Kila mwaka ifikapo Mei 16, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kiume. Ni siku ya kuangazia maisha ya wavulana, changamoto wanazokutana nazo, na namna tunavyoweza kuwasaidia kukua katika mazingira salama na yenye msaada.
Lakini, kwa bahati mbaya, siku hii mara nyingi hupita bila kelele, bila mjadala, bila hatua madhubuti. Na kama jamii, tunapaswa kujiuliza: Je, tunawalea wavulana wetu kwa njia bora? Tunawalinda? Tunawaandaa kuwa wanaume bora wa kesho?
Tumekuwa tukiwahimiza wavulana wetu kuwa wagumu, wasiokuwa na uoga, wasiolia. Lakini, kwa kufanya hivyo, tumekuwa tukiwakataza kuwa binadamu kamili. Wakati wasichana wakihimizwa kueleza hisia na kutafuta msaada, wavulana mara nyingi huambiwa, “Wewe ni mwanaume,” au “Wanaume hawalii.”
Lakini sisi sote tunajua kuwa maumivu ya ndani hayaangalii jinsia. Mtoto wa kiume anaweza kuwa na huzuni, hofu, au tashwishwi kama mtoto mwingine yeyote. Tunahitaji kujenga mazingira yanayompa nafasi ya kuelewa hisia zake na kujifunza namna ya kuzishughulikia.
Kumlinda mtoto wa kiume ni pamoja na kumpa uhuru wa kuwa yeye, bila hofu ya kubezwa au kudhalilishwa.
SOMA ZAIDI: Ni Muhimu Wazazi na Walezi Tuanze Kujadili Baleghe na Watoto Wetu Bila Hofu
Tuwaache watoto wa kiume waishi katika utoto wao. Tumekuwa tukiwaharakisha watoto hawa kukua. Pale ambapo baba hayupo, mara nyingi tunamwambia mvulana mdogo: “Wewe sasa ni kichwa cha familia.”
Lakini ukweli ni kwamba bado ni mtoto, anahitaji kucheza, kuuliza maswali, na kujifunza kwa utulivu. Tusimvike mzigo wa utu uzima kabla hajakomaa. Kumuachia utoto wake ni sehemu ya kumjengea afya ya kiakili na ya kihisia nzuri.
Wakati mwingine, bila kujua, tumekuwa tukiwaongoza watoto wetu kwa ukali tukiamini kwamba mwanaume anapaswa kulelewa hivyo. Lakini je, ni aina gani ya wanaume tunaotaka kuwalea? Kama tungependa kulea wanaume wa kesho watakaoheshimu watu wote, watakaoomba msamaha bila aibu na wanaoelewa kuwa upole na huruma ni ishara ya nguvu, si udhaifu, basi inabidi tubadilike.
Tuwafundishe watoto wetu wa kiume kuwa kuwa mwanaume bora hahitaji kuamrisha watu, au kulazimisha vitu bali ni kujitambua, kuwajibika, na kujali watu na vitu vinavyomzunguka.
Mara nyingi, tunapozungumza kuhusu afya ya uzazi, au mahusiano salama, tunawaelekeza zaidi wasichana. Lakini wavulana nao wana haki ya kufundishwa mapema kuhusu heshima, ridhaa, mipaka ya mwili, na mahusiano yenye tija na afya.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Huugua Wote Kwa Wakati Mmoja?
Tusisubiri hadi waingie umri wa balehe; tuanze mazungumzo haya mapema, kwa lugha rahisi na ya uwazi. Tuwape maarifa yatakayowasaidia kujenga mahusiano mazuri na yenye staha katika maisha yao.
Wavulana pia hupitia unyanyasaji wa kimwili, kihisia, na hata kingono lakini hawatoi taarifa kwa sababu jamii imewafundisha kunyamaza. Wakipitia changamoto hizi, mara nyingi huogopa kusema kwa hofu ya kudharauliwa au kutokuaminiwa.
Kama jamii tunapaswa, kuwaamini na kuwasikiliza wanapojieleza, kuwapa msaada wa kisaikolojia na kisheria na kuondoa aibu inayozunguka suala zima la wavulana kudhalilishwa na kufanyiwa ukatili.
Watoto wetu wa kiume pia,hukumbana na changamoto nyingi shuleni na mitaani kuanzia msukumo kutoka kwa marafiki (peer pressure), hadi kupoteza mwelekeo kwa sababu ya kukosa msaada wa kihisia.
Tunahitaji walimu, akina baba, na walezi wa kiume ambao ni kielelezo bora cha utu na uwajibikaji, kusimama katika nafasi zao ili kuwaongoza watoto wa kiume. Programu za shule zinazojumuisha ujuzi wa maisha, kujitambua, na afya ya akili ziongezeke. Pia, tujenge mazingira rafiki yatakayowasaidia kupaza sauti, kuuliza maswali, na kujifunza kwa uhuru.
SOMA ZAIDI: Je, ni Kweli Kwamba Malezi ya Sasa Yamekuwa Magumu Kuliko ya Zamani?
Tusiwaachie tu wazazi jukumu la kulea wanaume bora wa kesho. Tunahitaji sera zinazojumuisha wavulana kwenye afua za kijinsia na maendeleo ya kijamii. Shule salama na zenye walimu waliofunzwa kuhusu malezi jumuishi.
Vyombo vya habari vinavyotoa taswira chanya ya ‘’uanaume’’ (positive masculinity). Jamii inayozungumza wazi kuhusu malezi bora ya watoto wa kiume na wa kike, ndiyo jamii inayoweza kuleta mabadiliko chanya.
Wavulana wa leo ndio waume, baba, viongozi, na wanajamii wa kesho, na sisi ndio tunaowalea. Tunapowaangalia tuone nafsi zinazohitaji kuelekezwa kwa upendo, heshima, na uelewa.
Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kiume, tuchukue hatua. Tuwalee wavulana wetu kwa njia itakayowajenga kuwa wanaume bora, wanaojali, na wanaotengeneza dunia salama kwa wote.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.