Kwa muda mrefu tumesahau amri za mahakama, au matamko ya wanasiasa, kufuta maamuzi ya vyombo vya michezo, hasa mpira wa miguu, kutokana na kanuni za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) na kikubwa zaidi ni imani kuanza kujengeka kuwa haki inatendeka.
Hata hivyo, kanuni ya FIFA inayozuia masuala ya mpira wa miguu kupelekwa mahakamani ilishakuwepo tangu zamani, lakini kwa kuwa haki ilikuwa haitendeki katika uendeshaji wa mpira wa miguu ngazi ya taifa, na utaratibu mbovu wa uendeshaji katika ngazi ya klabu, ulisababisha wanafamilia washinde mahakamani kutafuta haki, au kutaka kuondoa uongozi ulioingia madarakani kinyemela, uliovunja katiba, au ulioshindwa kufanya kazi zake vizuri.
Wakati huo haikuwa ajabu kwamba wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), lakini ikiitwa FAT, wamefika Dodoma kwa ajili ya kikao, lakini kinapotaka kuanza tu, inafika taarifa ya mahakama kuwa kikao hicho kimezuiwa hadi shauri kuu lililofunguliwa na mwanafamilia litakapotolewa uamuzi.
Na wakati mwingine ilikuwa mbinu tu ya viongozi ambao walilazimika kuitisha mkutano mkuu kikatiba, lakini wakaona kunaweza kufikiwa uamuzi wa kuwaondoa, na hivyo wakatafuta watu wa kuwafungulia kesi na baadaye kuomba amri ya muda ya mahakama kuuzuia mkutano huo. Zilijaa sinema!
Kwa hiyo, imani huzaa utulivu katika uongozi na uendeshaji wa taasisi yoyote ile. Imani isipokuwepo, watu hutafuta njia nyingine za kufanikisha mambo yao wanayoona wanastahili.
SOMA ZAIDI: TFF Isisubiri CAS, Ianze Kujiwajibisha Sakata la Yanga v Simba
Wakati Bodi ya Ligi (TPLB) ilipoahirisha mechi ya watani wa jadi ya Simba na Yanga bila kuzingatia kanuni ipasavyo, shabiki mmoja aliandika barua kwa kumtumia mwanasheria ikionyesha kusudio la kwenda mahakamani kupinga maamuzi hayo.
Hata hivyo, mtu huyo hadi sasa hajatekeleza nia yake ya kwenda mahakamani, jambo ambalo ni ahueni kwa mpira wa miguu.
Hawa watu wapo wengi wanasubiri muda ufike wajilipue kwa kuwa wanajua kuwa adhabu yoyote ya kufungiwa kujihusisha na mpira haiwaathiri vyovyote vile kwa kuwa wana shughuli zao nyingine.
Hawa watu wanasubiri waone mambo hayaendi sawa na walio na mamlaka wameziba masikio na ndipo huchukua hatua kama hizo.
Mgomo wa Yanga
Uamuzi wa klabu ya Yanga kusema msimamo wao wa kugomea tarehe mpya ya mechi iliyoahirishwa kijanjajanja, upo palepale, hali inayoweza kuzua tafrani iwapo TFF na TPLB nao wataona wana nguvu nma mamlaka ya kupanga siku ya mchezo huo na atakayegomea, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni.
SOMA ZAIDI: Simba Wameonyesha Njia Ujenzi wa Viwanja
Kanuni zinataka timu ambayo imegomea kwenda uwanjani ipoteze pointi tatu na baadaye kupokonywa pointi 15, hali ambayo itamaanisha Yanga, yenye pointi 70 hadi sasa, kupoteza jumla ya pointi 18, na hivyo kuupoteza ubingwa ambao imeushikilia kwa miaka mitatu mfululizo.
Viongozi wa Yanga wanaweza wasiende mahakamani kudai haki yao, lakini wale watu walio tayari kujilipua, kama yule aliyeandika barua ya kusudio la kwenda mahakamani, wakachukua jukumu hilo na hivyo mpira kuingia matatizoni.
Bila shaka, agizo la TFF litakuwa ni kuitaka Yanga imfute uanachama huyo aliyeenda mahakamani, lakini kwa kuwa atakuwa tayari ameshafungua kesi, hilo halitaathiri mwenendo wa kesi hadi hapo uamuzi utakapotolewa.
Ni vigumu kujua huyo atakayefungua kesi, atawasilisha ombi gani la amri ya muda ya kuzuia mambo fulani yasifanyike, lakini uamuzi wowote wa kwenda mahakamani utaathiri taifa kwa ujumla, hasa wakati huu ambao nchi inajiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) yatakayofanyika mwaka huu hapa Tanzania, Kenya na Uganda.
Hilo ni moja tu, lakini taswira zilizoonekana katika mechi mbili za hivi karibuni kwenye benchi la ufundi wakati Simba ikicheza dhidi ya Mashujaa na JKT, zinatoa picha kuwa kuna mambo mengi yanapingwa kuhusu uendeshaji wa ligi, na hasa uamuzi.
SOMA ZAIDI: Kama Ligi za Wilaya na Mkoa Hazisikiki, Kuna Haja ya Kuwa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Dar es Salaam?
Haya yakizidi kukomaa, uwezekano wa wanafamilia kuchukua mkondo mwingine wa kudai haki, au kutaka kunyoosha mambo, utakuwa mkubwa zaidi na ikifikia hapo, soka letu litarudi mahakamani kama ilivyokuwa enzi hizo.
Utamaduni wa heshima
Itakuwa ajabu kama TFF na TPLB eti watataka Yanga itii kanuni wakati hazikuzingatia kanuni zilipoahirisha mchezo. Heshima inataka yule anayetaka kuheshimiwa, aheshimu kwanza. Ndio utamaduni wa heshima.
Usipowaheshimu watu, nao hawatakuheshimu. Usipoheshimu kanuni, nao hawataziheshimu, ndio kanuni ya maisha.
Wakati tunasubiri hatima ya mechi ya Yanga na Simba, ni busara hatua muhimu za kusafisha dosari iliyotokea wakati wa kuahirisha mechi kwanza ili kurejesha imani kwamba mchezo unaendeshwa kwa haki.
Hoja kwamba Yanga inapotezaje imani kwa uongozi ambao umekuwa madarakani wakati klabu hiyo ikitwaa ubingwa mara tatu haina mashiko. Unaweza kuwa na mlinzi ambaye amekulinda katika matukio mengi makubwa, lakini siku atakapobainika alikuwekea sumu kwenye chakula, na ikagundulika kabla ya kukila, hataaminika milele.
SOMA ZAIDI: TFF Wagombane na Simba, Yanga Katika Maendeleo, Siyo Kutuhumiana Kuhusu Hujuma
Popote panapotokea dosari, watu huangalia ukubwa wa hiyo dosari, na kama ilikuwepo dhamira au ilitokea kwa bahati mbaya.
Kadri mambo yanavyokwenda ndivyo inavyozidi kuonekana kama kulikuwa na dhamira ovu katika kuahirisha mchezo. Yanga walipolalamika na kuonyesha kutokuwa na imani na uongozi wa TPLB, baba wa mpira, yaani rais wa TFF, akaibuka na kauli ya kuwaponda watoto wake. Wakimbilie wapi?
Kesi ya Yanga waliyofungua Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) iliporejeshwa nchini, kiongozi wa juu wa mpira akasema walifurahi tangu klabu hiyo ilipopeleka rufaa CAS. Kauli isiyoonyesha kuwajibika na inayoondoa imani kwa uongozi.
Imani imepungua
Haya na mengine mengine yanaashiria kwamba imani kwa mamlaka zinazoongoza na kusimamia mpira inazidi kupungua, hivyo ni muhimu kwa mamlaka kuliona hilo mapema na kujirekebisha.
Hali hii isiporekebishwa, watu wataanza kurudi mahakama kutafuta njia nyingine ya kudai haki. Najua kulikuwa na kesi ya kupinga adhabu maarufu Tanzania ya kifungo cha maisha cha kutojihusisha na mpira. Najua kulikuwa na waamuzi walioshtaki mahakamani kudai malipo yao, hadi walipoitwa kando kuyamaliza.
Hizi ni dalili tosha kuwa mpira wetu unaweza kurudi mahakama na hivyo kukawa na hatari ya mambo mengi kusimamishwa wakati wa kusubiri uamuzi wa mashauri makuu.
Tusifike huko. Kiburi cha kujiendeshea mambo kiholela eti kwa sababu ni mamlaka, kiishe na kurejesha unyenyekevu wa kuzingatia sheria na kanuni.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.