Mara nyingi inaanza na mtoto mmoja kupiga chafya. Hatukupata muda wa kutulia, tayari mwingine ana homa, mwingine analalamika koo linauma, na ndani ya siku chache, nyumba nzima inakuwa kama wodi ndogo ya wagonjwa. Kama sisi ni wazazi au walezi, bila shaka tumejikuta kwenye hali hii zaidi ya mara moja.
Lakini kwa nini hali hii hutokea? Kwa nini ugonjwa unapoingia kwa mtoto mmoja tu, wengine wote hufuata kwa kasi? Na zaidi ya yote, tufanye nini kuwalinda watoto wetu—na sisi wenyewe—hususan msimu huu wa baridi unaoambatana na wimbi la mafua na maambukizi ya virusi?
Msimu wa mvua na baridi nchini mwetu huambatana na ongezeko la maambukizi ya mfumo wa hewa, kama mafua, kikohozi, na homa za virusi. Mwaka huu, hali imekuwa mbaya zaidi: vituo vingi vya afya vimeripoti idadi kubwa ya watoto wanaougua, hali inayowapa mzigo mzito wazazi na walimu pia.
Takwimu kutoka Wizara ya Afya zinaonesha kuwa maambukizi ya mfumo wa hewa kwa watoto walio chini ya miaka 10 huongezeka kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30 katika msimu wa baridi. Hii ni ishara tosha kwamba kama watoto wetu wanaumwa mara kwa mara kipindi hiki, hatuko peke yetu.
Watoto wetu wanashirikiana kwa karibu sana. Wanacheza pamoja, wanagusa kila kitu kwa pamoja, na mara nyingine hata kushirikiana vikombe au vyombo. Maambukizi yanapoingia kwa mmoja, huenea kwa urahisi kwa wengine wote. Mfumo wa kinga wa watoto bado unaendelea kukua, hali inayowafanya wawe rahisi kuambukizwa mara kwa mara.
SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Malezi ya Sasa Yamekuwa Magumu Kuliko ya Zamani?
Pia, hawajaweza kuwa na uwezo wa kujihadhari na kujikinga kwa kuepuka kula au kugusa sehemu tofauti zinazoweza kuwa na vimelea vya virusi, hivyo hujikuta wakisambaza baambukizi kwasi kutoka kwa mmoja Kwenda mwingine.
Katika shule na maeneo mengine ya mikusanyiko wanakocheza watoto, ni vigumu watoto kuwa na umbali au nidhamu ya usafi. Wengi wetu pia tunaishi kwenye nyumba zenye nafasi ndogo, hivyo ni changamoto kutenga mtoto anapougua. Tukitaka kuzuia hali hii isiendelee, tunahitaji kujikita kwenye usafi wa msingi lakini wa kudumu.
Tuwafundishe watoto wetu kunawa mikono kwa sabuni na maji ya kutiririka mara kwa mara. Tuwahimize kutumia kiwiko wanapopiga chafya au kukohoa, na tusafishe mara kwa mara vitu wanavyogusa sana—milango, meza, simu, midoli, na kadhalika. Na kwa walio wadogo sana basi tujitahidi kuhakikisha usafi wao wa mazingira, vyakula na mwili.
Tuwe na uhakika kuwa watoto wetu wanapata mlo kamili wenye virutubisho muhimu kama mboga za majani, matunda, na vyakula vya protini. Tuwape vinywaji vya joto kama uji wa lishe, supu au maji ya uvuguvugu.
Tukigundua mmoja anaumwa, tuchukue hatua mapema. Kama tunaweza, tumtenge kwa muda ili wasisambaziane zaidi na tuwe makini na usafi wa vyombo, taulo, na mashuka. Tuwape mapumziko ya kutosha na tusiwapeleka shule au chekechea wakiwa wagonjwa.
SOMA ZAIDI: Wazazi Waliopo Kimwili Lakini Wasiopatikana Kihisia Hukuza Watoto Wasiojali Thamani ya Upendo
Tumuone mtaalamu wa afya endapo mtoto atakuwa na homa kali isiyoshuka, kushindwa kula au kunywa, kupumua kwa shida, au dalili za upungufu wa maji mwilini kama midomo mikavu au macho kuzama. Tuwe waangalifu na matumizi ya dawa—tusitumie dawa bila ushauri wa daktari.
Ni rahisi kuchoka tunapowahudumia watoto wagonjwa kila siku. Tujitafutie muda wa kupumzika, kula vizuri, na kuomba msaada pale inapobidi. Tuna jukumu la kuwalinda watoto wetu, lakini hatuwezi kufanya hivyo ikiwa sisi wenyewe hatuko salama kimwili na kiakili.
Kila tunapopitia hali kama hii ya watoto kuumwa kwa pamoja, ni rahisi kuhisi tumeelemewa. Lakini sisi si wazazi wa kwanza wala wa mwisho kupitia hali kama hii. Na kwa msaada wa taarifa sahihi, hatua za haraka, na kushirikiana kama jamii, tunaweza kuipitia salama
Hali hii ya mafua na virusi inaweza kuendelea kwa muda, lakini sisi tukiwa na uelewa sahihi, tunaweza kuwasaidia watoto wetu kupona haraka—na kujilinda pia. Afya ya familia zetu inaanzia nyumbani. Tuchukue hatua, tushirikiane, na tusikate tamaa.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.