The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

TFF Isisubiri CAS, Ianze Kujiwajibisha Sakata la Yanga v Simba

Kama TFF isipowashughulikia wahusika, basi ni dhahiri viongozi wa juu walihusika kwa njia moja au nyingine kufanya uamuzi huo wa hovyo ambao unazidi kukomaa.

subscribe to our newsletter!

Uongozi wa sasa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndio unaoongoza kwa kuwaadhibu watu wa familia ya mpira wa miguu kwa kutumia kamati maarufu ya maadili, huku kamati nyingine zikiwa hazina shughuli za mara kwa mara, au zimelala.

Pengine ni kutokana na kamati hiyo kuwa mpya wakati wa uongozi uliopita, lakini ukiangalia awamu ya kwanza ya uongozi wa sasa, bado unaweza kuamuwa ndio unaongoza kwa kutoa adhabu nyingi kwa familia ya mpira kulinganisha na awamu nyingine.

Pamoja na ukweli kwamba kamati ya maadili inatakiwa iwawajibishe watu wote walio kwenye familia ya mpira bila ya kujali nafasi zao kwenye uongozi, bado haujaweza kuwashughulikia viongozi na watendaji kadiri inavyopaswa.

Labda ni rais wa zamani tu, Jamal Malinzi, ndiye aliyeadhibiwa na kamati hiyo lakini ni baada ya Serikali kumuweka mahabusu kwa makosa ya ufisadi na hivyo kutokuwepo madarakani kwa miaka miwili, hali iliyolazimisha TFF kufanya uchaguzi mpya.

Kutoshughulikiwa kwa wakosaji katika uongozi na utendaji hakumaanishi kwamba shirikisho lina viongozi safi na wasiofanya makossa, la hasha.

SOMA ZAIDI: Simba Wameonyesha Njia Ujenzi wa Viwanja

Tumeshuhudia makossa mengi ya kiutendaji, likiwemo kubwa la kuzuiwa kuipeleka Taifa Stars kwenye mechi za kirafiki nje kutokana na kujiingiza kwenye mashindano mengine katika kipindi hichohicho.

Uhairishaji holela wa mechi

Makosa ya mechi kuahirishwaahirishwa yamekuwa sugu sasa na yamefikia kugusa hadi mechi za watani wa jadi, ambazo, kwa utamaduni wetu, si rahisi kuzichezea kutokana na klabu hizo za Simba na Yanga kufuatiliwa na mamilioni ya watu, baadhi wakisafiri, wengine wakifanya biashara, na hata ofisi za kazi kuathiriwa na mahudhurio.

Kilele cha makosa hayo ni kuahirishwa kwa mechi tatu nje ya muda wa kikanuni na bila ya maelezo ya kutosha kwa umma na mashabiki ambao ndio wanaovuta wawekezaji na kampuni nyingine kwenye mpira wa miguu.

Mechi za Simba na Yanga, Simba na Kagera na Simba na Yanga zimeahirishwa hovyo ndani ya kipindi cha miaka mitatu na kusababisha tafrani kubwa kwa umma, hasa mashabiki waliofika uwanjani wakitegemea kuona burudani kutoka kwa timu wanazozipenda.

Ni kilele cha makossa hayo kwa sababu yamekuwa yakifanyika kwa klabu nyingine, lakini kutokana na klabu hizo kutokuwa na sauti na kutofuatiliwa, imekuwa inaonekana ni kawaida.

SOMA ZAIDI: Kama Ligi za Wilaya na Mkoa Hazisikiki, Kuna Haja ya Kuwa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es Salaam?

Uwajibikaji

Kwa kuwa hicho ni kilele, kwa maana tatizo sasa limekuwa kubwa, ungetegemea mamlaka za soka, TFF na Bodi ya Ligi Tanzania (TPBL), zingekuwa zimebanwa na shughuli za kutafuta wahusika waliokiuka kanuni kwa makusudi wakati wa kuahirisha mechi kwa madai kuwa wanaliokoa soka la Tanzania.

Ajabu ni kwamba baadhi wameshajitokeza hadharani na kuonyesha ni jinsi gani wamebobea katika uvunjaji wa kanuni kwa kueleza kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kuepuka klabu moja kati ya hizo kushuka daraja kwa kuwa ni jambo baya.

Katika kipindi hiki, hatujaona mwenyekiti wa Kamati ya Maadili akiwaita mbele ya kamati yake watu waliohusika kuahirisha mechi kujua chanzo ni nini ili sheria zichukue mkondo wake.

Serikali, ambayo huwa hatutaki iingilie masuala ya michezo, ndio imekuwa ya kwanza kuwajibika kwa kuziita pande zote na kuzungumza nazo kujua tatizo liko wapi, ingawa haijatoa taarifa yake kuwa iliona nini na kushauri taasisi isiyoingiliwa ifanye nini.

Katika kipindi hicho, hatujaona viongozi wa juu wakionyesha kukasirishwa na kitendo cha kuahirisha mechi kiholela, na badala yake wametoa matamko ambayo yanaonyesha kuwa tatizo si TFF wala TPLB, bali ni hao viongozi wa klabu wanaotaka waendeshaji wa ligi wajiuzulu.

SOMA ZAIDI: TFF Wagombane na Simba, Yanga Katika Maendeleo, Siyo Kutuhumiana Kuhusu Hujuma

Shauri CAS

Tabia za viongozi wa juu ndio zimesababisha Yanga, ambayo imesema haitacheza mechi itakayopangwa upya, iende Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) kupinga uamuzi wa TPLB wa kuahirisha mechi kiholela.

Pamoja na kuomba shauri hilo lijadiliwe kwa haraka, inawezekana uamuzi ukatoka baada ya takriban raundi tatu au nne za Ligi Kuu kuisha, jambo linaloweza kuwa baya zaidi.

Lakini kama TFF itaonyesha kuwajibika kwa kutafuta chanzo cha tatizo na kuwashughulikia wahusika, ni dhahiri wahusika wanaweza kulegeza misimamo na kukubaliana kumalizaa tatizo kiungwana.

Kama TFF itakuwa inasubiri uamuzi wa CAS, itakuwa haionyeshi kuwajibika kwa makossa ambayo viongozi na watendaji wake ni sehemu ya tatizo. Kwa vyovyote vile, viongozi wa TPLB wanahusika katika uahirishaji mechi kiholela na wao ndio walitakiwa wawe wa kwanza kufikishwa mbele ya Kamati ya Maadili wakati huu ambao unasubiriwa uamuzi wa CAS.

Maelezo

Hawa ndio wanatakiwa waeleze sababu iliyowasukuma kutoa msimamo kwamba mechi ya Simba na Yanga iliyopangwa kufanyika Machi 8, itachezwa kama ilivyopangwa licha ya Simba kusema kuwa haingecheza kutokana na kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla?

SOMA ZAIDI: Sakata la Simba, Yanga na TFF: Ni Muhimu Serikali Ilinde Mashabiki Kisheria

Hawa ndio wanatakiwa waeleze sababu ya kikao kuitwa tena mchana siku ya mechi na kufikia uamuzi wa kuahirisha eti kwa sababu kulionekana viashiria vya vurugu na rushwa? Hawa ndio wanatakiwa waeleze ni nani aliitisha kikao hicho na ajenda zilikuwa ni nini?

Hawa ndio wanatakiwa waeleze ni chombo gani cha usalama kilitumia intelijensia yake kung’amua viashiria vya vurugu kama Jeshi la Polisi, ambalo hutuma wawakilishi wake kwenye kikao cha maandalizi ya mechi kuzihakikishia timu usalama, haikutoa taarifa ya uwezekano wa vurugu?

Hawa ndio wanatakiwa waeleze walitumia intelijensi gani kung’amua viashiria vya rushwa kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inaeleza kuwa haikuwa na taarifa zozote za viashiria vya rushwa?

Hawa ndio wanatakiwa waleze kikao hicho cha kuahirisha mechi kilihudhuriwa na wajumbe wangapi na walipatikana vipi siku ya hekaheka za mechi? Hawa ndio wanatakiwa waeleze nani alimuagiza kamishna wa mechi aandike taarifa yake kabla ya tukio la mechi na aliandika akiwa wapi kwa kuwa eneo lake kubwa la kazi ni uwanjani?

Kama yalikuwa ni maagizo, yalitoka kwa nani?

Hawa wakiweza kujibu maswali haya na mengine wakiwa na ushahidi, itaonekana kweli kulikuwa na umuhimu wa kuahirisha mechi na hivyo taratibu nyingine kufuatwa.

SOMA ZAIDI: Waliovurunda ‘Dabi ya Kariakoo’ Walazimishwe Kuomba Radhi Hadharani

Upana wa tatizo

Tatizo hilo pia inabidi liangaliwe kwa mapana yake. Ilikuwaje mechi ya misimu miwili iliyopita ikaahirishwa muda kwa staili hiyo hiyo ya uamuzi kufanywa saa chache kabla ya muda wa mechi kuanza? 

Haohao ndio wanatakiwa waeleze ilikuwaje wakaahirisha mechi kwa sababu tu wachezaji wa Simba wana mafua na kuiacha Kagera Sugar ikienda uwanjani peke yake msimu uliopita?

Kama TFF isipowashughulikia wahusika, basi ni dhahiri viongozi wa juu walihusika kwa njia moja au nyingine kufanya uamuzi huo wa hovyo ambao unazidi kukomaa.

Kama ambavyo watu wa familia ya mpira wa miguu wamekuwa wakiadhibiwa kwa adhabu hadi za kutojihusisha kabisa na mpira, ndivyo ambavyo wahusika katika sakata hili wanatakiwa wawajibishwe ili kujenga nidhamu na weledi katika usimamizi na uendeshaji mpira wa miguu nchini.

Tunataka kuona msumeno ukikata wakati wa kwenda mbele na kurudi nyuma. Tumechoka kusikia adhabu dhidi ya wadau pekee. Sasa tuone na ndani ya shirikisho.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×