sheria za Bungehazipaswi kukizana na sheria au Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anaeleza Kisabo.
Wachambuzi wa siasa wanaona kuwa kutoshiriki kwa CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa 2025 kunaweza kudhoofisha ushindani wa kisiasa na kuathiri uhalali wa mchakato mzima wa uchaguzi. Almasi Mohammed ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa visiwani Zanzibar amesema kuwa suala kutokusaini maadili, si jambo ambalo linamvua mtu asiwe sehemu ya uchaguzi.
”Kanuni maadili zinakuja kutengeneza muamala mzuri wa kuelekea kwenye siasa za uchaguzi kwamba vipi tutaendesha uchaguzi, lugha ambazo zinapaswa zizungumzwe na vitu kama hivyo .Kwa hiyo inaweza ukawa usisaini, lakini haina maana kwamba hautakuwa katika misingi na hizo kanuni,” anasisizita Almas.
Hoja ya Almas inafanana no hoja inayoelezwa na Rais wa zamani wa Chama cha Mawakili, Fatma Karume ambaye anasisitiza Kanuni za Maadili ni sheria, vyama itazifuata vinaposaini au visiposaini.
Akiongea katika hafla ya utiaji saini Kanuni za Maadili mnamo Aprili 12, 2025, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele alieleza kuwa bado kuna nafasi ya wadau kupata tafsiri kwenye vyombo vingine.
“Lakini hii Haizuii ufafanuzi mwingine wowote na vyombo vyote vya sheria. Katiba inasema mfafanuzi wa mambo ya sheria na mwamuzi hasa wa mwisho ni Mahakama, sisi jibu lilotolewa hapa na Mkurugenzi ni namna tunavyotafsiri sisi, alieleza Jaji Mwambegele.