The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Ni Muhimu Wazazi na Walezi Tuanze Kujadili Baleghe na Watoto Wetu Bila Hofu

Baleghe si jambo la watoto wetu peke yao; ni safari tunayopaswa kuitembea nao. Tukiwasikiliza na kuwaheshimu, tunawajengea msingi wa maisha yenye afya, heshima, na uelewa.

subscribe to our newsletter!

Siku za nyuma kidogo, haikuwa jambo la kawaida wazazi wetu kutufundisha waziwazi kuhusu mabadiliko ya mwili, au hisia tulizokuwa tukianza kuhisi kipindi cha baleghe. 

Mara nyingi tuliambulia warsha zisizoeleweka, au onyo lisilo na maelezo. Tuliogopa kuuliza, tukaogopa kuhukumiwa. Lakini sasa tumepewa nafasi mpya, nafasi ya kulea kizazi kilicho na uelewa, ujasiri na afya bora ya kimwili na kihisia.

Wazazi wa kizazi hiki tunakabiliwa na changamoto mpya, hasa uwanda mpana wa upatikanaji wa taarifa zenye mkanganyiko juu ya suala la baleghe na mambo mengine ya afya ya uzazi kwa watoto wetu. Uzuri ni kwamba hatupaswi kuwa na hofu, mabadiliko haya ni fursa adhimu kwetu kufanya mabadiliko kwa kuzungumza nao na kuwapa taarifa sahihi.

Tunaweza kuanza mazungumzo ambayo sisi hatukuwahi kupewa. Tunaweza kuwasaidia watoto wetu kuelewa mabadiliko ya balehe kwa ukweli, uwazi, upendo, na maadili bila aibu wala vitisho.

Tunawezaje kufanya hivyo?

Kwanza, ni muhimu tuelewe balehe ni nini. Balehe ni kipindi cha mpito kutoka utoto kwenda utu uzima. Ni mchakato wa mwili kujiandaa kwa uwezo wa kuzaa, lakini pia ni mlango wa mabadiliko ya kihisia, kijamii, na hata kitabia. 

SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Huugua Wote Kwa Wakati Mmoja?

Kwa kawaida, balehe huanza kati ya umri wa miaka nane hadi 14, japokuwa baadhi ya watoto huanza mapema, au kuchelewa, kidogo. Kisaikolojia, kipindi hiki cha mpito hutambuliwa kama kipindi cha dhoruba na msongo.

Katika kipindi hiki, watoto wetu huanza kujiuliza maswali mengi kwa sababu, kwa baadhi yao, mabadiliko haya huja ghafla. Wengine huogopa au kuona aibu. Tukiwakimbia katika kipindi hiki, tunaiachia nafasi mitandao ya kijamii, marafiki, au mazingira kuwapatia majibu yasiyo sahihi. Wanatuhitaji sana kwa ushauri na muongozo katika kipindi hiki.

Hivyo, ni muhimu tuwasaidie watoto kufahamu mabadiliko haya ya kimwili. Kwa wasichana, mabadiliko ya balehe huwa dhahiri zaidi na mara nyingi huanza mapema. 

Tunapaswa kuwasaidia kuelewa na kukubali mwili wao unavyobadilika. Mabadiliko haya ni kama: kuota maziwa au matiti; kuota nywele sehemu za siri na kwapani; kutokwa na ute ukeni; maumivu yatokanayo na kupevuka kwa yai kwenye mlango wa uzazi; kuanza kupata hedhi; na mwili kubadilika umbo, nyonga kuwa pana, na kiuno kuwa chembamba.

Kwa wavulana, mabadiliko haya ni pamoja na kuota nywele sehemu za siri na kifuani, kuota ndevu; kubadilika kwa sauti kuwa nzito; kuongezeka kwa misuli na urefu; kukua kwa uume na korodani; na kupata ndoto nyevu ambayo ni kawaida kabisa.

SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Malezi ya Sasa Yamekuwa Magumu Kuliko ya Zamani?

Watoto wengi huogopa kuzungumzia haya. Wengine hujiuliza kama wana tatizo. Tukieleza mapema, wanapokumbana na hali hizi, watazielewa na kuzichukulia kama sehemu ya maisha si jambo la aibu au la kuogopa.

Hedhi 

Kwa wasichana, hedhi ni moja ya hatua kuu za balehe. Kwa bahati mbaya, hadi leo bado kuna unyanyapaa juu ya hedhi katika jamii zetu. Wasichana huambiwa ni uchafu, au huogopeshwa kuwa wako tayari kuolewa.

Tuwe tofauti. Tufundishe ukweli kwamba hedhi si ugonjwa, si uchafu, na ni ishara ya afya ya mfumo wa uzazi. Kwamba ni muhimu kutumia pedi salama, au vitambaa safi vinavyosafishwa vizuri. 

Pia, wasichana wanapaswa kubadilisha pedi mara kwa mara, kuosha mikono kabla na baada, na kuzingatia usafi. Tuwaambie pia: hedhi huja na dalili tofauti, wakiona maumivu makali, au mabadiliko yasiyo ya kawaida, wawasiliane nasi, au na daktari.

Zaidi ya hayo, tuwaondolee aibu. Tusiwafiche. Tusiwaite kwa majina ya kuwadhalilisha wanapopitia siku zao. Tukiwapa nafasi ya kuzungumza, wanajenga ujasiri na heshima juu ya miili yao.

Mabadiliko ya kihisia

SOMA ZAIDI: Wazazi Waliopo Kimwili Lakini Wasiopatikana Kihisia Hukuza Watoto Wasiojali Thamani ya Upendo

Katika kipindi hiki, watoto wetu huanza kuhisi hisia kali ambazo mara nyingine huwa ngumu hata kwao kuzitafsiri. 

Tunaweza kushuhudia: mabadiliko ya tabia ghafla, kujitenga, kuwa na hasira, au huzuni, pasipo sababu ya wazi, kujitafuta, utambulisho wao, mavazi yao, sauti zao, kuvutiwa na watu wa jinsia nyingine, hizi ni hisia mpya wanazotaka kuzielewa vizuri ili kuweza kukabiliana nazo.

Wengi wetu tumeshawahi kushangaa: “Kwa nini mtoto wangu amekuwa mkali hivi ghafla na si tabia yake?” Hili ni jambo la kawaida katika balehe. Sio utovu wa nidhamu, bali ni mwili na akili kuanza kujitafuta na kujielewa upya. 

Tunachotakiwa kufanya ni kusikiliza, kuwa watulivu, na kuwaongoza. Tuwasaidie kuwa na lugha ya kueleza hisia zao. Tuwaambie: “Ni sawa kuhisi huzuni. Hata sisi tulihisi hivyo. Lakini uko salama. Tuko pamoja nawe.”

Kuweka mipaka

Katika dunia ya sasa, ambapo watoto wanakumbana na taarifa nyingi kupitia simu, runinga na mitandao, tusipozungumza nao mapema kuhusu kujilinda, huenda tukawaacha hatarini. 

SOMA ZAIDI: Wazazi na Walezi, Uelewa Juu ya Mahusiano Yenye Afya ni Muhimu kwa Watoto Wetu

Tuwafundishe kwamba miili yao ni ya thamani na ni wao pekee wanaopaswa kuamua nani auguse na kukataa kuguswa ni haki. Pia, kusema HAPANA si dhambi; ni ulinzi wa utu wao. Tuwaeleze watoto kuwa wakihisi kutishiwa wanaweza kuja kwetu bila kuogopa hukumu.

Kama wazazi, baleghe si jambo la watoto wetu peke yao; ni safari tunayopaswa kuitembea nao. Tukiwasikiliza na kuwaheshimu, tunawajengea msingi wa maisha yenye afya, heshima, na uelewa.

Tukumbuke, sio lazima tuwe na majibu yote. Lakini ikiwa tupo tayari kusikiliza, kuwa na mazungumzo ya kweli, na kujifunza pamoja nao, basi tunawapa zawadi kubwa sana ambayo sisi pengine hatukupewa.

Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×