The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

‘CHADEMA G55’: Makovu ya Uchaguzi, Ushawishi Hafifu na Ndoto za Kujiletea Mabadiliko Binafsi Nyuma ya Kivuli cha Mbowe

Moja ya changamoto inayoeleza kuwakabili wanachama hao walioondoka CHADEMA ni ushawishi hafifu huku wengi wakiwaeleza kama watekelezaji wa mkakati unaoratibiwa na wengine

subscribe to our newsletter!

Hama hama ya wanachama waliokuwa sehemu ya waliomuunga mkono Mwenyekiti wa zamani wa CHADEMA, Freeman Mbowe katika uchaguzi wa ndani wa CHADEMA imeendelea. Mitandao iliyotumiwa wakati wa uchaguzi ikielezwa kutumiwa kuwashawishi waliomuunga mkono Mbowe, kuhama chama hicho.

Wakati sehemu kubwa ya wachambuzi wakieleza juu ya ushawishi mdogo ya wanaohama CHADEMA, hasa mbele ya wananchi wa kawaida, ahadi ya kushiriki uchaguzi kupitia chama kipya, kupata kati ya viti 10 mpaka 20 ya chama kipya watakachoenda, na kupata viti maalum imekuwa ikitumika kuwavutia wanachama hao.

Makovu ya uchaguzi

Baadhi ya hoja kubwa zinazotajwa na wanachama waliohama CHADEMA ni kwanza kutokubaliana na msimamo wa CHADEMA wa No Reform, No Election, lakini pili wameendelea kusema kuwa wale waliomuunga mkono Freeman Mbowe wameendelea kubaguliwa na kutukanwa, hoja ambayo wanachama wengine walijitokeza na kuipinga.

“Ambacho kinaendelea kwenye chama kuanzia siku ile ya uchaguzi mpaka leo ni ubaguzi mkubwa wa wanachama ambao wanaitwa ni timu ya Mbowe,”alieleza Benson Kigaila aliyekuwa kiongozi wa Sekretarieti ya CHADEMA toka mwaka 2004.

“Wanabaguliwa kuanzia kwenye kamati kuu mpaka kwenye misingi. Kila mtu anayejulikana kwamba alimuunga mkono Mbowe anaitwa msaliti,” aliongeza zaidi akiongea na wanahabari mnamo Mei 07, 2025.

“Kwa maoni yangu kama tungetaka kuita watu wasaliti, ingekuwa ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti aliyekuwa anagombea kiti cha Mwenyekiti na Mwenyekiti akiwa yupo; ingewezekana wale ndio wasaliti,” Kigaila alifafanua zaidi. Kigaila alikuwa akitangaza rasmi kujiondoa katika chama hicho mnamo Mei 07, 2025 pamoja na Salum Mwalimu na Catherine Ruge.

Salumu Mwalimu aliyekuwa pamoja na Kigaila katika kuongea na waandishi wa habari naye akasisitiza kwamba CHADEMA imepoteza dira.

“Unaweza ukashinda kwa hila, unaweza ukashinda kwa upanga, kwa njama, unaweza ukashinda kwa uwongo, unaweza ukashinda kwa ulaghai. Unaweza ukashinda kwa kila namna iliyo ovu na utashinda.Lakini unapaswa pale mara baada ya kushinda ujitathmini, ujipime ujue sasa wewe ni kiongozi wa watu,” alieleza Salum Mwalimu aliyekuwa kiongozi mwandamizi ya Sekretarieti ya CHADEMA kwa miaka 10

“Huwezi ukashinda kwa hiliba ukadhani utaongoza chama kwa hiliba,” aliongeza Mwalimu anayefahamika kama moja ya mtu wa karibu zaidi wa mwenyekiti aliyepita wa chama hicho Freeman Mbowe.

Katika mkutano huo na wanahabari, Catherine Ruge aliyekuwa moja ya waasisi wa kikundi cha ‘CHADEMA G55’walioandika waraka uliosambaa mnamo Aprili 03, 2025, wakieleza kupinga hoja ya No Reform, No Election; alieleza kuwa sababu kubwa ya kujiondoa CHADEMA ni kuminywa kwa uhuru wa maoni na yeye kupinga msimamo wa chama hicho.

“Naona kabisa sihitajiki na sitakiwi CHADEMA, na siwezi kukaa sehemu ambayo sihitajiki na sehemu ambayo sina furaha, kwa maisha yangu furaha yangu ni kipaumbele. Kwa nini mawazo ya watu yapigwe rungu? Aliuliza Ruge; “Kwa sababu sisi tulitaka mjadala, na kujadili masuala sio kuwatukana watu, kuwaita majina.”

Wachambuzi wengi wameendelea kueleza kinachotokea CHADEMA, pamoja na kutofautiana maoni lakini pia kuna hali ya wale waliokuwa wakimuunga mkono Freeman Mbowe kwenye uchaguzi kutoridhika na matokeo ya uchaguzi.

“Watanzania wanajua wengi hawa walioko G55 ni wale ambao walikua hawamuungi mkono Tundu Lissu wakati wa uchaguzi kwa hiyo haiwashangazi Watanzania kuona bado wakiendelea kuwa na upinzani wa namna hiyo,” anaeleza Mwanasheria na Mchambuzi, Thobias Messanga.

“Inasikitisha kwamba suala la uchaguzi linajenga chuki badala ya kuwa ni hatua muhimu ya kidemokrasia. Inaonekana hali ya kutoridhika au ni hali ya wale watu kutoamini kwamba wanaweza kushindwa uchaguzi,” aliongeza zaidi.

Chambo ya Kuhama

Baadhi ya wanachama waliojing’oa wengi wameendelea kusubiri mpango wa kujiunga na chama kipya,ikitegemewa mpango wa kuhamia chama kipya utakamilika hivi karibuni.

Chambo inayotajwa na baadhi ya waliofikiwa ndani ya CHADEMA wanaeleza ni kuelezwa kuwa tayari kuna makubaliano yatakayohakikisha wanapoenda wanakuwa na nguvu ya kisiasa. Ikimaanisha uhakika wa kupata viti vya ubunge na kupata rasilimali za kushiriki uchaguzi. Hata hivyo wachambuzi mbalimbali wameonesha kuwa kutokana na kuwa kuna watu wengine wanaovuta kamba za maamuzi ya fukuto la G55, hii imesababisha wengi wao kufanya maamuzi ya papara, bila kuzingatia ushawishi mdogo walio nao.

“G55 hawana athari yeyote watakayoitengeneza baada ya wao kuhama CHADEMA. Uamuzi wao unaonekana zaidi ni wenye papara na ambao unaonekana kuna ushawishi au kuna vitu ambavyo vinawasukuma kufanya yale ambayo wameyafanya kufanya bila mpangilio,” alieleza mchambuzi wa siasa Luqman Maloto akiongea na The Chanzo.

The Chanzo ilimuuliza John Mrema kuhusu suala la ni wapi kundi la G55 linaweza kuelekea, ambapo alieleza bado kundi hilo lipo kwenye mashauriano na kuzungumza na vyama mbalimbali vya siasa isipokuwa CHADEMA na CCM.

“Bado tupo kwenye mashauriano ni wapi panafaa kwenda kufanya siasa ukifika wakati wa kusema na kukubaliana tutasema wala si jambo la kificho,” alieleza John Mrema. “Unaona watu wengi wanaendelea kuhama kutoka CHADEMA kutuunga mkono kwa sababu wamesikia ukweli. Sasa CHADEMA kimekuwa sio chama cha siasa tena bali kikundi cha wanaharakati.”

Moja ya chama ambacho kimekuwa kikitajwa zaidi, CHAUMMA kimeeleza kuwa hakuna mazungumzo yaliyofanyika mpaka sasa. Hata hivyo, akiongea na The Chanzo, mnamo Mei 14, 2025, Mwenyekiti wa chama cha CHAUMMA, Hashimu Rungwe aliwakaribisha wanachama hao wanao ondoka CHADEMA.

“Hawa watu sijui kama wameshataja chama husika [wanachoenda], lakini hapa bado hawajafika. Kama watapiga hodi mlango uko wazi. Kwa sababu bado tunahitaji wanachama, hivi ni vyama vya wananchi,” alieleza kiongozi wa chama hicho Hashimu Rungwe.

Rungwe alienda mbali zaidi kueleza kuwa chama hicho kiko tayari kujadiliana kuhusu nafasi mbalimbali za uongozi na kwenye uchaguzi unaokuja ikiwa wanachama hao wapya watataka kujiunga na CHAUMMA.

Sehemu kubwa ya wana-CHADEMA hao wanao ondoka wameendelea kusisitiza juu ya ndoto zao za kugombea uchaguzi wa 2025, huku wakikosoa msimamo wa chama hicho wa ‘bila mabadiliko hakuna uchaguzi’, kuwa umeishia kuzima ndoto zao. Jambo hili limewafanya watafute jukwaa lingine la kujiletea mabadiliko hayo binafsi.

Ushawishi Hafifu

Moja ya changamoto inayoeleza kuwakabili wanachama hao walioondoka CHADEMA ni ushawishi hafifu huku wengi wakiwaeleza kama watekelezaji tu wa mkakati na mpango unaoratibiwa na wengine, wao wakiwa watu wa kutumwa kuongea hiki na kile, kusogea hapa na pale.

“Huu ni mradi wa mfumo, katika kuhakikisha kwamba wanaigawa CHADEMA. Wametumia uchaguzi wetu wa ndani ya chama kama mlango wa kuingilia kuwashawishi wale wachache walioshindwa ili waweze kuwashawishi wanachama waweze kukihama chama,” anaeleza Nice Gisunte Mwenyekiti wa BAWACHA Ilala, ambaye ni moja ya waliokuwa waratibu wa kampeni za Mbowe.

“Ninasema ya kwamba ni mradi kwa sababu hata mimi hao viongozi wakuu wenye mradi wao walinifikia na mimi. Walinifikia kwa maana wakiamini mimi ni mwenzao tulikua timu moja wakati wa uchaguzi wa mheshimiwa Mbowe,” aliendelea kufafanua Gisunte akiongea na wanahabari mnamo Mei 13, 2025.

“Wamenifikia kunishawishi kuhama chama na mpango wao wamenishirikisha, tunajua ya kwamba wanaelekea CHAUMMA na wameahidiwa ya kwamba wataachiwa majimbo yapatayo thelathini, wameahidiwa kupatikana kwa viti maalum,” aliendelea kufafanua. “Hivyo na mimi walikuwa wananishawishi kwamba niende nitapata viti maalum. Wameahidiwa fedha kwa ajili ya kufanya kampeni milioni 100 mpaka 200 kila jimbo.”

Hoja kubwa inayotajwa juu ya umoja huu wa G55 ni kutoa uhalali wa kisiasa kwenye uchaguzi unaokuja ambao CHADEMA, chama kikubwa zaidi cha upinzani nchini kimeeleza hakitashiriki kama hakuna mabadiliko ya muhimu yatakayofanyika. Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wameendelea kuonesha wasiwasi juu ya ushawishi walionao G55 na kama watakuwa na mchango wowote katika mazingira ya kisiasa nchini.

“Viongozi ambao wameondoka ambao G55, ukimuangalia Kigaila, John Mrema wote wale walikua ni sekretarieti ya CHADEMA. Huwezi kuwapa turufu kwamba wanapokwenda wataweza kujenga ushawishi mkubwa; kwa sababu hawajawahi hata siku moja, wao wenyewe kusimama na kujenga ushawishi mtu mmoja mmoja na kushinda angalau jimbo,” anaeleza Luquman Maloto.

“Hapa kuna kujidanganya kwamba kwa kujiondoa kwao, pengine wataifanya CHADEMA ionekane dhaifu; hata kama itakuja kuonekana hivyo baadae lakini haitakua sababu ni wao kundoka,” aliongeza Maloto.

Hata hivyo wengi wameendelea kuonya kuwa pamoja na ushawishi mdogo walionao G55 bado CHADEMA inahitajika kufanya jitihada za kuunganisha chama, ili kuondoa mparaganyiko unaoweza kubadilika na kuwa udhaifu wa kudumu ndani ya chama.

“Sioni kama G55 wana nguvu sana, mwisho wa siku wataonekana kama ni watu ambao hawakuwa na msimamo, kwa sababu wangeweza kupigana vita vyao ndani ya chama,” anaeleza Mwanasheria na Mchambuzi Fortunata Kitokesy. “Hata hivyo, nyumba yeyote ikiwa na nguzo tano ikatoka moja, uimara wake unapungua.”

Kivuli cha Mbowe

Ukimya wa Mwenyekiti wa zamani wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kwenye suala hili ambalo baadhi ya watu wake wa karibu wameonekana kuwa mbele, umeendelea kuacha maswali kwa wafuatiliaji wa mambo. Jambo hili lilifanya Katibu wa Chama, John Mnyika kueleza kuwa aliongea na Mwenyekiti huyo wa CHADEMA juu ya mambo yanayoendelea.

“Nimewasiliana na Mwenyekiti Mstaafu Freeman Mbowe amenieleza hana dhamira ya kugombea urais, ubunge au uongozi wa chama chochote cha siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” aliandika Mnyika kwenye ukurasa wake wa X mnamo May 08, 2025.

Na kuongeza: “Natambua kuwa wachache waliojiondoa, baadhi yao wamekuwa wakitumia jina lake kushawishi baadhi ya viongozi wa chama na wenye nia ya kugombea kujiondoa kwenye chama kwa madai kuwa anawaunga mkono na anajiandaa kugombea urais kupitia Chama kingine.”

The Chanzo ilipowauliza baadhi ya wanachama wa CHADEMA waliokuwa wakimuunga mkono Mbowe juu ya maoni yao hasa katika suala la mashaka ya kutajwa kwake katika hama hama ya vikundi vidogo vya wana-CHADEMA; walieleza ni jambo ambalo hawana maoni nalo na kwa wengine, ukimya mkali ulitawala.

Journalism in its raw form.

The Chanzo is supported by readers like you.

Support The Chanzo and get access to our amazing features.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Did you enjoy this article? Consider supporting us

The Chanzo is supported by readers like you.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts

×
×