Mnamo miaka ya 1990 mwishoni, na mwanzo mwa miaka ya 2000, ‘Matajiri wa Tanga’ walitikisa sana kwenye nyanja ya usafiri wa abiria. Matajiri hawa wa Tanga walivuma sana na kampuni za mabasi kama Tawfiq (baadae Executive na sasa Falcon), Takrim (baadae ikibadili biashara na kujikita kwenye usafirishaji wa mizigo), Taqwa, Tahfif, Tawheed, Bembea, nakadhalika.
Nilisafiri sana kwa mabasi haya, hasa kati ya miji ya Moshi, Kilimanjaro na Mwanza kupitia nchini Kenya. Barabara za Tanzania zilikuwa mbovu sana miaka hiyo, hivyo kuyalazimu baadhi ya mabasi yanayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kanda ya Ziwa na Jiji la Kampala, Uganda, kupitia nchini Kenya.
Mabasi ya Tawfiq na Takrim yalikuwa maaarufu zaidi kwa safari hizi. Yalikuwa yakifanya safari katika miji mikubwa kote Afrika Mashariki, kwa maana ya Kenya, Uganda, na Tanzania. Miji hii hasa ilikuwa Nairobi, Mombasa, Kampala, Arusha, Dar es Salaam, na Mwanza.
Mambo ya kuvutia
Mambo kadhaa yalinivutia katika mabasi hayo na pengine ndiyo sababu ya kuyakumbuka hata sasa. Mojawapo ya mambo haya ni aina ya ‘body’ zake (zilizokuwa zinajengwa Kenya) ambazo zilikuwa na starehe, hasa viti murua vya kulaza, kuliko zile zilizojengwa Tanzania. Kadhalika, yalikuwa na rangi za kuvutia sana, hasa Takrim na Tahfif.
Jambo lingine nililovutiwa nalo ni yale maneno yaliyokuwa yakiandikwa katika ‘mud flaps,’ au kapeti, kubwa upande wa nyuma wa basi yenye ujumbe tofauti wa kuelimisha au kuburudisha. Wakati mwingine baadhi ya mabasi yaliandikwa majina ya watu maarufu. Nakumbuka mojawapo lilikuwa na jina la kocha wa zamani wa timu ya Brazili, Mario Zagallo!
SOMA ZAIDI: Usafiri wa Umma Unaweza Kuwa Rafiki Zaidi kwa Watu Wenye Ulemavu?
Safari moja ninayoikumbuka sana ni ya kutoka mjini Moshi kwenda Mwanza, nadhani mwaka 1999, kwa basi la Tawfiq. Basi lile lilikuwa linaitwa “Charada Pekee” kufuatana na lilivyokuwa limeandikwa kwenye ‘kapeti’ nyuma.
Kwa kiasi kikubwa mabasi yalitambulika kwa utaratibu huu, tofauti na sasa ambapo namba za usajili ndio hutumika zaidi ukiacha jina la kampuni husika. Dereva wa basi lile alikuwa mtu wa makamo, kati ya miaka 60 na 65 hivi. Wenzake walimuita “Babu Charada.” Naikumbuka safari hii kwa mambo kadhaa.
Siku hiyo sikubahatika kupata nafasi ya kukaa (siti) tangu Moshi nilipopanda basi mpaka tulivyofika mjini Bunda katika mkoa wa Mara. Nakumbuka tulipokuwa stendi ya Bunda alipanda bwana mmoja aliyekuwa akielekea Mwanza. Baada ya kuniona nimekaa kwenye kiti aliniamuru nimpishe akae kwa maana yeye ni mtu mzima na mimi ni mtoto.
Kweli nilikuwa mvulana mdogo wa miaka 17 tu. Kwa jinsi nilivokuwa na uchovu wa kusimama, au wakati mwingine kukaa kwa shida, tena kwenye kigoda, kitendo cha kuamriwa na mtu huyo kumpisha kiti akae kilinipa hasira. Sikumjibu chochote zaidi ya kumtazama tu, huku nikidhihirisha ghadhabu yangu.
Kondakta wa basi aliona tukio na kuingilia kati. “Mzee, huyo dogo unavyomuona hapo kasimama tokea Moshi, ndio sasa amepata siti.” Mtu yule alionesha mshangao kigodo na kwenda kutafuta nafasi sehemu nyingine bila kusema neno lolote.
Safari ndefu
Safari zile zilikuwa zikichukua mpaka masaa 30, kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza. Kwa abiria waliokuwa wakipanda basi mjini Moshi au Arusha, sehemu kubwa ya safari ilifanyika usiku, upande wa Kenya.
SOMA ZAIDI: Maendeleo Kutokea Chini? Hii ni Hadithi ya Ushirika wa Daladala Dar es Salaam
Ukiacha umbali wa safari, mabasi yalikuwa hayaruhusiwi kusafiri wakati wa usiku nchini Tanzania kutokana na usalama duni miaka ile. Kilikuwa ni kipindi kilichogubikwa na wimbi la utekaji mabasi, hasa mikoa ya magharibi mwa Tanzania.
Baada ya kusimama kwa muda mrefu tangu tuondoke mjini Moshi, uchovu na usingizi vilinilazimu kukaa kwenye kigoda. Hivi vilikuwa vinatolewa kwa abiria waliokosa siti, jambo la kawaida kabisa wakati ule. Hakukuwa na utaratibu wa abiria kutosimama ndani ya basi (‘levo siti’) kama sasa.
Nakumbuka alikuwepo mama mmoja mwenye watoto watatu ama wanne, wadogo. Wote hawakuwa na ‘siti.’ Mama yule alipata shida sana na watoto wale. Wakati mwingine baadhi walinilalia kwani mama yule hakuweza kuwamudu wote. Nami ilibidi niwe mvumilivu tu kutokana na hali ilivyokuwa.
Burudani ya muziki ndani ya basi ilitufanya baadhi tusahau karaha hizo. Ila kwa upande wangu burudani kubwa kabisa alikuwa ni dereva wa basi, Babu Charada, aliyekuwa anapiga porojo sana na wenzake hasa zinazohusu maisha na mikasa yake katika kazi ya udereva. Nilivutiwa sana na simulizi zake maana nilipenda sana mambo ya udereva, magari na usafirishaji.
Simulizi
Babu Charada alikuwa mahiri kweli wa kusimulia hadithi, hasa kwa kutaja taarifa muhimu kama aina (kabila) ya lori/basi alilokuwa akiendesha wakati wa mkasa/tukio fulani alilokuwa akisimulia, wapi alikuwa akitokea/kuelekea, nakadhalika. Wakati huu wote Babu Charada alikuwa akitafuna mirungi na ‘Big G.’
SOMA ZAIDI: Simulizi za Wapiga Debe Wanawake Stendi ya Magufuli: ‘Sisi Siyo Mateja’
Hii ilikuwa ni desturi ya madereva wengi wakati ule hasa wa masafa marefu wakati wa usiku. Iliaminika kuwa mirungi inawaondolea usingizi madereva. Nilibahatika kusikia simulizi za Babu Charada usiku ule maana nilikuwa eneo la karibu kabisa na kiti cha dereva.
Mbali na umahiri wa simulizi, Babu Charada alikuwa dereva mahiri hasa katika ubadilishaji gia ukisindikizwa na mbwembwe za ukanyagaji mafuta na matumizi ya breki ya injini (engine braking) maarufu kama “kupiga bobishi.” Utaalamu huu hufanya injini za aina fulani za magari makubwa kutoa mlio wa kuvutia sana.
Mpaka sasa sijawahi fahamu sababu hasa iliyowafanya Matajiri wa Tanga kupendelea sana mabasi aina ya “Nissan Diesel-UD.” Basi la “Charada Pekee” lilikuwa ni aina ya Nissan Diesel-UD.
Herufi za “UD” ni kifupi cha maneno ya Kiingereza Ultimate Dependability yanayomaanisha “kutegemewa kwa hali ya juu kabisa.” Labda Nissan Diesel-UD zilikuwa za kutegemewa sana na matajiri hawa wa Tanga kwa umadhubuti wake!
Ronald Ndesanjo anahusudu mambo ya udereva, magari na usafirishaji. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ronald.ndesanjo@gmail.com au X kama @ronaldndesanjo. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.